read

Aya 42-44: Ewe Maryam Mwenyezi Mungu Amekuteua

Maana

Na Malaika waliposema: Ewe Maryam! Hakika Mwenyezi Mungu amekuteua na akakutakasa na akakuteua juu ya wanawake wa ulimwenguni.

Kwanza Mwenyezi Mungu amemtaja mama yake Maryam, mimba na nadhiri yake; kisha akamtaja Zakariya mlezi wa Maryam; akamtaja tena Maryam na kuruzukiwa kwake na Mwenyezi Mungu bila ya hisabu. Kisha akamtaja Zakariya, maombi yake na kukubaliwa kwake maombi. Hivi sasa anarudia tena kwa Maryam kama ilivyo kawaida ya Qur'an, kuingilia suala jengine ambalo linafungamana na suala la kwanza, kisha tena kulirudia suala la pili.

Makusudio ya kuteuliwa kwa kwanza, ni kukubaliwa kuwa waqfu wa kuitumikia nyumba ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu hilo lilikuwa likihusika na wanaume, na kwa pili, ni kuzaa Mtume bila ya kuguswa na mtu yeyote. Inasemekana kuwa kuteuliwa kwa pili ni kutilia mkazo kuteuliwa kwa kwanza.

Kuhusu kutakaswa, mwenye Tafsir Al-manar anasema: "Kumefasiriwa kutakasika kwa maana ya kukosekana hedhi. Na imepokewa kuwa bibi Fatima Zahra hakutoka hedhi, na ndio maana akaitwa Zahra."

Tunaloliona kuwa lina nguvu ni kwamba kutakasika ni usafi wa Maryam, wa kutakasika na kila shubha kuhusu kuzaa kwake.

Kongamano la wanavyuoni limeafikiana kuwa Maryam hakuwa Mtume; na wala hakuna Mtume mwanamke. Mwenyezi Mungu anasema: Na hatukutuma kabla yako isipokuwa wanaume tuliowapa wahyi." (12:109).

Na utume umekoma kwa Muhammad s.a.w.w Ama kule kuzungumza na Malaika, hakumaanishi kuwa yeye ni Mtume; hata mama yake Musa pia alizungumza na Malaika; kama Aya hii isemavyo: "Na tukampa wahyi mama yake Musa ya kwamba mnyonyeshe … (28:7).

Tutafafanua zaidi kuhusu kuteuliwa Maryam Inshaallah.

Ubora Wa Qur'an Kwa Wakristo

Yametangulia maelezo kwamba ujumbe wa Kinasara kutoka Najran ulikwenda Madina kumhoji Mtume wa Mwenyezi Mungu kuhusu utume wake, huku ukilingania uungu wa Isa, Mtume akawasomea: Ewe Maryam hakika Mwenyezi Mungu amekuteua na kukutakasa."

Kusoma kwa Mtume Aya hii kwa ujumbe wa kikristo wa Najran, ambao umekuja kuhojiana naye, ni dalili ya mkato juu ya utukufu wa uislam na ukweli wa Mtume Mtukufu. mayahudi hawakuichunga haki kwa kusema uongo na kumzulia Maryam pamoja na kuleta tuhuma kuhusu kuzaliwa kwake, lakini Mwenyezi Mungu amewakadhibisha na akaandika katika kitabu chake (Qur'an) usafi wake, na akakata njia zote za uzushi.

Lau kama Muhammad hakuwa mkweli katika ujumbe wake na kutojiamini, basi angelificha hilo (la Maryam) kwa wakristo kwa namna ambayo mayahudi walimtukana Maryam na kumfanya mwongo.

Uislam kwa Aya hii umewatendea wema wakristo, wema mkubwa mno; lau si hivyo yangelisikika mengi kutoka kwa baadhi ya waislam wakati wa kugombana, kama yale yaliyosikika kwa mayahudi kuhusu Maryam mtakatifu.

Lakini mwislamu anajua kuwa utakatifu wa bibi Maryam ni sehemu ya uti wa mgongo wa itikadi yake; na kwamba kumtusi ni kufru na ni kutoka katika uislam. Yatakuja maelezo zaidi katika kufasiri Aya (5:82) Inshaallah.

Ewe Maryam! Mnyenyekee Mola wako na usujudu na urukuu pamoja na wanaorukuu.

Alimwamrisha ibada kwa kujiandaa na jambo kubwa ambalo ni kumzaa Isa (a.s.). Jambo lolote kuu ni lazima liwe na maandalizi. Pia Mwenyezi Mungu alimwamrisha kuswali na kutoa Zaka madamu yuko hai.

Hizi ni habari za ghaibu tunazokupa wahyi.

Msemo unaelekezwa kwa Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu; maana yake ni kuwa unayowaambia watu kwa ujumla na yale unayowahusisha wakristo na ujumbe wa Najran, kama vile kisa cha Maryam na mama yake, mke wa Imran na kisa cha Zakariya na Yahya, yote hayo na mengineyo hukuyasoma katika kitabu wala hukuyasikia kutoka kwa wasimulizi, kwa sababu wewe husomi na huandiki.

Yote hayo ni ujuzi wa ghaibu na ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na, hii ni hoja kwa wahasimu wako, na ni dalili ya ukweli wako. Wasimulizi kamwe hawakunukuliwa kusema kuwa ujumbe wa Najran uliweza kujibu au kupinga hoja hii.

Nawe hukuwa nao walipotupa kalamu zao nani kati yao atamlea Maryam na hukuwa nao walipokuwa wakishindana.

Kalamu ni kitu maarufu, ni ile ambayo inaandikiwa; na makusudio yake hapa ni mishale waliyokuwa wakipigia kura.

Maana kwa ujumla ni kuwa kuwafahamisha kwako habari hii na undani huu kuhusu Maryam na Zakaria, kwamba hukusoma wala kusikia, basi imebakia kuwa umeona tu, lakini inajulikana kuwa kuna mamia ya miaka kati yako na kisa hicho (hivyo hukuona). Kwa hivyo basi kujua kwako habari hizo ni kwa wahyi tu.

Kwa ufupi kisa hicho cha kutupa 'kalamu' kwa kupiga kura, ni kwamba, Hanna, mke wa Imran alipomzaa Maryam alikuwa ameweka nadhiri kuwa atumikie Baitul-Maqdis. Na alimzaa baada ya kufa baba yake (Imran). Basi makuhani na makasisi wa Israil wakashindana kuhusu atakayemlea. Hatimaye wakapiga kura ambayo ilimwangukia Zakariya, mume wa mamake mdogo. Akawa ndiye mlezi na msimamizi wake.

Nani Bibi Mkuu Wa Wanawake Wa Ulimwenguni?

Imekwishaelezwa kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimwambia Maryam: "Na akakuteua juu ya wanawake wa ulimwengu."

Aya hii imeleta kutofautiana kati ya wanavyuoni wa Kiislamu; kwamba je, Maryam binti Imran ndiye bora zaidi au Fatima binti Muhammad?

Kundi katika wanavyuoni wamesema kuwa wanawake bora ni wane Maryam binti Imran, Asiya binti Muzahim (mke wa Firaun), Khadija bint Khuwaylid na Fatima bint Muhammad. Hadith hii imetajwa katika Sahih sita; pia nimeiona katika Tafsir tabari, Razi, Bahrul-muhit, Ruheil-bayan, Maraghi na Al-Manar.
Wengine wamesema Maryam ndiye bora kutokana na Aya hii. Mashia na baadhi ya Masheikh wa Kisunni wamesema kwamba Fatima ni bora zaidi. Mwenye Tafsir Bahrul- muhit, wakati alipofasiri Aya hii: Alisema: "Baadhi ya Masheikh wetu wamesema: Yale ambayo wameyasema wanavyuoni waki- wanukuu masheikh wao ni kwamba Fatima ni bora wa wanawake waliotangulia na watakao- fuatia; kwa sababu yeye ni sehemu ya Mtume."

Wale wanaosema Fatima ni bora, wametolea dalili hilo kutokana na Hadith Mutawatir zili- zopokewa kutoka kwa baba yake akisema: "Fatima ni sehemu yangu, atakayemkasirisha ndio amenikasirisha mimi." Ama kauli yake Mwenyezi Mungu kuhusu Maryam: "Na akakuteua juu ya wanawake wa ulimwenguni," makusudio yake ni wanawake wa ulimwenguni wa wakati wake si wakati wote. Ibara hii ni maarufu na imezoeleka; kama kusema: "Fulani ndiye mshairi hodari zaidi ya watu wote." Hapo anakusudiwa kuwa ni mshairi zaidi kwa wakati alioko au kwa watu wake tu.

Mifano ya hilo katika Qur'an ni mingi, kama vile kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema kuhusu wana wa Israil: "Na tukawafadhilisha juu ya walimwengu."(45:16)

Hakuna hata mmoja aliyehitalifiana na wenzake kuwa makusudio ya Aya hii ni walimwengu wa wakati wao. Au kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na Ismail na Al-Yasan na Yunus na Lut na wote tumewafadhilisha juu ya walimwengu." (6:86)

Hakuna yeyote anayesema kuwa Lut ni bora kuliko Isa au kwamba ni sawa, au kuwa Ismail ni bora kuliko babake. Aya nyingine ni ile isemayo: "Hakika mimi nimekuta mwanamke anawatawala; naye amepewa kila kitu…" (27:23) Yaani kila kitu kwa wakati wake.

Turudie kwenye wanawake wane ambao imepokewa Hadith kwamba wao ni wanawake bora. Tukiwaangalia bila ya kutilia maanani Hadith na Aya tutaona kwamba kila mmoja kati- ka wao ana ubora wake kwa upande wake kuliko wengine.

Asiya mke wa Firauni alimwamini Mungu kwa Ikhlas akimtegemea Yeye peke Yake kuwa ndiye muhifadhi wake, wakati huo akiwa katika nyumba ya mtu mwovu zaidi kuliko yeyote, aliye kiongozi wa ukafiri na ulahidi. Akadhihirisha imani yake, hali ya kuupinga ukafiri na ufisadi wa Firaun na kupinga dhulma na utaghuti wake.

Firaun akamlaza ardhini kwa kumpigilia vigingi mpaka akafa akiwa shahidi wa haki na imani. Karama hii hawakuwa nayo wanawake wengine watatu. Bibi Maryam karama yake ni kumzaa Bwana Masih bila ya baba. Karama hii hakuwa nayo mwanamke yeyote duniani.

Bibi Khadija yeye ni wa kwanza kumwamini na kumsadiki Mtume wa Mwenyezi Mungu; akaswali yeye na Ali pamoja na Mtume (s.a.w.) - Swala ya kwanza katika uislam.

Ndiye yeye aliyejitolea mali yake kwa ajili ya kuinusuru dini hii. Hivyo kwa mali yake na himaya ya Abu Twalib uislamu ulisimama na kuimarika. Karama hii nayo hakuwa nayo mwanamke yeyote ulimwenguni.

Ama Fatima yeye ni sehemu ya Mtume, vilevile ni nafsi yake kwa umbo, tabia na taqwa; linamridhisha Mtume lile analoliridhia yeye na linamuudhi lile linalomuudhi yeye. Yeye ni mama wa Hassan na Hussein mabwana wa vijana wa peponi. Na, ni mke wa bwana wa mbingu na ardhi baada ya Mtume. Karama hii nayo hakuwa nayo Khadija (mamake) wala Asiya au Maryam.

Ama kutofautisha ubora katika karama hizi, ni kama kujaribu kutofautisha ubora kati ya waridi na asmini au kati ya mahurulain wawili. Lakini inatosha kwa Fatima awe na jambo moja tu kutokana na baba yake, ambaye ni bora ya Mitume. Katika Sahih Bukhari Juz.5 mlango wa sifa za ukoo wa Mtume, kuna Hadith ya Mtume isemayo: "Fatima ni bibi (mkuu) wa watu wa peponi."

Ikiwa Fatima ni sehemu ya Mtume, basi mumewe Ali ni nafsi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Nafsi zetu" (3:61).

Maelezo

Utafiti huu unaungana na utafiti uliotangulia katika Tafsir ya Aya 36 ya Sura hii kifungu "Fatima na Maryam."

إِذْ قَالَتِ الْمَلَائِكَةُ يَا مَرْيَمُ إِنَّ اللَّهَ يُبَشِّرُكِ بِكَلِمَةٍ مِنْهُ اسْمُهُ الْمَسِيحُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ وَجِيهًا فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَمِنَ الْمُقَرَّبِينَ {45}

Waliposema Malaika: Ewe Maryam! Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria neno litokalo kwake; jina lake ni Masih mwana wa Maryam; mwenye heshima duniani na akhera na ni miongoni mwa waliokurubishwa.

وَيُكَلِّمُ النَّاسَ فِي الْمَهْدِ وَكَهْلًا وَمِنَ الصَّالِحِينَ {46}

Na atasema na watu katika uchanga na katika utu uzima na atakuwa miongoni mwa watu wema.

قَالَتْ رَبِّ أَنَّىٰ يَكُونُ لِي وَلَدٌ وَلَمْ يَمْسَسْنِي بَشَرٌ ۖ قَالَ كَذَٰلِكِ اللَّهُ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۚ إِذَا قَضَىٰ أَمْرًا فَإِنَّمَا يَقُولُ لَهُ كُنْ فَيَكُونُ {47}

Akasema: "Mola wangu! Nitakuwaje na mtoto na hali hajanigusa mtu yeyote?" Akasema: Ndivyo hivyo, Mwenyezi Mungu huumba anavyotaka anapohukumu jambo, huliambia'kuwa'likawa.

وَيُعَلِّمُهُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَالتَّوْرَاةَ وَالْإِنْجِيلَ {48}

Na atamfundisha kuandika na hekima na Tawrat na Injili.

وَرَسُولًا إِلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ أَنِّي قَدْ جِئْتُكُمْ بِآيَةٍ مِنْ رَبِّكُمْ ۖ أَنِّي أَخْلُقُ لَكُمْ مِنَ الطِّينِ كَهَيْئَةِ الطَّيْرِ فَأَنْفُخُ فِيهِ فَيَكُونُ طَيْرًا بِإِذْنِ اللَّهِ ۖ وَأُبْرِئُ الْأَكْمَهَ وَالْأَبْرَصَ وَأُحْيِي الْمَوْتَىٰ بِإِذْنِ اللَّهِ ۖ وَأُنَبِّئُكُمْ بِمَا تَأْكُلُونَ وَمَا تَدَّخِرُونَ فِي بُيُوتِكُمْ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ مُؤْمِنِينَ {49}

Na Mtume kwa wana wa Israil. Mimi nimewajia na Ishara kutoka kwa Mola wenu, hakika mimi nitawafanyia kama namna ya ndege katika udongo; kisha nimpulizie awe ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na niwaponye vipofu na wenye mbalanga. Niwafufue wafu kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na niwaambie mnavyovila na mtakavyoweka akiba. Hakika katika haya ipo ishara kwenu mkiwa ni wenye kuamini.

وَمُصَدِّقًا لِمَا بَيْنَ يَدَيَّ مِنَ التَّوْرَاةِ وَلِأُحِلَّ لَكُمْ بَعْضَ الَّذِي حُرِّمَ عَلَيْكُمْ ۚ وَجِئْتُكُمْ بِآيَةٍ مِنْ رَبِّكُمْ فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ {50}

Na msadikishaji wa yale yaliyokuwa kabla yangu katika Tawrat, na ili niwahalalishie baadhi ya mliyoharamishiwana nimewajia na ishara kutoka kwa Mola wenu, kwa hiyo mcheni Mwenyezi Mungu na mtiini.

إِنَّ اللَّهَ رَبِّي وَرَبُّكُمْ فَاعْبُدُوهُ ۗ هَٰذَا صِرَاطٌ مُسْتَقِيمٌ {51}

Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu na ni Mola wenu basi mwabuduni. Hii ndiyo njia iliyonyooka