read

Aya 79-80: Kuweni Watumishi Wa Mungu

Maana

Haiwezekani kwa mtu aliyepewa na Mwenyezi Mungu Kitabu na hekima na Unabii kisha awaambie watu: Kuweni wa kuniabudu mimi badala ya Mwenyezi Mungu.

Hapana mwenye shaka kwamba haiwezekani kwa mtu kupewa kitabu, hukumu na utume kuwaambia watu wamwabudu, kwa sababu hiyo ni kufuru na Mwenyezi Mungu hawachagui makafiri. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: "Na hakika tumewachagua kwa ujuzi juu ya walimwengu wote" (44:32)

Aya hii Tukufu ni jibu la wale wanaowawekea mitume na mawali baadhi ya sifa za Mungu. Vilevile ni ushahidi kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwatakasa Mitume.

Kwamba Mtume ana yakini kuwa yeye ni mja miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu pekee ndiye mwenye kuabudiwa. Sasa itawezekanaje yeye awatake waja wamwabudu yeye au waaabudu Malaika. Yeye anawaamrisha wawe waalimu na watumishi wa Mwenyezi Mungu kwa vitendo.

Imeelezwa katika Hadith kwamba mtu mmoja alimwambia Mtume: "Tukusujudie?" Mtume akajibu: "La, haitakikani kusujudiwa yeyote zaidi ya Mwenyezi Mungu." Mwengine naye alisema: "Je unataka tukuabudu na tukufanye Mungu." Akasema Mtume: "Mwenyezi Mungu anihifadhi na hilo! Sikuamrishwa hivyo wala sisemi hivyo."

Ama kisa cha Imam Ali kuwachoma moto wale waliomnasibisha uungu ni mashuhuri kiasi cha kutohitajiwa kutajwa. Kila mwenye kuwataka watu wamwabudu, basi ni kafiri; na kila mwenye kuwataka wamtukuze kwa makusudio ya kujitukuza na kujiweka juu, basi ni fasiki.

Unaweza kuuliza: "Aya imekusanya matamko matatu: Kitabu, hekima na unabii: na kila tamko maana yake yako wazi hayahitaji tafsir kama yakiwa peke yake. Lakini yakiwa pamoja katika jumla moja na yakaunganishwa, basi yanahitaji tafsir. Kwa sababu, maana yake yanaingiliana; hasa kupewa kitab na unabii. Na tunajua kuwa kuungana maneno kunamaanisha tofauti na kubadilika. Sasa kuna njia gani ya kutofautisha matamko hayo matatu?

Jibu: Makusudio ya Kitabu ni Kitabu kilichoteremshwa na Mwenyezi Mungu kama Tawrat, Zabur, Injil na Qur'an. Makusudio ya hekima ni elimu na sunna za utume. Mwenyezi Mungu anasema Kuhusu Yahya: "Na tulimpa hekima akiwa mtoto (19:12)

Ama unabii maana yake ni maarufu; nao ingawaje unalazimisha kujua Kitabu na Sunna, lakini kuyajua hayo mawili hakulazimishi unabii. Kila nabii anajua Kitabu na Sunna, lakini sio kila anayejua Kitabu na Sunna ni nabii. Aya hii iko katika mfano wa Aya isemayo:"Hao ndio ambao tumewapa Kitabu na hekima na unabii". (6:89).

Lakini kuweni watumishi wa Mwenyezi Mungu kwa kuwa mnafundisha kitabu na kwa kuwa mnakisoma.

Yaani Mtume anawaambia watu kuweni wajuzi wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu, wenye kukitumia na wenye kuwafundisha wengine, Sheikh Muhammad Abduh anasema: "Aya inafahamisha kuwa mtu atakuwa mtumishi wa Mwenyezi Mungu kwa kukijua Kitabu, kukifundisha kwa watu na kukitangaza. Na ni uthibitisho kuwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu hakuwi kwa elimu pekee, bali ni lazima kuwa pamoja na vitendo."

Wala hatawaamrisha kuwafanya Malaika na manabii kuwa waungu.

Yaani Mtume haamrishi wala hatamwamrisha yeyote kuwafanya wengine kuabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu.
Je, atawaamrisha ukafiri baada ya kuwa nyinyi Waislamu?

Wao ni Waislamu kwa sababu wao wamemwamini nabii na wakachukua kauli yake. Mwenye kumwamini nabii yeyote wakati wowote yeye ni mwislamu kwa mujibu wa istilahi ya Qur'an. Ufafanuzi wa hilo umetangulia katika kufasiri Aya ya 19 ya Surah hii.

Mwenye kufuatilia Aya za Qur'an na Hadith za Mtume wa Mungu, ataona kuwa miongoni mwa mambo ya asili yanayojitokeza zaidi, ambayo uislam unatofautiana na dini nyengine, ni kusisitiza kuwa haifai kwa hali yoyote kuinasibisha sifa ya Mungu kwa kiumbe, awe mtume, mfalme au walii.

Siri ya kulitilia mkazo hilo ni kwamba umbile la mtu linapondokea sana kwenye kutopea kama tunavyoshuhudia hilo kwa baadhi ya watu wa dini.

Pamoja na sisitizo hilo, lakini utawakuta waislam waliotopea (Ghulat) na kwamba Waislam leo - tukiwa katika karne ya ishirini - wanawanasibishia wafu mambo ambayo hayafai kuyanasibisha isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu peke yake, asiyekuwa na mshirika.

وَإِذْ أَخَذَ اللَّهُ مِيثَاقَ النَّبِيِّينَ لَمَا آتَيْتُكُمْ مِنْ كِتَابٍ وَحِكْمَةٍ ثُمَّ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مُصَدِّقٌ لِمَا مَعَكُمْ لَتُؤْمِنُنَّ بِهِ وَلَتَنْصُرُنَّهُ ۚ قَالَ أَأَقْرَرْتُمْ وَأَخَذْتُمْ عَلَىٰ ذَٰلِكُمْ إِصْرِي ۖ قَالُوا أَقْرَرْنَا ۚ قَالَ فَاشْهَدُوا وَأَنَا مَعَكُمْ مِنَ الشَّاهِدِينَ {81}

Na Mwenyezi Mungu alipochukua ahadi kwa manabii. Nikiwapa kitabu na hekima; kisha akawajia mtume msadikishaji wa yale yaliyo pamoja nanyi, ni juu yenu kumwamini na kumsaidia. Akasema: Je, mmekubali na mmechukua ahadi yangu kwa hayo? Wakasema: Tumekubali. Akasema: basi shuhudieni, na mimi ni pamoja nanyi katika mashahidi.

فَمَنْ تَوَلَّىٰ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ {82}

Na atakayegeuka baada ya hayo, basi hao ndio mafasiki.

أَفَغَيْرَ دِينِ اللَّهِ يَبْغُونَ وَلَهُ أَسْلَمَ مَنْ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَإِلَيْهِ يُرْجَعُونَ {83}

Je, wanataka dini isiyokuwa ya Mwenyezi Mungu na hali waliomo mbinguni na ardhini wanamtii yeye wapende wasipende. Na kwake yeye watarejeshwa.