read

Aya 269: Hekima

Maana

Neno Hekima hutumiwa kwa maana nyingi, kama vile maslahi; mfano: "Hekima ya kitu hiki ni jambo fulani." Maana nyingine ni mawaidha; mfano: Hekima ni kitu (anachotafuta) kilichompotea "mumin," Pia lina maana ya elimu na fahamu; kama anavyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t.): "Na hakika tulimpa Lukmani hekima ..." (31:12) Maana nyingine ya neno hekima ni Utume, Mwenyezi Mungu anasema: ".... Na tukampa hekima na kukata hukumu." (38:20)

Vilevile neno hili linatumiwa kwa maana ya elimu ya Falsafa. Msemaji mmoja amesema: "Hekima ni elimu ya Fiqh", mwengine amesema ni elimu zote za kidini, watatu akasema ni kumtii Mwenyezi Mungu tu.

Vyovyote ilivyosemwa au itakavyosemwa, ni kwamba neno hekima haliwezi kutoka kwenye maana ya usawa na kukiweka kitu mahali pake kwa kauli na vitendo.
Kwa hivyo mwenye hekima ni yule anayekihukumu kitu na kukileta kwa mujibu wa akili na hali ilivyo, sio kwa mujibu wa mapendeleo na matakwa. Kitu hicho hawezi kukifanyia haraka kabla ya muda wake au kukizuilia na wakati wake au kukipeleka kombo na mipaka yake.

Kwa hali hiyo basi, hekima haihusiki na mitume na mawalii tu au na wanafalsafa na wataala- mu tu, bali kila mwenye kufanya vizuri amali yoyote na akaiweka sawa, basi huyo ni mwenye hekima katika amali hiyo; awe ni mkulima au mfanyakazi, mwajiri au mwajiriwa. Vilevile ni sawa awe ni muhuburi, malenga, hakimu au askari, n.k. Sharti la kwanza na la mwisho la hekima ni kuthibiti lengo la kitendo kiakili, kisharia, kidunia na kidini.

Hapana mwenye kutia shaka kwamba ambaye hekima ni mwongozi wake atakuwa mwema katika nyumba mbili (duniani na akhera). Imam Jaffar Sadiq (a.s.) anasema: "Hakumneemesha Mwenyezi Mungu mja neema kubwa na tukufu zaidi kuliko hekima. Mwenyezi Mungu anasema: "Na aliyepewa hekima hakika amepewa heri nyingi na hawakumbuki ila wenye akili." Yaani hajui yeyote siri ya hekima aliyoitoa Mwenyezi Mungu isipokuwa mwenye kumtakasia Mwenyezi Mungu nafsi yake. Hekima ni uongofu, ni uthabiti wa vianzio vya mambo na ni kituo cha mwisho wa mambo."

Hapa inaonyesha kuwa kuna tofauti kati ya elimu na hekima. Elimu ni kujua mambo na mfungamano uliopo wa mambo hayo; vile vile kujua athari yake ya kheri au ya shari. Ama hekima inaamrisha akili kufuata usalama, kufuata dini iliyo sawa na kukitumia kitu mahala pake, palipoumbwa kwa ajili yake. Mfano elimu inatengeza chembechembe za bomu na kutengeneza maroketi, lakini haiangalii lengo lake, la kheri au la shari; wala haikatazi hili na kuamrisha lile.

Lakini hekima haijishughulishi na utafiti wa mabomu na uvumbuzi wa maroketi hayo isipokuwa inaangalia matumizi ya maroketi hayo na kumwelekeza binadamu lile litakalo mfanya kupata kheri na ufanisi sio uovu.1

وَمَا أَنْفَقْتُمْ مِنْ نَفَقَةٍ أَوْ نَذَرْتُمْ مِنْ نَذْرٍ فَإِنَّ اللَّهَ يَعْلَمُهُ ۗ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنْصَارٍ {270}

Chochote mtoacho, au nadhiri mnazoweka, basi Mwenyezi Mungu anakijua. Na madhalimu hawana wasaidizi.

إِنْ تُبْدُوا الصَّدَقَاتِ فَنِعِمَّا هِيَ ۖ وَإِنْ تُخْفُوهَا وَتُؤْتُوهَا الْفُقَرَاءَ فَهُوَ خَيْرٌ لَكُمْ ۚ وَيُكَفِّرُ عَنْكُمْ مِنْ سَيِّئَاتِكُمْ ۗ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ {271}

Mkizidhihirisha sadaka ni vizuri; Na kama mkitoa kwa siri na kuwa- pa mafukara, basi hivyo ni bora zaidi kwenu na yatawaondokea baadhi ya maovu yenu na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mnayoyatenda.
  • 1. Nimesoma kwamba katika mataifa makubwa kuna mabomu ambayo moja linaweza kuwa na mpasuko wa tani mil- ioni mia moja, na kwa muda mchache tu, linaweza kuua watu milioni mia na ishirini; na kwamba kuna mabomu yana shabaha ya hali ya juu. Hii inatufahamisha uongo wa propaganda za wagunduzi wa vyombo hivyo, kwamba eti lengo lake ni usalama na ufanisi wa binadamu na kumchukua binadamu hadi mwezini kustarehe.