read

Aya 31-32: Kumpenda Mwenyezi Mungu

Maana

Sema: Ikiwa mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni.

Yeyote anayempenda Mwenyezi Mungu, analazimika kumpenda Mtume wa Mweneyezi Mungu na Ahlu Bait wake, kwa sababu Mtume anawapenda. Na yeyote anayempenda Mtume, analazimika kumpenda Mwenyezi Mungu, Mapenzi hayo mawili hayaachani. Mwenyezi Mungu anasema: Mwenye kumtii Mtume basi ndio amemtii Mwenyezi Mungu (4:80)

Kwa sababu Mtume ndiye anayemsemea Mwenyezi Mungu na ndio ubainifu wake; vinginevyo mtu atakuwa ni adui. Yaani mwenye kufanya uadui na Mtume na Aali zake, basi ndio amejiwekea uadui na Mwenyezi Mungu, atake asitake. Kwa hivyo watu wa dini nyingine ambao wanalingania imani ya Mungu kisha wanamfanyia uadui Muhammad (s.a.w.) basi wao ndio maadui zaidi katika maadui wa Mwenyezi Mungu.

Kama mtu atasema kuwa kutojua kwao utume wa Muhammad ni udhuru; basi jibu ni kuwa hakuna udhuru kabisa kwa yule anayefuata mapenzi yake na akawa anawafuta tu mababu zake, isipokuwa baada ya kuthibitisha na kuangalia dalili zote juu ya utume wa Muhammad. Na, yeyote atakayeangalia dalili hizi kwa mtazamo wa uadilifu na kuchunga haki, ataamini na kunyeyekea. Hakuna maana ya pendo la mdogo kwa mkubwa na mtumishi kwa bwana wake, isipokuwa ni utii na kufuata.

Na, kila anayependa yale anayoyachukia Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na akachukia yale anayoyapenda Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, basi yeye ni adui wa Mungu na Mtume wake; hata kama atafikiriwa kuwa ni katika wapenzi. Kwa sababu yale yanayodhaniwa kwake kuwa yeye ni mpenzi bila ya kuwako na athari yoyote, haya yatakuwa njozi tu.

Sema: Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume, na wakikataa, basi hakika Mwenyezi Mungu hawapendi makafiri.

Dhahiri ya Aya hii inaonyesha kuwa hakika ya dini ni kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, na kwamba kuuacha utiifu huo kunalazimisha ukafiri, bali ni ukafiri hasa kwa dhati yake, kutokana na kauli yake hiyo: "Na wakikataa, basi hakika Mwenyezi Mungu hawapendi Makafiri."Na wala hakusema hakika Mwenyezi Mungu hawapendi waasi au atawaadhibu, kwa maana kuwa Mungu ameuzingatia uasi kuwa ni ukafiri, sio sababu ya ghadhabu na adhabu tu.

Jambo hili lina hatari na kuhofisha sana, kiasi ambacho hawatabakia kwenye dini na kwenye uislamu isipokuwa wachache kabisa, ila ikiwa makusudio ya ukafiri hapa ni uasi; kama ilivyo katika Aya hii:
Na ni haki ya Mwenyezi Mungu juu ya watu kuhiji Nyumba hiyo kwa mwenye kuweza njia ya kuendea na anayekufuru basi Mwenyezi Mungu si mhitaji kwa walimwengu (3:97)

Kwa hali yoyote iwayo, sisi tunaamrishwa kidini na kisharia kumtendea kiislamu kila mwenye kutamka shahada mbili, kama vile urithi, ndoa, utwahara, na kulinda mali na damu yake. Yasiyokuwa hayo ataachiwa mwenyewe Mwenyezi Mungu (s.w.t.) sisi hatuna majukumu nayo.

إِنَّ اللَّهَ اصْطَفَىٰ آدَمَ وَنُوحًا وَآلَ إِبْرَاهِيمَ وَآلَ عِمْرَانَ عَلَى الْعَالَمِينَ {33}

Hakika Mwenyezi Mungu alimchagua Adam na Nuh na watoto wa Ibrahim na watoto wa Imran juu ya walimwengu wote.

ذُرِّيَّةً بَعْضُهَا مِنْ بَعْضٍ ۗ وَاللَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ {34}

Kizazi cha wao kwa wao na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.

إِذْ قَالَتِ امْرَأَتُ عِمْرَانَ رَبِّ إِنِّي نَذَرْتُ لَكَ مَا فِي بَطْنِي مُحَرَّرًا فَتَقَبَّلْ مِنِّي ۖ إِنَّكَ أَنْتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ {35}

Aliposema mke wa Imran: Mola wangu! Nimeweka nadhiri kwako aliyemo tumboni mwangu kuwa wakfu. basi nikubalie hakika wewe ndiwe usikiaye uliye mjuzi.

فَلَمَّا وَضَعَتْهَا قَالَتْ رَبِّ إِنِّي وَضَعْتُهَا أُنْثَىٰ وَاللَّهُ أَعْلَمُ بِمَا وَضَعَتْ وَلَيْسَ الذَّكَرُ كَالْأُنْثَىٰ ۖ وَإِنِّي سَمَّيْتُهَا مَرْيَمَ وَإِنِّي أُعِيذُهَا بِكَ وَذُرِّيَّتَهَا مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ {36}

Alipomzaa alisema: Mola wangu! Nimemzaa mwanamke - Na Mwenyezi Mungu anajua sana aliyemzaa - Na Mwanamume si kama mwanamke na nimemwita Maryam. Na mimi namkinga kwako, yeye na kizazi chake (uwalinde) na shetani aliyefukuzwa.

فَتَقَبَّلَهَا رَبُّهَا بِقَبُولٍ حَسَنٍ وَأَنْبَتَهَا نَبَاتًا حَسَنًا وَكَفَّلَهَا زَكَرِيَّا ۖ كُلَّمَا دَخَلَ عَلَيْهَا زَكَرِيَّا الْمِحْرَابَ وَجَدَ عِنْدَهَا رِزْقًا ۖ قَالَ يَا مَرْيَمُ أَنَّىٰ لَكِ هَٰذَا ۖ قَالَتْ هُوَ مِنْ عِنْدِ اللَّهِ ۖ إِنَّ اللَّهَ يَرْزُقُ مَنْ يَشَاءُ بِغَيْرِ حِسَابٍ {37}

Basi Mola wake akamkubalia kwa kabuli njema na akamkuza makuzi mema. Na akamlea Zakariya. Kila mara Zakariya alipoingia Mihrab hukuta vyakula. Akasema: Ewe Maryam unatoa wapi hivi. Akasema: Vinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila hesabu.