read

Aya 52-54: Ni Nani Wasaidizi Wangu

Haki Na Manufaa

Hakuna yeyote mwenye akili timamu anayeweza kuipinga haki na kuitanguliza batili, isipokuwa kwa tamaa ya nafsi, au kutatizika katika fahamu yake, au kutojua dalili, au dosari katika utoaji dalili.

Ni wazi kwamba dalili za manabii zimetosheleza kabisa kuthibitisha unabii wao katika pande zote, mpaka kufikia kuondoa makosa ya fikra na mikanganyo, kiasi ambacho hazibakishi dalili zao hoja yoyote ya kuipinga haki, isipokuwa inadi na kiburi.

Yeyote mwenye kutafuta sababu iliyowafanya wapinzani kuwafanyia vitimbi mitume na kupinga ujumbe wao - baada ya kuona dalili na miujizaataona ni sababu ya manufaa ya kibinafsi na kupupia mali na jaha. Ushahidi wa hakika hii kutoka katika vitabu vya Mwenyezi Mungu na Hadith za Mtume, hauna idadi. Miongoni mwa mifano hiyo ni: Mataghuti wapenda anasa katika watu wa Nabii Hud, walipinga, si kwa lolote isipokuwa tu, aliwaambia: Je, manajenga juu ya kila mwinuko ukumbusho wa upuuzi? Na mnajijengea majengo ya fahari ili mkae milele? Na mnaposhambulia, mnashambulia kwa jeuri (28:127-130)

Matajiri katika watu wa Nabii Shuaib walimtisha na kumwambia: "Ewe Shuaib hivi Swala zako zinakuamrisha tuyaache waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu au tuache kufanya tupendavyo katika mali zetu … Lau si jamaa zako tungelikupiga mawe." (11: 87, 91)

Kosa lake tu, ni kuwa aliwaambia: "Na enyi watu wangu! Timizeni kipimo na mizani kwa uadilifu wala msiwapunguzie watu vitu vyao; wala msiwe waovu katika nchi mkafanya uharibifu" (11:85)

Qarun alikuwa tajiri sana katika watu wa Musa na ni mtu aliye karibu zaidi naye kiudugu, lakini pamoja na hayo alimfanyia uadui alipompa waadhi huu "Na ufanye wema kama alivyokufanyia wema Mwenyezi Mungu wala usitafute kufanya ufisadi katika nchi; hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wafisadi." (28:77)

Abdalla bin Ubayya alikuwa ni katika viongozi na matajiri wa Madina. Mtume alipohamia huko, alipatwa na wivu; akamwambia Mtume maneno ya kutokubaliana naye. Sa'ad bin Ubada akamwambia Mtume: "Usiyatilie maanani maneno yake; kwani sisi tulikuwa tunataka kumpa Ufalme, naye anaona kuwa wewe umemnyang'anya."1 Yatosha kuwa ni dalili ya hakika hii, kauli yake Mwenyezi Mungu: "Kila alipowajia Mtume na lile ambalo nafsi zao halilipendi, wengine waliwakadhibisha na wengine wakawaua." (5:70)

Walimkadhibisha Bwana Masih (Yesu) na kujaribu kumuua, kwa sababu yeye aliwapa mwito wa mapenzi, uadilifu, usawa na kutolimbikiza dhahabu na huku wengine wana njaa na mahitaji. Miongoni mwa mafunzo yake ni: "Msilimbikize mali ardhini. Tajiri kuingia mlango wa mbinguni ni kama kamba nene kuingia kwenye tundu ya sindano."

Maana

Isa alipohisi ukafiri wao.

Kabla ya kuzaliwa nabii Isa, mayahudi walikuwa wakiamini Masih atakayekuja. Alipowajia na hoja na miujiza, walitofautiana; wakamwamini maskini na wanyonge ambao hawakuhofia kupoteza mali wala jaha, lakini matajiri na wenye jaha walimkanusha kwa kuhofia vyeo vyao na chumo lao; kama ilivyo kwa yeyote anayekuja kutengeza; awe mtume au si mtume, hata kama watamjua kuwa ni mkweli mwenye haki.

Baadhi ya wafasiri wamekosea waliposema kuwa Mayahudi walimkataa Muhammad kwa vile ni Mwarabu wa kizazi cha Ismail, na kwamba kama angekuwa ni myahudi wa kizazi cha Is-haq (a.s.) basi wangelimkubali! Mbona Isa alikuwa myahudi, lakini pamoja na hayo walimpiga vita na kujaribu kumuua na kutaka kumsulubu. Vilevile Muhammad waliompiga vita ni Mamwinyi wa Kiquraish. Siri ya hapa na huko ni moja tu, kupigania dunia na manufaa na wala sio ubaguzi wa kikabila.
Vyovyote, itakavyokuwa, ni kwamba Isa alihisi watu wake waking'ang'ania ukafiri kwa inadi, na akapata tabu kutoka kwao; kama alivyopata tabu Muhammad (s.a.w.w.) kutoka kwa watu wake; ndipo Isa aliposema: "Ni nani watakuwa wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu", yaani ni kina nani hao na wako wapi waumini wa kuinusuru na kuihami dini ya Mwenyezi Mungu, na ambao wataendeleza tabligh baada yangu? Kwani kila mwenye ujumbe hana budi kuwa na wasaidizi watakaomwamini na kumwakilisha kwa watu.

Wanafunzi wakasema: "Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu, tumemwamini Mwenyezi Mungu nawe shuhudia kuwa sisi ni Waislamu. Mola wetu! Tumeamini uliyoyateremsha na tumemfuata Mtume, basi tuandike pamoja na wanaoshuhudia."

Kusema sisi ni waislamu ni dalili kwamba dini ya Mwenyezi Mungu ni moja tu tangu mwanzo hadi mwisho wa kikomo. Dini yenyewe ni uislamu ndiyo waliyokuja nayo mitume wote. Tofauti iko kwenye baadhi ya hukumu na sura ya ibada tu. Kwa hivyo basi, kila anayemwamini Mwenyezi Mungu, Vitabu Vyake na Mitume Yake, basi huyo ni mwislam, hata kama atajiita mkristo au yahudi. Ufafanuzi wa hilo umetangulia katika kufasiri Aya 19 ya Sura hii.

Kauli ya wanafunzi: "Tuandike pamoja na wanaoshuhudia." Ni dua yao kumwomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) awajaalie katika fungu la waumini walioshuhudia umoja wa Mungu na kuwa na uaminifu, ili wafuzu yale waliyofuzu wenye ikhlasi wenye kuridhiwa; na wapate karama kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.).

Katika tafsir nyingi imeelezwa kuwa wanafunzi walikuwa kumi na wawili. Baadhi ya wafasiri wametaja majina yao na kazi zao. Lakin sisi tunanyamaza kutokana na Hadith isemayo. "Nyamazeni aliyoyanyamazia Mwenyezi Mungu."

Mwenyezi Mungu Ni Mbora Wa Wafanya Hila

Na wakapanga hila; na Mwenyezi Mungu akapanga hila; na Mwenyezi Mungu ni mbora wa wapanga hila.

Kuna Aya nyingi nyingine zinazofanana na Aya hii, kama zifuatazo: Na wanapanga hila; na Mwenyezi Mungu anapanga hila; na Mwenyezi Mungu ni mbora wa wapanga hila. (8:30.).

Na wakapanga hila na sisi tukapanga hila, na hali hawatambui. (27:50). Sema: Mwenyezi Mungu ni mwepesi zaidi wa kupanga hila, hakika wajumbe wetu wanaandika hila mnazozipanga (10:21).

Makusudio ya hila kwa makafiri na wanafiki, ni vitimbi, hadaa, hiyana na kupanga njama. Ama hila ya Mwenyezi Mungu, makusudio yake ni kuzitangua hila na njama za wenye hila; kama ilivyosema Aya: "Na hila mbaya hazimpati ila yule aliyezifanya." (35:43).

Katika Qur'an kuna sifa nyingi sana alizosifiwa Mwenyezi Mungu ambazo kwa dhahiri zinaonekana kuwa hafai kusifiwa nazo mfano: Mwenye shukrani, Mumin, Mwingi wa toba na Mwenye kiburi. Lakini ukiyafikiri vizuri maana yake, utayaona yako mahali pake.

Maana ya Mwenye shukrani ni kwamba yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawalipa thawabu wenye kushukuru na watiifu. Mumin maana yake yeye ndio chimbuko la amani na salama. Mwingi wa toba, ni kwamba yeye anakubali toba za wenye kutubia. Na mwenye kiburi ni kwamba kila kilichomo ulimwenguni ni duni kwake yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kwa maana hayo, inatubainikia kuwa hila ni haramu ikiwa itakusudiwa kumdhuru mwengine; na itakuwa halali ikiwa itakusudiwa kujikinga na madhara ya mtu binafsi au mwengine.

Hebu tutaje mifano miwili ya kubatilisha hila za Makfiri na vitimbi vyao: Mayahudi walipanga hila ya kumuua Isa (as), lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akaipan-gua njama yao, pale alipomfananisha Yahudha na Isa, yule myahudi aliyehimiza kuuliwa Isa, na akampaza Isa mbinguni.

Maquraish kwa pamoja walipanga kummaliza Muhammad, kwa kumchagua kijana kutoka kila ukoo, wampige kwa panga zao akiwa amelala na damu yake iwe kwa wote. Lakini Mwenyezi Mungu akapangua hila zao, pale alipomwamuru kutoka Makka na Ali alale kitandani pake ili watu wafikirie kuwa Muhammad hajasafiri, walipovamia nyumba wakamkuta Ali ndiye aliyelalala kitandani .

إِذْ قَالَ اللَّهُ يَا عِيسَىٰ إِنِّي مُتَوَفِّيكَ وَرَافِعُكَ إِلَيَّ وَمُطَهِّرُكَ مِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا وَجَاعِلُ الَّذِينَ اتَّبَعُوكَ فَوْقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ ۖ ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأَحْكُمُ بَيْنَكُمْ فِيمَا كُنْتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ {55}

Aliposema Mwenyezi Mungu: "Ewe Isa! Mimi nitakufisha. Na nikuinue kwangu, na nitakutakasa na wale waliokufuru, na nitawaweka wale waliokufuata, juu ya wale waliokufuru, mpaka siku ya kiyama. Kisha marejeo yenu yatakuwa kwangu, nitahukumu baina yenu katika yale mliyokuwa mkihitalifania.

فَأَمَّا الَّذِينَ كَفَرُوا فَأُعَذِّبُهُمْ عَذَابًا شَدِيدًا فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَمَا لَهُمْ مِنْ نَاصِرِينَ {56}

Ama wale waliokufuru, nitawaadhibu adhabu kali katika dunia na Akhera, na hawana wa kuwanusuru.

وَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَيُوَفِّيهِمْ أُجُورَهُمْ ۗ وَاللَّهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ {57}

Na wale walioamini na wakatenda matendo mema, atawalipa ujira wao. Na Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kudhulumu.

ذَٰلِكَ نَتْلُوهُ عَلَيْكَ مِنَ الْآيَاتِ وَالذِّكْرِ الْحَكِيمِ {58}

Haya tunayokusomea ni katika Ishara na mawaidha yenye hekima.
  • 1. Katika kufasiri Aya 61 ya Sura hii, tutaeleza vile ujumbe wa Najran ulivyoamini utume wa Muhammad, lakini wakakataa kukiri kwa sababu ya malipo wanayoyapata kutoka kwa mfalme.