read

Aya 33-37: Mama Wa Maryam

Neno Maryam katika lugha ya Kiibrania lina maana ya mtumishi wa Bwana (Mola). Na Mihrabu kwa Waislamu ni pale anaposimama Imam, na kwa Wakristo ni pale wanapopaita madhabahu

Maana

Hakika Mwenyezi Mungu alimteua Adam na Nuh na watoto wa Imran na watoto wa
Ibrahim juu ya walimwengu wote.

Muhammad bin Yusuf aliye mashuhuri kwa jina la Abu Hayan Al-Andalusi, katika Tafsir yake kubwa inayoitwa Al-bahrul Muhit anasema: Amesoma Abdullah; "Na kizazi cha Muhammad juu ya viumbe wote." (Qiraa) hiki kikiwa sawa au si sawa lakini Aya ya Tat-hir inasema: Hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwaondolea uchafu watu wa nyumba (ya Mtume) na kuwatakasa kabisa kabisa." (33:33),

Inatosha kuwa Aya hii ni dalili ya kuwa Mwenyezi Mungu amekiteua kizazi cha Muhammad (s.a.w.) na cheo chao na utukufu wao,yeye ni bora wa mitume wote basi kizazi chake pia ni bora ya vizazi vyote: bali ni kwamba wanachuoni wa umati wake ni kama mitume wa Bani Israil au ni bora kuliko mitume wa Bani Israil - sikumbuki tamko la Hadith yenyewe - hasa wakiwa wanavyuoni wenyewe ni kutokana na kizazi chake kitakatifu.

Vyovyote itakavyokuwa, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameanza kwa kutaja Adam kwa sababu yeye ndiye baba wa kwanza wa watu kisha akamtaja Nuh ambaye ni baba wa pili wa watu kwa sababu wakazi wote wa duniani wanatokana na kizazi chake cha watoto wake watatu; Sam, Ham na Yafith, baada ya tufani iliyomaliza watu wote.
Mwenyezi Mungu aliwateua Adam na Nuh wao wenyewe tu, ndio maana hakutaja kizazi. Ama Ibrahim na Imran aliwateua pamoja na vizazi. Ibrahim naye ni baba wa mitume wote baada ya Nuh, kwani tangu wakati wa Ibrahim hakukuwa na Mtume ila atakuwa ametokana na kizazi chake.

Kwa dhahiri ni kwamba makusudio ya Imran ni baba wa Maryam babu wa Isa, sio baba yake Musa. Kwa sababu jina hili limekuja tena mara ya pili, aliposema; "Aliposema mke wa Imran" Mfano huu uko katika mfano wa jina linalokuja katika jumla mbili kwa muundo mmoja; kama vile kusema; Mtukuze Zedi, hakika Zedi ni mtu mwema. Kwa hiyo basi makusudio ya kizazi cha Imran ni Bwana Masih na mama yake Maryam.

Inasemekana kwamba Imran (baba yake Musa) alikuwa na bint aitwaye Maryam aliyekuwa mkubwa wa Musa; na kwamba baina ya Imran huyu na Imran babu wa Isa kuna miaka 1800. Makusudio ya viumbe wote ni kwamba kila mmoja wa waliotajwa alichaguliwa katika watu wa wakati wake tu sio kila wakati.

Kizazi cha wao kwa wao

Hakuna mwenye shaka kwamba Nuh anatokana na Adam na kwamba Ibrahim na kizazi chake wanatokana na Nuh; na Imran anatokana na Ibrahim. Kwa hiyo kulielezea hilo ni sawa na kufafanua kilichofafanuliwa, na maneno ya Mwenyezi Mungu, ni wajibu kuyachukulia kwa mfumo mzuri. Sasa nini makusudio ya habari hii?

Jibu: Makusudio sio kutoa habari kwamba wa mbele anatokana na wa nyuma, la! Isipokuwa makusudio - kama ilivyo dhahiri ya mfumo wa maneno - ni kuwasifu; na kwamba wao wanafanana katika utakatifu na ubora.

Baada ya utangulizi huu, twende kwenye kisa cha mke wa Imran, mama yake Maryam na nyanya yake Isa (a.s.). Kwa ufupi ni kwamba Qufadh bin Qubail Mwisrail, alikuwa na binti wawili mmoja akiitwa Hana aliyeolewa na Imran- ambaye ni Mwisrail vilevile - aliyemzaa Maryam. Na wa pili ni Isha aliyeolewa na Zakariya na kumzaa Yahya. Kwa hiyo Yahya bin Zakaria na Mariam mamie Isa, mama zao ni ndugu na wala sio Isa na Yahya; kama watu walivyozoea. Hivi ndivyo ilivyo katika Majmal-Bayan.

Imran akafa huku Hanna akiwa na mimba, akaweka nadhiri kuwa aliyemo tumboni awe mtumishi wa Baitul-Maqdis. Akajidhalilisha kwa kumfanyia ikhlas Mwenyezi Mungu ili aikubali nadhiri yake. Hii ilikuwa inajuzu katika dini yao wala haijuzu katika dini ya kiislamu. Yeye alikuwa akitazamia kuzaa mtoto wa kiume, kwa sababu nadhiri ya mahekalu ilikuwa maarufu kwa watoto wa kiume tu.

Alipomzaa mtoto wa kike alimwelekea Mwenyezi Mungu na kusema:"Nimezaa mwanamke… "Na mwanamume si sawa na mwanamke na nimemwita Maryam."

Mwenyezi Mungu akaikubali nadhiri ingawaje alikuwa mtoto mke. Waisrail wakabishana, kila mmoja akitaka kumlea Maryam. Ubishi ulipozidi waliafikiana wapige kura. Mshindi akawa Zakariya mume wa mamake mdogo.Wakati huo Zakariya alikuwa ndiye mkuu wa hekalu la kiyahudi. Akamshughulikia sana. Ikawa kila Zakariya anapokwenda kumtazama Maryam anakuta chakula, na walikubaliana kuwa asiendewe na yeyote, akamuuliza kwa mshangao:

Unatoa wapi hivi? Akasema: Vinatoka kwa Mwenyezi Mungu. –

Yaani moja kwa moja kutoka kwa Mungu bila ya

Hakika Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.

Hakuna mwenye kutia shaka kwamba karama hii ni ya Maryam (a.s.). Ama kukanusha karama hii kuwa ati chakula alichokuwa akikiona Zakariya kwa Maryam kilitoka kwa wafadhili wa kike waumini, ni kinyume na dhahiri ya Aya. Kwani karama hii ina ukubwa gani zaidi ya kumzaa Isa bila ya baba. Ikiwa karama hiyo ya chakula inatiliwa shaka, basi hii ya kuzaa itatiliwa shaka zaidi.
Maana ya "Akamkuza makuzi mema" ni kwamba yeye alikulia na tabia njema, kumtii Mwenyezi Mungu na kumwabudu. Imepokewa Hadith kutoka kwa Ibn Abbas kwamba Mariam alipofikia umri wa miaka tisa alikuwa akifunga mchana na kuswali usiku, mpaka akawashinda watawa. Inasemekana kwamba hakuwahi kufanya kosa lolote.

Fatima Na Maryam

Alitokewa na mfano wa karama hii bibi wa wanawake Fatima bint wa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Katika Tafsir Ruhul-Bayan ya Sheikh Ismail Haqi wakati wa kufasiri kisa cha Maryam kuhusu chakula anasema: "Mtume alishikwa na njaa katika wakati wa kahati (ukame).

Fatima akamletea mikate miwili na nyama, mara alipoona sahani imeshehenezwa mkate na nyama, alisema "umevipata wapi hivi? Akajibu: "Vinatoka kwa Mwenyezi Mungu.

Hakika Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila hisabu." Mtume akasema: "Sifa njema ni za ambaye amekushabihisha na bibi wa Bani Isriali.' Kisha Mtume akamwita Ali, Hassan, Hussein na watu wa nyumbani kwake; wakala, wakashiba na chakula kikabaki kama kilivyo, Fatima akakigawanya kwa majirani zake."

Katika kitabu Dhakhairul-Uqaba cha Muhibbudin Attabari imeandikwa kuwa, siku moja Ali alikopa Dinar ili akawanunulie chakula watu wake. Akakutana na Mikdad bin As-wad, akiwa katika hali ya mfazaiko alipomuuliza, alisema: "Nimeacha familia yangu wanalia kwa njaa." Basi Ali akampa ile dinar, akaenda zake kuswali nyuma ya Mtume.

Baada ya Swala Mtume alimuuliza Ali, "Je una chochote kwako tukale?" Kama kwamba Mtume alipewa wahyi wa kwenda kula kwa Ali. Basi Ali akawa amechanganyikiwa hana la kujibu. Mtume akamshi- ka mkono Ali wakaenda kwa Fatima, walipofika tu wakakuta chakula. Ali akasaili: "Umekipata wapi hiki?"

Mtume akasema: "Hiyo ni thawabu za Dinar; inatoka kwa Mwenyezi Mungu naye humruzuku amtakaye bila ya hisabu. Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu aliyekufanya kama Zakariya na akamfanya Fatima mfano wa Maryam. Kila mara Zakariya alipoingia Mihrab hukuta riziki." isha Muhibuddin akaongeza kusema: "Ameitoa Hadith hii Al-Hafidh Dimeshqi katika Arbaina Twiwal.

Katika Sahih Muslim mlango wa fadhila za binti wa Mtume imeelezwa kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alimwambia binti yake Fatima. "Hivi huridhii kuwa wewe ni bibi mkubwa wa waumini au bibi mkubwa wa umma huu." Anasema Seyyid Muhsin Al-Amin katika kitabu A'yanushia Juz. 2 sera ya Zahra, akimnukuu Bukhari katika Sahih yake; kwamba Mtume alisema: "Fatima ni bibi mkubwa wa wanawake wa peponi."

Vilevile Ibn Sibagh Al-Malik katika Fausulul-muhimma amemnukuu Ahmad katika Musnad akipokea kutoka kwa Mtume kwamba amesema: "Fatima ni bibi mkubwa wa wanawake wa ulimwengu."

Katika kitabu Dhakhairul-uqaba cha Muhibbuddin Attabari amesema: Siku moja Mtume alikwenda kumwangalia Fatima alipokuwa mgonjwa, akamuuliza "Waonaje ewe mwanangu?"

Akajibu: "Naumwa sana na njaa yanizidisha ugonjwa." Mtume akasema: "Ewe mwanangu huridhii kwamba wewe ni bibi mkubwa wa wanawake wa ulimwengu wote? Akasema: "Maryam bint Imran atakuwa nani basi?"

Mtume akajibu: "Yule ni bibi mkubwa wa wanawake wa wakati wake, na wewe ni bibi mkubwa wa wanawake katika dunia na akhera."

Kisha Tabari akasema kuwa Hadith hii imetolewa na Abu Umar na Al-Hafidh Abul-Kassim Dimeshqi. Ufafanuzi uliobakia utakuwa katika tafsir ya Aya 42.

هُنَالِكَ دَعَا زَكَرِيَّا رَبَّهُ ۖ قَالَ رَبِّ هَبْ لِي مِنْ لَدُنْكَ ذُرِّيَّةً طَيِّبَةً ۖ إِنَّكَ سَمِيعُ الدُّعَاءِ {38}

Pale pale Zakariya akamwomba Mola wake, akasema: Mola wangu nipe kutoka kwako mtoto mwema hakika wewe ndiwe usikiaye maombi.

فَنَادَتْهُ الْمَلَائِكَةُ وَهُوَ قَائِمٌ يُصَلِّي فِي الْمِحْرَابِ أَنَّ اللَّهَ يُبَشِّرُكَ بِيَحْيَىٰ مُصَدِّقًا بِكَلِمَةٍ مِنَ اللَّهِ وَسَيِّدًا وَحَصُورًا وَنَبِيًّا مِنَ الصَّالِحِينَ {39}

Mara Malaika wakamlingania hali amesimama akiswali kwenye Mihrab kwamba Mwenyezi Mungu anakubashiria (kupata mtoto) Yahya atakayekuwa mwenye kusadikisha neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu na Bwana na mtawa na Nabii anayetokana na watu wema.

قَالَ رَبِّ أَنَّىٰ يَكُونُ لِي غُلَامٌ وَقَدْ بَلَغَنِيَ الْكِبَرُ وَامْرَأَتِي عَاقِرٌ ۖ قَالَ كَذَٰلِكَ اللَّهُ يَفْعَلُ مَا يَشَاءُ {40}

Akasema: Mola wangu! Nitapataje mtoto na hali ukongwe umenifikia na mke wangu ni tasa! Akasema: Ndivyo hivyo Mwenyezi Mungu hufanya apendalo.

قَالَ رَبِّ اجْعَلْ لِي آيَةً ۖ قَالَ آيَتُكَ أَلَّا تُكَلِّمَ النَّاسَ ثَلَاثَةَ أَيَّامٍ إِلَّا رَمْزًا ۗ وَاذْكُرْ رَبَّكَ كَثِيرًا وَسَبِّحْ بِالْعَشِيِّ وَالْإِبْكَارِ {41}

Akasema: Mola wangu niwekee alama akasema alama yako ni kutozungumza na watu siku tatu isipokuwa kwa ishara tu. Na umtaje Mola wako sana na mtakase wakati wa jioni na asubuhi.