read

Aya 77: Asiye Na Ahadi Hana Dini

Maana

Arrazi anasema katika kufasiri Aya hii: "Yanaingia katika Aya hii yote aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu, yale aliyoyatolea hoja, yaliyochukuliwa kutoka upande wa Mtume na yanaingia yale yanayomlazimu mtu mwenyewe. Kwa sababu yote hayo ni katika ahadi ya Mwenyezi Mungu ambayo ni lazima kuitekeleza."

Katika Hadith imeelezwa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) hakuhutubia hotuba yoyote isipokuwa alisema: "Asiye kuwa na uaminifu hana imani na asiyekuwa na ahadi hana dini."

Aya hii na Hadith hii na nyinginezo zinatufahamishia kuwa Uislam unafungamana na tabia na maadili; ndipo ukawajibisha kutekeleza mambo yote ya lazima ya kuamiliana na wengine; na ukakuzingatia kuwa ni kuamiliana na Mwenyezi Mungu, hata kama ni kuamiliana na mlahidi kwa sharti ya kuwa muamala wenyewe usipingane na misingi ya kimaadili; vinginevyo kutakuwa ni batili hakufai.

Vilevile kwa upande wa hukumu, ambapo uislam umemwajibishia kadhi kusikiliza sauti ya dhamiri na hoja ya kitabia kabla ya kusikiliza kauli ya wanaogombana.

Nadharia ya tabia; ndio mkazo wa kwanza wa sharia za kiislamu kwa kawaida zake zote na hukmu zake. Kwa ajili hii Mwenyezi Mungu amewatishia wale wanaovunja ahadi na wasiokuwa na uaminifu kwa kitisho ambacho hakumtisha yeyote katika wafanyao madhambi makubwa; pale aliposema:

Hao hawatakuwa na sehemu yoyote akhera, wala Mwenyezi Mungu hatasema nao wala hatawatazama siku ya kiyama wala hatawatakasa, nao watapata adhabu iumizayo.

Ama siri ya kuhimiza huku na kutoa tisho kwa wasiotekeleza ahadi ni kuchunga maslahi ya watu, kuweko kutegemeana kati ya watu na kuchunga haki, mambo ambayo ndio msingi wa amani na nidhamu.

وَإِنَّ مِنْهُمْ لَفَرِيقًا يَلْوُونَ أَلْسِنَتَهُمْ بِالْكِتَابِ لِتَحْسَبُوهُ مِنَ الْكِتَابِ وَمَا هُوَ مِنَ الْكِتَابِ وَيَقُولُونَ هُوَ مِنْ عِنْدِ اللَّهِ وَمَا هُوَ مِنْ عِنْدِ اللَّهِ وَيَقُولُونَ عَلَى اللَّهِ الْكَذِبَ وَهُمْ يَعْلَمُونَ {78}

Na hakika miongoni mwao kuna kundi linalopinda ndimi zao kwa Kitabu ili mpate kuyadhani hayo kuwa ni ya Kitabu wala si ya Kitabu. Na wanasema: Haya yametoka kwa Mwenyezi Mungu, na hali hayakutoka kwa Mwenyezi Mungu; na wanasema uwongo juu ya Mwenyezi Mungu na hali wanajua