read

Aya 45-51: Maryam Mungu Akubashiria

Lugha

Mwenye Tafsir Bahrul-muhit amenukuu kauli saba kuhusu sababu za kuitwa Masih (mpakaji au mpangusaji):
Kupaka baraka, kupaka dini wakati wa kuzaliwa, kutwaharika na dhambi na kupanguswa na mbawa za Jibril. Vile vile kupakwa uzuri, kupangusa uchafu kwa sababu mama yake alikuwa hatoki hedhi wala hakuchafuka na damu ya nifasi.

Lisilowezekana Kiakili Na Kidesturi

Jambo lisilowezekana ni lile ambalo halikufanyika wala haiwezekani kufanyika siku za baadae. Nalo liko namna mbili: Kwanza ni kutowezekana kufanyika hilo lenyewe kidhati na kiakili, kwamba akili haikubali kuwezekana kutokea kwa namna yoyote; kama kuwa pamoja mambo mawili yaliyo kinyume: Mfano kuwa mtu ni mumin na wakati huo huo ni kafiri; au kipofu awe anaona na wakati huo huo awe kipofu, au bubu na msemaji wakati huo huo. Kwa hiyo jambo hilo litakuwa haliwezekani kiakili na kikawaida.

Namna ya pili: Ni kutozuilika kuwepo kwake kidhati na akili, bali inawezekana kwa namna fulani, lakini kwa kawaida halitokei.

Mifano yake ni mingi sana, Qur'an tukufu imetaja matukio mengi sana; kama vile kukaa Ibrahim katika moto bila ya madhara yoyote kugeuka nyoka fimbo ya Musa, kusimama maji ya bahari kama milima, kuyeyuka chuma kama mshumaa kwa ajili ya Daud, nabii Suleiman kujua matamshi ya ndege na kufufuliwa Uzair baada ya miaka mia.

Mfano mwengine ni wa Isa kuzaliwa bila ya baba, kuzungumza wakati wa kuzaliwa, kufufua wafu, kuwaponya vipofu na wenye mbalanga bila ya tiba yoyote na kuwaambia watu vile walivyokula na walivyoviweka akiba katika majumba yao bila ya kuviona; au kumwambia mtu matukio yote haya.

Na yote haya na mengineyo ambayo yanawezekana kutokea, lakini sio kikawaida. Lau kama ingekuwa muhali kutokea, basi yasingewezekana kutokea kwa Mitume na wasiokuwa Mitume. Kwa hiyo ikiwa matukio haya yanawezekana kutokea na tena wahyi ukayatolea habari kutokea kwake waziwazi, basi ni wajibu kwa kila mumin kuyakubali bila ya kusita.

Kundi la wanafalsafa na wafasiri wametaja njia nyengine za kuumbwa Isa bila ya tone la manii ya baba, lakini waliyoyasema hayana msingi wowote. Ilivyo hasa ni kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ni muweza wa kila kitu, anafanya kitu kiweko kwa neno 'Kun' (kuwa) kutokana na kitu ambacho hakikuwepo. Na hekima yake ilipitisha ililotaka, basi limekuwa alilolitaka.

Sisi hatuna ulazima wa kujua kiini cha matukio aliyoyaleta Mwenyezi Mungu yasiyo ya kawaida; wala kujua vipi yametokea. Huenda akili zetu zikawa zinashindwa kujua kama zilivyoshindwa kujua hakika ya roho ambayo ni katika amri ya Mola.

Ndio! Tunaloweza kufahamu ni athari zake na natija zake, lakini sio kiini chake na hakika yake. Kwa hiyo Aya zinazomhusu Masih (a.s.) na zinazofanana nazo zinazohusu mambo mengine, tutazifasiri kwa misingi hii.

Maana

Waliposema Malaika: Ewe Maryam! Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria neno litokalo kwake; jina lake ni Masih Isa mwana wa Maryam.

Makusudio ya Malaika hapa ni Jibril kutokana na kauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Na tukampelekea Roho wetu, akajifananisha kwake sawa na mtu (19:17) Ambapo makusudio ya Roho hapo ni Jibril. Amemtaja kwa tamko la wengi kwa sababu yeye ndiye kiongozi wa Malaika. Neno litokalo Kwake ni kusema Kwake "Kun fayakun" (kuwa ikawa)

Mwenye heshima duniani na akhera na ni miongoni mwa waliokurubishwa.

Heshima yake duniani, ni kufanywa mtakatifu na kuadhimishwa na watu mpaka siku ya ufu- fuo. Ama heshima yake huko akhera, ni utukufu wa daraja yake kesho kwa Mungu.
Na atasema na watu katika uchanga na katika utu uzima na atakuwa miongoni mwa watu wema.

Kusema katika uchanga ni kwa ajili ya kumtakasa mama yake na walivyomsingizia mayahudi kuwa alitembea na Yusuf Seremala; Mungu awalaani! manaswara wamedai kuwa hakusema uchangani. Ibn Abbas anasema: "Maneno ya Isa yalikuwa muda mchache na sio zaidi ya yaliyoelezwa katika Qur'an; kisha hakusema mpaka alipofikia makamo ya kusema, kama walivyo watoto wengine. Kauli hii inasaidiwa na mazingatio. Kwa sababu lengo la kuzungumza kwake ni kumwepusha mama yake na tuhuma na wasiwasi wa watu; na lengo likapatikana kwa aliyoyasema.

Na katika utuuzima.

Yaani atawazungumzia watu Wahyi akiwa ni mtu mzima Huu ni muujiza mwengine wa kufahamisha Utume wake. Kwa sababu, hilo ni kulitolea habari jambo la ghaibu kwamba yeye ataishi mpaka marika ya utuuzima. Inasemekana kuwa aliishi duniani miaka thelathini. Na, inasemekana kwamba aliletewa wahyi akiwa na umri wa miaka thelathini. Na akaishi miaka mitatu baadaye.

Akasena: "Mola wangu! Nitakuwaje na mtoto na hali hajanigusa mtu yeyote?"

Swali hili ni la kutukuza uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa sababu ni jambo lisilo la kawaida, hakuna wajihi wowote wa waliyoyaeleza baadhi ya wafasiri kwamba yeye aliuliza kuwa je, atazaa kwa ndoa? Hakuna wajihi wa swali hili kwa sababu jibu lake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Akasema: "Ndivyo hivyo; Mwenyezi Mungu huumba anavyotaka, anapohukumu jambo, huliambia 'kuwa' likawa." Linafahamisha kuwa yeye Maryam alikuwa akijua kwamba yeye atazaa bila ya kuingiliwa.

Na atamfundisha kuandika na hekima na Tawrat na Injili

Maana ya neno 'kitab' (katika lugha ya kiarabu) ni masdar ya kuandika, lakini mara nyingi linatumiwa kwa maana ya kitabu. Makusudio yake hapa, ni maana yake halisi (kuandika), kwa sababu kutajwa Tawrat na injil baada yake, kunatilia nguvu kuchukulia maana ya kuandika: Wengine wamesema maana yake ni kitabu na kwamba kutajwa Tawrat na Injil baada yake ni kutilia umuhimu tu; kama ilivyo katika kauli Yake Mwenyezi Mungu: Angalieni sana Swala na ile Swala ya katikati (2:238)

Hekima, ni kuliweka jambo mahali pake. Na Tawrat na Injil, Aya hii ni dalili mkataa kuwa Tawrat ndio nguzo ya kwanza ya dini ya kinaswara na kwamba Injil ni endelezo la Tawrat na baadhi ya marekebisho; kama vile kuhalalisha baadhi ya yaliyoelezwa kuwa ni haram, kunakoelezwa na kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na ili niwahalalishie baadhi ya yale mliyoharamishiwa."

Na Mtume kwa wana wa Israil

Mwenyezi Mungu alimtuma Muhammad (s.a.w.w.) kwa watu wote kama inavyosema Aya: "Na hatukukutuma ila kwa watu wote mtoaji bishara na muonyaji. Lakini watu wengi hawajui." (34:28)

Ama Isa akiwa Mwisrail, yeye alitumwa kwa watu wake, kutokana na muktadha wa dhahiri ya Aya hii, kuufanya ujumbe wake kuwa ni kwa watu wote, kunahitaji dalili.

Hakika mimi nimewajia na ishara kutoka kwa Mola wenu.

Msemo huu unatoka kwa Isa kuwaambia watu wake Waisrail akiwatolea hoja ya ukweli wa utume wake, kwamba yeye anayo miujiza inayofahamisha kuwa ametumwa na Mwenyezi Mungu; kama anavyotaja miujiza yenyewe kwa kusema:

"… Hakika mimi nitawafanyia kama namna ya ndege katika udongo, kisha nimpulizie, awe ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na niwaponyeshe vipofu na wenye mbalanga na niwafufue wafu kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na niwaambie mnavyovila na mtakavyoweka akiba majumbani mwenu. Hakika katika haya ipo ishara kwenu mkiwa ni wenye kuamini."
Hii ni miujiza minne:

1. Wa kwanza: Ni kuleta uhai katika udongo na kufanya ndege.

2. Pili: Kuponya aliyezaliwa kipofu na mwenye mbalanga.

Inasemekana elimu ya tiba likuwa imeendelea sana katika wakati wa Isa (a.s), lakini pamo- ja na kuendelea kwao, Madaktari mabingwa walishindwa na magonjwa haya mawili (upofu na mbalanga) ndipo Mwenyezi Mungu akayapoza kupitia mkono wa Isa bila ya tiba yoyote, ukiwa ni muujiza unaofahamisha utume wake.

3. Tatu: kumrudishia uhai maiti.

4. Nne: kuelezea mambo ya ghaibu kutokana na wanavyokula na wanavyoweka akiba.

Si kazi yetu kufanya utafiti wa kujua siri ya miujiza hii, au vipi ameleta uhai na kuponya maradhi yasiyotibika bila ya dawa; na kama tuking'ang'ania kufanya utafiti wa hayo, basi tutaishia kwenye shub'ha na giza.

Linalobaki kwetu ni kusalimu amri na kuitambua hekima ya Mwenyezi Mungu na amri Yake ambayo Bwana Masih (a.s.) ameieleza wazi wazi na kwa kuikariri, kuwa yeye ameifanya kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, ili aufunge mlango wa wanaofikiri umungu wa Isa.

Tumetangulia kueleza katika Tafsir ya 2:225 kwamba Mwenyezi Mungu anaupitisha utaratibu wa maumbile kwenye desturi ya kawaida ya kimaumbile; isipokuwa kama hekima Yake ikitaka kufanya vingine kwa matakwa Yake ya kuumba ambayo ni ibara ya 'kuwa'. Hapo tena hakuna nafasi ya desturi wala kawaida.

Ama Isa kuelezea mambo ya ghaibu, kulikuwa ni kwa kupitia wahyi, na wala hakuhusika nako yeye pekee, bali mitume wote walielezea mambo ya ghaibu. Nuh alitengeneza safina kabla ya tufani, Shuaib alitolea habari mwisho wa maisha ya watu wake, Muhammad (s.a.w.) alitoa habari ya kuwa warumi wata washinda wafursi na ushindi wa watu wake dhidi ya dola zote hizo mbili na Imam Ali naye alitolea habari mapinduzi ya Zenj na mengineyo, mpaka akaambiwa: "Amirul-mumin! Hakika umepewa elimu ya ghaibu." Akasema: "Siyo ilimu ya ghaibu, bali ni mafundisho kutoka kwa mwenye elimu." Akimaanisha Mtume (s.a.w.) ambaye naye ameichukua kutokana na Wahyi.

فَلَمَّا أَحَسَّ عِيسَىٰ مِنْهُمُ الْكُفْرَ قَالَ مَنْ أَنْصَارِي إِلَى اللَّهِ ۖ قَالَ الْحَوَارِيُّونَ نَحْنُ أَنْصَارُ اللَّهِ آمَنَّا بِاللَّهِ وَاشْهَدْ بِأَنَّا مُسْلِمُونَ {52}

Alipohisi Isa ukafiri wao alisema: "Nani watakuwa wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu?" Wanafunzi wakasema: "Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu. Tumemwamini Mwenyezi Mungu nawe shuhudia kuwa sisi ni Waislamu.

رَبَّنَا آمَنَّا بِمَا أَنْزَلْتَ وَاتَّبَعْنَا الرَّسُولَ فَاكْتُبْنَا مَعَ الشَّاهِدِينَ {53}

"Mola wetu! Tumeyaamini uliyoyateremsha, na tumemfuata Mtume, basi tuandike pamoja na washuhudiao."

وَمَكَرُوا وَمَكَرَ اللَّهُ ۖ وَاللَّهُ خَيْرُ الْمَاكِرِينَ {54}

Na wakapanga hila; na Mwenyezi Mungu akapanga hila; na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kupanga hila.