read

Aya 261-263: Punje Moja Inayotoa Mashuke Saba

Maana

Mwenye kufuatilia Aya za Qur'an na kuzingatia maana zake atazikuta kuwa zinatilia umuhimu misingi mitatu: Kueneza mwito wa Kiislamu, Jihadi na kutoa mali katika njia ya Mwenyezi Mungu. hiyo ni kwamba misingi hii mitatu ina athari kubwa katika kuupa nguvu uislamu na kuenea kwake. Kwa hivyo Qur'an imehimiza misingi hiyo kwa mifano mbalimbali ya kupendekeza na kutisha.

Zimeshatangulia Aya kadhaa za kuhimiza Jihadi na kutoa mali, na zitakuja nyingine. Hivi sasa mbele yetu kuna zaidi ya Aya kumi zinazozungumzia kutoa mali; katika hizo kuna zinazomwahidi mtoaji badali ya mia saba au zaidi; nyingine zinakataza kufuatishia sadaka kwa masimbulizi na udhia; pia kuna nyingine zinazoamrisha kutoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa nia safi, na zinazoelezea kuwa kutoa kuwe kumetokana na chumo halali na zuri, sio chumo la haramu na baya n.k.1

Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu, ni kama mfano wa punje moja iliyochipuza mashuke saba; katika kila shuke pana punje mia. Na - Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa Mjuzi.

Wameulizana wafasiri, vipi Mwenyezi Mungu amepigia mfano punje inayotoa mazao haya na inajulikana kuwa haiko? Baadhi yao wakajibu kwamba hilo ni fumbo la wingi, sio kitu hasa. Wengine wamesema kuwa hayo ni makadirio; kwamba mwenye akili akijua kuwa punje yake itamletea mia saba, basi atatoa bila ya kusita.

Hapana shaka kuwa wafasiri wameuweka mbali sana mfano huu, kwa vile wao wamelinganisha kilimo kilivyokuwa wakati wao; ambapo hakukuwa na zana zozote zaidi ya ng'ombe, punda na jembe la mkono. Lau wengelikuwa wakati huu wasingeona ajabu yoyote katika mifano ya Mwenyezi Mungu, baada ya elimu kuingia katika kila kitu na zana na pembejeo za kilimo zinazotumiwa.

Zaidi ya hayo kutoa kwa Mola hakupungui wala hakudhibitiki. Kwa hiyo ongezeko la mia saba sio kiwango cha mwisho cha fadhila zake na kutoa Kwake.
Kwa ajili hiyo ndipo akasema: "Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye."

Kama ambavyo ongezeko la mia saba linaweza kuzidi, basi vile vile linaweza kupungua, kulingana na hali ya kutoa kwenyewe. Huenda shillingi moja anayoitoa mtu na huku anaihitaji ikawa bora mbele za Mwenyezi Mungu kuliko shilingi elfu zinazotolewa na aliyetosheka nazo. Vile vile shilingi moja inayotolewa kwa ajili ya kuinua haki, dini na maadili, au inayotolewa katika manufaa ya watu na kuwatoa katika dhulma na ufukara, shilingi hiyo ambayo athari yake itabaki na manufaa yake kudumu muda mrefu, ni bora mara millioni kuliko maelfu yanayotumiwa katika anasa na maarusi ya watoto.

Wale wanaotoa mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu, kisha wasifuatishie kile walichotoa na masimbulizi wala udhia, wana ujira wao kwa Mola wao.

Mwenye Majmaul Bayan amesema: "Kusimbulia ni kumwambia uliyempa: Je, sikukufanyia wema? Au je, sikukupa? Na adha ni kusema: "Mwenyezi Mungu anipumzishe kwa kuniepusha nawe na aniondolee balaa kwa ajili yako."

Maana ni kuwa, kutoa kunakobadilishiwa ziada na Mwenyezi Mungu, ni kule ambako mwelekeo wake ni kwa Mwenyezi Mungu peke Yake, sio kwa kutaka umashuhuri na kujionyesha na kuaibisha, kwa sababu hilo linabatilisha thawabu.

Kauli njema na kusamehe ni bora kuliko sadaka inayofuatishiwa na udhia.

Kauli njema ni maneno yanayokubaliwa na nyoyo. Makusudio ya kusamehe hapa ni kumsamehe mwenye kuomba ikiwa anaomba kwa lazima, au kutoa ufedhuli ikiwa mtu hakupata alichoomba; kama ilivyo kwa baadhi ya waombaji. Yaani kumkabili muombaji kwa maneno mazuri na kuwa na subira naye, ni bora mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko kutoa kwenye kukabiliana na maudhi. Mtume (s.a.w.) anasema: "Muombaji akiomba msimkate maneno mpaka amalize, kisha mjibuni kwa upole; ama iwe ni kumpa (japo) kichache au kumwambia vizuri"

Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi.

Wa sadaka zote na twaa, na sisi ni mafukara tunaohita- ji msaada wake, upole wake na thawabu zake.

Mpole.

Hafanyi haraka kutoa adhabu katika maisha haya, isipokuwa anamwacha muasi mpaka siku isiyokuwa na shaka.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُبْطِلُوا صَدَقَاتِكُمْ بِالْمَنِّ وَالْأَذَىٰ كَالَّذِي يُنْفِقُ مَالَهُ رِئَاءَ النَّاسِ وَلَا يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۖ فَمَثَلُهُ كَمَثَلِ صَفْوَانٍ عَلَيْهِ تُرَابٌ فَأَصَابَهُ وَابِلٌ فَتَرَكَهُ صَلْدًا ۖ لَا يَقْدِرُونَ عَلَىٰ شَيْءٍ مِمَّا كَسَبُوا ۗ وَاللَّهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ {264}

Enyi mlioamini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na udhia; kama yule anayetoa mali yake kwa kuwaonyesha watu; wala hamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likafikiwa na mvua kubwa na ikaliacha tupu. Hawana uwezo wa chochote katika walivyovichuma; na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu makafiri.

وَمَثَلُ الَّذِينَ يُنْفِقُونَ أَمْوَالَهُمُ ابْتِغَاءَ مَرْضَاتِ اللَّهِ وَتَثْبِيتًا مِنْ أَنْفُسِهِمْ كَمَثَلِ جَنَّةٍ بِرَبْوَةٍ أَصَابَهَا وَابِلٌ فَآتَتْ أُكُلَهَا ضِعْفَيْنِ فَإِنْ لَمْ يُصِبْهَا وَابِلٌ فَطَلٌّ ۗ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ {265}

Na mfano wa wale wanaotoa mali zao kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na uimara wa nafsi zao ni kama mfano wa bustani iliyo mahali pa juu, ikafikiwa na mvua kubwa ikatoa mazao yake maradufu; na isipofikiwa na mvua kubwa, basi manyunyu (huitoshea). Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayotenda.
  • 1. Baadhi ya wafasiri wapya wamesema kwamba Aya hizi zinaweka utaratibu wa uchumi. Lakini kwa hakika ziko mbali na hayo, kwa sababu utaratibu wa uchumi kwanza kabisa unaangalia nyenzo za uzalishaji na wazalishaji wenyewe; na Aya hizi hazikuelezea hilo, isipokuwa zimewahimiza matajiri kutoa mali zao katika njia ya Mungu