read

Aya 258: Aliyehojiana Na Ibrahim

Maana

Mwenyezi Mungu, katika Aya iliyotangulia, amebainisha kuwa mtawala wa waumini ni Mwenyezi Mungu, na kwamba wao wanatoka katika giza la shaka kuingia kwenye mwangaza wa uongofu na imani. Na makafiri watawala wao ni mataghuti wanaowatoa kwenye mwangaza wa kimaumbile na kuwaingiza katika giza la ukafiri na upotevu.

Baada ya hapo anatoa kisa, kwa Mtume wake mtukufu juu, ya Mumin aliyetoka kwenye giza la shaka na kuingia katika nuru ya imani, katika Aya ijayo. Na kisa cha kafiri aliyehojiana na Ibrahim juu ya Mola wake baada ya kutoka kwenye nuru ya kimaumbile kwenda kwenye giza la ukafiri, katika Aya hii.

Je, hukumjua yule aliyehojiana na Ibrahim juu ya Mola wake, kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme? Ibrahim aliposema: Mola wangu ni yule ambaye huhuyisha na kufisha. Yeye akasema: 'Mimi pia na huhuyisha na kufisha'

Hii ni hoja anayoitaja Mwenyezi Mungu kwa Mtume na kwa watu wote katika mfumo wa kus- taajabu pamoja na kukanusha.

Ibrahim (a.s.) alitoa mwito wa kutupiliwa mbali masanamu na mataghuti na kuwa kwenye dini ya uadilifu na usawa, lakini akapingwa na watawala., sio kwa kuona mwito wake sio sawa, bali ni kwa kuhofia manufaa na chumo lao na kupupia wasishuke vyeo vyao.

Kama kawaida walianza kujadiliana na Ibrahim kwa maneno; waliposhindwa wakawa hawana la kusema, ispokuwa walitangaza vita na wakajaribu kummaliza kwa kumchoma katika moto; sawa na wanavyofanya wakoloni hivi sasa - wanaeneza propaganda za upotevu kwa njia ya magazeti, radio na mashirika ya habari yaliyonunuliwa; wakishindwa wanaanza kampeni za mapinduzi, wakishindwa hutupa mabomu ya Napalm kwa watu wanyonge wasiokuwa na hatia yoyote.

Basi yule ambaye amepetuka mpaka kwa mali na jaha alimuuliza Ibrahim: "Ni nani Mola wako?" Ibrahim akajibu: "Mola wangu ni yule anayempa uhai anayemtaka kisha huuondoa na wala hana anayeshirikiana naye katika hilo."

Yule Taghuti akasema: "Mimi pia ninaweza hivyo." Akawaleta watu wawili; akamwua mmoja wao na kumwacha mwingine. Ibrahim alipoona kujigamba kwa Taghuti kwa kutegemea, maneno na kujitia kutofahamu hoja na maana halisi yaliyokusudiwa, alileta mfano mwingine ambao hauwezi kuingizwa makosa wala madai yoyote, akasema:

Hakika Mwenyezi Mungu hulichomoza jua Mashariki, basi wewe lichomoze Magharibi. Akafedheheka yule aliyekufuru.

Kwa sababu alishindwa kubabaisha na kupotosha. Hivi ndivyo anavyojaribu kufanya kila mbatilifu - kujisifu na kufanya hila; hila zinaposhindwa hudangana akawa hana la kufanya.

Kundi la wafasiri wamesema kuwa ni jawabu la pili la Ibrahim; la kwanza ni 'Ambaye huhuisha na kufisha' na la pili ni 'Basi wewe lichomoze magharibi' ili akate mjadala upesi bila ya kurefusha.

Razi na Sheikh Muhmmad Abduh, wanasema kuwa hilo ni kuleta mfano mwingine ili kufafanua zaidi dalili; kwa maana yakuwa yule ambaye anatoa uhai ndiye ambaye analichomoza jua kutoka mashariki; na kama ukiweza kuwafunika watu wako kwa mfano wa kwanza basi utashindwa kuwafunika katika mfano huu.

Vyovyote itakavyokuwa, iwe ni majibu mawili au mifano miwili, lakini ni kwamba kafiri alishindwa na kuzibwa mdomo; na alishindwa kwa vile hana haki, naye hana haki, kwa vile ni kafiri.

Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.

Ambao wamejidhulumu kwa kuinusuru batili na kuipinga haki.

Aya haikutaja jina la Taghuti kwa sababu, muhimu ni kupata mazingatio ya kisa sio jina la mhusika. Imetangaa kwamba alikuwa ni Namrud bin Kan'an bin Sam bin Nuh. Inasemekana kwamba yeye ndiye wa mwanzo kuvaa taji kichwani; akatakabari na kudai uungu. Tutarudia kuelezea kisa cha Ibrahim na watu wake katika Sura ya Anbiya (Mitume) na sehemu nyinginezo.

أَوْ كَالَّذِي مَرَّ عَلَىٰ قَرْيَةٍ وَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا قَالَ أَنَّىٰ يُحْيِي هَٰذِهِ اللَّهُ بَعْدَ مَوْتِهَا ۖ فَأَمَاتَهُ اللَّهُ مِائَةَ عَامٍ ثُمَّ بَعَثَهُ ۖ قَالَ كَمْ لَبِثْتَ ۖ قَالَ لَبِثْتُ يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ ۖ قَالَ بَلْ لَبِثْتَ مِائَةَ عَامٍ فَانْظُرْ إِلَىٰ طَعَامِكَ وَشَرَابِكَ لَمْ يَتَسَنَّهْ ۖ وَانْظُرْ إِلَىٰ حِمَارِكَ وَلِنَجْعَلَكَ آيَةً لِلنَّاسِ ۖ وَانْظُرْ إِلَى الْعِظَامِ كَيْفَ نُنْشِزُهَا ثُمَّ نَكْسُوهَا لَحْمًا ۚ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ قَالَ أَعْلَمُ أَنَّ اللَّهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ {259}

Au kama yule aliyepita karibu na mji nao umeangukiana sakafu zake, akasema: Mwenyezi Mungu atauhuisha vipi (mji) huu baada ya kufa kwake? Mwenyezi Mungu akamfisha kwa miaka mia, kisha akamfufua, akamuuliza: Umekaa muda gani? Akasema: Nimekaa muda wa siku moja au sehemu ya siku. Akasema: Bali umekaa miaka mia, tazama chakula chako na kinywaji chako hakikuharibika. Na mtazame punda wako na ili tukufanye uwe ni ishara kwa watu. Na itazame mifupa jinsi tunavyoinyanyua, kisha tunaivisha nyama. Basi yalipombainikia alisema: Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.