read

Aya 282-283: Deni

Maana

Mwisho mwisho wa Sura hii Mwenyezi Mungu ametaja hukumu za sharia zinazofungamana na Zaka, riba, deni, biashara na rahani. Masuala ya Zaka na riba yamekwisha tangulia. Hivi sasa tuko katika baadhi ya masuala ya deni, rahani na biashara.

Aya imetilia umuhimu sana kuandika deni na kuweko ushahidi; ambapo Mwenyezi Mungu ameamrisha kuandika kwa kuanza kusema: "Iandikeni" Pili, akasema: "Wala msichoke kuiandika" Na mara ya tatu, amebainisha hekima ya kuandika na kuweko ushahidi kwa kusema "Hayo ndiyo uadilifu zaidi na imara zaidi na karibu zaidi kutofanya shaka."

Pamoja na hayo mafaqihi wengi hawakuwajibisha kuandika deni na kuuza, wala kuweko ushahidi. Wameichukulia amri ya hilo kuwa ni sunna. Kauli yao hiyo ya suna inatiliwa nguvu na kuwa baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuamrisha kuandika na kuweko ushahidi, amesema: "Kama mmeaminiana, basi aliyeaminiwa atekeleze amana";

Yaani kama mdai akimwamini mdaiwa bila ya kuandika wala ushahidi, basi ni juu ya mwenye kudaiwa kutekeleza. Hii ni ruhusa dhahiri ya kuacha kuandika na ushahidi. Itakuja tafsiri ya Aya hii Inshaallah.

Enyi mlioamini! Mnapokopeshana deni kwa muda uliowekwa, basi liandikeni.

Neno Tadayantum lina maana mbili: Kudaiana kwa mali na kulipiziana. Imam Ali (a.s.) anasema: "Kama utakavyomfanya (mwenzako) nawe utalipwa."Ilipokuwa neno tadayan-tum linachukua maana hizi mbili, ndio maana Mwenyezi Mungu akasema: "Tadaayan tum bidaynin. Ili kuondoa dhana ya kukusudia maana ya kulipa." Makusudio ya "Muda uliowekwa" ni muda wa kwisha deni uliotajwa iwe mwaka au mwezi, n.k.

Kusema Kwake Mwenyezi Mungu:"Basi liandikeni" ni amri ya kuandika deni, na amri inafahamisha wajibu, lakini imekuwa ni sera ya waislamu tangu zamani kutolazimika kuandika deni na kuweko ushahidi. Kwa hiyo amri ikachukuliwa kuwa ni suna na mwongozo.

Mkopo Na Deni

Mkopo unashirikiana na deni katika kuwa mtu ananufaika nao kwa kuutumia, na ni haki ya mtu katika dhima. Lakini mkopo unatofautiana na deni katika kuwa kitu chenye kukopwa kinalipwa cha aina hiyo hiyo katika jinsi yake na sifa; ukikopa pesa, basi dhima yako ni kulipa pesa, ni lazima urudishe mfano wake, sio kima.

Ama deni,1dhima inathibiti kutokana na sababu fulani; kama kukopa, bei ya mkopo, kuoa kwa mahari ya kulipa baadaye jinai na mengineyo. Kwa hiyo deni ni kiujumla na linalipwa mfano wake likiwa na mfano; au kima ikiwa halina mfano

Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu.

Ilivyokuwa lengo la kuandika deni ni kudhamini haki ya mdai na mdaiwa na kuondoa ubishi kati yao, basi ni wajibu mwandishi awe mwaminifu mwenye kujua hukumu ya dini. Kwani kama akiwa mbumbumbu au mwenye upendeleo, basi lengo litakuwa limebatilika.

Unaweza kuuliza, kwa nini amesema aandike mwandishi kwa uadilifu na asiseme aandike mwandishi mwadilifu?
Jibu: Kwa sababu kuandika si sharti mwandishi awe mwadilifu; kama ilivyo kwa kadhi, mufti na imam wa jamaa katika Swala. Kwa sababu lengo la kuandika deni ni kudhamini na kuhifadhi haki; kama tulivyoeleza. Kwa hivyo inatosha mwandishi kuwa mwadilifu kwa upande huu tu; na wala sio katika kauli zake na vitendo vyake vyote.

Kwa sababu hiyo inawezekana kusema kuwa Aya hii inafahamisha kuwa shahidi sio lazima awe na uadilifu wa kisheria, bali inatosha kutegemea kuwa ni mkweli na mwadilifu katika ushahidi wake, bila ya kumpendelea yeyote; na tutauchukulia uadilifu wa shahidi ulioelezwa katika hadithi kuwa ni uadilifu wa kiwango fulani na sio uadilifu kwa ujumla.

Kama ukisema kuwa kumpa shahidi hukumu ya mwandishi ni kutumia Qiyas na wewe si unasema Qiyas ni batili?

Jibu: Mwandishi ni shahidi hata kama haitwi hivyo. Kwa maneno mengine, shahidi ni aina mbili - wa kutamka na kuandika; huyu anashuhudia kwa kuandika na yule anashuhudia kwa kutamka; na kuandika ni ndugu wa kutamka.

Wala mwandishi asikatae kuandika kama vile alivyomfunza Mwenyezi Mungu; basi na aandike.

Makusudio ya alivyomfunza ni alivyomwamrisha; na alivyoamrishwa, ni kuandika kwa uadilifu, bila ya kupendelea. Kusema kwake "basi na aandike" ni kutilia mkazo kauli Yake "asikatae."Siri ya mkazo huu, ni kwamba wale waliokuwa wanajua kuandika wakati ule walikuwa kidogo sana, endapo mwandishi atakataa huwa vigumu kumpata mwingine.

Unaweza kuuliza kuwa kauli Yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) "wala mwandishi asikatae" ni katazo, na katazo linafahamisha uharamu; kwa maana hiyo basi, ni wajibu kwa mwandishi kukubali kuandika deni; na tunajua kuwa kuandika huku ni suna sio faradhi. Sasa itakuwaje tanzu izidi asili?

Jibu: Kama ambavyo kauli Yake Mwenyezi Mungu "basi iandikeni" tumeichukulia kuwa sunna, basi kauli Yake "Wala mwandishi asikatae" tunaichukulia kuwa ni makuruhu tu, wala sio haramu; isipokuwa ikiwa kuacha kuandika kutasababisha ufisadi na kusababisha wote wawili kuingia katika haramu, hapo ndio itakuwa kukataa ni haramu. Lakini hilo ni kwa upande wa kukinga ufisadi sio upande wa kuandika deni.

Na aandikishe yule ambaye iko juu yake haki; na amwogope Mwenyezi Mungu Mola wake; wala asipunguze chochote katika deni.

Ambaye haki iko juu yake ni mdaiwa. Maana ni kuwa ni wajibu kwa mdaiwa kutamka wazi-wazi mbele ya mwandishi, bila ya kupunguza, ili iwe ni ikrari yake kwa haki ya mwenyewe inayomlazimu yeye au warithi wake kulipa; haki inaweza kupotea kama hakuna uthibitisho wa madai.

Haya kwa uchache ndiyo yaliyo wajibu kwa mdaiwa juu ya aliyemkopa, ambaye amemsaidia kumaliza matatizo yake wakati wa dhiki.

Nimewaona watu wengi wakimnyeyekea mwenye mali kwa upole kabisa kwa kutaraji kukopeshwa ili kumaliza matatizo. Basi mara mtu anaposaidiwa, anageuka adui na kukataa deni, eti kwa vile tu mwenye mali anataka haki yake. Mbali ya kuwa wema kuulipia maovu ni haram kisheria, lakini hilo linaonyesha ukhabithi na ushenzi.

Kumshukuru Muumba Na Muumbwa

Mwenyezi Mungu anasema: "...kwamba unishukuru Mimi na wazazi wako ..." (31: 14) Katika Hadith imesemwa: "Hamshukuru Mwenyezi Mungu asiyewashukuru watu". Hadith nyingine inasema: "Mwenye kutendewa wema na mtu, akamshukuru Muumba kwa kusema "Shukrani ni za Mwenyezi Mungu", na akamsahahu aliyemtendea wema, basi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) haikubali shukrani mpaka amshukuru aliyemfanyia wema." Kwa sababu hiyo ndio ukawa mashuhuri msemo: "Asiyeshukuru kiumbe, hamshukuru Muumba." Ulazima huu una siri nyingi:
1. Akili na sharia zinahukumu wajibu wa kumshukuru yeyote mwenye kutenda vizuri; na mwenye kuacha shukrani hii, basi amemwasi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni na uasi kukanusha neema za Mwenyezi Mungu (s.w.t.).

2. Hadhi ya mtu ni hadhi ya Mwenyezi Mungu. Hadith imesema: "Mwenyezi Mungu atamwambia mja katika waja wake: Kwa nini hukunitembelea nilipokuwa mgonjwa?" Mja atasema: "Kutakata na maovu ni kwako, wewe ni mlezi wa waja, huugui wala huumwi." Mwenyezi Mungu atasema: "Alikuwa mgonjwa nduguyo mumin wala hukumtembelea. Naapa kwa utukufu wangu, lau ungalimtembelea ungelinikuta mbele yake na ningeliziangalia haja zako na kukutekelezea; na hayo ni kwa heshima ya mja wangu na Mimi ni Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu."

3. Kumshukuru mwenye kukufanyia jambo zuri ni kutekeleza amana. Na kutekeleza amana ni dalili ya ukweli na amani, bali ndio asili ya fadhila. Kwani unapopatikana utekelezaji, ndipo hupatikana ukweli, ikhlasi, uaminifu na kujitolea. Na utekeleza ji haugawanyiki - mwenye kumtekelezea amana aliyemtenda wema, basi pia huwatekelezea watu wake, marafiki zake, nchi yake na watu wote kwa ujumla. Na asiyetekeleza amana kwa aliyemfanyia wema au kujitia hamnazo, basi hufanya hivyo hivyo kwa watu wake, marafiki zake, na nchi yake. Ndio maana kukasemwa:"Asiyetekeleza amana hana dini."

4. Inavyopendeza zaidi ni kutekeleza amana wakati wa shida. Kwa sababu kutekeleza wakati wa neema ni kutekeleza kwa ajili ya mali sio kwa ajili ya mwenye mali na ni kwa ajili ya dunia sio kwa ajili ya mwenye dunia.

Na kama yule ambaye juu yake iko haki ni mpumbavu au mnyonge au yeye hawezi kutaja mwenyewe, basi ataje msimamizi wake kwa uadilifu

Mpumbavu hapa ni yule mbadhirifu aisyeweza kutumia mali vizuri mnyonge ni mtoto mdogo, na asiyeweza kutaja ni mwenda wazimu, wote hawa hawafai kuandikisha au kufanya ikrari yoyote; isipokuwa ni lazima wasimamiwe mambo yao na wasimamizi (mawalii) wao wanaowaangalia.

Wasimamizi ni aina mbili: Msimamizi mahsusi ambaye ni baba na babu wa upande wa kwa baba; na msimamizi wa kiujumla ambaye ni hakimu wa sharia aliye mwadilifu au Mujtahid. Huyu hana usimamizi mpaka akosekane babu na baba. Ufafanuzi wa Swala hili uko kwenye kitabu Fiqh Imam Jaffar Sadiq.

Na muwashuhudishe mashahidi wawili katika watu wenu wanaume.

Hili ni jambo la pili katika mambo aliyoyazingatia Mwenyezi Mungu katika deni: La kwanza ni kuandika na pili ni ushahidi. Kanuni za kutungwa zimeweka sheria ya kupatikana mashahidi wawili katika mikataba rasmi; sawa na ilivyokuja katika Qur'an.

Shia Imamiya na Hanafi, wanasema sharti hilo ni, itakapokuwa mwenye kutolewa ushahidi ni mwislamu. Ama akiwa si mwislamu, basi ushahidi wa watu wa mila unakubaliwa kwa mila zao.

Malik na Shafi wamesema haukubaliwi ushahidi wa asiyekuwa Mwislamu hata kama anawashuhudia asiyekuwa mwislamu. Haya yanapatikana katika kitabu Mughni na Fathul Qadir mlango wa ushahidi.

Kama hakuna wanaume wawili, basi ni mwanamume mmoja na wanawake wawili kati- ka wale mnaowaridhia kuwa mashahidi.

Haki za kimali zinathibiti kwa ushahidi wa wanaume wawili, au mwanamume mmoja na wanawake wawili au mwanamume mmoja na yamini, kwa maafikiano ya madhehebu yote; isipokuwa Abu Hanifa. Yeye anasema hautoshi ushahidi wa mtu mmoja na yamini.

Qur'an Tukufu imetaja ushahidi wa wanaume wawili na mwanamume mmoja na wanawake wawili tu. Ama kuthibiti haki ya kimali kwa shahidi mmoja na yamini kumefafanuliwa na Hadith.
Unaweza kuuliza: Je, inathibiti haki ya mali kwa ushahidi wa wanawake tu? Kisha je, inaweza kuthibiti kwa ushahidi wa wanawake wawili na yamini, kama ilivyo kwa mwanamume mmoja na yamini?

Jibu: Madhehebu yote yameafikiana kuwa haki za mali hazithibiti kwa ushahidi wa wanawake bila ya mwanamume na bila ya yamini, wametofautiana katika kuthibiti kwa ushahidi wa wanawake wawili na yamini. Malik na Imamiya wamesema inathibiti, wengine wamesema haithibiti.

Kauli Yake Mwenyezi Mungu "katika wale mnaowaridhia," inachukuliwa maana mbili: Kwanza ni kuwa makusudio ya kuridhia ni kuhusisha radhi kwa ushahidi wenyewe hasa, bila ya kuangalia hali ya shahidi. Kwa hiyo hakuna ulazima wa uadilifu wa shahidi, bali itatosha kwa Kadhi kutegemea kwamba ushahidi unaambatana na tukio; kama ulivyo ushahidi katika kanuni zilizotungwa, ambapo kadhi pekee ndiye anayekadiria ushahidi.

Maana ya pili ni kuridhia hali ya shahidi mwenyewe, kwa hivyo lazima shahidi awe mwadilifu., tamko la Aya linachukua maana zote mbili, lakini hadith na fatwa za Mafaqihi zinatilia nguvu matakwa ya uadilifu kwa shahidi mwenyewe, Imam Ali (a.s.) anasema: "Mshuhudieni ambaye mnaridhia dini yake, uadilifu wake utengeneo wake na kujiepusha kwake na dhambi."

Kwa hivyo wakitoa ushahidi waadilifu wawili, basi ni juu ya Kadhi kuhukumu kwa mujibu wa ushahidi wao; ni sawa awe ameelewa kutokana na kauli yao au hakuelewa kwa kuchukulia Hadith. Ama akishuhudia asiyekuwa mwadilifu, hawezi kuhukumu kwa ushahidi wao isipokuwa kama amepata kuelewa kutokana na kauli yao, kiasi ambacho kujua ndio kutakuwa ni matokeo ya hukumu, sio ushahidi wa asiyekuwa mwadilifu.

Ili kama mmoja wao akipotea, mmoja wao amkumbushe mwingine.

Hapa pana maswali mawili:

Kwanza, kwa nini amesema: "Ili kama mmoja wao akipotea, mmoja wao amkumbushe mwingine." Na wala asiseme: Amkumbushe mwingine tu.

Kuna haja gani ya kurudia nomino iliyo wazi katika jumla mbili ambazo hazikutengana kwa mbali wala karibu?

Hilo limejibiwa kwa njia nyingi, bora yao ni kuwa, ulipokuwa ushahidi wa wanawake wawili ni sawa na ushahidi wa mwanamume mmoja, basi ni wajibu kuukusanya ushahidi wa hao wanawake wawili, ili kwamba akisahau kitu, mwingine amkumbushe. Akimaliza, anaanza wa pili naye akisikilizwa na mwenzake wa kwanza, kama alivyofanya yeye. Kwa hiyo utakuwa ushahidi wa kila mmoja wao unatimiza ushahidi wa mwengine.

Maana hayo hayawezi kuja, isipokuwa kwa kurudi neno 'Mmoja wao' ili uweko mfungamano wa wawili, lau angelisema: amkumbushe mwengine tu, basi maana yangalikuwa: "Ili akisahau mmoja akumbushwe na wa pili. Kwa hiyo mmoja atakuwa anasema na mwingine ni mkumbushaji tu, na hayo siyo makusudio yake."

Kwa ujumla ni kuwa, si wajibu kuwakusanya pamoja mashahidi wakiwa wanaume; bali kuwatenganisha ni bora. Lakini kwa wanawake ni kinyume na hivyo.

Swali la pili: Kuna siri gani ya kuwa ushahidi wa wanawake wawili unalingana na ushahidi wa mwanamume mmoja?

Swali hili limejibiwa kwa njia nyingi. Miongoni mwazo ni kuwa mwanamke ana akili dhaifu. Kauli ya kushangaza ni kuwa kuna baadhi ya wafasiri wanaosema kuwa: Mwanamke ni mpole.

Kama kauli hii ingelikuwa sawa, basi ingelikuwa upole ni nusu ya ushahidi, hata kama ni mwanamume; na kila asiyekuwa mpole basi ni shahidi kamili, hata kama ni mwanamke!
Kauli yenye nguvu ni kuwa aghlab mwanamume anaweza kuzuwia hisia zake zaidi kuliko mwanamke. Na, jibu sahih zaidi ni kwamba ni juu yetu kuikubali amri hata kama hatujui hekima yake.

Kwa ujumla ni kwamba Kadhi mara nyingine anaweza kutegemea ushahidi wa mwanamke mmoja na kupata kujua kutokana na kauli yake zaidi, kuliko kutegemea ushahidi wa wanaume kumi wasiokuwa waadilifu. Na, inajuzu Kadhi kutoa hukumu kwa kujua kuliko- tokana na mwanamke, maadamu ni nyenzo ya kujua au kupata uhakika.

Na mashahidi wasikatae waitwapo.

Akikuita mdai, ili umtolee ushahidi juu ya haki au deni, basi ni wajib kifaya (wa kutosheana) juu yako kuitikia wito wake; yaani kama akitekeleza mwingine umuhimu huu, basi wajibu utakuwa umekuondokea; vinginevyo utakuwa na jukumu mbele ya Mwenyezi Mungu. Dalili ni Aya hii na Hadith Tukufu: "Atakapokuita mtu ili umshuhudilie juu ya haki au deni, basi usirudi nyuma."

Wala msichoke kuiandika ikiwa ni ndogo au kubwa, mpaka muda wake.

Makusudio ni kuhimiza kuandika deni bila ya kutofautisha uchache wake au wingi wake, maadamu lengo ni kuchunga kusitokee tofauti na mizozo.

Haya ndiyo uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu na imara sana kwa ushahidi na ni karibu zaidi kutofanya shaka.

Yaani kuandika deni na kulishuhudilia ndiyo bora na imara na ni karibu zaidi kuondoa shaka.

Unaweza kuuliza: Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameamrisha kuandika. Kwanza, katika kauli yake: "Basi iandikieni"Pili. "Wala msichoke kuandika" Tatu, ameishiria hekima ya hilo, kwamba kuandika ndio bora na imara. Lakini pamoja na yote hayo mafaqihi wamefutu kuwa ni suna kuandika, sio wajibu. Wameendelea nalo hilo tangu zamani mpaka sasa. Nasi tuko pamoja nao kwa hilo, lakini kuna jambo jengine lisilokuwa kuandika deni na kulishuhudia, nalo ni kuwa mafaqihi wamewajibisha kadhi kuhukumu kwa mujibu wa ubainifu wenye uadilifu, hata kama hakupata kujua kitu kutokana na ubainifu huo.

Na hilo si ni kufuata tamko tu? Jambo ambalo mafaqihi hawakulifuata, katika suala la kuandika, kuwa ni njia ya kuthibitisha, kama ubainifu, wakasema: "Haijuzu kuhukumu kwa maandishi mpaka akipata kujua kitu kutokana na maandishi na aridhike." Je, amri hii iliyokaririka haifahamishi kuwa kuandika ni njia ya kuthibisha haki.?

Jibu: Amri ya kuandika deni ili kuilinda haki kwenye kuthibiti, ni jambo moja, na kuzingatia ubainifu wenye uadilifu kuwa ni njia ya kuthibitisha haki, ni jambo jengine. Kwa hiyo ni wajibu kuhukumu kwa mujibu wa ubainifu, sawa awe mwenye kuhukumiwa amekiri au amekanusha.

Ama kuandika hapana budi kuulizwa mshtakiwa, akikiri, basi litakuwa ni suala la kukiri, na kama akikanusha, basi utahitajika uthibitisho kujaribu kupata uhakika kwa uchunguzi kwa kutumia njia nyingine; kama vile ushahidi, yamini au na kulinganisha hati ya mwandishi. Kwa hivyo basi maandishi peke yake hayatoshi, kuwa ni njia inayojitegemea.

Ila ikiwa ni biashara ya mkono kwa mkono mnayopeana baina yenu, basi si vibaya kwenu msipoiandika.

Hapa maneno yanahusu biashara ya mkono kwa mkono na ruhusa ya kuacha kuandika. Biashara ya mkono kwa mkono ni ile biashara ya kupeana muda huo huo. Maana ya mnayoopeana baina yenu, ni kutoka mkono moja hadi mwengine, muuzaji anachukua thamani kutoka kwa mnunuzi na mnunuzi naye anachukua kile kilichotolewa mali kutoka kwa muuzaji.

Maana ya Aya kwa ujumla, ni kwamba si vibaya kuacha kuandika katika biashara ambayo thamani yake inatolewa muda huo huo.
Ama siri ya kuacha kuandika, ni kwamba biashara hii hufanyika mara kwa mara kati ya watu; lau wangelikalifishwa kuandika kwa kila biashara, basi kungalikuwa na mashaka kwao hasa katika vitu vidogo.

Vyovyote itakavyokuwa ni kwamba sheria tukufu imewaachia watu mambo ya biashara kwa kiasi cha maslahi yao. Ikiwa maslahi yako kwenye kuandika, basi na waandike; kama ilivyo katika biashara ya viwanja, magari, n.k. Na, kama maslahi ni kuacha kuandika, kama biashara ya vyakula na mavazi, basi na waache.

Mwenyezi Mungu alipoamrisha kuandika deni na biashara au kuruhusu kuacha ni amri ya kupendekeza na kuongoza kwenye mambo ambayo yatawaepushia tabu na matatizo. Hata hivyo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawakataza na kuharamisha hadaa, riba na kula mali kwa batili bila ya kutoa chochote.

Unaweza kuuliza; Kusema kuwa si vibaya kuacha kuandika biashara ya mkono kwa mkono inafahamisha kuwa ni vibaya kuacha kuandika deni. Kwa hivyo basi, kuandika deni ni wajibu kinyume na wanavyosema mafaqihi kuwa ni suna na wala si wajibu.

Jibu: Makusudio ya kauli Yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) "Basi si vibaya kwenu msipoiandika," ni kukanusha ubaya na madhara ya kidunia, sio kukanusha dhambi na madhara ya kiakhera na kuwa kuandika ni wajibu.

Na wekeni mashahidi mnapouziana

Mafaqihi wote wameafikiana kuwa kushuhudia biashara ni sunna sio wajibu, isipokuwa watu wa madhehebu ya Dhahiri (Dhahiriya) wanasema ni faradhi sio sunna, kwa kuchukulia dhahiri ya tamko.

Wala asitiwe tabu mwandishi wala shahidi

Wanaouziana wakiafikiana kuandika na ushahidi basi ni juu ya mwandishi kuandika kwa uadilifu na shahidi kushuhudia kwa haki. Yamekwishatangulia maelezo kuhusu asitiwe tabu, katika kufasiri Aya ya 233.

Na kama mkifanya hivyo; basi hakika hilo ni ufasiki kwenu.

Ufasiki ni kutoka katika twaa ya Mwenyezi Mungu; na kila anayefanya kitu kilichokatazwa na Mwenyezi Mungu au kuacha kitu kilichoamrishwa na Mwenyezi Mungu, basi huyo ni fasiki aliyetoka katika twaa ya Mwenyezi Mungu mwenye kustahili ghadhabu na adhabu Yake.

Na Mcheni Mungu.

Kwa kutii amri Zake zote na makatazo yake yote.

Na Mwenyezi Mungu anawaelimsha; na Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.

Anawaelimisha yale yaliyo na heri kwenu katika dini na dunia. Kimsingi ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hatufundishi Yeye moja kwa moja; wala haitii elimu katika akili zetu na nyoyo zetu; isipokuwa anatuelimisha kupitia wahyi anaouteremsha kwa Mitume Wake.

Wahyi huu unakusanya kila lile lililo na mwongozo na kutuongoza kwenye maslahi yanay- odhamini kudumu kwetu na utangamano wetu.

Usufi

Masufi wote au baadhi wanasema hakuna njia ya maarifa na kumjua Mwenyezi Mungu na wahyi Wake na sharia na siri Zake isipokuwa kwa imani na takua (kumcha Mungu). Mwenye kumcha Mwenyezi Mungu, basi ndio amemjua na amejua sharia Yake na hukumu Zake; na ndio ameijua akhera na vituko vyake.
Vilevile atakuwa ameifahamu Qur'an na Hadith bila ya darasa au taaluma yoyote. Hii wanaiita elimu ya ki-Mungu na wakatoa dalili kwa kauli Yake Mwenyezi Mungu:

Na mcheni Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu anawaelimisha.

Lakini tamko la Aya linakataa dalili hii. Kwa sababu lau ingelikuwa kama walivyosema basi, kinahw, tamko Yuallimukum lingejazimishwa kuwa ni jawabu la Ittaqu na lingeambatanishwa na herufi Fai na wala sio kwa herufi Wau.

Zaidi ya hayo maana katika fikra ya kauli hii ya kisufi, inafanana na kauli ya mtu aliyepagawa akisema: "Hakika nyumba haitimii kujengwa ila baada ya kukaliwa, na kwamba nguo haikamiliki kushonwa ila baada ya kuvaliwa."

Sijui Masufi wanadai vipi hali hii; na hali imekuja hadith mutawatir kutoka kwa Mtume (s.a.w.) inayosema: "Tafuteni elimu japokuwa China" na" Elimu ni kwa kujifundisha". Sisi hatuna shaka kabisa kwamba nadharia inadhihirika kwa kufuatilia na kutenda, na kwamba mtaalamu mwenye kufanya kazi, hufungukiwa na mambo mapya. Lakini hili ni jambo jengine na kuwa taqwa ni nyenzo ya maarifa ni jambo jengine.

Na kama mkiwa safarini na hamkupata mwandishi, basi ni itakayo kabidhiwa rahani

Baada ya Mwenyezi Mungu kuamrisha kuandika deni kwa ajili ya kulihifadhi, amejaalia rahani ndio tegemeo badala ya kuandika, kama kukiwa na udhuru.

Mafaqihi wameafikiana kwamba rahani haitimii bila kukabidhiana. Wametoa dalili kwa kauli hii: "Basi ni rahani itakayokabidhiwa" Ufafanuzi uko katika vitabu vya Fiqh; kama vile Fiqhul Imam Jaffar Sadiq Juzuu ya 4.

Unaweza kuuliza: Rahani inajuzu katika safari na nyumbani, na pamoja na kupatikana mwandishi au kukosekana; sasa nini makusudio hapa ya kuleta sharti la safari na kukosekana mwandishi?

Baadhi ya wafasiri wamelipuuza swali hili, ingawaje linaweza kumjia kila mwenye kujua hukumu za sheria. Wengine wamejibu kuwa Mwenyezi Mungu amepitisha kwa aghlabu, kwa kuwa wakati huo ilikuwa ni nadra kupatikana mwandishi safarini. Lakini iinavyoonekana ni kwamba pia aghlabu ni kukosekana rahani katika safari. Kwani ni nani anayechukua vitu vinavyoweza kuwekwa rahani katika safari, isipokuwa kwa nadra tu?

Jibu: sahihi ni kwamba Aya kwa dhahiri inafahamisha kutojuzu rahani nyumbani, kwa kuchukulia kuwa sharti limefahamika; yaani kama hamko safarini basi hakuna rahani. Lakini dhahri hii haijuzu kuitegemea baada ya kuthibiti kwamba Mtume (s.a.w.) aliyeshukiwa na wahyi, hakuitumia dhahiri hiyo.

Yeye aliwahi kuweka rahani deraya yake kwa myahudi alipokuwa nyumbani Madina. Wala hii sio Aya pekee ambayo tunaiacha dhahiri yake kwa Sunna ya Mtume.

Na ni kwa sababu hii ndipo umma wa kiislam umesema, kwa kauli moja, kwamba haijuzu kuchukulia dhahiri ya Aya katika Aya za hukumu ya sharia, ila baada ya utafiti wa Hadith za Mtume zilizopokewa kutolea dalili Aya Tukufu.

Na kama mmoja wenu akimwamini mwengine,basi aliyeaminiwa atekeleze uaminifu wake, na amche Mungu, Mola wake

Yaani mdeni akiwa na dhana nzuri kwa mdaiwa, akampa bila ya cheti wala rahani au ushahidi wowote wa kutegemea, basi ni juu ya mdaiwa aiendeleze ile dhana nzuri na amrudishie mdai haki kamili.

Zaidi ya hayo hukumu hii ni ya ujumla haihusiki na deni tu, bali inachanganya amana zote. Mwenyezi Mungu amesema "Hakika Mwenyezi Mungu anawaamrisha kutekeleza (kuzirudisha) amana kwa wenyewe..." (4:58)

Mtume naye anasema: "Msiangalie Swala ya mtu na Saumu yake, na wingi wa Hijja zake na umaarufu wake; na kuvuma kwake usiku, lakini angalieni ukweli wa mazungumzo yake na utekelezaji wake wa amana."

Imam Zainul Abidini (a.s.) anasema: "Lau kwamba aliyemuua baba yangu ananiwekea amana upanga aliomuulia baba yangu, basi nitamrudishia."

Wala msifiche ushahidi. Na atakayeuficha, basi hakika moyo wake ni wenye kuingia dhambini

Kuna tofauti kati ya kuchukua ushahidi na kuutekeleza. Maana ya kuuchukua ushahidi ni kuitwa ushuhudie haki au deni. Hapa kukubali ni wajib kifaya (wa kutosheana) na wala sio wajib ayni; kama tulivyyoeleza huko nyuma. Ama kuutekeleza ni kukuita mwenye haki baada ya wewe kuuchukua ushahidi, ili utoe katika mahakama; hapa huwezi kukataaa ikiwa haki haitaweza kuthibiti bila ya ushahidi wako, na kukawa hakuna madhara. Kama hutafanya basi utakuwa na dhambi kutokana na kauli Yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) "Wala msifiche ushahidi"

Na makusudio ya moyo wake kuingia dhambini, ni kwamba yeye ataadhibiwa adhabu ya kukusudia dhambi, kwa sababu kukusudia ni katika sifa za moyo.

لِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ وَإِنْ تُبْدُوا مَا فِي أَنْفُسِكُمْ أَوْ تُخْفُوهُ يُحَاسِبْكُمْ بِهِ اللَّهُ ۖ فَيَغْفِرُ لِمَنْ يَشَاءُ وَيُعَذِّبُ مَنْ يَشَاءُ ۗ وَاللَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ {284}

Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Na kama mkidhihirisha lililo katika nafsi zenu, au mkilificha, Mwenyezi Mungu atawataka hisabu ya hilo; kisha amghufirie amtakaye, na amwadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
  • 1. Tofauti ya maneno haya mawili ipo katika lugha ya kiarabu, kama ilivyoelezwa-mfasir