read

Aya 270-271:Chochote Mtoacho

Maana

Tena amerudia Mwenyezi Mungu kutaja kutoa na kukutilia mkazo kwa kusema:

Chochote mtoacho au nadhiri mnazoweka basi Mwenyezi Mungu anakijua

Neno kutoa linakusanya kila kinachotolewa; kiwe cha wajibu au suna, kingi au kichache cha utii au maasi na kisiri au kidhahiri.
Maana ya nadhiri kilugha ni ahadi; na kisharia ni kujilazimisha mtu kutenda jambo fulani au kuliacha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Tamko lake ni kusema yule mwenye kuweka nadhiri: "Ni juu yangu kufanya jambo fulani kwa ajili ya Mwenyezi Mungu." Haitoshi kukusudia tu, bila ya kusema, wala kusema bila ya kumtaja Mwenyezi Mungu au kutaja mojawapo ya majina yake matukufu. Lau anasema: "Nimeweka nadhiri kufanya kitu fulani likiwa jambo fulani", hiyo haiwezi kuwa nadhiri kwa kutokuwa na jina la Mwenyezi Mungu.

Vilevile nadhiri haiwezi kuwa kabisa, ikiwa imefungamana na jambo la haramu au makuruhu. Wakati wa Mtume (s.a.w.w.) mtu mmoja aliweka nadhiri ya kusimama tu bila ya kukaa wala kuwa kivulini, akiwa amefunga na asizungumze na mtu; Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akasema: "Mwamuruni azungumze akae kivulini na aendelee na Saumu yake." Maana ya "Mwenyezi Mungu anakijua" ni kuwa Mwenyezi Mungu anajua lengo lolote la kutoa litakalokuwa na kulipatia malipo; ikiwa ni heri basi ni heri na kama ni shari basi ni shari tu.

Na madhalimu hawana wasaidizi.

Makusudio ya madhalimu ni wote bila ya kuvua, wakiwa ni pamoja na wale wasiotoa chochote au wanaotoa vibaya au kwa ria. Vilevile wale wanaotoa kwa masimbulizi na adha au kuweka pasipokuwa mahali pake. Wengine ni wale wanaovunja ahadi na wasiotekeleza nadhiri. Wote hawa na walio mfano wao hawatakuwa na wasaidizi wala waombezi watakaowazuiilia na mateso ya Mwenyezi Mungu.

Kama mkizidhihirisha sadaka ni vizuri.

Yaani hakuna umakuruhu katika kudhihirisha sadaka maadam makusudio yake ni kwa ajili ya kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Imam Jaffar Sadiq aliulizwa kuhusu mtu anayefanya jambo la kheri, watu wakamwona akafurahi. Imam akasema: "Hapana ubaya; kila mtu anapenda kuonekana na watu kwa kheri, ikiwa hakufanya hilo kwa ajili ya huko kuonekana."

Na kama mkitoa kwa siri na kuwapa mafukara, basi hivyo ni bora zaidi kwenu.

Hapana shaka kwamba kuficha sadaka ni bora kuliko kuidhihirisha, kwa sababu kunakuwa mbali na shubuha ya ria na kudhihirisha haja ya mafukara mbele ya watu. Huwa mara nyingine kudhihirisha sadaka kuna maslahi; kwa mfano ikiwa ni kwa kutaka kutoa mfano kwa wengine, hapo kudhihirisha kutakuwa bora zaidi.

Inasemekana kuwa kuificha sadaka ya sunna ni bora kuliko kuidhihirisha; na kinyume chake kwa sadaka ya wajibu.

Hatujui hoja ya ufafanuzi huu na Hadith ya "Sadaka ya siri inazima ghadhabu ya mola" inakusanya ya wajibu na suna; kama ambavyo Aya inakusanya fukara mwislamu na asiyekuwa mwislamu. Mafaqihi wametoa fatwa ya kutoa sadaka ya sunna kwa asiyekuwa mwislamu akiwa ni muhitaji kutokana na kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu:"Kulinywesha kila ini la joto kuna malipo."

Na yatawaondokea baadhi ya maovu yenu.

Neno Min hapa ni baadhi, kwa sababu sadaka haifuti madhambi yote isipokuwa inafuta baadhi tu.

Na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyatenda

Maadam Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anajua siri, sawa na anavyojua dhahiri, basi siri ni bora, kwa sababu hilo liko mbali na ria, isipokuwa kama katika kudhihirisha kuna maslahi; kama kuwaonyesha mfano wengine ili watende. Na wenye ikhlasi wengi wanaficha sadaka zao; wanajitoleakwenyemamboyakherikwamajinayawatuwenginewema.

لَيْسَ عَلَيْكَ هُدَاهُمْ وَلَٰكِنَّ اللَّهَ يَهْدِي مَنْ يَشَاءُ ۗ وَمَا تُنْفِقُوا مِنْ خَيْرٍ فَلِأَنْفُسِكُمْ ۚ وَمَا تُنْفِقُونَ إِلَّا ابْتِغَاءَ وَجْهِ اللَّهِ ۚ وَمَا تُنْفِقُوا مِنْ خَيْرٍ يُوَفَّ إِلَيْكُمْ وَأَنْتُمْ لَا تُظْلَمُونَ {272}

Si juu yako kuwaongoza, lakini Mwenyezi Mungu humwongoza amtakaye. Na mali yoyote mnayoitoa ni kwa kwa ajili ya nafsi zenu, wala hamtoi ila kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu. Na mali yoyote mnayoitoa mtalipwa kwa ukamilifu wala hamtadhulumiwa.

لِلْفُقَرَاءِ الَّذِينَ أُحْصِرُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ لَا يَسْتَطِيعُونَ ضَرْبًا فِي الْأَرْضِ يَحْسَبُهُمُ الْجَاهِلُ أَغْنِيَاءَ مِنَ التَّعَفُّفِ تَعْرِفُهُمْ بِسِيمَاهُمْ لَا يَسْأَلُونَ النَّاسَ إِلْحَافًا ۗ وَمَا تُنْفِقُوا مِنْ خَيْرٍ فَإِنَّ اللَّهَ بِهِ عَلِيمٌ {273}

Ni kwa ajili ya mafukara waliozuiliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu, wasioweza kwenda huku na huko katika ardhi. Asiyewajua hali zao anawadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia.
Utawafahamu kwa alama zao; hawaombi watu wakang'anga' nia. Na mali yoyote mnayoitoa, kwa hakika Mwenyezi Mungu anaijua.

الَّذِينَ يُنْفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ سِرًّا وَعَلَانِيَةً فَلَهُمْ أَجْرُهُمْ عِنْدَ رَبِّهِمْ وَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ {274}

Wale watoao mali zao usiku na mchana kwa siri na dhahiri, wana ujira wao kwa Mola wao; wala haitakuwa hofu juu yao wala wao hawatahuzunika.