read

Aya 64-68: Njooni Kwenye Neno La Usawa

Maana

"Sema enyi watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno la usawa baina yetu na baina yenu. Kwamba tusimwabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu wala tusimshirikishe na chochote, wala baadhi yetu wasiwafanye baadhi kuwa ni miungu, zaidi ya Mwenyezi Mungu."

Mayahudi, wanaamini Tawrat, Wakristo wanaamini Tawrat na Injil, na waislam wanaamini Tawrat, Injil na Qur'an.
Vitabu vyote hivi vitatu kwa pamoja vinakubali kuwa kuna mwenye kuutengeneza ulimwengu mwenye hekima, lakini wakristo wameingia ndani sana, wakamfanya Mungu kuwa na washirika, wakamnasibishia mtoto na wakawafanya maaskofu wao ni miungu wanaowahalalishia na kuwaaharamishia.

Imepokewa Riwaya kuwa Adiy bin Hatim alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu: "Hakika Mwenyezi Mungu anasema katika kitabu chake kitukufu: "Wamewafanya makasisi wao na watawa wao kuwa ni waungu badala ya Mwenyezi Mungu." (9:31). Lakini wakristo hawawaabudu wanavyuoni na watawa." Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) akasema: "Kwani si walikuwa wakiwahalalishia na kuwaharamishia, na nyinyi munakubali maneno yao?"

"Ndiyo." Adiyo akajibu.
Mtume akaongeza: "Basi ndio hivyo."

Bado tukiwa katika karne ya ishirini tunasoma magazetini kwamba fulani amekutana na Baba (Mtakatifu) na akambariki. Vilevile makadinali na maaskofu wakuu, hutoa baraka. Ama Waislamu, wao wanaitakidi kwamba baraka haiwezi wala haitakuwa ila kutoka kwa Mwenyezi Mungu: Rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake ziko juu yenu." (11:73)

Ama Mayahudi, walimkana Isa (a.s.) na wakajaribu kumsulubu, wakamkana Muhammad (s.a.w.w.) wakiwa wanajua ukweli wake. Mwenyezi Mungu anasema: "Lakini yalipowajia yale waliyokuwa wakiyajua waliyakanusha. Basi laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya makafiri" (2:89)

Mtume alijadiliana na watu wa Kitabu kwa mjadala mzuri, na akawapa aina kadhaa za dalili zilizowanyamazisha, lakini bado waling'ang'ania ukafiri. Kisha akawaita kwenye maapizano, lakini wao wakaona bora watoe kodi kwa unyonge, kuliko kuikubali haki.

Pamoja na yote hayo alijitahidi ili waamini; kama ilivyo kawaida yake na kila mpinzani mpaka Mwenyezi Mungu akamwambia: "Na wengi katika watu hawatakuwa wenye kuamini hata ukijitahidi vipi." (12:103) "Hata ukiwa na jitihada ya kuwaongoza, lakini Mwenyezi Mungu hamuongozi yule anayepoteza." (16:37)

Kwa kutilia mkazo hoja kwa wapinzani na kuwadhihirishia hakika mbele ya Mtume na watu wote, ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia kuwa aachane na kujadiliana nao na kuapizana nao,na afuatane nao na njia hii ambayo anaishuhudia kila mwenye akili kuwa ni haki na uadilifu, bali ni njia ya wazi.

Njia yenyewe ni kuwaita kwenye lile linalokubaliwa na akili na vitabu vya dini kuwa nyote mlingane sawa katika kumwabudu Mwenyezi Mungu pekee asiye na mshirika; na wala wengine wasiwaabudu wengine. Pia baadhi ya watu wasiwe juu ya wengine. Na hili ndilo neno la uadilifu.

Wakikataa semeni: "Shuhudieni kuwa sisi ni Waislamu."

Yaani kama hawakukubali hata dhahiri hii na kuwa na inadi ya ushirikina, basi achana nao, na wewe pamoja na wale waliokuamini waambieni, sisi ni Waislamu. Kuwashuhudisha makafiri kuhusu uislamu wa waislam, kuna faida mbili:

1. Kuwatambulisha makafiri kwamba wao hawawajali na ukafiri wao na kwamba Muhammad na walio pamoja naye wanaiamini haki na kuitumia hata kama watakufuru watu wa Mashariki na Magharibi.

2. Kuonyesha kuwa waislamu wanatofautiana na wengine kwa kumwabudu Mwenyezi Mungu mmoja pekee, wala hawafanyi baadhi kuwa waungu kinyume na Mwenyezi Mungu, au kuweko na yeyote mwenye mamlaka ya kuhalalisha, kuharamisha na kufuta madhambi; kama ilivyo kwa wasiokuwa waislamu.

Enyi watu wa Kitab! Kwa nini mnabishana juu ya Ibrahim, na hali Tawrat na Injil havikuteremshwa ila baada yake? Basi hamfahamu?
Qur'an imewajadili watu wa Kitabu kwa akili na mantiki, kwenye maapizano na kwenye neno la usawaambalo ni kumwamini Mungu peke yake. Kisha ikarudia tena mjadala na watu wa Kitabu; kama kawaida yake kulieleza jambo, halafu kueleza jengine hatimaye kulirudia lile la kwanza. Imerudia kuelezea kauli za watu wa Kitab na ubatilifu wake. Imetaja kauli ya mayahudi kwamba Ibrahim alikuwa myahudi na kauli ya manaswara kwamba Ibrahimu alikuwa mnaswara.

Qur'an Imejibu madai haya waziwazi, kuwa uyahudi ulitokea baada ya Musa, na baina ya Musa na Ibrahim kulikuwa na miaka elfu mbili. Unaswara nao ulizuka baada ya Isa na baina ya Isa na Ibrahim kuna miaka elfu; kama ilivyoelezwa katika Tafsir Rawhul bayan basi itakuwaje aliyetangulia awe katika dini ya aliyekuja nyuma? Basi hamfahamu?

Kauli ya wayahudi na wanaswara inatukumbusha kichekesho kimoja wanachokisimulia walebanon: Kwamba watu wawili walikuwa wakisafiri pamoja. Walipokuwa wakizungumza mmoja akamuuliza mwenzake:

• "Umewahi kuhiji Makka Tukufu?"

• "Ndio, nimetekeleza Al-hamdulillah"

• " Umeona Zamzam huko?"

• "Ndio, ni msichana mzuri sana!"

• " Vipi wewe, si msichana! Ni kisima cha maji bwana!

• " Ah! Basi wamekichimba baada ya kuhiji mimi."

Hekaya za madhehebu na vikundi vilivyozuka baada ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) zinafanana kidogo na hoja za mtu huyo. Kila anayechukua dini yake kutoka kwa mtu yeye huwa ni aina hii isipokua kama itamthibitikia nukuu kutoka kwa Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) kama vile kuthibiti Hadith Thaqalayni ambayo imewajibisha kufanya ibada kwa kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlul Bait wa Mtume. Na ikavifanya sawa viwili hivyo . Tumeyafafanua hayo katika tafsir ya (2:39).

Je, nyinyi ni wale mliojadiliana katika lile ambalo mnalolijua. Mbona (sasa) mnabishana katika lile msilolijua na Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye na nyinyi hamjui (kitu).

Mtu anaweza akahusika kujua jambo fulani au maudhui fulani. Hapo anaweza kujadiliana na kubishana; na wala sio lazima awe yuko sawa katika maneno yake na mjadala wake wote, isipokuwa la muhimu ni kuwa awe anajua japo kwa ujumla. Ama kujadiliana na kubishana katika jambo asilolijua kabisa, basi ni ujinga na upumbavu.

Watu wa Kitab wana dini yao wanayoitakidi; kwa hiyo kuna uwezekano wa kufanya mjadala unaohusiana na dini zao ijapokuwa kwa dhahiri lakini kufanya mjadala kuhusu dini ya Ibrahim hakuna njia yoyote hata kwa dhahiri, kwa sababu wao hawajui chochote.

-Ibrahim hakuwa myahudi wala mnaswara (mkristo) lakini alikuwa mwenye kuachana na dini potofu, na kushikamana haki, mwislamu wala hakuwa katika washirikina.

Hakuwa myahudi kwa sababu, baina yake na Musa kulikuwa miaka elfu, wala itikadi yake haiambatani na dini ya kiyahudi, kwa sababu imegeuzwa sio ile aliyokuja nayo Musa (a.s.). Wala hakuwa mkristo, kwa sababu baina yake na Isa ilipita miaka elfu mbili wala itikadi yake haiambatani na itikadi ya dini ya kimasihi, kwa sababu imegeuzwa, siyo aliyokuja nayo Isa (a.s.).

Ikiwa Ibrahim hakuwa mwislamu kwa maana iliyozoeleka, lakini alivyo yeye alikuwa mwislamu na imani yake inaambatana na imani ya uislamu. Kwa sababu, alikuwa akimwamini Mwenyezi Mungu na kumtakasa na shirk na kufananisha.

Na huu ndiyo msingi wa asili ya dini ya Kiislam. Kwa hiyo, linabainika jibu la swali la atakayeuliza: Kwa nini Ibrahim ni mwislamu na Qur'an imeteremshwa baada yake? Umetangulia ufafanuzi kwamba Mitume wote walikuwa waislamu katika tafsir ya Aya ya 19 ya Sura hii.

Ama kauli yake Mwenyezi Mungu Hakuwa katika washirikina, ni kuwapinga wanaswara waliosema kuwa Masih ni mtoto wa Mungu wayahudi waliosema na Uzair ni mtoto wa Mungu na waarabu waliokuwa wakiabudu masanamu, vikundi vyote hivi vitatu vilijihusisha na Ibrahim.

Hakika watu wanaomkurubia zaidi Ibrahim ni wale waliomfuata Mtume huyu na walioamini pamoja naye.

Yaani wenye haki ya kujinasibisha na dini ya Ibrahim ni wale walioitikia mwito wake au wale ambao itikadi yao inaambatana na yake; kama Muhammad na walio pamoja naye. Imamu Ali anasema: "Hakika watu walio karibu zaidi na manabii ni wale wanaojua zaidi waliyokuja nayo, kisha akasoma Aya hii akaendelea kusema: "Hakika mpenzi wa Muhamamd ni yule anayemtii hata kama yuko mbali naye kiudugu; na hakika adui wa Muhammad ni yule anayemwasi Mwenyezi Mungu, hata kama akiwa karibu naye Muhammad kiudugu."

Na Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa waumini, wale wanaomwamini Yeye bila ya kuwa na mshirika; na wala hawamtegemei yeyote kwa kuondolewa madhara na kutaka manufaa.

Hakuna kitu kinachofahamisha utukufu wa Imam Ali (a.s), ikhlasi yake, na kuepukana kwake na malengo ya kidunia, kuliko kauli hii na kuacha kujiambatanisha na udugu ingawaje anajua kuwa yeye ndiye mtu wa karibu zaidi na Mtume kwa udugu. Yeye anategemea utukufu kutokana na nafsi yake na amali yake tu, na wala sio kutafuta asili na udugu au kwa kufunika mambo.

وَدَّتْ طَائِفَةٌ مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ لَوْ يُضِلُّونَكُمْ وَمَا يُضِلُّونَ إِلَّا أَنْفُسَهُمْ وَمَا يَشْعُرُونَ {69}

Kikundi katika watu wa Kitabu wanapenda kuwapoteza; wala hawapotezi ila nafsi zao, na hali hawatambui.

يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لِمَ تَكْفُرُونَ بِآيَاتِ اللَّهِ وَأَنْتُمْ تَشْهَدُونَ {70}

Enyi watu wa Kitabu! Mbona mnazikataa Ishara za Mwenyezi Mungu na, hali nyinyi mnashuhudia?

يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لِمَ تَلْبِسُونَ الْحَقَّ بِالْبَاطِلِ وَتَكْتُمُونَ الْحَقَّ وَأَنْتُمْ تَعْلَمُونَ {71}

Enyi watu wa Kitabu! Mbona mnaichanganya haki na batili, na mnaficha haki na hali mnajua?