read

Aya 272- 274: Si Juu Yako Kuwaongoza

Maana

Si juu yako kuwaongoza, lakini Mwenyezi Mungu humwongoza amtakaye.

Yametangulia maelezo katika Aya ya 26 ya Sura hii kwamba neno Huda (uongofu) linatumiwa kwa maana nyingi; miongoni mwayo ni ubainifu na (uongofu), hiyo ni kazi ya Mtume. Maana nyengine ni tawfiki kutoka kwa Mwenyezi Mungu ya kuandalia njia ya kufanya kheri; nyingine ni kuongoka, yaani kukubali nasaha na kuzitumia, huku kunategemezwa kwa mja. Pia neno hilo lina maana ya thawabu na mengineyo.

Maana ya uongofu katika "Si juu yako kuwaongoza" ni kuongoka na kukubali nasaha; yaani, kuitumia kwao haki si juu yako wewe, isipokuwa ni juu yako kufikisha haki tu. "... Basi juu yako ni kufikisha na juu yetu ni hisabu." (13:40)

Maana ya uongofu katika ; "Lakini Mwenyezi Mungu humwongoza amtakaye" ni tawfiki kati- ka njia ya kheri.

Inasemekana kuwa sababu ya kushuka "Si juu yako kuwoangoza" ni kwamba waislamu walikuwa hawatoi sadaka isipokuwa kwa watu wa dini yao, ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Mtume Wake kwa Aya hii na akataka kuwabanishia waislamu wote kwamba kafiri haadhibiwi kwa sababu ya kufuru yake kwa kunyimwa riziki na kudhikishwa ili alazimike kuamini; na haifai kwa yeyote kufanya hivyo hata kama ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. " ...Basi je wewe utawalazimisha ili wawe waumini?" (10:99).

Aya inafahamisha kwamba sadaka ya sunna au ya wajibu inajuzu kuwapa wasiokuwa waislamu, lakini kauli ya Mtume (s.a.w.): "Nimeamrishwa kuchukua sadaka kutoka kwa matajiri wenu na kuitoa kwa mafukara wenu", inahusu sadaka ya sunna tu sio ya wajibu.

Na mali yoyote mnayoitoa ni kwa ajili ya nafsi zenu.

Huenda mtu akadhania kuwa kutoa ni hasara kwake na ni kuwanyima watoto wake na ndugu zake. Ndipo Mwenyezi Mungu akaondosha dhana hii, kwamba mwenye kutoa inam- rudia yeye kheri na nafuu katika dunia na akhera.
Katika akhera atapata malipo na thawabu. Ama katika dunia, Sheikh Muhammad Abduh anasema: "Kutoa kunazuia mafukara kuwafanyia ubaya matajiri, kwa sababu mafukara wakiwa na dhiki, watakwenda kuwaibia matajiri, kuwaudhi na kuwanyang'anya. Kisha uovu wao huu unawaendea wengine; mara nyingine ufisadi huo huenea kwa ujumla na kuondoa raha na amani."

Sijui kama Sheikh Muhammad Abduh ameitoa fikra yake hii kutoka vyama vya wafanyakazi ambavyo vimewaletea matatizo matajiri na kuwalazimisha kukubali haki nyingi za wafanyakazi.

Wala hamtoi ila kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu.

Yaani, maadamu mnakusudia radhi ya Mwenyezi Mungu katika kutoa kwenu, basi Mwenyezi Mungu atakubali. Ni sawa muwe mumempa mwislamu au asiyekuwa mwislamu kwa sharti ya kuwa iwe ni mali nzuri sio mbaya. Pia kusiweko na masimbulizi na maudhi.

Inasemekana kuwa Aya ina maana ya kukataza kwa njia ya kutolea habari; yaani msitoe isipokuwa kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu.

Na mali yoyote mnayoitoa mtalipwa kwa ukamilifu wala hamtadhulumiwa.

Hata kutoa kukiwa kwa asiyekuwa mwislamu, lakini hamtapunguziwa chochote katika malipo, ikiwa mliyempa ni muhitaji.

Watu Wa Sufa (Upenuni)

Kuna jamaa waliohamia Madina, wakiacha miji yao mali zao na watu wao. Hapa Madina hawakuwa na maskani yoyote wala jamaa na hawakuwa na nyezo za kujichumia maisha, wala hawakuweza kusafiri kutafuta riziki.

Idadi yao ilikuwa watu mia tatu, wengine wanasema ni mia nne. Wakawa wako msikitini tu, wakiabudu na kuzilinda nyumba za Mtume.

Pia walikuwa wakijifundisha Qur'an na kuihifadhi, jambo ambalo lilikuwa ni katika twaa bora zaidi, kwa sababu huko ni kuihifadhi dini. Wakati huo huo walikuwa wakitoka pamoja na Mtume katika kila vita. Walikuwa wakikaa upenuni mwa msikiti ndio maana wakaitwa watu wa upenuni (Ahlu Sufa).

Mtume (s.a.w.), alikuwa akiwahimiza na kuwaambia: "Furahini enyi watu wa Suffa; yeyote atakayekuwa na sifa mlizo nazo nyinyi katika umma wangu, basi yeye ni katika marafiki zangu."

Hao ndio wanaofaa zaidi kupewa sadaka. Kwa sababu wao ndio walioshukiwa na Aya hii:

Ni kwa ajili mafukara waliozuiwa katika njia ya Mwenyezi Mungu, wasioweza kwenda huku na huko katika ardhi. Asiyewajua hali zao anawadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia. Utawafahamu kwa alama zao; hawaombi watu wakang'ang'ania.

Mwenyezi Mungu katika Aya hii amewataja watu wa Sufa kwa sifa tano:-

1. Kujitolea kwa Jihadi na kutafuta elimu. Hiyo ndiyo maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu "waliozuiwa katika njia ya Mwenyezi Mungu", kwa sababu mvivu hawezi kuambiwa kuwa ameifunga nafsi yake katika njia ya Mwenyezi Mungu.

2. Kushindwa kuchuma: ndiyo makusudio ya kusema kwake: "Wasioweza kwenda huku na huko."

3. Kujizuia, Mwenyezi Mungu anasema: "Asiyewajua hali zao anawadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia."

4. Kuonekana kuwa ni mafukara kwa hali yao tu, sio kwa sababu ya kuombaomba: ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu: "Utawafahamu kwa alama zao."

5. Kuacha kuomba vilivyo mikononi mwa watu kwa kunga'ang'ania: Kwenye hilo Mwenyezi Mungu ameashiria kwa kusema "Hawaombi watu wakang'ang'ania".

Tumetaja katika tafsiri ya Aya ya 177 katika Sura hii, kwamba kuomba bila ya dharura ni haram.

Wale watowao mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhahiri, wana ujira wao kwa Mola wao; wala haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.

Mwenyezi Mungu ametaja hukumu ya kutoa katika Aya kumi na nne mfululizo, ya mwisho ikiwa ni hii ambayo ni muhtasari wa yaliyotangulia na kutilia mkazo fadhila ya kutoa katika nyakati zote, iwe ni usiku au mchana, na kwa siri au kwa dhahiri.

Razi ametaja kauli nyingi katika sababu za kushuka Aya hii, miongoni mwa hizo ni ile iliy- opokewa kutoka kwa Ibn Abbas, kwamba Ali bin Abu Twalib (a.s.) alikuwa na dirham nne tu, akatoa kwa siri na nyingine kwa dhahiri, ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii.

Zaka

Zaka sio sadaka ya sunna, kwa sababu sadaka huitoa mwislamu kwa hiyari, wala haihitaji kufikia kiwango fulani na haina jengine zaidi ya kukusudia kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu peke Yake; na malipo yake yanaanzia maradufu ya kumi hadi maradufu ya mia saba na zaidi ya hapo, kiasi ambacho hakina mwisho kulingana na lengo la kutolewa kwake.

Ama Zaka, ni faradhi, ni haki ya lazima katika mali ya kiwango fulani na hutolewa kwa anayestahiki. Ni ya tatu katika nguzo tano za uislamu ambazo ni: Shahada mbili, Swala, Zaka, Saumu na Hijja. Baadhi ya wenye ghera na uislamu wanaona kuwa Zaka ni mpango wa uchumi au ni utaratibu fulani wa kiuchumi wa kiislamu. Wengine wanaichukulia kuwa ni kodi ya mali za matajiri.

Ukweli ni kwamba Zaka si kodi au mpango fulani wa kiuchumi. Kwa sababu sharti ya msin- gi ya kukubaliwa Zaka, ni nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, bila hivyo haikubali- wi kabisa. Na kodi au utaratibu wa kiuchumi hauzingati sharti hii.

Zaidi ya hayo, utaratibu wa kiuchumi, kwa maana ya kisasa, kwanza unaangalia nyezo za uzalishaji; kama vile ardhi, madini na viwanda. Mfumo wa kibepari unazingatia kuwa ni milki ya mtu binafsi anayeimiliki. Ama mfumo wa kijamaa unazingatia kuwa ni milki ya umma inayoongozwa na serikali. Na Zaka haiangalii haya kabisa.

Ama kodi nayo inasimamiwa na kiongozi wa nchi katika kupatikana kwake na kuitoa; haiwezekani kwa mtoaji kwa hali yeyote kuacha kuitoa kwa kiongozi, ambaye ndiye mwenye uwezo wa kuitumia.

Mafaqihi wote wanasema kuwa mwenye kumiliki mali anaweza kutoa Zaka bila ya idhini ya kiongozi, naye anaweza kuaminiwa, bila ya ushahidi wowote au kiapo, akisema kuwa amekwishatoa. Sasa Zaka na kodi ni wapi na wapi? Bali mafaqihi wamejuzisha kwa mkusanyaji Zaka kuitoa kwa mafukara yeye mwenyewe bila ya kuipeleka kwenye Baitul Mal (hazina ya Waislamu).

Imam Ali (a.s.) alimwambia mmoja wa wanaokusanya Zaka: "Tumia mali uliyonayo kwa wenye watoto wanaohitaji na wenye njaa."Kwa dhahiri ni kwamba kodi haina matumizi haya kabisa.

Mtu anaweza kusema: Faradhi ya zaka maana yake ni kukubali kwamba ufukara lazima uwepo, na kwamba uislamu unaukabili ufukara kwa sadaka, jambo ambalo natija yake ni kuweko tabaka ya utajiri na umasikini?

Jibu: Matumizi ya Zaka hayakufungika kwa fakiri na maskini tu, isipokuwa katika jumla ya matumizi yake ni maslahi ya umma, ambayo Mwenyezi Mungu ameyaeleza kwa ibara ya sabilillah (njia ya Mwenyezi Mungu) katika Aya nyingi. Kwa hiyo kama hakukupatikana fukara, basi Zaka hutumiwa katika njia hii. Kwa hali hiyo, Zaka hailazimishi kuweko fukara kwa namna yoyote, wala Zaka sio ikrari ya kusema ufukara ni chapa isiyoepukika.
Pili: wajibu wa jamii ni kuwatunza masikini ili wasiwe ombaomba na wazururaji. Jambo hili linapatikana hata katika miji ya kijamaa ambayo haikubali utabaka.

Tatu: Tutamfanyaje mgonjwa asiyeweza hata kununua dawa na mwenye njaa ambaye hana njia yoyote ya kupata chakula katika jamii inayoongozwa na ufisadi. Je tuache mpaka hali itakapokuwa nzuri na umasikini utakapoondoka? Au tuweke kanuni itakayodhamini maisha yao? Je, inawezekana kupatikana mabadiliko kwa msitari wa kalamu? bila ya kupi- tia vipindi vingi?

Hakika Uislamu unapiga vita aina zote za unyonge. Na Mtume (s.a.w.) aliutolea mawaidha. Baadhi ya riwaya zinasema: "Ufukara unakurubia kuwa kufuru". "Mwislamu mwenye nguvu ni bora kuliko mnyonge."

Ujumbe wa Mwenyezi Mungu una lengo la heshima ya mtu na utengeneo wake; na ufukara ni upungufu na madhila na ni mashaka na balaa. Kwa hivyo haiwezekani uislamu kuukubali. uislamu haukatai kuweko katika jamii tajiri na tajiri zaidi au mwenye nguvu na mwenye nguvu zaidi, isipokuwa unachokataa ni kuweko fukara na mnyonge.

Uislamu haukuweka Zaka kwa ajili ya masikini tu kama inavyodhaniwa bali ni kwa kutatua matatizo mengi, ukiwemo umasikini kama upo. Vilevile utumwa, ambapo unapatiwa uhuru na mali ya Zaka. Matatizo mengine ni kuhudumia askari wanaopigana Jihadi, na mengineyo katika maslahi ya umma; kama vile kujenga shule, hospitali, barabara na miradi ya maji. Tutaeleza ufafanuzi wa matumizi ya Zaka katika Sura ya (9:60) Inshallah.

Lau tunakadiria kuwa mtu ataweza kupitiwa na wakati ambao hauna masikini na mahitaji yote ya umma yametoshelezwa, kiasi ambacho matumizi ya Zaka hayatapatikana kabisa, basi bila shaka itaachwa. Na wakati huo utafika tu; kama ilivyokuja Hadith katika Sahih Bukhari Juzuu ya 9 mlango wa Fitan; anasema Mtume s.a.w.w: "Toweni sadaka, utakuja wakati mtu atatemebea na sadaka yake asipate wa kuikubali."

Zaidi ya hayo, uislamu umemwajibishia mtoaji Zaka wakati anapompatia muhitaji kutomuudhi na kutomvunjia heshima yake na asikwaruze hisia zake. Kwamba huko kutoa ni wajibu wake na ni deni ambalo hapana budi kulitekeleza. Kwa kutilia mkazo maana haya Qur'an inasema: "Na ambao katika mali yao iko haki maalum kwa ajili ya aombaye na anayezuilika kuomba." (70:24-25)

Yamekwishatangulia maelezo katika tafsiir ya Sura hii Aya (262-263) kuhusu kuudhi. Pamoja na kuwa Uislamu umezishinda sheria zote za dini zingine na za kufanywa na watu kwa kuweka sheria hii ya Zaka sheria hii ya kibinaadamu ambayo hawakuigundua waweka nidhamu ispokuwa baada ya Uislamu kwa mamia ya miaka na kuiita 'dhamana ya jamii', pamoja na yote hayo jambo bora zaidi kuwapa wahitaji katika mtazamo wa kiislamu, ni kuwaandalia kazi inayonasibiana na uwezo wao ili wahisi thamani ya uhai. Mwenyezi Mungu humpenda mja wake mumin anayejishughulisha na kazi.

Mwisho tunamaliza maelezo haya kwa kauli ya Imam Ja'far Asswadiq (a.s): "Kila kiungo katika viungo vyako kina Zaka ya Mwenyezi Mungu: Zaka ya jicho ni kuzingatia na kulifumba na mambo ya haramu, Zaka ya sikio ni kusikiliza elimu na hekima, Zaka ya ulimi ni kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuwapa nasaha Waislamu, Zaka ya mkono ni kutoa na Zaka ya mguu ni kuhangaikia jihadi na kusuluhisha watu."

الَّذِينَ يَأْكُلُونَ الرِّبَا لَا يَقُومُونَ إِلَّا كَمَا يَقُومُ الَّذِي يَتَخَبَّطُهُ الشَّيْطَانُ مِنَ الْمَسِّ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا إِنَّمَا الْبَيْعُ مِثْلُ الرِّبَا ۗ وَأَحَلَّ اللَّهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا ۚ فَمَنْ جَاءَهُ مَوْعِظَةٌ مِنْ رَبِّهِ فَانْتَهَىٰ فَلَهُ مَا سَلَفَ وَأَمْرُهُ إِلَى اللَّهِ ۖ وَمَنْ عَادَ فَأُولَٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ {275}

Ambao wanakula riba, hawainuki, ila kama ainukavyo ambaye amezugwa na shetani kwa wazimu. Hayo ni kwa sababu wanasema kuwa biashara ni kama riba. Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara na ameharamisha riba. Na aliyefikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake, akakoma, basi yake ni yaliyokwishapita na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Lakini wanaorejea, basi hao ndio watu wa motoni; wao ni wenye kukaa humo milele.

يَمْحَقُ اللَّهُ الرِّبَا وَيُرْبِي الصَّدَقَاتِ ۗ وَاللَّهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ كَفَّارٍ أَثِيمٍ {276}

Mwenyezi Mungu huipunguza riba na huizidisha sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila kafiri afanyae dhambi.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ لَهُمْ أَجْرُهُمْ عِنْدَ رَبِّهِمْ وَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ {277}

Hakika wale walioamini wakafanya vitendo vizuri na wakasimamisha Swala na wakatoa Zaka, wao watapata ujira wao kwa Mola wao, wala haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَذَرُوا مَا بَقِيَ مِنَ الرِّبَا إِنْ كُنْتُمْ مُؤْمِنِينَ {278}

Enyi mlioamini! Mcheni Mungu na acheni yaliyobaki katika riba, ikiwa mmeamini.

فَإِنْ لَمْ تَفْعَلُوا فَأْذَنُوا بِحَرْبٍ مِنَ اللَّهِ وَرَسُولِهِ ۖ وَإِنْ تُبْتُمْ فَلَكُمْ رُءُوسُ أَمْوَالِكُمْ لَا تَظْلِمُونَ وَلَا تُظْلَمُونَ {279}

Na kama hamtafanya, basi jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkiwa mmetubu, basi haki yenu ni rasilimali zenu; msidhulumu wala msidhulumiwe.

وَإِنْ كَانَ ذُو عُسْرَةٍ فَنَظِرَةٌ إِلَىٰ مَيْسَرَةٍ ۚ وَأَنْ تَصَدَّقُوا خَيْرٌ لَكُمْ ۖ إِنْ كُنْتُمْ تَعْلَمُونَ {280}

Na kama ana dhiki, basi angoje mpaka awe na uwezo. Na kama deni mkizifanya sadaka, basi ni bora kwenu ikiwa mnajua.

وَاتَّقُوا يَوْمًا تُرْجَعُونَ فِيهِ إِلَى اللَّهِ ۖ ثُمَّ تُوَفَّىٰ كُلُّ نَفْسٍ مَا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ {281}

Na iogopeni siku ambayo mtarud- ishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi ilipwe iliyoyachuma; nao hawatadhulumiwa.