read

Aya 72-74: Kuamini Asubuhi Na Kukufuru Jioni

Maana

Kikundi katika watu wa Kitabu kilisema: Yaaminini yale waliyoteremshiwa wale walioamini, mwanzo wa mchana na yakataeni mwisho wake, huenda wakarudi nyuma.

Yaani warudi nyuma Waislamu. Aya inaonesha hadaa na njama walizokuwa wakizifanya viongozi wa watu wa Kitabu. Wakidhihirisha uislamu Asubuhi na kurtadi jioni, ili angalau waweze kuzitia shaka baadhi ya nafsi dhaifu za waislamu, ziseme kuwa lau si kuwa wameona Muhammad si mkweli wasingelitoka katika uislamu baada ya kusilimu.

Unaweza kuuliza; je, waliwahi kufanya hila zao hizi walizozipanga, au ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimpa habari Mtume wake na kuwafedhehesha kabla ya kuzitekeleza?

Jibu: Inavyofahamisha Aya ni kwamba wao walisema. Ama kuwa walifanya baada ya kusema au hawakufanya; hayo yamenyamaziwa na Aya. Na, sisi vilevile tunayanyamazia yale aliyoyanyamazia Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo basi hakuna wajihi wowote wa waliyoyaeleza baadhi ya wafasiri kwamba wao waliswali Swala ya asubuhi pamoja na Mtume kisha wakarejea jioni na kuswali sala yao ili watu waone kuwa wao wameona upotevu, isipokuwa kama ni riwaya sahihi.

Wala msimwamini ila yule anayefuata dini yenu.

Baadhi wameifahamu vibaya Aya hii na kuitolea ushahidi kuwa ni katika maneno ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na kwamba eti sio maneno ya mayahudi, bali hata nimemsikia mtu zaidi ya mmoja akisema Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alikusudia kwa Aya hii kuwa tusimwamini yeyote isipokuwa aliye kwenye dini yetu.

Ilivyo hasa ni kwamba Aya hii ni sehemu ya maneno ya wapinzani wenye vitimbi katika watu wa Kitabu. Mwenyezi Mungu ameyanukuu kwa kuwasimulia wao; yaani baadhi ya watu wa Kitabu waliwaambia wengine:"Silimuni mchana na mkufuru jioni." Vilevile wakasema: "Wala msimwamini ila yule anayefuata dini yenu."

Sema hakika uongozi hasa ni uongozi wa Mwenyezi Mungu.

Jumla hii imeingia kati, aliyoambiwa Mtume na Mwenyezi Mungu kabla ya kumalizika masimulizi. Makusudio yake ni kujibu jaribio la watu wa Kitab na hadaa yao ya kudhihirisha uislam, kisha kurtadi, ili kuzitia shaka baadhi ya nafsi dhaifu za wafuasi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.).

Kwamba hadaa hii haina lolote. Kwa sababu uislam hauwezi kuondolewa au kuyumbishwa na vitimbi na hadaa. Mwenyezi Mungu anasema: "Na ambaye ameongozwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumpoteza" (39:37)

Kuwa atapewa yeyote mfano wa mliyopewa nyinyi au wawahoji mbele ya Mola wenu.

Huu ndio mwisho wa masimulizi ya watu wa Kitabu hapa. Kwa ufupi ni kuwa viongozi wa watu wa Kitabu walikuwa wakiitakidi kwamba inawezekana Mwenyezi Mungu kumpeleka Mtume asiyekuwa mwisrail; na kwamba haukusimama kwao tu. Lakini baada ya kuja Muhammad (s.a.w.) walidhihirisha hasadi na wivu, ati vitabu vyao na dini yao inawajibisha Mtume awe ni katika Bani Israil tu.

Walidhihirisha hayo wakiwa wanajua kuwa wao ni waongo tena wataaadhibiwa na kuhojiwa kesho mbele ya Mwenyezi Mungu. Wakaogopa haya yasiwafikie waislamu wasije wakapata nguvu. Kwa hiyo baadhi yao wakawaambia wengine: Tahadharini kusema mbele za waislam kwamba sisi watu wa Kitab tunaitakidi kuwa inawezekana kuletwa Mtume asiyekuwa mwisrail. Au kusema mbele ya waislam kuwa sisi tutahojiwa na kushindwa kesho kwa sababu ya kuficha kwetu haki na kuipinga.

Kwa maneno mengine ni kwamba watu wa Kitabu hasa mayahudi walijua kabisa kuwa wao wako katika upotevu kwa sababu ya kumkadhibisha kwao Muhammad (s.a.w.w.) na wakaogopa kuwafahamisha waislam hakika hii. Ndipo wakausiana kuficha upotevu wao na kuonyesha kuwa Mtume hawi na hatakuwa mwarabu.

Hii ndiyo tabia ya mayahudi tangu walipopatikana hadi leo na mpaka siku ya mwisho. Wanasema uongo huku wakijua kuwa wao ni waongo, wakijificha kwa kuleta mikanganyo.

Lakini mara moja wanafedheheka. Wala Qur'an sio kitabu pekee kilichosajili makosa na uchafu wao, bali vitabu vyote vya kidini hasa Injil, vitabu vya historia, magazeti na idhaa; zote hizo zimekariri historia yao mbaya.

Hii ndiyo siri ya kuwekewa vikwazo na kuteswa na uma mbali mbali; kuanzia Fira'un hadi Hitler. Hakuna taifa lolote duniani kuanzia zamani hadi sasa lililoungana nao isipokuwa Amerika tu, "Kwa sababu kufanana na kitu kunavutiana".

Sema hakika fadhila iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humpa amtakaye na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mjuzi.

Wafasiri wanasema makusudio ya fadhila hapa ni kuhusishwa utume; na kwamba kuko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humchagua kumpa utume yule anayefaa, awe mwisrail au mwarabu; na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu amekwishawajibu mayahudi waliotangaza kwamba Mungu hapeleki mtume isipokuwa kutokana na wao.

Haya ndiyo waliyoyasema wafasiri na wakatoa dalili kwamba mfumo wa Aya unafahamisha hilo. Kwa sababu uko katika mazungumzo ya watu wa Kitabu, madai yao ya uongo na hila zao.

Lakini tunavyoona sisi ni kuwa neno fadhila katika Aya linabaki katika ujumla wake; na kwamba linakusanya utume, hekima, uongofu, uislam na mengineyo. Linathibiti katika kujibu mayahudi; kama vile linavyothibiti kiujumla. Kwa sababu utume ni katika jumla ya mafungu ya fadhla.

وَمِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ مَنْ إِنْ تَأْمَنْهُ بِقِنْطَارٍ يُؤَدِّهِ إِلَيْكَ وَمِنْهُمْ مَنْ إِنْ تَأْمَنْهُ بِدِينَارٍ لَا يُؤَدِّهِ إِلَيْكَ إِلَّا مَا دُمْتَ عَلَيْهِ قَائِمًا ۗ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا لَيْسَ عَلَيْنَا فِي الْأُمِّيِّينَ سَبِيلٌ وَيَقُولُونَ عَلَى اللَّهِ الْكَذِبَ وَهُمْ يَعْلَمُونَ {75}

Na katika watu wa Kitabu yuko ambaye ukimwamini na mrundo wa mali atakurudishia. Na katika wao yuko ambaye ukimpa amana ya dinari moja hakurudishii, isipokuwa ukimsimamia hayo ni kwa kuwa walisema: "Hatuna lawama kwa wasiojua kusoma" Na wanamzulia uwongo Mwenyezi Mungu, na hali wanajua.

بَلَىٰ مَنْ أَوْفَىٰ بِعَهْدِهِ وَاتَّقَىٰ فَإِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُتَّقِينَ {76}

Sivyo hivyo, bali anayetimiza ahadi na akamcha Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu huwapenda wacha Mungu