read

Aya 28-30: Urafiki Na Kafiri

Lugha

Neno Awliya lina maana ya wasimamizi, Makusudio yake hapa ni marafiki kwa maana ya wasaidizi

Maana

Waumini wasiwafanye makafiri kuwa ni marafiki badala ya waumini (wenzao).

Mwenyezi Mungu hakutosheka na kukataza tu urafiki na makafiri kwa kusema ni haramu; kama vile uongo na kusengenya, bali amekuzingatia kuwa ni kufuru, kwa dalili ya neno lake:

Na mwenye kuyafanya hayo, basi hana kitu kwa Mwenyezi Mungu.

Kwani dhahiri ya kauli hiyo ni kuwa Mwenyezi Mungu yuko mbali na aliye na urafiki na makafiri; na aliye mbali na Mwenyezi Mungu, basi yeye ni Kafiri. Hili linatiliwa nguvu na Aya hizi: "Na atakayefanya urafiki nao miongoni mwenu, basi huyo atakuwa pamoja nao." (5:51). Huwapati watu wanaoamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho kuwa wanawapenda wale wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume Wake; hata wakiwa ni baba zao au watoto wao au ndugu zao au jamaa zao."(58:22)

Dhahiri ya Aya hizi inafahamisha kuwa mwenye kumfanya kafiri kuwa rafiki basi naye ni kafiri. Hata hivyo kuna aina mbali mbali za kumfanya rafiki, nyingine zinawajibisha ukafiri na nyingine haziwajibishi. Ufafanuzi ni kama ufatavyo:

Aina Za Urafiki Na Kafiri

Kila aliyesema: Laillaha Illa Ilah Muhammadun rasulullah. Basi anakuwa na lile walilonalo waislamu wengine, na wao wako na lile alilo nalo, isipokuwa akiwafanya makafiri kuwa ni marafiki katika mojawapo ya hali zinazofuata:

1. Kuwa radhi na ukafiri wao, na hili ni muhali kwa mwislam kwa sababu kuridhia ukafiri ni ukafiri.

2. Kujikurubisha kwa makafari kwa upande wa dini kwa kujaribu kufasiri Aya za Mwenyezi Mungu Mtukufu, na Hadith za Mtume Wake kwa yale yanayoafikiana na mapenzi ya makafiri, maadui wa Mwenyezi Mungu na Mtume, kiasi ambacho tafsiri hiyo itapingana na misingi ya kiislamu na kiitikadi. Ikiwa kwa makusudi na kujua. Huu vile vile ni ukafiri. Unaweza kuuliza: Mtu anayefanya hayo kwa ukaidi ni kafiri bila ya wasiwasi wowote, lakini mwenye kuyafanya kwa kupuuza tu, inafaa awe fasiki tu, sio kafiri; sawa na mwenye kuacha Swala akiwa anaamini kuwa ni wajibu na akanywa pombe akiwa anaamini kabisa kuwa ni haramu? Jibu: Kutofautisha kati ya mkaidi na mpuuzaji kunakuja kwenye Fur'uu (matawi); kama vile Swala, kunywa pombe n.k. Ama kwenye mambo yanayorudia kwenye Usul (Misingi) ya dini na itikadi; kama vile umoja wa Mungu, utume wa Muhammad n.k. Basi kutamka tu kitu kinachokanusha kunawajibisha ukafiri. Ni sawa mtamkaji awe ametamka kwa ukaidi au kwa kupuuza.

3. Kuwa kachero au jasusi wa makafiri dhidi ya waislamu, Huyu ataangaliwa. Ikiwa amefanya hivyo kwa tamaa ya mali au jaha basi atakuwa mwenye makosa aliye fasiki, ama akifanya kwa sababu ya kuwapenda makafiri kwa kuwa wao ni makafiri na kwa kuwachukia waislamu kwa kuwa ni waislamu, basi huyo ni kafiri bila ya shaka yoyote.

4. Kuwapenda makafiri na huku akiwa anajua kabisa kwamba wao wanawapiga vita Waislamu wakiwa wanataka kuwadhalilisha na kuwatumia, basi huyu atakuwa ni mwenye dhambi na mshirika wa dhalimu katika udhalimu wake, hata kama huyo dhalimu ni mwislamu.

5. Kuwataka msaada makafiri wenye amani dhidi ya makafiri wasiokuwa na amani. Msaada huu unafaa kwa maafikiano ya Ijmai (kongamano).

Watu wa historia na wafasiri wamenukuu kwamba Mtume (s.a.w.w.) aliwekeana mkataba wa kusaidiana na Bani Khuzaa inagawaje walikuwa washirikina. Pia alimtaka msaada Safwan bin Umayya - kabla hajasilimu - kwenye vita ya Hawazan. Vilevile aliwataka msaada Mayahudi wa Bani Qaynuqa na akawagawanyia mali.

Bali yamekuja maelezo kutoka kwa Allama Hili kwamba kundi la mafakihi wamejuzisha kutaka msaada kutoka kwa makafiri katika kuwapiga vita waislamu walio madhalimu. Kwa sababu kuwataka msaada kunaambatana na haki, si kwa ajili ya kuibatilisha batili.

6. Kufanya urafiki kwa sababu za mambo ya kawaida yaliyozoeleka, kama kushirikiana katika kazi au biashara na mengineyo mengi ambao hayahusu dini. Urafiki huu pia unafaa kwa kongamano la maulamaa. Kwa sababu kumpenda kafiri kutakuwa haramu kama kutapelekea kufanyika jambo la haramu, ama kukiwa sio wasila wa kufanya maasi, basi si haramu; bali huenda kukawa kunapendekezwa kama kuna manufaa na heri kwa nchi au watu. Na, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameamrisha upendano, kuzoweyana na kusaidiana kwa watu wote bila ya kuangalia dini au mila zao. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: "Mwenyezi Mungu hawakatazi kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakupigana nanyi kwa ajili ya dini wala hawakuwafukuza katika miji yenu. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao uadilifu."(60:8).

Sisi hatuna shaka kwamba katika makafiri kuna walio na hulka nzuri na tabia njema - ya ukweli, uaminifu na utekelezaji - kuliko wale tunaowaita na kujiita waislamu. Na kwamba kufanya urafiki nao ni bora zaidi - kibinadamu na kimaslahi ya umma - kuliko wale vibaraka wahaini wanaojionyesha kwa dini ya kiislamu.

Maelefu ya rehema na amani yamwendee yule aliyesema: "Aliye karibu ni yule aliye karibu kwa tabia. Huenda aliye karibu akawa mbali zaidi ya aliye mbali na aliye mbali akawa karibu zaidi ya aliye karibu." Hakika hii huitambua mtu kimaumbile tu bila ya hisia zozote.

Taqiya

Ila mtakapojilinda nao kwa kujihifadhi.

Historia ya Taqiya inaanzia na historia ya uislamu siku ulipokua dhaifu, na shujaa wa kwanza alikuwa Ammar bin Yasir, pale aliposilimu yeye, baba yake na mama yake; wakaadhibiwa na makafiri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wakavumilia adhabu na adha bila ya kulalamika. Mtume akawapitia wakiwa wanaadhibiwa: Hakuzidisha chochote Yasir zaidi ya kusema: "Hali ndio hii ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu." Mtume naye akasema: "Vumilieni enyi familia ya Yasir hakika ahadi yenu ni pepo." Akawa Yasir na mkewe Sumaiya ndio mashahidi wa kwanza katika uislam.

Washirikina wakamlazimisha Ammar kusema maneno kuhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu, akasema kwa ajili ya kujikinga na madhara kwa ajili ya nafsi yake. Hapa baadhi ya Maswahaba wakasema kuwa Ammar amekufuru; Mtume akasema: "Hapana hakika Ammar imani imemtanda kuanzia utosini hadi nyayoni…"

Ammar akaja kwa Mtume akiwa analia na kujuta. Mtume akampangusa machozi na kuuwaambia: "Usilie, hata kama watarudia, basi wewe rudia uliyoyasema." Hapo ikashuka Aya kumhusu Ammar: "Mwenye kumkufuru Mwenyezi Mungu baada ya kumwamini (ana adhabu kubwa) isipokuwa yule aliyelazimishwa hali ya kuwa moyo wake umetulia kwenye imani." (16:106)

Hakuna waliohitalifiana kuwa Aya hii, ilishuka kwa mnasaba huo wa Ammar. Kimsingi linalozingatiwa ni kuenea tamko, sio sababu za kushuka Aya. Na tamko hapa linamwenea kila mwenye kulazimishwa hali ya kuwa moyo wake umetulia kwenye imani. Kisha ndipo ikashuka Aya hii tunayoifasiri kutilia mkazo Aya hiyo ya kuhusu Ammar, kama zilivyo

Aya nyingine zifuatazo: Na akasema mtu mmoja Mumin katika watu wa firaun afichaye imani yake …(40:28) "… Isipokuwa vile mnavyolazimishwa" (6:119)
Ruhusa ya Taqiya haikuja kwenye kitabu cha Mwenyezi Mungu tu, bali katika Hadith vilevile. Ar-Razi katika Tafsir Kabir, na Sayyid Rashid Ridha katika Tafsir Al-Manar, na wengine wanasema: "Musailama Al-Kadhab aliwashika watu wawili katika swahaba wa Mtume, mmoja akamwambia: "Je, washuhudia kuwa mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu?"

Yule mtu akasema: "Ndio," basi akamwacha. Yule wa pili alipomwambia hivyo hivyo, alikataa, basi akamuua. Mtume alipopata habari hizo alisema: "Yule aliyeuawa amekufa na yakini yake na ukweli wake pongezi ni zake. Ama yule mwengine ameruhusiwa, (kufanya hivyo) hana neno."

Kuna Hadith katika Tafsir Al-Manar kwamba Bukhari katika Sahih yake akimnukuu Aisha anasema: "Mtu mmoja alibisha hodi kwa Mtume, Mtume akajisemea: "Mtu mbaya huyo", kisha akamruhusu kuingia na akazungumza naye vizuri."

Yule mtu alipoondoka Aisha akamwambia Mtume: "Si umesema uliyoyasema kuhusu mtu huyu, kisha umezungumza naye vizuri? Mtume akasema; "Hakika mwovu zaidi wa watu ni yule anayeachwa na watu kwa kujikinga na shari yake."

Na katika Bukhari tena kuna Hadith ya Abu Dardai inayosema: "Sisi tunatabasamu kwenye nyuso za watu na nyoyo zetu zinawalaani."

Zaidi ya hayo kuna Hadith nyingine zinafahamisha kujuzu Taqiya (kujikinga) kama vile Hadith: "Hapana dhara wala kudhuriana." Na "Umati wangu umesamehewa yale wanay- olazimika nayo." Hadith zote hizi mbili ni Mutawatir kwa upande wa Sunni na Shia.

Kwa kutegemea kitabu cha Mwenyezi Mungu na Hadith Mutawatiri za Mtume zilizo sahihi basi Sunni na Shia wamekongamana kwa kauli moja kuwa Taqiya inafaa. Anasema Al- Jasas mmoja wa Maimam wa Kihanafi katika juzuu ya pili ya kitabu Ahkamul Qur'an Uk. 10 chapa ya 1347 A.H. Ninamnukuu: "Ila kwa kujilinda nao" Yaani ni kuhofia kuangamia nafsi au baadhi ya viungo kwa hiyo kujilinda nao kwa kudhihirisha ukafiri bila ya kuutaikidi … Na hilo limeafikiwa na watu wa elimu."

Ar-Razi katika tafsiri yake amemnukuu Hassan Al-Basri akisema: "Taqiya inajuzu mpaka siku ya Kiyama". Vilevile amemnukuu Shafi kwamba yeye amejuzisha Taqiya kwa waislamu wote, ikiwa anamhofia mwislam mwenziwe katika tofauti zinazorudia masuala ya dini.

Mwenye Tafsir Al-Manar naye anasema kuhusu Aya hii: "Mwenye kutamka neno la kufru akiwa anajikinga na kuangamia kwa kulazimishwa sio kwa kuukubali ukafiri au kwa sababu ya kupenda dunia kuliko akhera, basi si kafiri na unakubaliwa udhuru wake kama alivyokubaliwa Ammar bin Yasir

Na amesema Sheikh Mustafa Azurqaa katika Kitabu Fiq-hul-Islam Fi Thawbihil Jadidi mada ya 600, anasema: "Kutishwa mtu kuuliwa kwa kulazimishwa ukafiri, kunamhalalishia kudhihirisha ukafiri ikiwa moyo umetulizana na imani."

Zaidi ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Hadith za Mtume na kongamano la Waislamu wa kisunni na kishia, pia akili inakubali Taqiya kwa sababu akili pia inaiona ni nzuri kutokana na desturi isemayo "Dharura inahalalisha yaliyokatazwa."

Kwa hiyo basi inatubainikia kuwa Taqiya ni kanuni ya sharia wanayoitegemea Mujtahid wa Kisunni na kishia katika kutoa hukumu.

Na kwamba dalili yake ni Qur'an, Hadith, kongamano na akili. Kwa ajili hiyo Taqiya inakuwa ni funzo la kiislamu kwa waislamu wote na kuaminiwa na madhehebu zote; na wala sio ya madhehebu maalum kama wanavyodhania Khawarij.

Hapa kuna swali linalojitokeza; nalo ni ikiwa Taqiya inafaa kwa Qur'an, Hadith, akili na kongamano kutoka kwa Shia na Sunni, kwa nini wanasibishiwe Shia tu, kiasi kwamba Masheikh wengi wa kisunni wameinasibisha kwa Shia na kuwakebehi nayo?

Jibu: Kunasibishiwa au kuwa mashahuri zaidi kwa Shia, huenda ikawa ni kwa sababu ya kuwa wao walilazimika kuitumia zaidi ya watu wengine kwa kuangalia vikwazo vingi walivyovipata wakati wa utawala wa Bani Umayya, Bani Abbas na waliowafuatia1.

Kwa sababu ya kulazimika Shia kuwa na Taqiya mara nyingi au zaidi kuliko wengine, ndio maana wakajishughulisha nayo na kuitaja katika vitabu vya fikh tena wakaifafanua kwa kubainisha mipaka yake na wakati wake wa kufaa kuifanya na kutofaa.

Muhtasari wa waliyoyasema ni: Inafaa kwa ajili ya kuondoa madhara ya nafsi, na haifai kwa ajili ya kuleta manufaa au kuingiza madhara kwa mwengine.

Ama yule anayeihusisha Taqiya na Mashia tu, ama atakuwa ni mjinga au atakuwa mwenye chuki. Hata hivyo hivi sasa Taqiya haitumiki (sana) baada ya kupita wakati wa hofu na vikwanzo.

Na anawatahadharisha Mwenyezi Mungu naye.

Yaani na dhati Yake ambayo inajua kila kitu, yenye uweza juu ya kila kitu na kumlipa kila mtu kwa amali yake.

Na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu.

Ambako italipwa kila nafsi ilichofanya.

Sema mkificha yaliyomo vifuani mwenu au mkiyadhihirisha Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo ardhini.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kujuzisha Taqiya na kuiruhusu kwa mwenye kulazimika, anasema: linaloangaliwa mbele ya Mwenyezi Mungu ni lile lililo moyoni: na yeye anayajua ya moyoni mkifanya siri au kuyadhihirisha.

Siku ambayo kila nafsi itakuta kheri iliyoitenda imehudhurishwa.

Lilivyokuwa Mwenyezi Mungu anajua kila kitu, muweza wa kila jambo; mkusanyaji wa watu siku isiyo na shaka. na mwadilifu asiyedhulumu, hayo yote yanamhakikishia mtu kukuta malipo ya amali yake.

Baadhi wanasema, mtu atakuta amali yake kesho ikiwa kama umbo zuri la kupendeza kama ni ya kheri; au kama ni mbaya basi itakuwa na umbo la kutisha.

Lakini inavyojulikana ni kwamba amali ni mambo ambayo hayabaki wala haiwezekani kuyarudisha na kuyaona. Kwa hiyo makusudio ni kuwa mtu siku ya kiyama ataona malipo ya amali yake sio hiyo amali yenyewe.

Na iliyoyatenda katika uovu, itapenda lau kama kungekuwa na masafa marefu baina ya uovu huo na yeye.

Herufi Wau hapa ni kuanza maneno; yaani mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu, hapo kesho atatamani kuweko na masafa kati yake na siku hiyo sawa na umbali wa Mashariki na Magharibi.

Na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja.

Hata waasi pia, kwa sababu amewalazimisha wanayoyaweza na amewahadharisha na mwisho mbaya wa maasi. Pia amefungua mlango wa toba kwa yule ambaye nafsi yake imefanya maovu. Kwa hiyo mwasi habaki na udhuru.

قُلْ إِنْ كُنْتُمْ تُحِبُّونَ اللَّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَحِيمٌ {31}

Sema: Ikiwa mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni Mwenyezi Mungu atawapenda na atawaghufiria madhambi yenu: na Mwenyezi Mungu ni mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.

قُلْ أَطِيعُوا اللَّهَ وَالرَّسُولَ ۖ فَإِنْ تَوَلَّوْا فَإِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ الْكَافِرِينَ {32}

Sema: Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume, kama wakikataa, basi hakika Mwenyezi Mungu hawapendi makafiri.
  • 1. Angalia kitabu chetu Ashia wal-hakimun na mwanzo wa juzu ya tatu ya sharh Nahajul-Balagha ya Ibn Abdul-Hadid, uone aina za adhabu na ukandamizaji usio na mfano.