read

Aya 275-281: Mnasaba

Maudhui ya sadaka na riba yote ni mali, ingawa kuna tofauti ambayo ni: Sadaka hutolewa bila ya kutaka kurudishiwa; ni tohara, safi na dhamana. Ama riba ni kutoa kwa kutaka kurudishiwa mali pamoja na ziada; ni tamaa, uchoyo, uchafu, unyang'anyi na maangamizo. Kwa hiyo maudhui ni sawa, lakini hukumu na lengo ni kinyume kabisa. Ikiwa vitu hutajwa kwa mifano yake basi pia hutajwa kwa vinyume vyake. Ndio maana ikaja hukumu ya riba mara tu baada ya hukumu ya sadaka (Zaka).

Kabla ya kuingilia kufasiri Aya, tutaanza kuonyesha riba inavyoeleweka katika sharia, dalili ya uharamu wake na yanayo sababisha uharamu.

Neno Riba

Neno 'riba' katika lugha maana yake ni ziada; kama alivyolitumia Mwenyezi Mungu katika Sura (22:5).

Katika sharia, riba inagawanyika kwenye mafungu mawili: Riba ya kukopesha na riba ya kuzidishiana katika bei.

Maana ya riba ya kukopesha, ni mtu kumkopesha mwingine kitu chochote na kumlazimisha yule aliyemkopesha manufaa yoyote kwa sababu ya kumkopesha; kama vile kukopesha shillingi kumi kwa sharti ya kurudishiwa kumi na moja. Au kwa yasiyokuwa manufaa ya mali; kwa mfano mkopeshaji kumshurutisha aliyemkopesha amfanyie kazi fulani au amwazime kitabu au kitu chochote. Mtume (s.a.w.) anasema "Kukopesha kokote kunakovutia manufa ni haramu." Hapo hakutofautisha aina ya manufaa.
Hata hivyo kama mkopaji akilipa deni pamoja na ziada ya ahsante, itafaa kwa mkopeshaji kuichukua. Mtume (s.a.w.) alikuwa akilipa deni pamoja na ziada, akisema:"Bora ya watu ni yule anayewakopesha watu vizuri."

Inatakikana tuzingatie kuwa riba inathibiti katika kukopesha kwa kushurutisha ziada na manufaa kwa namna yoyote ile ya ziada, ni sawa iwe ziada ya kipimo cha mizani ujazo, urefu au idadi. Vilevile ni sawa iwe ni katika namna ya mali iliyokopeshwa au namna nyingine. Kwa maneno mengine riba ya kukopesha haina tofauti katika dhati ya kitu kwa kitu au manufaa.

Ama riba ya bei ni kuzidishiana kitu kil kile, na masharti yake ni mawili:

Kwanza ni kupeana kwa ziada aina hiyo hiyo kwa jina lake la uhakika, kama kuuza ngano kwa ngano, au kuuza ngano nzima kwa unga wa ngano, kwa sababu unga umetokana na ngano nzima. Vilevile Wanga (nishaa) na unga, kwani vyote viwili vimetokana na asili moja ambayo ni ngano.

Dalili ya pili ni kuwa wanavyouziana viwe vinaweza kupimwa kwa ujazo au mizani tu. Kwa hiyo hakuna riba kwa vinavyouzwa kwa idadi; kama mayai. Inawezekana kuuzwa yai moja kwa mawili. Pia hakuna riba kwa kinachouzwa kwa kuonyeshana; kama nguo na wanyama.

Kwa ufupi ni kwamba riba ni haramu katika deni kwa namna yoyote ile, na katika bei ni haramu kwa vinavyopimwa kwa namna yoyote, kwa sharti ya kuwa vyote viwili viwe ni jinsi moja. Hayo tumeyafafanua zaidi katika kitabu chetu Fiqhul-Imam Jaffar Sadiq (a.s.) Mlango wa Riba.

Uharamu

Riba ni haramu kwa nukuu ya Qur'an, Hadith mutawatir na kongamano la Waislamu wote, tangu siku za Mtume (s.a.w.) mpaka leo. Bali uharamu wake hauhitaji dalili, kwa sababu ni katika mambo yaliyo wazi; kama vile wajibu wa Swala na uharamu wa zina.

Kwa sababu hiyo ndipo mafaqihi wakahukumu kwamba mwenye kukanusha uharamu wa riba, basi ni kafiri, kwa vile amekanusha dharura ya dini iliyothibiti.

Kama ilivyo haramu kuchukua riba, pia ni haramu kuitoa. Hadith ya Mtume inasema: "Ameilaani Mwenyezi Mungu riba, mwenye kuila, mwenye kuuza, mwenye kununua, mwandishi wake na shahidi wake."

Sababu Ya Haramu

Mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu, kwamba Yeye ndiye mwenye kuweka sharia ya halali na haramu, basi hawezi kutaka mengi zaidi ya wahyi katika kuharamishwa riba.

Na kama ikitokea kuuliza sababu, basi haulizi kwa sababu ya kujikinaisha, isipokuwa ni kwa kutaka kufahamu tu; au kwa ajili ya kuwakinaisha wale walioelezewa na Aya hii:

"Na anapotajwa Mwenyezi Mungu pekee yake, mioyo ya wale wasioamini akhera huchafu- ka, na wanapotajwa wale asiyekuwa yeye wanafurahi." (39:45).

Vyovyote iwavyo ni kwamba wametaja sababu kadha za kuharimishwa riba. Miongoni mwa sababu hizo ni kama ifuatavyo:- Kupingana na misingi ya kibinadamu; kama vile kufanyiana wema, kusaidiana na kuoneana huruma.

Kuwa hiyo riba maana yake ni kula mali ya batili. Kwa sababu mwenye kula riba anaichukua bila ya kufanya lolote.

Mtu anaweza kusema kuwa anayechukua riba hufanya kitu, kwa sababu mali yake anaitoa kwa aliyekopa ambaye anaitumia na kunufaika nayo. Kwa hivyo hali ya riba ni sawa na kukodisha ardhi, nyumba au mnyama.
Mtu akisema hivyo tutamjibu: Kuna tofauti kubwa kati ya kukodisha na riba, kwani mwenye kukodisha hana jukumu la kulipa kile alichokikodisha, kama kikifa au kikihariibika, isipokuwa kama yeye ndiye aliyesababisha. Lakini chenye kukopwa kikiharibika, basi mwenye kukopa atakilipa.

Kwamba mwenye kuchukua riba hupata faida daima na mwenye kukopa hupata hasara; matokeo yake, matunda yote yanaishia kwa mchukuaji riba Baadhi ya maprofesa wa mambo ya uchumi wa Ulaya wameijua aibu hii. Miongoni mwa hao wataalamu ambao wameinukia katika nidhamu za riba, ni Dkt. Schacht, Mjerumani, Meneja wa zamani wa Benki alisema katika mhadahara alioutoa Damascus mnamo mwaka 1953:

"Tukifanya mahesabu tutajua kuwa mali yote katika dunia inaishia kwenye idadi ndogo sana ya wanaokula riba. Hiyo ni kwa sababu anayekopesha kwa riba, daima hupata faida katika kila kitu, wakati ambapo mwenye kudaiwa kwa riba anatazamia kupata faida na hasara; hatimaye ndipo mali yote inaishia kwa yule mwenye uhakika wa faida. Nadharia hii iko njiani kuthibitika. Kwani wenye mali humiliki maelfu ya pesa. Ama wenye milki wote, na wenye viwanda ambao wanakopa kutoka katika mabenki, n.k. hawana lolote isipokuwa ni waajiriwa tu, wakiwatumikia wenye mapesa ambao wanachukua matunda ya jasho lao."

Kuna baadhi ya wataalamu wa kiuchumi waliothibitisha kwamba msingi na asili ya fikra ya riba unatokana na mayahudi, na watu wengine wamechukua fikra hiyo kutoka kwao, hayo hayako mbali, kwani historia ya mayahudi wa kale na wa sasa inathibitisha kuwa Mungu wao, dini yao heshima ya siasa yao ni mali tu peke yake haina mshirika; na njia yoyote ya kuleta mali ni tukufu, hata kama ni umalaya, ukuwadi, uasi, wizi, unafiki au ria na uovu wowote ule.

Maana

Ambao wanakula riba, hawainuki, ila kama ainukavyo ambaye amezugwa na shetani kwa wazimu.

Shetani hamzugi yoyote, wala hana uwezo wowote wa kumfanya mtu kuwa mwenda wazimu. Isipokuwa hiyo ni tash'bihi na kuleta karibu ufahamu wa watu wanaosema kuhusu mtu aliiyepatwa na wazimu: "Amepagawa na Shetani."

Maana ya Aya ni kwamba hali ya wanaofanya riba, ni sawa na hali ya mwenda wazimu ambaye amezugwa, katika matendo yake, na kuwa shaghalabalaghala. Imepokewa Hadith kutoka kwa Ibn Abbas kuwa watu wa riba watafufuka kutoka makaburini mwao kama wenda wazimu, hiyo itakuwa ndio alama yao kwamba wao ni wala riba.

Hayo ni kwa sababu wamesema kuwa biashara ni kama riba.

Wamehalalisha riba kwa kuleta falfasa ya kuwa biashara na riba zinafanana kwa njia zote; basi kwa nini riba nayo isiwe halali? Si mtu anaweza kuuza kitu cha thamani ya shilling tano kwa shilingi sita na kwamba mtu anaweza kuuza kwa bei ya taslim shilingi moja tu na kwa mkopo shiling mbili? Kwa hiyo, eti inatakikana kuweko na ruhusa ya mtu kutoa shilingi kumi mpaka mwezi ujao kwa shilingi kumi na moja.

Mwenyezi Mungu anayajibu madai haya kwa kusema:

Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara na ameharamisha riba.

Njia ya majibu hayo ni kuwa, kule kufanana kwa kidhahiri hakufanyi kuwa ndio kufanana kabisa. Kwani biashara ni kazi ya kibiashara yenye kutafuta manufaaa; mwuzaji anakuwa kati ya kupata faida na hasara, kwa hivyo faida yake ni mavuno ya taabu yake, na wala sio kula mali ya batil, ambapo riba ni faida tu na kuchukua ziada bila ya jasho, kwa hiyo inakuwa ni kula mali ya batili.

Kwa ajili hiyo ndio Mwenyezi Mungu akahalalisha biashara na akaharamisha riba. Basi kutofautiana kihukumu ni dalili ya kutofautiana kihali na kinyume chake.
Na aliyefikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake, kisha akakoma, basi yake ni yaliyokwisha pita.

Yaani aliyekuwa amechukua riba, kabla ya kuteremshwa Aya ya kuiharamisha kisha akaacha baada ya kuharamishwa, Pia yule mwenye kusilimu sasa ikiwa amechukua riba kabla ya kusilimu kwake, si wajibu kurudisha baada ya kusilimu. Aya hii ni sawa na ile inayosema: "Wala msiwaoe wake waliowaoa baba zenu, isipokuwa yale yaliyokwishapita ..." (4:22)

Kuacha kuchukulia mambo yaliyopita, kuko katika mambo mengi, hasa mambo ya mali. Wameeleza sababu kuwa ni kutoleta matatizo ya kiuchumi.

Na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu

Wametaja njia nyingi katika kufasiri ibara hii, kiasi ambacho akili haiwezi kutosheka, ambalo tumelifahamu sisi ni kuwa mwenye kuchukua riba bila ya kujua hukumu yake na akaacha baada ya kujua makatazo ya Mwenyezi Mungu kwa kumtii, basi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atamsaidia na kumtosheleza kwa halali yake. Kwa sababu ameacha haramu kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu; na mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu atamtoshea.

Lakini wanaorejea, basi hao ndio watu wa motoni; wao ni wenye kukaa humo milele.

Maana yake ni kuwa wale ambao hawafuati amri ya Mwenyezi Mungu wala kuacha makatazo yake na kuendelea kula riba kwa inadi na kupuuza, basi watawekwa milele motoni. Kwa sababu mfano wa inadi hii hauwi isipokuwa kutokana na kafiri mkanushaji.

Mwenyezi Mungu huipunguza riba na huizidisha sadaka. Na Mwenyezi Mungu ham- pendi kila kafiri afanyaye dhambi.

Yaani mwenye kula riba hutaka ziada katika mali yake, lakini riba kwa hakika ni kupungua mali na uchafu ulioharamishwa. Na haramu hutoa mali kutoka kwa aliye nayo na inafanya matumizi ya riba yawe kama matumizi ya mali ya kunyang'anya, zaidi ya hayo ni dhambi na adhabu.

Kimsingi ni kuwa kila linalokuwa ni sababu ya kumkasirisha Mwenyezi Mungu na adhabu, basi ni uchafu na upungufu na ni amali ya shetani.

Ama sadaka, inasafisha mali na kuitakasa na inaifanya thabiti miliki ya mwenye kutoa sadaka na Zaka. Vilevile inaleta radhi ya Mwenyezi Mungu na thawabu Yake. Huo ndio ukamilifu na ziada hasa. Kwa maneno mengine ni kwamba wingi, wa mali ya haramu ni uchache, na uchache wa mali ya halali ni wingi.

Kafiri afanyae dhambi ni yule anayefanya inadi ya kula riba bila ya kushtuka na ni yule anayeendelea kufanya inadi ya kukataa kutoa Zaka, na kutoshtuka na vitendo vya Mwenyezi Mungu na kiaga chake.

Kwa kutegemea Aya hii, yafaa kusema kuwa waislamu wengi wakati huu ni makafiri wafanyao dhambi, kwa sababu ya kung'angania riba na kuacha kutoa Khums na Zaka.

Hakika wale walioamini wakafanya vitendo vizuri na wakasimamisha Swala na wakatoa Zaka, wao watapata ujira wao kwa Mola wao, wala haitakuwa hofu juu yao, wala hawatahuzunika.

Aya hii iko dhahiri katika maana, haihitaji tafsiri, zaidi ya hayo tafsiri yake imekwishapita katika Aya ya 25 na 82 ya Sura hii. Isipokuwa ameirudisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ahadi hii kwa kufuatisha ahadi baada ya kiaga na kinyume. Kwa hiyo alipoelezea kiaga cha wanaofanya riba amefuatishia ahadi kwa watu wema.

Kwa ujumla Aya kwa dhahiri inafahamisha kuwa imani ya nadharia tu, bila ya vitendo si chochote.

Enyi mlioamini! Mcheni Mungu na acheni yaliyobaki katika riba, ikiwa mmeamini.

Kusema: Acheni yaliyobaki katika riba kunafahamisha kuwa uharamu sio katika yale yaliy- opita nyuma, kama tulivyoeleza.

Na kama hamtafanya, basi jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu Na Mtume Wake.

Na hakuna jambo linalowajibisha kutangaza vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kwa anayeng'angania kula riba ila, ni kwa kuwa yeye ni kafiri au yuko katika hukumu ya kafiri; hata kama kula kwake riba ni kwa kupuuza tu, si inadi. Lakini riwaya zilizopokewa kutoka kwa Masum zimegawanya kula riba katika mafungu mawili.

Kwanza, ni yule anayekula kwa kuifanya halali. Huyo ni kafiri bila shaka yoyote, kwa sababu amekana dharura ya dini. Imam Jaffar Sadiq (a.s.) aliambiwa fulani anakula riba na anaita 'lubba" (kiini), akasema: "Nikimpata nitaikata shingo yake."

Pili, ni kula kwa kupuuza hukmu ya Mwenyezi Mungu pamoja na kuamini uharamu wake. Huyu atatakiwa kutubia mara ya kwanza na ya pili; kama akiendelea atauliwa. Imepokewa kutoka kwa Imam Sadiq (a.s.) kuwa mwenye kula riba atatiwa adabu baada ya kubainika, akirudia atatiwa adabu, akirudia atauliwa. Imesemekana kuwa atauliwa mara ya nne.

Na mkiwa mmetubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu; msidhulumu wala msidhulumiwe.

Yaani msimdhulumu mdaiwa kwa kumtaka zaidi ya rasilmali; wala msidhulumiwe kwa kupunguziwa rasilimali.

Na kama ana dhiki basi angoje mpaka awe na uwezo.

Kila mwenye kudaiwa riba, au isiyokuwa riba haijuzu kumdhiki ikiwa ana uzito; kama ambavyo pia haifai kwa mdaiwa kuchelewesha deni akiwa na uwezo. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) anasema: "Kama ambavyo si halali kwa mdeni wako kukucheleweshea deni akiwa na uwezo, vilevile si halali kwako nawe kumdhikisha akiwa na uzito."

Kiwango cha mwenye dhiki ni ambaye hamiliki chochote zaidi ya nyumba yake ya kukaa na vitu vyake vya dharura; kama nguo, vitabu na vyombo vya nyumbani vya lazima. Vilevile zana zake za kufanyia kazi zinazompatia chakula chake na cha familia yake na gharama yake ya siku moja. Vyote hivi si wajibu kuviuza kwa kulipa deni. Hayo tumeyataja kwa ufafanuzi katika kitabu 'Fiqhul-Imam Jaffar Sadiq' mlango wa Muflis.

Na kama (deni) mkizifanya sadaka, basi ni bora kwenu ikiwa mnajua.

Hapana shaka kwamba kumsamehe deni mwenye dhiki ni fadhila katika dini, bali ni katika utii mkubwa. Kwani hilo ni kumfanya apumue na kuweza kutekeleza haja zake vizuri. Imekuja Hadithi: "Mwenye kumvumilia mwenye uzito au kumsamehe, Mwenyezi Mungu atampa kivuli siku ambayo hakutakuwa na kivuli isipokuwa kivuli cha Mwenyezi Mungu."

Mafaqihi wameafikiana kwa kauli moja kuwa mwenye kukopa katika dharura ya halali, kisha akashindwa kulipa, atalipiwa deni lake kutoka katika hazina ya waislamu (Baitul Maal).

Imam Jaffar Sadiq (a.s.) anasema: "Mwenye kuchukua riziki hii kwa uhalali kwa ajili yake na ya watoto wake, ili airudishe baadae anakuwa kama mpigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Akishindwa kulipa na amkope Mwenyezi Mungu na Mtume wake."

Maana ya kumkopa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ni kwamba deni lake litalipwa kutoka katika hazina ya waislamu. Na hilo ni kuitumia katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Qur'an imelieleza hilo kwa kusema:
"Sadaka hupewa: mafukara na masikini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao na katika kuwakomboa watumwa na wenye madeni na katika njia ya Mwenyezi Mungu na wasafiri,. Ni faradhi inayotoka kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hekima." (9: 60)

Kauli yake Mwenyezi Mungu "Ikiwa mnajua" ni kutilia mkazo kufanya kitu kwa kujua; yaani maadamu mnajua kuwa kumsamehe deni mwenye dhiki ni heri, basi ni juu yenu kufanya kwa kujua kwenu hili.

Imesemekana kuwa makusudio ya kujua ni kufanya; yaani mkiwa ni wafanya heri, basi litoeni sadaka deni kwa mwenye dhiki. Maelezo haya hayako mbali, na kauli ya Imam Ali (a.s.) anasema: "Elimu iko na matendo, mwenye kujua hufanya, elimu hubaki kwa kuifanyia kazi, vinginevyo huondoka."

Wataalamu wengi wa kisasa hawaiti nadharia yoyote kuwa ni elimu mpaka wauone ukweli wake kwa kufuatishia na majaribio.

Na iogopeni siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi ilipwe iliyoyachuma, nao hawatadhulumiwa.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kukataza riba kwa mkazo na kuamrisha kumfanyia subi- ra mdaiwa mwenye dhiki, au kumsamehe, katika Aya saba, kisha anafuatisha Aya anay- owahofisha waasi na siku ya hisabu na malipo na adhabu yake. Katika Majmaul Bayan imeelezwa kuwa Aya hii ni ya mwisho kumshukia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) na kwamba yeye aliishi siku 21 tu baadaye.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا تَدَايَنْتُمْ بِدَيْنٍ إِلَىٰ أَجَلٍ مُسَمًّى فَاكْتُبُوهُ ۚ وَلْيَكْتُبْ بَيْنَكُمْ كَاتِبٌ بِالْعَدْلِ ۚ وَلَا يَأْبَ كَاتِبٌ أَنْ يَكْتُبَ كَمَا عَلَّمَهُ اللَّهُ ۚ فَلْيَكْتُبْ وَلْيُمْلِلِ الَّذِي عَلَيْهِ الْحَقُّ وَلْيَتَّقِ اللَّهَ رَبَّهُ وَلَا يَبْخَسْ مِنْهُ شَيْئًا ۚ فَإِنْ كَانَ الَّذِي عَلَيْهِ الْحَقُّ سَفِيهًا أَوْ ضَعِيفًا أَوْ لَا يَسْتَطِيعُ أَنْ يُمِلَّ هُوَ فَلْيُمْلِلْ وَلِيُّهُ بِالْعَدْلِ ۚ وَاسْتَشْهِدُوا شَهِيدَيْنِ مِنْ رِجَالِكُمْ ۖ فَإِنْ لَمْ يَكُونَا رَجُلَيْنِ فَرَجُلٌ وَامْرَأَتَانِ مِمَّنْ تَرْضَوْنَ مِنَ الشُّهَدَاءِ أَنْ تَضِلَّ إِحْدَاهُمَا فَتُذَكِّرَ إِحْدَاهُمَا الْأُخْرَىٰ ۚ وَلَا يَأْبَ الشُّهَدَاءُ إِذَا مَا دُعُوا ۚ وَلَا تَسْأَمُوا أَنْ تَكْتُبُوهُ صَغِيرًا أَوْ كَبِيرًا إِلَىٰ أَجَلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ أَقْسَطُ عِنْدَ اللَّهِ وَأَقْوَمُ لِلشَّهَادَةِ وَأَدْنَىٰ أَلَّا تَرْتَابُوا ۖ إِلَّا أَنْ تَكُونَ تِجَارَةً حَاضِرَةً تُدِيرُونَهَا بَيْنَكُمْ فَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَلَّا تَكْتُبُوهَا ۗ وَأَشْهِدُوا إِذَا تَبَايَعْتُمْ ۚ وَلَا يُضَارَّ كَاتِبٌ وَلَا شَهِيدٌ ۚ وَإِنْ تَفْعَلُوا فَإِنَّهُ فُسُوقٌ بِكُمْ ۗ وَاتَّقُوا اللَّهَ ۖ وَيُعَلِّمُكُمُ اللَّهُ ۗ وَاللَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ {282}

Enyi mlioamini! Mnapokopeshana deni kwa muda uliowekwa, basi liandikeni; na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu. Wala mwandishi asikatae kuandika kama vile alivyomfunza Mwenyezi Mungu; basi na aandike. Na aandikishe yule ambaye iko juu yake haki; na amwogope Mwenyezi Mungu Mola wake; wala asipunguze chochote katika deni. Na kama yule ambayeuu yake iko haki ni mpumbavu au mnyonge au yeye hawezi kutaja mwenyewe, basi na ataje msimamizi wake kwa uadilifu. Na muwashuhudishe mashahidi wawili katika watu wenu waume, kama hakuna wanaume wawili, basi ni mwanamume mmoja na wanawake wawili, katika wale mnaowaridhia kuwa mashahidi, ili kama mmoja wao akipotea, mmoja wao amkum- bushe mwingine. Na mashahidi wasikatae waitwapo. Wala msichoke kuiandika ikiwa ndogo au kubwa, mpaka muda wake. Hayo ndiyo uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu na imara sana kwa ushahidi na ni karibu zaidi kutofanya shaka. Ila ikiwa ni biashara ya mkono kwa mkono mnayopeana baina yenu, basi si vibaya kwenu msipoandika. Na wekeni mashahidi mnapouziana, wala asitiwe tabu mwandishi wala shaidi. Na kama mkifanya hivyo, basi hakika hilo ni ufasiki kwenu. Na mcheni Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu anawaelimisha; na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

وَإِنْ كُنْتُمْ عَلَىٰ سَفَرٍ وَلَمْ تَجِدُوا كَاتِبًا فَرِهَانٌ مَقْبُوضَةٌ ۖ فَإِنْ أَمِنَ بَعْضُكُمْ بَعْضًا فَلْيُؤَدِّ الَّذِي اؤْتُمِنَ أَمَانَتَهُ وَلْيَتَّقِ اللَّهَ رَبَّهُ ۗ وَلَا تَكْتُمُوا الشَّهَادَةَ ۚ وَمَنْ يَكْتُمْهَا فَإِنَّهُ آثِمٌ قَلْبُهُ ۗ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ {283}

Na kama mkiwa safarini na hamkupata mwandishi, basi ni rahani itakayokabidhiwa. Na kama mmoja wenu akimwamini mwingine, basi aliyeaminiwa atekeleze uaminifu wake na amche Mungu, Mola wake. Wala msifiche ushahidi. Na atakayeuficha, basi hakika moyo wake ni wenye kuingia dhambini. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi kwa mnayoyatenda.