read

Aya 38-41: Zakariya

Maana

Pale pale Zakariya akamwomba Mola wake, akasema: Mola wangu nipe kutoka kwako mtoto mwema.

Tumekwishaeleza kuwa Zakariya alikuwa mume wa mama mdogo wa Maryam na kwamba yeye ndiye aliyemlea. Zakariya hakuwa na mtoto; na alipoona utengeneo wa Maryam na karama alizokuwa nazo, basi aliingiwa na mapenzi ya baba na kupenda kuzaa, Akamwomba Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu; na Mwenyezi Mungu akamwitikia maombi yake.

Mara Malaika wakamlingania, hali amesimama akiswali kwenye Mihrabu kwamba Mwenyezi Mungu anakubashiria (kupata mwana) Yahya.

Yahya ni jina alilopewa na Mwenyezi Mungu kabla ya kuzaliwa, na hakupewa jina hilo yoyote kabla yake kama ilivyoeleza Aya ya 7 katika Sura Maryam. Kwa hiyo basi hakuna haja ya kufanya utafiiti kwamba je, jina hili ni la Kiibrania au la kiarabu, kama ilivyo katika baadhi ya tafsir.

Hata hivyo, linaingia katika lugha, kwa maana ya uhai na linanasibika jina lake pamoja na kuuhuisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) utasa wa mama yake.

Mwenye kusadikisha neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu

Inasemekana kuwa neno la Mwenyezi Mungu ni ishara ya Isa ambaye Mwenyezi Mungu amemuumba kwa neno 'Kuwa' bila ya baba. Lakini kwa ujumla neno linachukuliwa kuwa ni Aya zake zote na hukumu zake.

Mwenye Majmaul-bayan anasema kuwa Yahya ni mkubwa kuliko Isa kwa miezi sita, yeye ndiye wa kwanza kumsadiki na kushuhudia kuwa kuzaliwa kwake ni muujiza kutoka kwa Mwenyezi Mungu; na hilo lilikuwa ni nguvu ya hoja kuhusu Isa. Kwa sababu watu walikuwa wakimwamini Yahya na kumkubalia anayoyasema.

Na atakayekuwa bwana kielimu, dini na tabia njema. Na mtawa, yaani anayejizuwia na kufanya madhambi. Inasemekana ni kujizuwia na wanawake. Na Nabii atokanaye na watu wema.

Manabii wote ni wema, bali ni Maasum; na Maasum ni zaidi ya uadilifu na wema. Kwa hiyo makusudio ya watu wema ni kuwa Zakariya anatoka katika kizazi kitakatifu. Haya yanaaafikiana na kauli ya Shia kuwa wazazi wote wa mitume ni wajibu wawe wanamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.

La kushangaza ni kauli ya badhi ya wafsiri - kama katika Tafsiri ya Razi - Kwamba makusudio ya neno Mina-swalihin ni kuwa hakuna nabii isipokuwa amefanya maasi au kudhamiria kuasi isipokuwa Yahya, hakuasi wala kudhamiria kuasi.

Mbali ya kuwa kauli hii inatia dosari cheo cha Mtume Muhammad (s.a.w.), pia inapingana na akili. Kwa sababu Mtume ameletwa kuondoa maasi; kama akiasi watu watatoa hoja kuwa yeye pia anafanya. Ametakata Mwenyezi Mungu na wayasemayo wasiojua.

Akasema: Mola wangu nitapataje mtoto na hali ukongwe umenifikia na mke wangu ni tasa! Akasema: Ndivyo hivyo hivyo; Mwenyezi Mungu hufanya apendalo.

Wanasema kuwa Zakariya aliposema haya, alikuwa na miaka 120 na mkewe miaka 98. Hapa kuna swali linalojitokeza, kuwa Zakariya aliomba Mwenyezi Mungu apewe mtoto mwema ikimaanisha kuwa yeye aliomba kitu kinachowezekana katika itikadi yake, sasa vipi tena arudi kuona ajabu alipopewa habari na Malaika?

Jibu: Hiyo haikuwa ni kutia shaka au kushangazwa, isipokuwa ni kuutukuza uwezo wa Mwenyezi Mungu ambao umepetuka mipaka na kawaida; kama vile mtu anavyomwambia mtu aliyetoa sana vitu vya thamani. "Vipi umefanya jambo asilolifanya yeyote isipokuwa wewe?"

Vilevile kuadhimisha huko na kustaajabu kunakusanya shukrani kwa Mwenyezi Mungu juu ya neema hii tukufu ambayo hata hakuifikiria. Vilevile tunapata faida kutokana na muujiza huu kwamba mtu asiyalinganishe matakwa ya Mwenyezi Mungu na lile ambalo yeye analiona linawezekana au la.

Akasema: Mola wangu! Niwekee alama:

Kwa kuwa kutunga mimba ni jambo lisilojulikana upesi, alipenda Zakariya kujua itakapotungwa mimba, ili aanze kushukuru tangu mwanzo. Kwa hiyo ndio akamwomba Mola wake amjaalie alama itakayomfahamisha kutungwa mimba. Ndipo Mwenyezi Mungu akasema:

Alama yako ni kutozungumza na watu siku tatu isipokuwa kwa ishara tu na umtaje Mola wako sana na mtakase wakati wa jioni na asubuhi.

Yaani alama ya kutungwa mimba ni kuwa ulimi wako utafungika na utashindwa kuzungumza na watu isipokuwa utaelewana nao kwa ishara utakuwa kama bubu, lakini ulimi wako utafunguka kiasi unachotaka wakati unapofanya ibada. Na huu ni muujiza wa pili baada ya mimba ya tasa.

Mwenye Tafsiri Al-Manar, akimnukuu Ustadh wake Sheikh Muhammad Abduh, anasema kuwa Mwenyezi Mungu alimwamrisha Zakariya ajishughulishe na dhikr na tasbih tu muda wa siku tatu bila ya kuzungumza na watu, basi atatoa ishara, baada ya siku tatu ndio atampa.

Tafsir ya kwanza ndiyo iliyo wazi na mashuhuri zaidi.

وَإِذْ قَالَتِ الْمَلَائِكَةُ يَا مَرْيَمُ إِنَّ اللَّهَ اصْطَفَاكِ وَطَهَّرَكِ وَاصْطَفَاكِ عَلَىٰ نِسَاءِ الْعَالَمِينَ {42}

Na Malaika waliposema: Ewe Maryam! Hakika Mwenyezi Mungu amekuteua na akakutakasa na akakuteuwa juu ya wanawake wa ulimwenguni.

يَا مَرْيَمُ اقْنُتِي لِرَبِّكِ وَاسْجُدِي وَارْكَعِي مَعَ الرَّاكِعِينَ {43}

Ewe Maryam! Mnyenyekee Mola wako na usujudu na urukuu pamoja na wanaorukuu.

ذَٰلِكَ مِنْ أَنْبَاءِ الْغَيْبِ نُوحِيهِ إِلَيْكَ ۚ وَمَا كُنْتَ لَدَيْهِمْ إِذْ يُلْقُونَ أَقْلَامَهُمْ أَيُّهُمْ يَكْفُلُ مَرْيَمَ وَمَا كُنْتَ لَدَيْهِمْ إِذْ يَخْتَصِمُونَ {44}

Hizi ni habari za ghaibu tunazokupa wahyi; nawe hukuwa nao walipotupa kalamu zao nani katika wao atamlea Maryam na hukuwa nao walipokuwa wakishindana.