read

Aya 55-58: Kuondoka Ulimwenguni

Kutofautiana Kuhusu Isa

Watu wametofautiana sana kuhusu nabii Isa. Wametofautiana kuhusu kupatikana kwake, tabia yake na hata kufa kwake; Kuna wanaosema kuwa hakuweko kamwe, na kwamba habari zake ni vigano tu, kauli hii ilijitokeza mnamo karne ya kumi na tisa (19) huko Ujerumani, Ufaransa na Uingereza.

Ni kauli ya kipumbavu kabisa; kwani ni sawa na kusema kuwa hakuna ukristo wala uislamu unaomwamini Isa. Wengine wamesema ni Mungu, wengine wakasema ni binadamu mayahudi nao wakasema kuhusu Isa na mama yake mambo ambayo yanaweza kuitingisha hata Arsh.

Ama waislamu wametofautiana kama ifuatavyo: Wengi wamesema hakufa na kwamba yeye yuko hai kimwili na kiroho mbinguni au mahali pengine popote; na atatoka duniani wakati wa mwisho mwisho wa dunia. Kisha hapo ndipo Mwenyezi Mungu atamuua mauaji ya kihakika. Waislamu wengine wamesema kuwa yeye amekwisha kufa mauti ya kiuhakika na kwamba iliyopazwa ni roho yake tu, sio mwili.

Tofauti hii ya Waislamu imetokana na kutofautiana dhahiri ya Aya; kama ifuatavyo: "…Na hawakumuuwa wala hawakumsulubu, lakini alifananishwa kwao. Na kwa hakika wale waliohitilafiana katika hayo wamo katika shaka nayo, hawana ujuzi nayo isipokuwa kufuata dhana tu; na hawakumuuwa kwa yakini. Bali Mwenyezi Mungu alimnyanyua kwake na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu na mwenye hekima." (4: 157 - 158).

Dhahiri Aya hii kwa kuongezea Hadith za Mtume, zinayonyesha kuwa nabii Isa yuko hai. Lakini Aya nyengine inayosema: Uliponifisha wewe ukawa mchungaji juu yao …" (5:117) pamoja na Aya hii tuliyonayo.
Maana yanayokuja haraka ni mauti. Na, maana ya dhahiri ni kuwa mimi nitakufisha na kukujaalia mahali patukufu kama ilivyo kuhusu Idris: "Na tulimwinua daraja ya juu kabisa." (19:57).

Au kama ilivyo kuhusu mashahidi: Wala usidhani wale waliouliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni wafu, bali wao wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao" (3:169)

Wale wanaosema kuwa Isa yuko hai kiroho na kimwili, wameleta taawili kuwa neno tawaf- faytani na Mutawaffika (kufisha) kwa njia nyingi zenye nguvu zaidi ni ile inayosema makusudio ni kufananishwa na mauti, si mauti ya kihakika. Kwa sababu anapopaazwa mbinguni anakuwa hana mfungamano tena na dunia; kwa hiyo anakuwa kama maiti.

Ama wale waliosema kuwa amekufa kiuhakika wameleta taawili ya neno Hawakumuua kwamba mayahudi hawakuua msingi wa Isa na mafundisho yake kwa sababu ya kumuua na kumsulubu. Lakini waliletewa mawazo tu, ya kuwa wameyamaliza mafunzo yake lakini bado yamesimama tu na yatabakia mpaka siku ya ufufuo.

Sisi tuko pamoja na kauli ya kwanza; kwamba Isa yuko hai, Mwenyezi Mungu alimwinua kwake baada ya kumkamilishia maisha yake duniani kwa namna isiyokuwa ya mauti. Tuko kwenye rai hii kwa kuangalia dhahiri ya Aya na yaliyopokewa kutoka kwa Sunni na Shia kwamba yeye bado yuko hai.

Lakini pamoja na hayo yote, sisi hatuoni faida yoyote ya kuhakikisha na kuangalia kwa undani kuhusu maudhui haya. Kwa sababu kuamini namna ya kubainika uhai wake hapa duniani, na kuinuliwa kwake si misingi ya dini wala misingi ya madhehebu.

Pia si katika matawi yake, isipokuwa ni maudhui ya nje yasiyofungamana na maisha yetu si kwa karibu wala mbali. Mwenyezi Mungu kesho kamwe hatauliza watu kwamba Isa alikufa vipi, au vipi alivyoinuliwa. Tunachopaswa kuamini ni kuwa Isa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, naye ameumbwa kwa neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu, na kwamba mama yake ni mtakatifu.

Zaidi ya hayo utafiti wa maudhui haya hauishii kwenye yakini ya kujua aina ya kwisha maisha ya Isa au kuinuliwa kwake. Kwa hiyo lililo bora ni kumwachia Mwenyezi Mungu (s.w.t.)."1

Aliposema Mwenyezi Mungu: Ewe Isa! Mimi nitakufisha na nikuinue kwangu.

Baada ya mayahudi kung'ang'ania kutaka kumwua Isa na kupanga njama. Mwenyezi Mungu alimpa bishara ya kumwokoa na kuvunjilia mbali vitimbi vyao na kwamba atamkamilisha muda wake kwa njia ya kawaida; atamgurisha kwenye ulimwengu mwengine ambako hatapata adha ya mtu yeyote na wala hakuna utawala wa yeyote ispokuwa Mwenyezi Mungu, hayo ndiyo maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

Nitakutakasa na wale waliokufuru.

Yaani nitakuweka mbali na uchafu wao na utangamano wao mchafu na shari wanayokutakia.

Na nitawaweka wale waliokufuata juu ya wale waliokufuru mpaka siku ya kiyama.

Makusudio ya kuwa juu hapa ni kwa kinafsi na kiukamilifu na wala sio kifalme na kimali. Hapana mwenye kutia shaka kwamba wale waliomwamini Isa ni bora kuliko waliomkadhibisha.

Kisha marejeo yenu ni kwangu niwahukumu katika yale mliyokuwa mkihitalifiana.

Hapa hapahitaji tafsir, kwani maana yaliyo dhahiri ndiyo yaliyokusudiwa. Zaidi ya hayo ni kwamba dhamir inaenea kwa wote waliohitalifiana kuhusu Bwana Masih katika sifa zake kila mahali na kila wakati.

Ama wale waliokufuru, nitawaadhibu adhabu kali katika dunia na akhera na hawana wa kuwanusuru.

Adhabu ya akhera inajulikana. Ama adhabu ya duniani ni kwamba yeye (kafiri) ni tofauti na mwislam katika vipengele vingi vya sharia, kama vile kufaa kumsengenya kafiri, au kuwa kafiri anauliwa akimuua mwislam, lakini mwislam hauliwi kwa kumuua kafiri, bali hana hata fidia - kama walivyosema mafakihi wengi - isipokuwa akiwa dhimii; lakini fidia ya dhimii inatofautiana na ya mwislam kwa tofauti kubwa2

Na ama wale walioamini na wakatenda matendo mema, atawalipa ujira wao; Na
Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kudhulumu,

Katika Hadith imeelezwa kuwa dhalimu na mwenye kuridhia dhulma ni sawa. Imam Baqir (a.s.) anasema: "Dhulma ni aina tatu: dhulma anayoisamehe Mwenyezi Mungu, dhulma asiyoisamehe Mwenyezi Mungu, na dhulma asiyoiacha Mwenyezi Mungu.

Ama dhulma anayoisamehe ni ile ya kujidhulumu mtu mwenyewe kati yake na Mola wake. Dhulma asiyoisamehe ni ile ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu, Ama dhulma asiyoiacha ni kuwadhulumu waja." Imam Ali (a.s.) anasema: "Kumdhulumu mnyonge ndio dhulma mbaya kabisa."

Haya tunayokusomea ni katika ishara na mawaidha yenye hekima.

Haya ni ishara ya yale ambayo Mwenyezi Mungu amemwelezea Mtume wake kuhusu habari za mamake Maryam, Maryam mwenyewe na Zakariya. Vilevile Yahya, Isa, wanafunzi, wayahudi na wapinzani.

Maana yake ni kuwa tumekusomea ewe Muhammad habari hii ili iwe hoja na dalili kwa yule unayejadiliana naye kuhusu Isa n.k. Ama kuwa habari hizi ni hoja ya Muhammad, ni kwamba yeye hajui kusoma wala hakuna mtu anayemwambia hayo.

Kwa hiyo inabaki kuwa kujua kwake habari hizi ni kwa njia ya wahyi tu kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Makusudio ya mawaidha yenye hekima ni Qur'an.

إِنَّ مَثَلَ عِيسَىٰ عِنْدَ اللَّهِ كَمَثَلِ آدَمَ ۖ خَلَقَهُ مِنْ تُرَابٍ ثُمَّ قَالَ لَهُ كُنْ فَيَكُونُ {59}

Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu, ni kama mfano wa Adam; alimuumba kutokana na udongo, kisha akamwambia kuwa akawa.

الْحَقُّ مِنْ رَبِّكَ فَلَا تَكُنْ مِنَ الْمُمْتَرِينَ {60}

Ni haki kutoka kwa Mola wako, basi usiwe miongoni mwa wenye shaka.

فَمَنْ حَاجَّكَ فِيهِ مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ فَقُلْ تَعَالَوْا نَدْعُ أَبْنَاءَنَا وَأَبْنَاءَكُمْ وَنِسَاءَنَا وَنِسَاءَكُمْ وَأَنْفُسَنَا وَأَنْفُسَكُمْ ثُمَّ نَبْتَهِلْ فَنَجْعَلْ لَعْنَتَ اللَّهِ عَلَى الْكَاذِبِينَ {61}

Na watakao kuhoji baada kukufikia elimu hii, waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake zetu na wana wanawake wenu, na nafsi zetu na nafsi zenu, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.

إِنَّ هَٰذَا لَهُوَ الْقَصَصُ الْحَقُّ ۚ وَمَا مِنْ إِلَٰهٍ إِلَّا اللَّهُ ۚ وَإِنَّ اللَّهَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ {62}

Hakika haya ni maelezo ya kweli, na hapana mola isipokuwa Mwenyezi Mungu Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwenye nguvu mwenye hekima.

فَإِنْ تَوَلَّوْا فَإِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ بِالْمُفْسِدِينَ {63}

Na wakikataa, basi hakika Mwenyezi Mungu anawajua waharibifu.
  • 1. Tutaelezea zaidi katika tafsir ya 4:158.
  • 2. Dhimmi ni kafiri anayeishi kwa amani na Waislam.