read

Aya 264-265: Musiharibu Sadaka Zenu.

Maana

Enyi mlioamini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na udhia; kama yule anayetoa mali yake kwa kuwaonyesha watu.

Katika Aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amebainisha kwamba kuacha kusimbulia na kuudhi ni sharti la kupatikana malipo na thawabu katika kutoa; na kukosa kutoa sadaka na kauli njema ni bora kuliko kusimbulia na kuudhi, vilevile kwamba mwenye kutoa bila ya masimbulizi na udhia, atapewa malipo na thawabu bila ya hisabu; Akapigia mfano hilo kwa punje moja inayomrudishia mkulima punje mia saba.

Baada ya kubainisha haya yote anampigia mfano, katika Aya hii mwenye masimbulizi na adha kuwa sawa na mnafiki anayejionyesha, ambaye anatoa mali yake kwa kutaka sifa kwa watu, sio kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na thawabu zake.

Wala hamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.

Yaani kitendo cha ria (kujionyesha) ni sawa na cha kafiri, kwa sababu wote hao hawataki radhi ya Mweneyzi Mungu. Kwa ajili hiyo ndipo zikaja Hadith Mutawatir kwamba ria ni shirk iliyojificha.

Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likafikiwa na mvua kubwa na ikaliacha tupu. Hawana uwezo wa chochote katika walivyovichuma.

Mwenyezi Mungu kwanza amemfananisha mwenye kusimbulia anayeudhi na mnafiki anayejionyesha; kisha akamfananisha na jabali ambalo juu yake pana udongo. Kwa dhahiri ni kwamba shabihi wa shabihi ni shabihi, kama vile rafiiki wa rafiki.

Kwa hiyo inakuwa, mwenye kusimbulia anayeudhi, mnafiki na mwenye kuudhi na mwenye kujionyesha ni sawa na udongo juu ya jabali, na adha na ria ni kama mvua ambayo inaon- dosha udongo huo.

Na kauli ya Mwenyezi Mungu: "Hawana uwezo wa chochote." Maana yake ni kuwa kama ambavyo hakuna yeyote katika viumbe anayeweza kurudisha udongo huo, vile vile hawawezi wenye kujionyesha na wenye kuudhi kurudisha sadaka zao. Makusudio ni kwamba wao hawatanufaika nayo katika dunia, kwa sababu imekwishawatoka mikononi mwao; wala hawatanufaika nayo katika akhera kwa kuharibiwa na adha na ria.

Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu makafiri

Makusudio ya kuongoza hapa, ni thawabu ya akhera, kwa sababu maneno yanahusu thawabu ya Mwenyezi Mungu. Na makusudio ya makafiri ni kila anayefanya amali kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Kuna Hadith tukufu inayosema; "Kitakapokuwa Kiyama, atanadi mnadi: 'wako wapi wale waliokuwa wakiwaabudu watu? Simameni mchukue malipo yenu kwa wale mliokuwa mkiwatumikia, kwa sababu mimi sikubali amali iliyochanganyika na kitu chochote katika dunia na watu wake.'"

Na mfano wa wale wanatoa mali zao kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na uimara wa nafsi zao, ni kama mfano wa bustani iliyo mahali pa juu, ikafikiwa na mvua kubwa ikatoa mazao yake maradufu, na kama isiponyeshewa na mvua kubwa, basi manyun-
yu (huitoshea).

Baada ya Mwenyezi Mungu kupiga mfano wa sadaka ya wenye kujionyesha na wenye kuudhi, amepiga mfano, katika Aya hii, sadaka ya mwenye kujitakasa; kama iliyo kawaida ya Mwenyezi Mungu kuleta mkabali wa vitu viwili vilivyo kinyume.
Ikiwa sadaka ya hao ni kama jabali lililofunikwa na mchanga, basi sadaka ya hawa ni kama bustani iliyo katika sehemu za miinuko, iliyojaa udongo ambao hauhofiwi kumomonyoka na kuondoka; sio kama ilivyo hali ya mchanga kidogo kwenye jabali; bustani hii huzaa matunda katika mwaka mara mbili zaidi ya inavyozaa bustani ya kawaida, wala haikauki kamwe kutokana na udongo wake ulivyo mzuri; inatosheka na mvua ndogo tu, kwa sababu ya rutuba yake na mazingira yake mazuri.

Ama kauli yake Mwenyezi Mungu: "Kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na uimara wa nafsi zao," ni kuonyesha mambo mawili:

Kwanza, waumini wanataka radhi ya Mwenyezi Mungu kutokana na kutoa.

Pili, kutoa huku kunatokana na msukumo wa nafsi zao wenyewe na wala sio msukumo unaotoka nje.
Inasemekana kwamba uimara wa nafsi zao ni kwa maana ya kwamba wao wanajitahidi kutii kwa kutoa. Maana haya yanaweza kuwa sawa ikiwa herufi Min hapa iko katika maana ya Lam; kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu: "Kwa ajili ya makosa yao waligharik- ishwa ..." (71:25)

Baada ya hayo yote, Aya mbili hizi ni katika muujiza wa fasihi ambao huwezi kuupata mahali pengine isipokuwa katika maneno yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Kwanza, sadaka ya adha na sadaka ya ria ameifananisha na udongo ulioko kwenye jabali ambao unaondolewa na upepo na mvua. Kisha katika mkabala wa sadaka ya hasara, amefananisha na sadaka ya faida - sadaka ya imani, nayo ni kama bustani yenye rutuba inayotoa mazao kila mwaka, iwe na mvua nyingi au kidogo.

أَيَوَدُّ أَحَدُكُمْ أَنْ تَكُونَ لَهُ جَنَّةٌ مِنْ نَخِيلٍ وَأَعْنَابٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ لَهُ فِيهَا مِنْ كُلِّ الثَّمَرَاتِ وَأَصَابَهُ الْكِبَرُ وَلَهُ ذُرِّيَّةٌ ضُعَفَاءُ فَأَصَابَهَا إِعْصَارٌ فِيهِ نَارٌ فَاحْتَرَقَتْ ۗ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّهُ لَكُمُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُمْ تَتَفَكَّرُونَ {266}

Je, mmoja wenu anapenda kuwa na kitalu cha mitende na mizabibu ipitayo mito kati yake, naye humo hupata mazao ya kila namna, na uzee ukamfikia, kisha ana watoto walio dhaifu; mara kifikiwe na kimbunga chenye moto kiungue? Hivi ndivyo anavyowabainishia Mwenyezi Mungu ishara ili mpate kufikiri.