read

Aya 267-268: Kutoa Katika Vizuri

Maana

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuhimiza sadaka katika Aya iliyotangulia na kubainisha ambayo anapaswa kusifika nayo mwenye kutoa sadaka, ikiwa ni pamoja na kumtakasia Mwenyezi Mungu katika sadaka yake na kujiepusha na ria, masimbulizi na kuudhi, sasa anataja sifa za sadaka yenyewe - kwamba inatakiwa iwe inatokana na mali nzuri na sio chafu. Hapo ndipo itakuwa sadaka imekamilika kwa njia zake. Mwenyezi Mungu anasema:

Enyi mlioamini! Toeni katika vizuri mlivyovichuma na katika vile tulivyowatolea kuto- ka ardhini

Lau tukiangalia Aya hii kwa dhahiri bila ya kuangalia Hadith za Mtume zilizobainisha wajibu wa kimali na kuweka kiwango cha kiasi chake na matumizi yake na pia aina yake, tungelifahamu kwamba katika mali yote anayochuma mtu kuna haki ya Mwenyezi Mungu ambayo anapaswa kuitoa kwa ajili ya radhi yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.), kwa sharti ya kutoa kizuri katika anavyovimiliki sio vibaya. Aya iliyo wazi zaidi ya hii ni ile inayosema: "Hamtapata wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda ..." (3: 92)

Kutoa huku ni wajibu katika mali yote; ni sawa iwe imetokana na ufundi, biashara au kilimo. Vilevile urithi, madini au kitu kingine chochote. Haya ndiyo yanayofahamishwa na matamko ya Aya. Kwa sababu kutoa kumekuja kwa tamko la amri ambayo inafahamisha wajibu. Kauli yake Mwenyezi Mungu: "Katika vizuri mlivyovichuma" inakusanya uchumi wote; na kauli yake; Na katika vile tulivyowatolea kutoka ardhini" inakusanya mimea, madini na siku hizi petroli.

Lakini Hadith za Mtume - ambazo ni tafsiri na ubainifu wa Qur'an hasa Aya za hukumu za sheria - zimeweka kiwango cha mali ya Zaka au Khums, vile vile nadhiri au kafara. Zikabainisha kiasi cha kutoa na wanaopewa. Wanavyuoni wa kifiqh wamelieleza hilo kwa ufafanuzi katika mlango wa Zaka, Khums, kafara na nadhiri. Kwa hiyo Aya itakuwa ni ya kuleta sharia hiyo ya kutoa na kutilia mkazo; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:"Na simamisheni Swala na toeni Zaka ..." (2:110)

Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya.

Inasemekana kuwa sababu ya kushuka Aya ni kwamba baadhi ya Waislamu walikuwa wakitoa sadaka zile tende mbovu. Na jumla hii ni kutilia mkazo jumla ya kwanza ambayo ni "toeni katika vizuri." Kwa ujumla ni kuwa toeni vizuri na wala msitoe vibaya. Mafaqihi wametoa fatwa kwamba mwenye kumiliki aina ya mali ambayo baadhi yake ni nzuri na baadhi ni mbaya, haijuzu kwake kutoa mbaya, bali atatoa ile yenye uzuri wa wastani. Kama akichagua ile ya hali ya juu, basi ni bora zaidi. Lakini kama mali yote ni mbaya inajuzu kutoa mali mbaya kwa sababu haki inafungamana na dhati ya kitu kinachotolewa.

Hali nyinyi wenyewe msingevipokea isipokuwa kwa kuvifumbia macho.

Hii ni hoja fasaha kwa yule anayetoa sadaka mbaya, Imam Ali (a.s.) anasema: "Kama unavyofanya nawe utafanyiwa."

Shetani anawatisha na ufukara na anawaamrisha ubakhili.

Maana ya kuwatisha na ufukara ni kuwatia wasiwasi wa kuwa na pupa na kuhofia kutoa, kuwa kunaleta ufukura na hali mbaya. Maana ya kuamrisha ovu ni kuhadaa kwa kutia kwake wasiwasi kufanya maasi na kuacha utii; kama vile ubakhili.

Na Mwenyezi Mungu anawaahidi msamaha utokao kwake na fadhila.

Mwenye kutoa vizuri katika mali yake kwa kutafuta radhi ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.), Mwenyezi Mungu amemuahidi mambo mawili:

Kwanza, kusamehe makosa yake mengi kama alivyosema: "Chukua sadaka katika mali zao, uwatakase na uwasafishe kwazo..." (9:103)

Pili, kumlipa kheri zaidi mwenye kutoa kuliko alichokitoa - Mwenyezi Mungu anasema: "... Na chochote mtakachokitoa, basi Yeye atakilipa naye ni mbora wa wanaoruzuku." (34:39)

Miongoni mwa maneno ya hekima ya Imam Ali (a.s.) ni: "Sadaka ni dawa yenye kuokoa," "Takeni riziki kwa sadaka" na "Fanyeni biashara na Mwenyezi Mungu kwa sadaka."

Ilipokuwa roho ya dini inatawala kwenye nafsi na kwenye mwelekeo wa malezi na tabia za watu, ilikuwa baba anampa mtoto wake pesa na kumwamrisha kutoa sadaka kwa fukara kwa kuitakidi kwamba sadaka itamwandalia njia ya tawfik na kufaulu.

يُؤْتِي الْحِكْمَةَ مَنْ يَشَاءُ ۚ وَمَنْ يُؤْتَ الْحِكْمَةَ فَقَدْ أُوتِيَ خَيْرًا كَثِيرًا ۗ وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ {269}

Humpa hekima amtakaye. Na aliyepewa hekima hakika amepewa heri nyingi na hawakumbuki ila wenye akili.