read

Aya 26-27: Humpa Ufalme Amtakaye

Maana

Dhahiri ya Aya kwa ukamilifu inalingana na hali ya waislamu katika siku za mwanzo wa Uislamu: ambapo wakati huo hawakuwa na ufalme, nguvu wala usultani. uislamu ulianza katika hali ya ugeni, kama alivyosema Mtume (s.a.w.w.). ufalme ulikuwa wa wafursi na warumi.

Lakini baada ya kuja ushindi wa Mwenyezi Mungu, mambo yaligeuka; aliye duni akawa mtukufu na mtukufu akawa duni. wafursi na warumi wakawa wanatawaliwa na waislamu baada ya kuwa wao ndio watawala.

Wasilamu wakawa watawala baada ya kuwa wanyonge wakiwaogopa watu, ndipo matakwa ya Mwenyezi Mungu yakathibiti aliyoyabainisha kwa kauli yake: "Na tukataka kuwaneemesha wale waliofanywa wanyonge katika ardhi na kuwafanya wawe viongozi na kuwafanya warithi." (28:5).

Sema: "Ewe Mola uliyemiliki ufalme wote"

Makusudio ya kumiliki ufalme, ni uweza wake juu ya kila kitu; ni kama kusema Mwenyezi Mungu amemiliki uwezo. Ameleta neno ufalme kwa sababu athari ya kumiliki kitu chochote ni uwezo wa mwenye kumiliki kukitumia wala hapana yeyote anayeweza au kumiliki kitu; isipokuwa kwa kumilikishwa na Mwenyezi Mungu na kupewa uwezo juu yake.

Humpa ufalme umtakaye

Aliwapa waislamu mwanzo pale walipoitikia mwito wa uislamu na kuutumia kwa vitendo.

Na humuondolea ufalme umtakaye

Aliuvua kutoka kwa wafursi, na warumi na washirikina kwa sababu ya kuikufuru haki.

Na humtukuza umtakaye, nao ni waislamu. Na humdhalilisha umtakaye nao ni wafursi, warumi na washirikina wa kiarabu.

Iko mikononi mwako kila heri.

Makusudio ya kuwa mikononi ni kuwa na uwezo. Heri inakusanya kila lenye manufaa liwe la kimaana au kimaada. Na Mwenyezi Mungu amewapa heri nyingi waislamu kwa baraka za uislamu.

Hakika wewe ni muweza wa kila kitu.

Dalili ya uweza ni kuuvua ufalme kutoka kwa wenye nguvu na kuwapa wanyonge.

Huingiza usiku katika mchana na huuingiza mchana katika usiku.

Ambapo sayari zinakuwa na harakati kwa uweza na msaada Wake; nyingine huzizunguuka nyingine, hapo hupatikana misimu ya mwaka; mara nyingine huchukua usiku katika mchana katika msimu fulani mpaka ukawa na masaa15 na mchana ukawa masaa 9. na mara nyuingine huuchuwa mchana katika usiku katika msimu mwingine mpaka ukawa na masaa 15 na usiku ukawa masaa 9.1

Na humtoa aliye hai kutoka aliye maiti.

Kama vile kumtoa mumin kutoka kwa kafiri na mtukufu kutoka kwa aliye dhalili.

Na humtoa maiti kutoka aliye hai.

Kama vile kumtoa kafiri kutoka kwa mumin na dhalili kutoka kwa mtukufu.

Na humruzuku amtakaye bila hisabu,

Kama alivyowaruzuku waislamu wa kwanza, ufalme na utukufu kwa baraka za uislamu. Na kama utauliza, kuwa je? ufalme wa mfalme dhalimu na usultani wake hutoka kwa Mungu na ni kwa utashi wake na matakwa yake?

Utalikuta jibu la swali lako hili katika tafsiri ya aya 246 Surah Al-Baqrah.

Zaidi ya hayo ni kwamba dhahiri ya Aya inatilia nguvu yale yaliyosemwa na kundi la wafasiri kuhusu sababu ya kushuka kwake. Kwa ufupi ni kwamba Mtume (s.a.w.) alipochukua hatua ya kuchimba handaki kwa ushauri wa Salman Farisi aliwakatia dhiraa arubaini kila sahaba kumi, na Salman alikuwa na nguvu, hivyo Ansar wakamtaka awe nao wakasema: "Salman ni wetu". Mtume akasema kauli yake iliyo mashuhuuri: "Salman ni katika sisi Ahlul-Bait.

Wakati Salman alipokuwa akichimba akakabiliwa na jiwe lililomshinda. Mtume alipoambiwa, alichukua sururu kutoka mikononi mwa Salman na kulivunja jiwe kwa mapigo matatu.

Katika mapigo hayo Mtume (s.a.w.) aliona ikulu ya Fursi, Roma na Yemen; akawaambia sahaba zake: "Umati wangu utatawala ufalme wa Kisra na Kaizari". Basi wanafiki waliposikia waliyachezea shere maelezo haya, ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii:

Sema: "Ewe Mola uliyemiliki ufalme wote! Humpa ufalme umtakaye na humwondolea ufalme umtakaye na humtukuza umtakaye na humdhalilisha umtakaye."

Ikiwa hii ndiyo sababu ya kushuka Aya hii au siyo, lakini dhahiri ya Aya haikatai, na matukio ya historia yanaunga mkono hilo.

لَا يَتَّخِذِ الْمُؤْمِنُونَ الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاءَ مِنْ دُونِ الْمُؤْمِنِينَ ۖ وَمَنْ يَفْعَلْ ذَٰلِكَ فَلَيْسَ مِنَ اللَّهِ فِي شَيْءٍ إِلَّا أَنْ تَتَّقُوا مِنْهُمْ تُقَاةً ۗ وَيُحَذِّرُكُمُ اللَّهُ نَفْسَهُ ۗ وَإِلَى اللَّهِ الْمَصِيرُ {28}

Waumini wasiwafanye Makafiri kuwa ni marafiki badala ya waumini (wenzao). Na mwenye kuyafanya hayo, basi hana kitu kwa Mwenyezi Mungu ila mtakapojilinda nao kwa kujihifadhi na anawatahadharisha Mwenyezi Mungu na Yeye mwenyewe marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu.

قُلْ إِنْ تُخْفُوا مَا فِي صُدُورِكُمْ أَوْ تُبْدُوهُ يَعْلَمْهُ اللَّهُ ۗ وَيَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ وَاللَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ {29}

Sema: Mkificha yaliyomo vifuani mwenu au mkiyadhihirisha Mwenyezi Mungu anayajua na anayajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo ardhini. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.

يَوْمَ تَجِدُ كُلُّ نَفْسٍ مَا عَمِلَتْ مِنْ خَيْرٍ مُحْضَرًا وَمَا عَمِلَتْ مِنْ سُوءٍ تَوَدُّ لَوْ أَنَّ بَيْنَهَا وَبَيْنَهُ أَمَدًا بَعِيدًا ۗ وَيُحَذِّرُكُمُ اللَّهُ نَفْسَهُ ۗ وَاللَّهُ رَءُوفٌ بِالْعِبَادِ {30}

Siku ambayo kila nafsi itakuta kheri iliyoitenda imehudhurishwa Na iliyoyatenda katika uovu, itapenda lau kungekuwa na masafa marefu baina ya uovu huo na yeye. Na anatahadharisha Mwenyezi Mungu na Yeye Mwenyewe, na Mwenyezi Mungu ni mpole kwa waja.
  • 1. Mwandishi amechukulia masaa ya Uarabuni ambako wako mbali na mstari wa Ikweta. Ama sisi tulio Afrika Mashariki ,tuko katika Mstari wa Ikweta ,usiku na Mchana katika vipindi vyote vya mwaka hautafautiani zaidi ya zaidi ya saa moja -Mtarjumu.