read

Aya 59-63: Mfano Wa Isa Ni Kama Wa Adam

Maana

Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam; alimuumba kutokana na udongo, kisha akamwambia kuwa akawa.

Wafasiri wanasema kuwa ujumbe wa Najran (Yemeni) ulimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.): "Kwa nini unamshtumu sahibu wetu?" (yaani Isa) Akasema: "Vipi?" Wakasema: "Wewe unasema kuwa yeye ni mja."

Akasema: "Ndiyo yeye ni mja wa Mwenyezi Mungu, na ni Mtume wake na ni tamko lake alilompelekea bikira Maryam."

Wakamuuliza: "Je, umekwishaona mtu asiyekuwa na baba?" Ndipo ikashuka Aya: "Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam" Ikiwa riwaya hii ni sahih au si sahihi, lakini haya ndiyo maudhui ya Aya hii hasa. Kwa sababu wakristo walikuwa, na bado, wanaendelea kutoa hoja ya itikadi yao kuwa Isa ni Mungu, kwa vile amezaliwa bila ya baba.

Lakini Mwenyezi Mungu ameivunja hoja yao hii kwa Adam; Ikiwa Isa ni mungu au mwana wa Mungu, kwa sababu ya kuzaliwa bila ya baba, basi Adam ndiye anayefaa zaidi kuwa Mungu, kwa sababu yeye amezaliwa bila baba wala mama. Hawakuijibu hoja hii, na wala hawatajibu mpaka siku ya mwisho.

Unaweza kuuliza kuwa inavyoonyesha kauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu alimuumba kwa udongo ni kwamba Mwenyezi Mungu alimtengeneza Adam kwa ukamilifu; kwa maana ya kuwa kuumba kulitangulia kauli ya "Kun fayakun", kwa hiyo kulikuwa hakuna haja tena ya kauli hii kwa sababu maana yake ni kuumba kilichoumbwa; na maneno ya Mwenyezi Mungu hayafai kuwa hivyo.

Jibu: Mungu alimuumba Adam kwa vipindi; miongoni mwa vipindi hivyo ni kwamba yeye alimuumba kwa udongo, kisha akatia roho. Kwa hiyo maana yanakuwa: "Ewe udongo! Kuwa mtu aliye na nyama, damu, hisia na utambuzi."

Mitume Na Maasi

Ni haki kutoka kwa Mola wako

Yaani haya tuliyokuteremshia na kukufahamisha kuhusu Isa ni haki kutoka kwa Mola wako.
Basi usiwe miongoni mwa wenye shaka.

Unaweza kuuliza kuwa ni muhali Mtume kutilia shaka aliyoyatolea habari Mwenyezi Mungu. Kwa sababu shaka inapingana na imani, sikwambii isma. Sasa makatazo haya ni ya nini? Wafasiri wamelijibu swali hili kwa majibu mawili: Kwanza: kwamba dhahiri inonyesha kuwa msemo unaelekezwa kwa Mtume, lakini makusudio ni wengine. Pili: makusudio ni kuendelea Mtume na yakini.

Njia zote mbili inabidi kuziangalia vizuri kwa sababu zinamaanisha kuwa haifai kwa Mwenyezi Mungu kuwakataza maasi mitume Yake. Ilivyo hasa ni kwamba Mwenyezi Mungu anaweza kuwakataza mitume maasi kwa vile kwanza hiyo ni amri ya mkubwa kwa mdogo. Pili: Isma si maumbile na tabia ya mitume mpaka iwe ni muhali kuweko uwezekano wa kufanya maasi. Kama ni hivyo basi wasingekuwa na ubora wowote. Wao wanaweza kufanya maasi, lakini hawafanyi maasi.

Kwa hiyo basi inafaa kwa Mwenyezi Mungu kuwapa makatazo, lakini makatazo yawe yanatoka Kwake Mwenyezi Mungu tu, sio kwa mtu mwengine. Kwa sababu hakuna aliye zaidi ya Mtume isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu tu.

Makatazo mengi yaliyokuja katika Qur'an yanachukuliwa kwa njia hii. Mfano kauli Yake Mwenyezi Mungu kumwambia kipenzi Chake Muhammad (s.a.w.w): "Wala usiwatii makafiri." (33:48).

Hatujui pengine wenyewe Mitume, walikuwa wakipenda makatazo haya kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.), bali pengine walikuwa wakiyataka hasa; kama vile Mumin mwema anavyotaka kupata mawaidha na kukumbushwa Mungu kutoka kwa mjuzi.

Mubahala

Na watakaokuhoji baada ya kukufikilia elimu hii, waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake wetu na wanawake wenu, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.

Hii ndiyo Aya inayojulikana kwa jina la Aya ya Mubahala (maapizano), nayo ni miongoni mwa Aya zilizo msingi wa kitabu.

Kusudio la kwanza la Aya hii Tukufu ni kuimarisha dini na kuuthibitisha ujumbe wa Muhammad kwa njia ambayo elimu na wanavyuoni hawakuizoweya, na ambayo haiwezi yeyote isipokuwa Muumbaji wa ardhi na mbingu.

Lakini ni njia ambayo inafahamika kiwepesi kwa mtu yeyote, awe mjuzi au si mjuzi. Kisa chenyewe kwa ufupi ni kama ifuatavyo:

Aya hii inafungamana na mwaka wa tisa tangu Mtume kuhamia Madina. Mwaka huo ulijulikana kwa jina la mwaka wa ugeni. Kwa sababu Mtume alipata wageni kutoka sehemu mbali mbali za Bara arabu kuja kutangaza utii wao kwake, baada ya Mwenyezi Mungu kuliinua neno la kiislamu na kuwapa ushindi waislam dhidi ya maadui zao.

Miongoni mwa ugeni alioupata Mtume, ulikuwa ni ujumbe wa watu sitini, wakristo kutoka Najran, Yemen. Inasemekana mlikuwa na wakubwa wao kumi na nne; akiwemo mkubwa wao na kiongozi wao, Abdul-Masih, mshauri wao, Ahyab akiwa na lakabu ya Sayyid na Askofu ambaye alitukuzwa sana na mfalme wa Roma, alimjengea kanisa na chuo na kumpatia mali na mshahara.

Mtume akawapokea kwa takrima. Ulipofika wakati wao wa kuswali, waligonga kengele na wakaswali katika Msikiti wa Mtume kuelekea Mashariki. Masahaba walipotaka kuwazuiya Mtume aliwakataza kwa kusema: "Waacheni."

Baada ya kutulia wageni hao, wakaanza kujadiliana na Mtume wa Mwenyezi Mungu kuhusu Isa wakidai kuwa yeye ni Mungu mara nyingine yeye ni mtoto wa Mungu na mara yeye ni watatu katika watatu. Wakaleta dalili ambazo tumekwisha zitaja na jinsi zilivyobatilishwa.

Aliyezibatilisha dalili za wakristo ni Mwenyezi Mungu mwenyewe, lakini kupitia kwenye ulimi wa Mtume (s.a.w.). Na, katika ugeni huo mlikuwa na maulama ambao ukweli hauwezi kujificha kwao; kama vile Abu Haritha ambaye alikuwa kiongozi wa dini wa msafara.

Yeye alikuwa na ndugu anayeitwa Kurzi. Abu Haritha baada ya kusikia aliyoyasikia kutokana na hoja za Mwenyezi Mungu zilizo wazi, alimwambia ndugu yake kwa siri kwamba Muhammad ndiye yule Mtume tuliyekuwa tukimngojea Nduguye akamwambia: "Sasa wangoja nini nawe una yakini na ukweli wake?"

Akamwambia: "Unajua, wafalme wametupa mali nyingi na wametutukuza sana, lau tukimwamini Muhammad watatuyang'anya kila kitu. Likamwingia moyoni hilo na akalificha; kisha akasilimu na kulisimulia ."
Ukweli wa riwaya hii hauhitaji dalili, kwa sababu hiyo yenyewe inafahamisha ukweli wake, na kiasi chake kinachukuliwa pamoja na riwaya hii; kama wanavyosema watu wa mantiki. Watu wengi waliokanusha haki na kuipinga, walifanya hivyo kwa sababu ya masilahi yao ya kibinafsi kama tulivyoelezea kwa ufafanuzi katika Aya ya 54 ya Sura hii.

Mtume aliujadili ujumbe wa Najran kuhusu Isa, na akajadiliana nao kwa hoja yenye kubatil- isha uwongo na mantiki ya kisawasawa yasiyokubali kuongezewa chochote. Walipong'ang'ania upinzani, Mtume aliukata mjadala na kuwataka kufanya jambo jengine lisilofanana na mjadala, lakini litakalomaliza ugomvi mara moja na kumaliza ubishi wote.

Aliwataka neno moja tu, ambalo hawezi kulikataa ila yule anayejijua kuwa ni mwongo. Tamko lenyewe ni 'Laana ya Mwenyezi Mungu iwe kwa waongo." Lakini tamko lenyewe litaambatana na muujiza ambapo utapanda ukelele kwenye kichwa cha mwongo na aone dunia yote ni moto.

Zimekuja Hadith Mutawatir katika vitabu vya Hadith na Tafsir, kama vile Sahih Muslim na Tirmidhi, Tafsir Tabari, Razi, Bahrul-Muhit, Gharaibul-Qur'an, Rawhul-Bayan, Al-Manar, Maraghib na nyenginezo nyingi. Hadith hizo zinaeleza kuwa, Mtume alitoka akiwa amem- beba Husein na kumshika mkono Hasan; Fatima na Ali wakimfuata nyuma akiwaambia nitakapoomba nyinyi itikieni amin.

Kiongozi wa kidini wa msafara akawaambia wenzake: "Enyi Manasara! Mimi ninaona nyuso ambazo, lau zitaomba jabali liondoke lilipo basi linaweza kuondoka. Kwa hiyo msiapizane nao msije mkaangamia" Kisha akasema: "Ewe Abul-Kassim tumeonelea tusiapizane na wewe." Akawaambia: "Basi silimuni," wakakataa; kisha wakasuluhishana watoe kodi.

Msafara ukarudi mikono mitupu, ukiwa umeshindwa na kufedheheka. Baada ya tukio hili, walisilimu wengi na kuwazidishia waumini imani na uthabiti.

Muhammad (s.a.w.w.) aliwaleta vipenzi vyake kwenye Mubahala akiwa na hakika ya ushin- di, kama kwamba uko mikononi mwake. Hakuna kitu kilichofahamisha uwazi na ukweli juu ya hoja ya utume wake kuliko tendo hili. Ni dalili iliyo wazi zaidi kuliko dalili ya mwangaza wa jua kuwa jua lipo. Sijui kama muujiza huu alikuwa nao Mtume mwengine yeyote. Ingawaje walikuwa wakiwaombea makafiri na kuitikiwa maombi yao.

Unaweza kuuliza: Mtume aliwataka baadhi ya makafiri waamini; waliposema: "Ewe Mwenyezi Mungu! Kama haya ni haki itokayo kwako, basi tupige kwa mvua ya mawe kuto- ka mbinguni au tuletee adhabu yoyote iumizayo."(8:32).

Lakini pamoja na hayo haikuwatukia adhabu hiyo.

Jibu: Mazungumzo tuliyo nayo yanahusu maapizano, ambayo yanathibiti kwenye mahojiano na madai tu; vilevile hayajuzu ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu au mjumbe wake kuhofia kutojitokeza ukweli wa mkweli. Ama kauli ya makafiri (Tupige mvua ya mawe kuto- ka mbinguni) hayo ya mvua ya mawe si katika maapizano. Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu ameahirisha adhabu yao mpaka siku ya kufufuliwa.

Ahlul Bait

Katika aliyoyasema Razi kuhusu tafsir ya Aya ya Mubahala ni: "Imepokewa kuwa Muhammad (s.a.w.) alipotoka akiwa katika kitambaa cheusi, alikuja Hassan (r.a) akamwingiza, akaja Hussein (r.a.) akamwingiza, kisha Fatima, kisha Ali (r.a..). Mtume akasema: "Hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwaondolea uchafu Ahlul bait watu wa nyumba ya Mtume na kuwatakasa kabisa kabisa." (33:33). Anaendelea kusema Razi.

Jua kwamba riwaya hii - kama wailivyoafikiana usahihi wake watu wa tafsir na Hadith - inafahamisha kuwa Hassan na Hussein walikuwa watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa sababu aliahidi kuwaita watoto akawaita, Hassan na Hussein (a.s), kwa hivyo hilo limewajibisha kuwa ni watoto wake.

Linalotilia mkazo hili ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na katika kizazi chake Daud na Suleiman… na Zakariya na Yahya na Isa….." (6: 84-85)

Inavyojulikana ni kwamba Isa ananasibishwa kwa Ibrahim kwa upande wa mama, sio wa baba.

Nimefanya utafiti mrefu wa maudhui haya katika kitab Fadhail Imam Ali (fadhila za Imam Ali) na nikaweka mlango maalum wa 'watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu.'

Hakika haya ni maelezo ya kweli, na hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu; na hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwenye nguvu mwenye hekima. Na wakikataa, basi hakika Mwenyezi Mungu anawajua waharibifu.

maneno haya ni ishara ya yaliyotangulia kuhusu Isa na kwamba yeye ni Mtume, wala si mtoto wa zina (wa haramu) kama wanavyodai mayahudi; wala pia siyo Mungu au mwana wa Mungu, kama wanavyodai wakristo. Asiyeamini uhakika huu basi achana naye ewe Muhammad, kwa sababu Mwenyezi Mungu anajua mfisadi na mpotevu na ana uwezo wa kumwadhibu.

قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْا إِلَىٰ كَلِمَةٍ سَوَاءٍ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ أَلَّا نَعْبُدَ إِلَّا اللَّهَ وَلَا نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا وَلَا يَتَّخِذَ بَعْضُنَا بَعْضًا أَرْبَابًا مِنْ دُونِ اللَّهِ ۚ فَإِنْ تَوَلَّوْا فَقُولُوا اشْهَدُوا بِأَنَّا مُسْلِمُونَ {64}

Sema: "Enyi watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno la usawa baina yetu na baina yenu. Kwamba tusimwabudu yo yote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala baadhi yetu wasiwafanye baadhi kuwa waungu zaidi ya Mwenyezi Mungu Wakikataa, semeni: "Shuhudieni ya kuwa sisi ni waislamu.

يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لِمَ تُحَاجُّونَ فِي إِبْرَاهِيمَ وَمَا أُنْزِلَتِ التَّوْرَاةُ وَالْإِنْجِيلُ إِلَّا مِنْ بَعْدِهِ ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ {65}

Enyi watu wa Kitabu! kwanini mnabishana juu ya Ibrahimu, na hali Tawrati na Injili havikuteremshwa ila baada yake? Basi, hamfahamu?

هَا أَنْتُمْ هَٰؤُلَاءِ حَاجَجْتُمْ فِيمَا لَكُمْ بِهِ عِلْمٌ فَلِمَ تُحَاجُّونَ فِيمَا لَيْسَ لَكُمْ بِهِ عِلْمٌ ۚ وَاللَّهُ يَعْلَمُ وَأَنْتُمْ لَا تَعْلَمُونَ {66}

Je, nyinyi ni wale mnaojadiliana katika lile mlilolijua. Mbona (sasa) mnabishana katika lile msilolijua? Na Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye, nyinyi hamjui (kitu).

مَا كَانَ إِبْرَاهِيمُ يَهُودِيًّا وَلَا نَصْرَانِيًّا وَلَٰكِنْ كَانَ حَنِيفًا مُسْلِمًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ {67}

Ibrahimu hakuwa myahudi wala mnaswara (mkristo), lakini alikuwa mwenye kuachana na dini potofu, na kushikamana na haki; wala hakuwa katika washirikina.

إِنَّ أَوْلَى النَّاسِ بِإِبْرَاهِيمَ لَلَّذِينَ اتَّبَعُوهُ وَهَٰذَا النَّبِيُّ وَالَّذِينَ آمَنُوا ۗ وَاللَّهُ وَلِيُّ الْمُؤْمِنِينَ {68}

Hakika watu wanaomkurubia zaidi Ibrahimu ni wale waliomfuata, na Mtume huyu na walioamini pamoja naye Na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa waumini.