read

Aya 259: Aliyepita Karibu Na Mji

Maana

Aya iliyotangulia ilikuwa ni mfano kwa kafiri ambaye amemfanya Taghuti kuwa ni mlinzi na mtawala wake, na kutoka katika mwangaza na kuingia katika giza; na Aya hii ni mfano wa Mumin aliyemfanya Mwenyezi Mungu kuwa mtawala wake; akatoka gizani na kuingia katika mwangaza.

Au kama yule aliyepita karibu na mji nao umeangukiana sakafu zake akasema: Mwenyezi Mungu ataufufua vipi (mji) huu baada ya kufa kwake?

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakufafanua jina la mji wala jina la aliyepitia. Hapo ndipo wakahitalifiana wafasiri - kwamba je, mtu huyo alikuwa kafiri, je alikuwa Uzairi (Ezra), Armila (Nehemia) au Khidhr? Vile vile wametofautiana kuhusu mji, je ulikuwa Baitil Maqdis au mji mwingine?Hakuna dalili yoyote juu ya hayo isipokuwa Hadith za Kiisrail tu.

Maana ya mji ulioangukiana sakafu zake ni kuwa hauna watu na majumba yamevunjika umebaki magofu; na swali lilikuwa la kuuliza kufufuliwa watu wa mji sio mji wenyewe.

Yule anayedai kuwa aliyepita katika mji alikuwa kafiri kwa vile alitia shaka katika kudura ya Mwenyezi Mungu, tunamwambia kuwa, sio kila anayepitiwa na shaka akilini mwake na akataka ufafanuzi, ni kafiri; bali ni kinyume cha hivyo. Ibrahim alimtaka Mola wake amuonyeshe anavyohuisha waliokufa na hali yeye alikuwa akilingania imani na yakini.

Zaidi ya hayo ni kwamba kutaka kujua zaidi kudura ya Mwenyezi Mungu ndio imani yenyewe. Kwa hivyo basi linabainika kosa la anayedai kuwa aliyepita mjini alikuwa kafiri sio kwa jengine ispokuwa tu, ati amesema: Mwenyezi Mungu ataufufua vipi (mji) huu baada ya kufa kwake?

Hapana! Huko sio kukanusha, isipokuwa kubomoka huko alikokuona kulimfanya apigwe na butwaa na kushindwa kujua njia ambayo itawarudishia uhai watu wa mji huo.

Mwenyezi Mungu akamfisha kwa miaka mia.

Hayo yalikuwa ni mauti ya hakika sio majazi. Hapo hapahitaji taawil.

Kisha akamfufua.

Alimfufua kama alivyokuwa. Wala si zito hilo kwa ambaye anauambia ulimwengu na kilicho katika ulimwengu 'kuwa', kikawa. Hakuna kitu cha ajabu kabisa kama kumlinganisha Muumbaji na viumbe katika uwezo Wake.

Hisabu Ya Kaburini

Akamuuliza: Umekaa muda gani?

Hili ni swali la kuthibitisha, sio la kutaka kufahamu.

Akasema: Nimekaa muda wa siku moja au sehemu ya siku.

Lau si Ijmai (kongamano la wanavyuoni) na hadithi ingeliwezekana kusema kuwa hakuna hisabu kaburini wala kuulizwa, isipokuwa siku ya ufufuo kwa kutegemea Aya hii na Aya nyingine inayosema: "Na siku kitakaposimama kiyama wataapa wenye makosa kuwa hawakudumu isipokuwa saa moja tu ..." (30:55)

Wala hakuna sababu ya wakosaji kuapa na kughafilika na muda uliopita toka kufa kwao isipokuwa kwa kukosa uhai, kwa sababu kuhisi muda hakuwi isipokuwa mtu huyo awe na uhai.

Sheikh Mufid katika kitabu Awailul Maqalat anasema kwamba, watu baada ya kufa wako tabaka nne: Tabaka ya kwanza ni yule aliyeijua haki na akaitumia. Huyu atapewa uhai mzuri baada ya mauti kabla ya kufufuliwa. Tabaka ya pili ni yule aliyeijua haki na asiitumie kwa inadi.

Huyu vile vile atakuwa hai lakini ataadhibiwa. Tabaka ya tatu ni yule aliyefanya madhambi na maasi kwa kupuuza, sio kwa inadi. Huyu uhai wake ni wenye kutiliwa shaka baada ya kufa na kabla ya kufufuliwa. Tabaka ya nne ni wenye kuzembea kufanya twaa bila ya inadi na walio wanyonge. Hawa hawatafufuliwa, bali watabaki katika ulimwengu wa mauti mpaka siku ya kufufuliwa.

Sheikh Mufid amechukua ugavi huu kutokana na riwaya za Ahlul bait (a.s.); miongoni mwa hizo ni: "Hataadhibiwa kila maiti, isipokuwa ataadhibiwa kwa ukafiri hasa na atapata neema kwa imani hasa; na wasiokuwa hawa wawili watapuuzwa na wala hawataulizwa mpaka siku ya ufufuo. "Haya tumeyazungumza kwa ufafanuzi katika kitabu Falsafatul Mabdai Wal Ma'ad mlango wa "Baina ya dunia na akhera" na mlango "Hisabu ya kaburi."

Akasema: Bali umekaa miaka mia, tazama chakula chako na kinywaji chako hakikuharibika.

Amesema hakikuharibika na hakusema havikuharibika, kwa maana ya kuwa chakula na kinywaji ni aina moja tu katika kuharibika haraka. Maana ya hakikuharibika ni kwamba havikubadilika, pamoja na kupita miaka, bali vimebakia katika hali yake. Huu ni muujiza wa Mungu, kwa sababu chakula na kinywaji huharibika haraka. Hapa nahofia yule anayejaribu kuiambatanisha Qur'an na sayansi asije akasema kuwa vilikuwa katika jokofu (friji).

Na mtazame punda wako

Jinsi alivyogeuka na kuoza, lakini chakula na kinywaji vimebakia katika hali yake. Huu ndio muujiza zaidi na kudhihirisha kudura inavyogeuza kawaida. Kwa sababu anga ndiyo inayoathiri, kinywaji kingeharibika kabla ya punda, kwa sababu ndiye mwenye nguvu kuliko chakula na kinywaji. Kwa hivyo kufa punda na kudumu chakula, ni dalili ya kuwa Mwenyezi Mungu hashindwi na kitu chochote.

Inasemekana kuwa punda alibakia hai miaka mia bila ya kinywaji wala chakula. Kwa hali zote mbili, ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliyafanya hayo ili aondoe kustaajabu kwa Uzayr na kuona kwake ajabu ya kufufuliwa kwa mji huo; na pia ili amfanye kuwa ni hoja ya kupatikana ufufuo kwa yule atakayejua hali yake katika watu wa wakati huo. Hayo ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.): "Na ili tukufanye uwe ni ishara kwa watu."

Na itazame mifupa jinsi tunavyoinyanyua, kisha tunaivisha nyama.

Wamehitalifiana kuhusu mifupa hii: Je ilikuwa ya Uzair au mifupa ya punda wake? Msemaji mmoja alisema kwamba hiyo ni mifupa ya mwenye punda, na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alifufua jicho lake kwanza ili aone sehemu iliyobakia ya mwili jinsi inavyokusanyika na kupata uhai lakini huku ni kujisemea tu juu ya Mwenyezi Mungu bila ya elimu.

Lenye nguvu zaidi ni kwamba hiyo ni mifupa ya punda kwa sababu mwenye punda alisema: "Nimekaa muda wa siku moja au sehemu ya siku." Kwani lau angeliiona mifupa yake ilivyoharibika, angelitambua urefu wa muda aliokaa Mwenyezi Mungu aliivika nyama; sawa na alivyoanza kumuumba. Imam Ali (a.s.) anasema: "Kuisha dunia baada ya kuweko sio ajabu kuliko kuianzisha."

Basi yalipombainikia alisema: Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
Aliyasema haya baada ya kupitiwa na majaribio binafsi yasiyo na shaka. Vipi atie shaka na yeye ameshuhudia kwa macho miujiza mitatu: Kurudishwa hai baada ya kufa, kufufuliwa punda wake na kudumu chakula chake miaka mia bila kuharibika.

Funzo tunalolipata kutokana na kisa hiki ni kwamba mwenye akili hatakikani kukanusha lile lisilotambuliwa na akili yake, au lisiloafikiana na aliyoyasoma katika kitabu au kusikia kuto- ka kwa mwalimu wake, bali inatakikana ajizuie hata lile analoona linatofautiana na kanuni za kimaumbile. Elimu imethibitisha kuwa hakuna kanuni ya maumbile kabisa.

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ أَرِنِي كَيْفَ تُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۖ قَالَ أَوَلَمْ تُؤْمِنْ ۖ قَالَ بَلَىٰ وَلَٰكِنْ لِيَطْمَئِنَّ قَلْبِي ۖ قَالَ فَخُذْ أَرْبَعَةً مِنَ الطَّيْرِ فَصُرْهُنَّ إِلَيْكَ ثُمَّ اجْعَلْ عَلَىٰ كُلِّ جَبَلٍ مِنْهُنَّ جُزْءًا ثُمَّ ادْعُهُنَّ يَأْتِينَكَ سَعْيًا ۚ وَاعْلَمْ أَنَّ اللَّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ {260}

Na Ibrahim aliposema: Mola wangu! Nionyeshe jinsi unavyofufua wafu. (Mwenyezi Mungu) akasema: Huamini? Akasema: Kwa nini! (naamini) Lakini upate kutulia moyo wangu. Akasema: Basi chukua ndege wanne na uwakusanye kisha (uwachinje) uweke juu ya kila jabali sehemu katika wao. Kisha waite, watakujia mbio. Na jua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.