read

Aya 285 – 286: Mtume Ameamini

Lugha

Makosa hutumiwa kwa maana tatu: Dhambi, kutokusudia, na kutofanya sawa. Maana hii ya mwisho, ndiyo iliyokusudiwa katika Aya.

Maana

Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake.

Hapa kuna swali linalojitokeza - kwamba kila Mtume anaamini wahyi ulioteremshwa kwake, vinginevyo hatakuwa Mtume. Kwa hiyo kulielezea hili kunafanana na kuliweka wazi ambalo tayari liko wazi, na kujaribu kulipata ambalo lipo, jambo ambalo haliwezekani katika maneno ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa hiyo hapana budi kuwe na lengo la kulielezea hilo. Ni lipi basi?

Jibu: Lengo sio tu kueleza kuwa Mtume (s.a.w.) amemuwamini Mwenyezi Mungu hapana! Kwani kila Mtume anazaliwa akiwa amemwamini Mwenyezi Mungu na Umoja wake, lakini sio kila Mtume anazaliwa akiwa Mtume, au kujua kuwa yeye ni Mtume isipokuwa Nabii Isa (a.s.) ambaye mara tu alipozaliwa alisema: "Hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu, amenipa kitabu na amenifanya Nabii" (19:30)

Muhammad (s.a.w.) hakushukiwa na wahyi mpaka alipofika miaka arobaini katika umri wake mtukufu. Alipoambiwa na Jibril mara ya kwanza "Soma kwa jina la Mola wako ambaye ameumba" (96: 1) Alitia shaka na akahofia isije ikawa sauti ile ni wasiwasi na mawazo tu, mpaka akamwambia mkewe mpenzi, Khadija, aliyekwenda naye kwa Waraqa bin Naufal; kisha akampa maelezo ya kutosha kwamba aliyemjia ni Malaika wala sio shetani.
Kwa hivyo basi inatubainikia kuwa lengo katika kauli yake Mwenyezi Mungu; "Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake" ni kwamba yaliyokuja katika Sura hii na mengineyo katika misingi ya imani na itikadi, maonyo, hukumu na kila aliyoyatolea habari Mtume, ni katika wahyi wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Na wahyi huo hakuuamini Mtume ila baada ya kupitiwa na shaka, utafiti na kuchunguza vizuri; na baada ya kufunuliwa na uhakika kabisa. Kwa hiyo kila analolielezea Mtume, basi linatoka kwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka yoyote.

Maelezo

Maulama wengi wa Kishia hawakubaliani na usahihi wa Kisa hiki, miongoni mwao ni Mwanachuoni Sayyid Muhammad Hussein Tabatabai katika Tafsir Al-Mizani anasema katika kufasiri sura ya Alaq (97:1), baada ya kutaja kisa cha Waraqa bin Naufal: Kisa hiki hakiwezi kuepukana na shaka. Kinachodhoofisha usahihi wake ni shaka ya Mtume (s.a.w.w.) kwa Wahyi wa Mwenyezi Mungu na kusitasita kwake na kudhani eti amezugwa na shetani?!

Linalotia shaka zaidi ni kwamba yeye alipata uhakika wa Utume wake kutoka kwa Mkristo na hali Mwenyezi Mungu anasema katika Qur'ani "Sema mimi nina dalili ya wazi itokayo kwa Mola wangu" (6:57) sasa dalili ya wazi ni kauli ya Waraqa? Na Aya isemayo.

"Sema hii ndiyo njia yangu, ninailingania kwa Mwenyezi Mungu kwa ujuzi, mimi na wanaonifuata" (12:108) Je, ujuzi ndio huo alioupata kwa Waraqa? Na ujuzi wa wale wanaomfuata unatokana na kumfuata yeye asiyekuwa na uhakika? "Mwenyezi Mungu anasema tena "Hakika sisi tumekuletea Wahyi kama tulivyompelekea Wahyi, Nuh na Manabii baada yake." (4:163)

Je, hao Mitume wengine kupata kwao wahyi kulitegemea watu kama kina Waraqa?.

Ilivyo ni kuwa wahyi wa utume nilazima uwe na uhakika kutoka kwa Mtume mwenye kuwa unatoka kwa Mwenyezi Mungu.

Katika kufasiri Aya hii (Ameamini Mtume) mwenye Tafsir Al-Mizan anasema: Ni kusadikisha imani ya Mtume na waumini Amewekwa peke yake Mtume kisha akaunganishwa na waumini kwa kumtukuza.

Hii ni desturi ya Qur'an katika maelezo yanayohusiana na kumtukuza Mtume kumtaja yeye kwanza kisha kufuatishia wengine; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

"Basi hapo Mwenyezi Mungu aliteremsha utulivu wake juu ya Mtume wake na Waumini" (48:26)
"Siku ambayo Mwenyezi Mungu hatamfedhehesha Mtume na wale walioamini pamoja naye." (66:8)

Kwa ujumla sura ya Baqara imeanzia kwa kueleza sifa wanazostahiki kuwa nazo wachamungu. Kama vile kuamini ghaib, kuswali, kutoa, kuamini Mitume na akhera, kinyume na makafiri na wanafiki.

Kisha ikaelezea hali ya watu wa kitabu; hasa Mayahudi ambao Mwenyezi Mungu aliwa- neemesha kwa neema mbali mbali, lakini wakakufuru badala ya kushukuru. Hivyo Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa aina mbali mbali za adhabu; kama kujiua, kugeuzwa kuwa manyani , kushuka vimondo adhabu kutoka mbinguni n.k

Mwisho sura inaelezea wasifu wa Mtume na wafuasi wake kwamba wao ni kinyume na watu wa Kitab walivyoikabili neema ya Mwenyezi Mungu. Wamesikia na kutii, hali ya kumwamini Mwenyezi Mungu, Malaika wake, Vitabu Vyake na Mitume Yake bila ya kum- bagua yeyote katika Mitume.

Na waumini; wote wamemwamini Mwenyezi Mungu na Malaika wake na vitabu vyake na Mitume wake: Hatutofautishi baina ya yoyote katika Mitume wake

Maana kamili ya kumwamini Mwenyezi Mungu sio kuitakidi kwamba Yeye ni Muumbaji wa ulimwengu tu, hapana, mumin wa kweli ni yule anayemwamini Mwenyezi Mungu na Mitume na vitabu vilivyoteremshiwa wao pamoja na yaliyomo ndani yake, ikiwa ni pamoja na misingi, hukumu, Malaika na mengineyo katika mambo ya ghaibu, bila ya kuacha mengine.
Mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu bila ya kuamini Vitabu Vyake na Mitume wake, au kuamini baadhi ya Vitabu Vyake na Mitume Wake, hukumu yake kesho mbele ya Mwenyezi Mungu ni hukumu ya asiyeamini kabisa.

Lau watu wa dini wangelichukua misingi ya kumwamini Mwenyezi Mungu na kila alilolileta, basi kusingekuwa na makundi na migogoro; lakini wao wameamini baadhi na wakakanusha baadhi, ndipo kukawa na uadui huu wa kuendelea.

Mwenyezi Mungu hakalifishi nafsi yoyote ila uweza wake.

Kwa sababu kukalifisha bila ya uwezo ni dhulma "... Na kwamba Mwenyezi Mungu si dhalimu kwa waja." (3:182) Lakini Ashaira wamejuzisha taklifa bila ya uwezo. Shia Imamiya na Muutazila wamekanusha.

Faida ya yale iliyoyachuma ni yake; miongoni mwa kheri. Na hasara ya iliyochuma ni yake. Miongoni mwa shari na maovu.

"Mwenye kufanya heri sawa na chembe ataiona. Na mwenye kufanya shari sawa na chembe ataiona" (99: 7 -8)

Miongoni mwa rehema za Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni kwamba mja akifanya wema humwandika hapo hapo, lakini akifanya uovu, humpa muda, akiomba msamaha na kujuta, hamwandikii kitu.

Baadhi ya wataalamu wanasema: Mtu hufanya wema kwa msukumo wa nafsi yake, kwa sababu ndio umbile lake; na hafanyi shari isipokuwa kwa vichocheo vya nje kama vile mazingira na malezi mabaya.

Kwa hali hiyo ndio maana Mwenyezi Mungu akatumia neno Kasaba katika heri lenye maana ya kuchuma tu na akatumia neno Iktasaba katika shari lenye maana ya kuchuma zaidi.

Mola wetu! Usituadhibu tukisahau au tukikosa.

Hapa kuna mushkeli mashuhuri ambao umezungumzwa sana na umejaribiwa kujibiwa katika elimu ya Usul na Tawhid. Mushkeli wenyewe kwa ufupi ni kwamba kukosea na kusahau hakuko chini ya matakwa ya mtu na uwezo wake. Kwa hiyo kuadhibiwa hakuko; kwa mfano mwenye kusahau kuswali au akakosea katika kufahamu hukumu ya sharia, anahukumiwa kuwa na udhuru. Kwa hivyo basi hakuna maana wala haja ya kuomba kuondolewa adhabu.

La kustaajabisha ni jinsi alivyojibu Sheikyh Muhammad Abduh - kama alivyonakili mwenye Tafsiri ya al Manar - kwamba mwenye kusahau na mwenye kukosea inafaa kuadhibiwa kwa dalili ya sharia ya kiislamu na sharia zilizowekwa na binadamu, ambazo zimewajibisha kulipa mtu aliyeharibu mali ya mwingine kwa makosa, kama aliyeuwa kimakosa.

Kushangaza kwake ni kwamba, makusudio ya kuadhibiwa katika Aya ni adhabu na majukumu ya kitabia, sio gharama. Kwa hiyo anayemuua mtu kimakosa au kuharibu mali kwa makosa haadhibiwi wala haulizwi kitu upande wa kitabia; isipokuwa atahukumiwa kulipa gharama ya kimali tu, sawa na mtu anayedaiwa.

Jibu sahihi ni kwamba kukosea na kusahau mara nyingine humtokea mtu baada ya kujichunga. Aina hii ndiyo ambayo mtu husamehewa wala haifai kumwadhibu.. Hayo ndiyo makusudio ya Aya tukufu. Na pengine kosa na kusahau hutokea kwa sababu ya kuzembea na kuacha kujihifadhi, kwa namna lau angezindukana na kujilinda hayangemtokea. Aina hii huwa mtu hasamehewi na inafaa kumwadhibu. Hilo, katika dua, ndilo linaloombwa liondolewe. Kwa hiyo hapo hakuna mushkeli tena.

Mola wetu! Wala usitutwike mzigo kama uliyowatwika wale waliokuwa kabla yetu. Mola wetu! Usitutwike tusiyoyaweza.
Makusudio ya mzigo hapa ni taklifa na mashaka. Mwenyezi Mungu aliwatwika wana wa Israil, pale alipowaamrisha kuswali Swala hamsini mchana na usiku na katika taklifa za mashaka ambazo wamezitaja wafasiri walipofasiri: "Kama ulivyowatwika wale waliokuwa kabla yetu" Kwa hivyo maana yanakuwa usitukalifishe yaliyo mazito.

Unaweza kuuliza: Kauli ya Mwenyezi Mungu; "usitutwike tusiyoyaweza" ina maana sawa na "usitutwike mzigo" ambapo hapo ni kuunganisha jumla zenye maana sawa?

Jibu:Kama tukiangalia jumla ya"usitutwike tusiyoyaweza" kuwa ni jumla mbali iliyoepukana na mfumo wa maneno, basi itakuwa hivyo.

Kwa sababu maana ya dhahiri ni usitutwike yaliyo na mashaka na sisi. Lakini tukiangalia kuwa iko pamoja na mfumo mzima wa maneno, itakuwa na maana ya: Usituadhibu adhabu tusiyoweza.

Kwa hiyo ikafasiriwa adhabu kuwa ni lile linalopelekea adhabu tusiyoiweza na kuivumilia. Sheikh Murtadha al Ansari katika kitabu chake kinachoitwa al Rasail mlango wa Baraa anasema: "Sio mbali kuwa makusudio ya tusiyoyaweza katika Aya ni adhabu na mateso, kwa hiyo maana ya usitutwishe tusiyoyaweza ni usitupe adhabu tusiyoiweza."

Na utusamehe na utughufurie na uturehemu

Msamaha, maghufira na rehema ni matamko yenye kukurubiana, tofauti ni ndogo kwamba msamaha ni kutoadhibiwa tu; maghufira ni kutoadhibiwa na kusitiriwa dhambi, na rehema ni kutaka kufadhiliwa na kuneemeshwa kwa thawabu.

Wewe ndiwe Mola wetu na utunusuru na makafiri.

Ambao wanaidharau dini ya Mwenyezi Mungu,na kumtukuza asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Katika Majmau imeelezwa kuwa imepokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.) kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) katika kila kifungu cha dua hii husema: "Nimefanya na nimeitikia (maombi)." Kwa hivyo basi ndipo ikawa sunna kusoma sana dua hii:

"Mola wetu! Usitutese kama tukisahau au tukikosea. Na usitutwike mzigo kama ulivyowatwika wale waliokuwa kabla yetu. Mola wetu! Usitutwike tusiyoyaweza na utusamehe na utughufirie na uturehemu wewe ndiwe Mola wetu na utunusuru na watu makafiri."