read

Aya 260: Ili Moyo Wangu Utulie

Maana

Maana ya Aya yako wazi, lakini wafasiri wanataka kupata sababu ya kusema kwa hali yoyote itakayokuwa. Kwa hiyo wakaulizana sababu iliyomfanya Ibrahim kuuliza hivi, pamoja na kujua kwamba yeye anaamini ufufuo kwa imani isiyo na shaka yoyote. Kisha wakahitalifiana katika jawabu lake kwa kauli kumi na mbili alizozitaja Razi.

Utafiti wao hauna msingi wowote, kwa sababu kuamini ghaibu hakupingani na kutaka kushuhudia kwa macho. Kwani kila mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na Malaika Wake na yaliyokuja katika vitabu vyake katika habari za ghaibu, anatamani kushuhudia kwa macho yale aliyoyaamini kwa njia ya ghaibu na wahyi, isipokuwa Ali bin Abu Twalib aliyesema: "Lau nitaondolewa pazia siwezi kuzidisha yakini (yangu)."

Vyovyote iwavyo Khalilurrahman (rafiki wa Mwenyezi Mungu) (a.s.) aliamini ufufuo kwa imani ya ghaibu kwa njia ya wahyi, kama Mitume wengine; kisha akapenda kushuhudia tukio kwa macho yake baada ya kushuhudia kwa moyo wake na akili yake. Kwa hilo zitatimia kwake njia zote za maarifa - kwa moyo, akili na majaribio.

Mwenyezi Mungu alilikubali ombi lake, akamwamrisha kuchukua ndege wane, awaku- sanye pamoja kisha awakatekate aweke fungu juu ya kila jabali; kisha awaite, watamjia
haraka kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Tunalomalizia katika Aya hii ni kwamba kutaka kufunuliwa siri ya uumbaji au ufufuo mara nyingine kunatokana na kutia shaka kwenye jambo hilo. Huko ndiko kunakopingana na kuamini kudura ya Mwenyezi Mungu na kuwa na imani na wahyi Wake na Mitume Yake.

Mara nyingine kunatokana na kupenda kujua mambo na kupata maarifa pamoja na kuamini kudura ya Muumbaji na kuwa na imani na Mitume; hata kama hakuona jinsi Mwenyezi Mungu anavyofufua watu; kama ilivyokuwa kwa Ibrahim. Ombi hili halidhuru imani, lakini ni vigumu kulipata, bali haiwezekani, isipokuwa kwa Mtume, kama Ibrahim ambaye imani yake haitingishiki kwa kitu chochote, hata kama Mwenyezi Mungu hangemwitikia maombi yake.

Kwa hivyo basi atakayeshartisha majaribio na kuona kuwa ndio sharti la kuamini kwake ufufuo, basi yeye ni kafiri kabisa. Lau angelikuwa ni mwenye kuamini kudura ya Mwenyezi Mungu kweli, asingelikuwa na haja ya sharti hili, kwa sababu kudura yake Mwenyezi Mungu haishindwi na kitu chochote mbinguni wala ardhini.

مَثَلُ الَّذِينَ يُنْفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ كَمَثَلِ حَبَّةٍ أَنْبَتَتْ سَبْعَ سَنَابِلَ فِي كُلِّ سُنْبُلَةٍ مِائَةُ حَبَّةٍ ۗ وَاللَّهُ يُضَاعِفُ لِمَنْ يَشَاءُ ۗ وَاللَّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ {261}

Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyochipuza mashuke saba; katika kila shuke pana punje mia. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mjuzi.

الَّذِينَ يُنْفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ ثُمَّ لَا يُتْبِعُونَ مَا أَنْفَقُوا مَنًّا وَلَا أَذًى ۙ لَهُمْ أَجْرُهُمْ عِنْدَ رَبِّهِمْ وَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ {262}

Wale wanaotoa mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu kisha wasifuatishie kile walichotoa na masimbulizi wala udhia, wao wana ujira wao kwa Mola wao, wala hawatakuwa na hofu, wala hawatahuzunika.

قَوْلٌ مَعْرُوفٌ وَمَغْفِرَةٌ خَيْرٌ مِنْ صَدَقَةٍ يَتْبَعُهَا أَذًى ۗ وَاللَّهُ غَنِيٌّ حَلِيمٌ {263}

Kauli njema na kusamehe ni bora kuliko sadaka inayofuatishiwa na udhia na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Mpole.