read

Aya 7 - 9

Yeye ndiye aliyekuteremshia Kitabu ndani yake zimo Aya zilizo waziwazi nazo ndizo msingi wa kitabu. Na nyingine zenye kufichikana.

Zilizo waziwazi ni Aya ambazo hazihitaji ufafanuzi na makusudio yake yanafahamika kwa njia ya mkato bila ya kuhitaji tafsiri, kuhusisha au kufutwa hukumu (Naskh). Wala haziwapi nafasi wale wenye maradhi ya kupoteza na kufikiri kwa taawili na kugeuza. Mfano: sema Yeye Mwenyezi Mungu ni mmoja … Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila jambo … Wala hadhulumu (hata amali) sawa na chembe Hakika Mwenyezi Mungu haamrishi uovu … Na kwamba Kiyama kitakuja hakuna shaka.

Na Aya nyenginezo ambazo anaweza kuzifahamu mwenye elimu na asiyekuwa na elimu. Ama Aya zenye kufichikana ziko aina nyingi: Kuna zinazofahamika kiujumla bila ya upambanuzi, mfano kauli yake Mwenyezi Mungu: Na tukampulizia katika roho yetu … (21:91)

Kwa hakika kujua roho yenyewe hasa ni nini, hiyo ni siri ya Mungu haijui yeyote hata wataalamu pia. Na wala sio sharti anayeambiwa kitu kuwa lazima ajue anayoambiwa kwa upambanuzi, bali inatosha tu kufahamu kiujumla.

Nyengine ni zile zinazofahamisha jambo linalokataliwa na akili mfano, kauli yake Mwenyezi Mungu: "Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema amestawi juu ya kiti cha enzi." (20:5)

Hapa akili inakataa kwamba Mwenyezi Mungu akae juu ya kiti, kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni zaidi ya wakati na mahali. Kwa hiyo hapo inabidi kuleta tafsiri kwa maana ya kutawala. Na hapana budi kuwa tafsiri (taawil) iwe ni dalili sahihi itakayotoa maana sahihi ya tamko; na hayo hawayajui isipokuwa watu maalum.

Aya nyingine iliyofichikana, ni kukubali tamko baina ya maana mbili na zaidi, mfano: Na wanawake walioachwa wangoje mpaka tohara tatu (2: 228). Hapo kuna 'Quruw' ambalo linakubali maana ya tohara na hedhi.

Nyengine ni kuwa tamko ni la kiujumla maana yake ya dhahiri yawaingiza wote ingawaje makusudio ni baadhi tu; mfano: "Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikatwe mikono yao" (5:38)

Hapo wametajwa wezi wote pamoja na kujulikana kuwa kuna wezi wengine hawakatwi; kama ikiwa mwizi ni baba wa aliyeibiwa, au mwaka wa njaa, au kilichoibwa kikiwa hakikuhifadhiwa, au thamani ya kilichoibiwa ikiwa chini ya robo dinari.

Nyengine ni kufutwa hukumu na kuwekwa nyengine; kama vile kuswali kuelekea Baitul Maqdis, ambapo ilifahamika kuthibiti Kibla hiki na ikaendelea hukumu mwanzoni mwa uislam, kisha ikaja hukumu ya kufuta hilo na Kibla kikawa Al-kaaba.

Sio sharti kutotarajiwa kujulikana Aya za kufichikana kabisa. Kwani aina zote ukiondoa ile ya kwanza, inawezekana kwa wanavyuoni wa Usul - wanaojua njia za taawili, hukmu za kuhusisha na za kiujumla, kufuta na kufutwa na kutilia nguvu baina hukumu mbili zinazopingana - kutoa hukmu za kuhusisha na za kiujumla, kupambanua baina ya kufuta na kufutwa, chenye nguvu na kisicho na nguvu na maana yanayoingilika akilini ambayo yamefanyiwa taawili baada ya kutoingilika akilini.

Ndio! Kwa asiyekuwa na elimu, hizo Aya za kufichikana zinabaki kuwa hivyo hivyo, kwa kuwa haijuzu kufanya taawili au kuchukua dhahiri inayokubali kuhusisha au kufutwa. Kwa ufupi ni kuwa wanavyuoni wanajua maana ya Qur'an ambayo kwao ni fasihi iliyo wazi. Kwa sababu haiwezekani kuwa Mwenyezi Mungu ateremshe maneno yasiyokuwa na maana au yasiyofahamiwa na yeyote. Itakuwaje hivyo ikiwa yeye mwenyewe Mwenyezi Mungu anaamrisha kuizingatia vizuri Qur'an; na mazingatio hayaji ila kwa kinachoingilika akilini; na kisichofahamika hakiwezi kuzingatiwa.

Unaweza kuuliza kuwa Mwenyezi Mungu amekisifu Kitabu Chake kitukufu kwamba Aya zake zote ni Muhkam (zenye maana wazi) pale alipotumia neno Uhkimat (11:1) Tena akasifu kuwa Aya zake zote ni Mutashabihat (zenye kufichikana) kwa kutumia neno Mutashabihat (39: 29). Na katika Aya hii tunayofasiri amekisifu kuwa baadhi yake ni zenye kufichikana na nyengine ziko wazi wazi. Je, Kuna njia gani ya mkusanyiko wa Aya hizi?

Jibu: Makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu katika neno Uhkimat ni kuwekwa kwa mpango na kwamba yote ni fasaha iliyo na maana sahihi. Kwa hiyo tafsiri ni:"(Hiki) ni Kitabu ambacho Aya zake zimepangwa vizuri".

Makusudio ya Mutashabihat (kufichikana) ni kibalagha na kimwongozo. Kwa hiyo tafsiri ni: "Kitabu chenye kushabihiana."
Na kuwa nyengine ni Muhkamat na nyengine ni Mutashabihat, ni kama tuliyvotangulia kuelezea kuwa ni baadhi ziko wazi na baadhi zinatatiza zinazohitaji tafsir na tafsir inahitaji maarifa na elimu.

Kwa hiyo hakuna mgongano baina ya Aya hizo tatu; ni kama mfano wa mwenye kusema: "Napenda safari, wala sipendi safari" lakini anakusudia kuwa anapenda safari katika nchi kavu lakini hapendi safari ya baharini. Sufi mmoja aliisema kumwambia Mola wake: Ee Mungu nimuonaye, hali yeye hanioni. Ee Mungu anionaye, wala mimi simuoni.

Anakusudia kwamba anamuona Mwenyezi Mungu akimfadhilisha lakini Mwenyezi Mungu hamuoni yeye akimtii, na Mwenyezi Mungu anamuona akimuasi wala yeye hamwoni akimwadhibu.

Swali la pili, nini makusudio ya msingi wa Kitabu? Jibu: Baada ya Mwenyezi Mungu kuelezea kwamba katika kitabu chake kuna Aya zenye kutatiza, ndipo akasema; lakini Aya za misingi ya itikadi - kama vile kumwamini Mwenyezi Mungu na kumwepusha na mshirika vilevile kuuamini utume wa Muhammad (s.a.w.) na siku ya mwisho - ziko wazi zenye kubainisha makusudio bila ya mikanganyo yoyote; wala hazina nafasi ya kufanyiwa taawili, kuhusishwa au kuwa imefutwa hukumu yake; anaweza kuzifahamu mjuzi na asiyekuwa mjuzi; wakati huo zikiwa ni msingi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa sababu zinaeleza itikadi, na nyenginezo ni matawi.

Kwa hiyo hakuna udhuru wowote kwa ugeni wa Yemen na wengineo kutaka Aya za kutatiza; kama vile Aya inayomsifu Isa kuwa roho wa Mwenyezi Mungu na kuacha Aya zilizo wazi-wazi zinazokanusha uungu wa Isa. Hakuna lolote kwa mwenye kujitia kutojua Aya wazi- wazi na kutaka Aya zinazotatiza isipokuwa ni maradhi ya moyo na kukusudia ufisadi tu.

Swali la tatu: Kwa nini amesema: Msingi wa kitabu na asiseme Misingi ya kitabu.

Jibu: Amefanya umoja kwa kubainisha kwamba mkusanyiko wa Aya zote nyepesi kufa- hamika ni msingi wa Kitabu na wala sio Aya moja pekee kuwa ni msingi; mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu.

"Na tulimfanya mwana wa Maryam na mama yake ishara." (23:50). Ishara moja, wala hakusema ni ishara mbili, kwa sababu kila mmoja ni fungu la kutimiza ishara kwa hiyo mama hawezi kuwa ishara bila ya mwana, na mwana hawezi kuwa ishara bila ya mama.

Wale ambao nyoyoni mwao mna upotofu wanafuata zile zinazotatiza kwa kutaka kuharibu na kutaka tafsiri yake.

Makusudio ya upotofu hapa ni kuiacha haki, na kutaka kuharibu ni ishara ya kwamba wenye makusudio mabaya wanatafuta yale yenye kutatiza na kuyafasiri kwa tafsiri ya kuharibu nyoyo na kuharibu watu na dini ya haki, kwa mfano wanatoa ushahidi kwa kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na tukampulizia roho yetu" kwamba Masih ni jinsi ya Mwenyezi Mungu kwa sababu kila mmoja ni roho, na wanajitia kutojua Aya zilizo waziwazi mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu:

"Hakika wamekufuru wale waliosema: Mwenyezi Mungu ni Masih mwana wa Maryam." (5:17)
"Hakuwa Masih ila ni Mtume, na wamepita Mitume kabla yake, na mama yake ni mkweli." (5:75)
"Hakika mfano wa Isa mbele za Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam; alimwumba kwa udongo kisha akamwambia kuwa akawa." (3:59) Zaidi ya hayo kuna Aya inayomuhusu Adam, isemayo: "Nikishamkamilisha na kumpuliza roho yangu …" (15:29)

Kwa hiyo basi kutokana na madai yao, Adam pia atakuwa ni Mungu. Katika Majmaul-bayan imeelezwa kuwa mwanzo wa Sura Al-imran mpaka zaidi ya Aya themanini, zimeshuka kwa ugeni wa Najran. Walikuwa watu sitini, wakafika Madina kwa Mtume. Ulipofika wakati wao wa kuswali walipiga kengele na wakaenda kuswali katika msikiti wa Mtume. Masahaba wakasema: "Mbona wanaswali msikitini kwako?" Mtume akasema: "Waacheni." Basi wakaswali wakielekea Mashariki.
Walipomaliza kuswali, Mtume alimwambia Seyyid na Aqib ambao walikuwa viongozi wa msafara na majibizano yakawa kama hivi ifuatavyo:

Mtume : Silimuni wakristo: Wakristo: Tumekwisha silimu .
Mtume : Mmesema uongo, si waislamu kwa kudai kwenu kuwa Mwenyezi Mungu ana mtoto,
kuabudu msalaba na kwa kula nyama ya nguruwe.
Wakristo : Ikiwa Isa si mtoto wa Mwenyezi Mungu, basi baba yake ni nani?
Mtume : Hamjui kwamba mtoto hufanana na baba yake?: "Hamjui kwamba Mwenyezi Mungu
yuko hai, hafi? Na Isa alitoweka?
Wakristo : "Ndio."
Mtume : Hamjui kwamba Mwenyezi Mungu ni msimamizi wa kila kitu?
Wakristo : Ndio
Mtume : Je, Isa anaweza hivyo?
Wakristo : La!
Mtume : Hivi hamjui kuwa Mwenyezi Mungu hali, hanywi wala haendi chooni?
Wakristo : Ndio
Mtume : Hamjui kuwa Isa alichukuliwa mimba na mama yake, kama wanawake wengine,
akanyonyeshwa na akalishwa chakula na kwamba Isa anakula ana kunywa na kwenda haja?
Wakristo : Ndio
Mtume : Basi atakuwaje Mungu?
Wakristo : Wakanyamaza wasiwe na la kusema. Ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha kuwahusu,
mwanzoni mwa Sura Al-imran kiasi cha Aya thamanini.

Na hajui tafsiri yake isipokuwa Mwenyezi Mungu na waliozama katika elimu.

Baadhi ya watu wanasema ni wajibu kuweka kituo kati ya neno Mwenyezi Mungu na waliozama; na kwamba waliozama ni maneno yanayoanza upya; kwa maana ya kuwa Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayejua Aya zenye kutatiza, na sio waliozama katika elimu.

Kitu cha kuangalia katika kauli hii ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni Mwenye hekima, hawezi kuwaambia watu wasivyovijua na asivyotaka wajue; kama tulivyobainisha. Kwa hiyo sahihi ni kuwa neno 'waliozama katika elimu, linaugana na Mwenyezi Mungu; na kwamba maana yake ni anajua tafsiri yake Mwenyezi Mungu na waliozama katika elimu. Amirul-muminin Ali (a.s.) anasema: "Hiyo ni Qur'an iliyonyamaza na mimi ni Qur'an inayosema."

Na Ibn Abbas alikuwa akisema: "Mimi ni miongoni mwa waliozama kaitka elimu; mimi nina- jua tafsiri yake …"

Kwa ujumla ni kwamba mwenye elimu ya haki ni yule anayeepuka kusema bila ya ujuzi. Bali huko kuzama katika elimu ni kuepuka kusema bila ya ujuzi. Iko Hadith isemayo: "Kuepuka yenye kutatiza ni bora kuliko kujingiza katika maangamizi."

Unaweza kuuliza kwa nini Mwenyezi Muangu (s.w.t.) amefanya baadhi ya Aya za Qur'an ziwe wazi na nyengine zilizofichika? Kwa nini asizijalie kuwa waziwazi zote? Ili aweze kufa- hamu mjuzi na asiyekuwa mjuzi?

Swali hilo limejibiwa kwa majibu mengi, lenye nguvu zaidi ni kwamba mwito wa Qur'an unamwelekea mjuzi na asiye na ujuzi, mwerevu na mjinga; na kwamba katika maana yako yaliyo maarufu na yenye kuzoeleka na wote hawahitajii elimu na kujifunza katika kuyajua; yanaweza kueleweka kwa ibara iliyo wazi anayoifahamu kila anayeambiwa. Maana nyengine yako ndani yasiyoweza kufahamiwa ila baada ya darasa na elimu. Wala haiwezekani kufahamika bila ya maandalizi hayo.

Hakika hii anaifahamu kila mtu. Basi hayo ndiyo yaliyofanya kuwa baadhi ya Aya ziwe dhahiri na nyengine za ndani; kuongezea kuwa mara nyengine hekima inataka kuweka maana ya ndani; kama kusema kwake Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume wake.

Hakika sisi au nyinyi tuko kwenye uongofu au upotevu ulio wazi (34:24)

Husema: "Tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu."
Hii ni jumla iliyoanza upya. Maana yake ni kuwa mjuzi wa haki husema kuwa Aya zilizo- fichikana na zile nyepesi zote ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na mwenye kuziacha nyepesi na kujishughulisha na za kutatiza tu, kwa kutaka kuharibu basi huyo ni mfisadi mwenye maradhi ya moyo.

Na hawakumbuki isipokuwa wenye akili

Wale ambao wanajua hekima katika kupatikana za waziwazi na zisizowazi katika Qur'an wala hawazifanyi zile zilizo wazi kuwa ni njia ya kupoteza.

"Mola wetu! Usizipotoshe nyoyo zetu baada ya kutuongoza na utupe rehema kutoka kwako. Wewe ndiwe mpaji mkuu."

Hiyo ni dua anayoiomba kila mjuzi mwenye ikhlasi kwa kuhofia asiingie makosani na kufanya uzembe katika kutafuta yaliyo sawa.

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَنْ تُغْنِيَ عَنْهُمْ أَمْوَالُهُمْ وَلَا أَوْلَادُهُمْ مِنَ اللَّهِ شَيْئًا ۖ وَأُولَٰئِكَ هُمْ وَقُودُ النَّارِ {10}

Hakika wale ambao wamekufuru hazitawafaa kitu mali zao na watoto wao kwa Mwenyezi Mungu; na hao ndio kuni za Moto.

كَدَأْبِ آلِ فِرْعَوْنَ وَالَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ ۚ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا فَأَخَذَهُمُ اللَّهُ بِذُنُوبِهِمْ ۗ وَاللَّهُ شَدِيدُ الْعِقَابِ {11}

Kama desturi ya watu wa firauni na wale waliokuwa kabla yao. Walikadhibisha Aya zetu. Mwenyezi Mungu akawatia adabu kwa sababu ya dhambi zao; na Mwenyezi Mungu
ni Mkali wa kuadhibu.

قُلْ لِلَّذِينَ كَفَرُوا سَتُغْلَبُونَ وَتُحْشَرُونَ إِلَىٰ جَهَنَّمَ ۚ وَبِئْسَ الْمِهَادُ {12}

Waambie wale waliokufuru: Mtashindwa na mtakusanywa mtiwe kwenye Jahannam; nako ni makao mabaya.

قَدْ كَانَ لَكُمْ آيَةٌ فِي فِئَتَيْنِ الْتَقَتَا ۖ فِئَةٌ تُقَاتِلُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَأُخْرَىٰ كَافِرَةٌ يَرَوْنَهُمْ مِثْلَيْهِمْ رَأْيَ الْعَيْنِ ۚ وَاللَّهُ يُؤَيِّدُ بِنَصْرِهِ مَنْ يَشَاءُ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَعِبْرَةً لِأُولِي الْأَبْصَارِ {13}

Hakika ilikuwa ni ishara kwenu katika yale makundi mawili yalipokutana. Kundi moja likipigana katika njia ya Mwenyezi Mungu na jingine kafiri, likawaona mara mbili zaidi kuliko wao kwa kuona kwa macho hakika katika hayo kuna mazingatio kwa wenye basara.