read

Aya 284: Kama Mkidhihirisha Yaliyomo Katika Nyoyo Zenu

Maana

Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Na kama mkidhi- hirisha lililo katika nafsi zenu, au mkilificha, Mwenyezi Mungu atawataka hisabu ya hilo.

Mara nyingine katika moyo wa mtu hupita mawazo mabaya asiyowezea kuyazuia; kama vile kutamani kubomoka nyumba ya fulani au akanyagwe na gari. Katika mawazo kama haya hakuna hisabu wala adhabu, maadamu ni mawazo tu yasiyoonekana athari ya vitendo au maneno yake. Kwa sababu haya yako nje ya uwezo, kukalifishwa nayo ni kukalifishwa yasiyowezekana.

Mara nyingine mtu huazimia maasi kabisa na kukusudia kuyafanya, mpaka anapokurubia kuyafanya, basi hurudi nyuma, ama kwa kumwogopa Mwenyezi Mungu au kuogopa watu. Basi ikiwa ni kwa kumwogopa Mwenyezi Mungu hupata thawabu, kwa sababu kunahisabiwa ni kutubia. Na, kama ni kwa kuwaogopa watu, basi hakuna malipo yoyote, si thawabu wala adhabu, kwa fadhila za Mwenyezi Mungu na ukarimu wake.

Kuna Hadith inayosema: "Mtu akikusudia wema na kisha asiufanye huandikiwa wema mmoja; na kama akiutenda, huandikiwa kumi. Na kama akikusudia uovu akaufanya, hundikiwa ovu moja, na kama hakuufanya, basi haandikiwi chochote."

Mara nyingine mtu huazimia kufanya maasi, na kuyafanya kwa vitendo. Maasi haya yako aina mbili: Kwanza ni kumwasi Mwenyezi Mungu waziwazi, bila ya kujali maneno ya watu na lawama zao. Hayo ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na kama mkidhihirisha yaliyomo katika nafsi zenu."
Aina nyingine ni ya kuficha maasi kwa unafiki na ria kufanya ufisadi kwa kujificha na kutangaza wema. Aina zote hizo anazijua Mwenyezi Mungu.

Kisha amghufirie amtakaye na amwadhibu amtakaye

Maadamu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni mfalme wa mbingu na ardhi Muweza wa kila kitu, asi anao uweza wa kusamehe amtakaye katika uasi na kumwadhibu amtakaye kutokana na inavyohukimilia hekima Yake. Muhyiddin Ibn al Arabi anasema katika tafsiri yake kwamba Mwenyezi Mungu anamsamehe mwasi akiwa ana nguvu katika imani yake, lakini akawa amezukiwa tu kufanya maasi, sio kuwa yameota mizizi katika nafsi yake, na humwadhibu muasi aliye mdhaifu wa imani ambaye maasi yameota mizizi katika nafsi yake.

آمَنَ الرَّسُولُ بِمَا أُنْزِلَ إِلَيْهِ مِنْ رَبِّهِ وَالْمُؤْمِنُونَ ۚ كُلٌّ آمَنَ بِاللَّهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِنْ رُسُلِهِ ۚ وَقَالُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۖ غُفْرَانَكَ رَبَّنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ {285}

Mtume na Waumini, wote wameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake, na wamemwamini Mwenyezi Mungu na Malaika Wake na Vitabu Vyake na Mitume Wake: Hatutofautishi baina ya yoyote katika Mitume wake. Na husema: Tumesikia na tumetii. Twaomba maghufira yako Mola wetu! Marejeo ni Kwako.

لَا يُكَلِّفُ اللَّهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ ۗ رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِنْ نَسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تَحْمِلْ عَلَيْنَا إِصْرًا كَمَا حَمَلْتَهُ عَلَى الَّذِينَ مِنْ قَبْلِنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تُحَمِّلْنَا مَا لَا طَاقَةَ لَنَا بِهِ ۖ وَاعْفُ عَنَّا وَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا ۚ أَنْتَ مَوْلَانَا فَانْصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ {286}

Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila uweza wake. Faida ya yale iliyoyachuma ni yake na hasara iliyochuma ni yake. Mola wetu! Usituadhibu tukisahau au tukikosa. Na usitutwike mzigo kama uliyowatwika wale waliokuwa kabla yetu. Mola wetu! Usitutwike tusiyoyaweza na utusamehe na utughufurie na uturehemu wewe ndio Mola wetu na utunusuru na watu makafiri.