read

Aya 81-83: Mshikamano Wa Mitume

Mtume Na Mrekebishaji

Hakuna tofauti kati ya mtume na mrekebishaji katika ukweli wa nia na ikhlasi katika amali. Lakini wanatofautiana kwa kuwa mtume hakosei. Kwa vile yeye anasema na kutenda kwa wahyi utokao kwa Mwenyezi Mungu. Ama mrekebishaji, hufanya kwa kutegemea mtazamo wake na jitihadi yake. Na mwenye kujitahidi hukosea na kusibu.

Kwa hivyo upo uwezekano wa kutofautiana katika jitihadi na mtazamo. Na imesihi kumwondokea jukumu akikosea.

Ama kutofautiana mitume kabisa, hilo haliwezekani. Kwa sababu wote wanategemea chim- buko moja - wahyi unaowaelekea wote. Kwa hivyo mitume ni sawa na wafanyikazi wa serikali katika kufikisha amri kwa wananchi.

Haya yanafungamana na kuwa Mwenyezi Mungu anapopeleka manabii wawili kwenye umma mmoja, wakati mmoja, basi watakuwa ni wenye kuafikiana katika kila kitu; kama ilivyotokea kwa Musa na Harun (a.s.). Na kama watakuwa katika nyakati mbalimbali, watakuwa wanaafikiana wote katika fikra na misingi; kama vile kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Ikiwa kutakuwa na tofauti, basi ni tofauti katika picha yake na katika hukumu za matendo ambazo zinakwenda na wakati. Hata hiyo nayo wanaikubali Manabii wote kuwa ni ukweli na haki na ni dharura. Kwa hivyo basi hakuna tofauti kabisa kati ya manabii wote na ni kwa ajili hiyo ndipo kila mtume alisadikisha nabii mwenzake aliyemtangulia.

Unaweza kuuliza kuwa inawezekana nabii kumsadikisha nabii mwenzake aliyemtangulia. Bali ndivyo ilivyo hasa: sisi tunaamini utume wa Isa na Muhammad; Ibrahim naye akaamini aliyokuja nayo Nuh; Musa akaamini waliyo kuja nayo wote wawili; Isa akaamini waliyokuja nayo wote watatu na Muhammad (s.a.w.w.) akaamini waliyokuja nayo wote. Hili linaingilika akilini sana. Lakini litaingilikaje akili kuwa nabii aliyetangulia amwamini atakayekuja baadae, ambaye bado hajapatikana?

Jibu: Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaampa wahyi Mtume aliyetangulia kwamba Yeye atamtuma Mtume baada yake na kubainisha jina lake na sifa zake. Na ni juu ya yule aliyetangulia kuwatangazia watu wa kizazi alicho yeye katika uma wake ili nao wawatangazie watakaofuatia. Kwa hivyo akija anayefuatia anakuta njia ya kusadikisha imani yake na ujumbe wake imeandaliwa.

Tumeyaeleza haya kuwa ni utangulizi na kurahisisha ufahamu Aya hizi zifuatazo.

Irabu

Inawezekana kusoma Lima kwa kuifanya herufi Lam ni ya Jarri. Kwa maana ya kuwa Mwenyezi Mungu alipochukuwa ahadi kwa manabii kwa kwa ajili kuwapa Kitabu na hikima. Na inawezekana kusoma Lama, kwa fat-ha kuifanya lamu ni ya kuanzia (Mubtada). kwa maana ya, Mwenyezi Mungu alipochukua ahadi kwa manabii: Nikiwapa Kitabu na hekima.

Maana

Na Mwenyezi Mungu alipochukua ahadi kwa Manabii: Nikiwapa kitabu na hekima; kisha akawajia mtume msadikishaji wa yale yaliyo pamoja nanyi, ni juu yenu kumwamini na kumsaidia.

Kutokana na mfumo wa maneno ulivyo inafahamika kuwa makusudio ya manabii hapa ni manabi na wafuasi wao na wala si manabii peke yao. Na makusudio ya mtume ni mtume Muhammad (s.a.w.w.); kama ilivyo Aya nyengine isemayo: "Na walipojiwa na mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwenye kusadikisha yale yaliyo pamoja nao kundi moja miongo- ni mwa wale waliopewa Kitabu lilitupa Kitabu cha Mwenyezi Mungu nyuma ya migongo yao kama kwamba hawajui." (2:101).

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) baada ya kuwabainishia mitume na umma unaowafuata, katika misingi na matawi, alichukua ahadi kwao wote kwamba wamwamini Muhammad (s.a.w.) na wamsaidie; kama ambavyo naye Muhammad anawasadikisha waliomtangulia na vitabu walivyoviacha, kama vile Tawrat na Injil.

Kuchukua ahadi kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa mitume ni kwa njia ya wahyi. Ama kwa wafuasi wa mitume ni kwa kupitia mitume. Yaani kila mtume anachukua ahadi kwa ulama wa umma wake kumwamini Muhammad na kumsaidia. Kwa maelezo ya ndani zaidi ni kwamba kuchukua ahadi kwa anayefuatwa ni lazima kuwe kwa mfuasi. Ikiwa ni wajibu kwa nabii kumwamini Muhammad basi imekuwa wajibu kwa wanaomfuata nabii huyo.

Maana ya umma kumwamini Muhammad na kumsaidia, ni kuitakidi kwamba yeye atakuja baada yao na walibashirie hilo. Mwenyezi Mungu anasema: "Na Isa aliposema: "Enyi wana wa Israil mimi ni mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu; nisadikishaye yaliyokuwa kabla yangu katika Tawrat na kutoa bishara ya mtume atakayekuja baada yangu jina lake ni Ahmad (61:6)"

Imam Ali (a.s.) anasema: "Mwenyezi Mungu hakupeleka Mtume yeyote ila huchukua ahadi naye kuhusu Muhammad (s.a.w.w.) na kumwamrisha kuchukua ahadi na watu kuwa watamwamini na kumsaidia, kama watazikuta zama zake"
Maana ya Umma kumwamini Muhammad (s.a.w.) na kumsaidia ni kumsadikisha wanavyuoni wao na viongozi wa dini zao na kuwatangazia wale wanaowategemea kwamba Muhammad bin Abdullah ndiye Mtume aliyebashiriwa na mitume, na kwamba jina lake liko katika Vitabu vya dini zao kama asemavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu. "Ambao humfuata mtume ummi ambaye humkuta ameandikwa kwao katika Tawrat na Injil …(7:157)

Na wala wasiyapindue maneno ya Mwenyezi Mungu kwa kufuru na inadi, kama alivyowaelezea Mwenyezi Mungu (s.w.t.): Hali ya kuwa baadhi yao walikuwa wanasikia maneno ya Mwenyezi Mungu kisha wanayabadili baada ya kuwa wanayafahamu; na hali wanajua. (2:75)

Akasema: Je, mmekubali na mmechukua ahadi yangu kwa hayo? Wakasema: Tumekubali.

Swali hapa ni la kuthibitisha na kutilia mkazo. Maana yake ni Mwenyezi Mungu aliziambia Umma kwa ndimi za mitume yao: Je, mmemkubali Muhammad na mmekubali ahadi? Umma ukasema: Ndio tumekubali wajibu wa kumwamini kumsaidia. Tumelikubali hilo na tumelazimiana nalo. Makusudio ya umma ni viongozi wa dini na wanavyuoni wao wanaojua vitabu vya dini.

Akasema: Shuhudieni; yaani akasema Mwenyezi Mungu kwa ndimi za mitume Yake kwa umma shuhudizaneni kwamba mmekubali utume wa Muhammad (s.a.w.w.) na wajibu wa kumsaidia.

Mimi ni pamoja nanyi katika mashahidi.

Mwenyezi Mungu na Malaika wake na mitume Yake wanashuhudia kuchukuliwa kwa ahadi ya wanavyuoni wa kidini, na kumkubali kwao Muhammad (s.a.w.w.), lakini pamoja na hayo wanavyuoni wa kiyahudi na wa Kinaswara walikana ahadi hii; wakamkadhibisha Muhammad na kumfanyia vitimbi na kiburi kama zilivyofafanua Aya zilizotangulia.

Na atakayegeuka baada ya hayo.

Yaani atakayegeuza kumwamini Muhammad baada ya kuchukua ahadi ya kumkubali na kumsaidia.

Basi hao ndio mafasiki.

Makusudio ya mafasiki hapa ni makafiri. Kwa sababu kila mwenye kugeuza Aya kutoka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na akakanusha utume miongoni mwa mitume ya Mwenyezi Mungu huku akijua utume wake basi yeye ni kafiri,

Je, wanataka dini isiyokuwa ya Mwenyezi Mungu na hali waliomo mbinguni na ardhi- ni wanamtii yeye wapende wasipende.

Watu wote wanamwamini Mwenyezi Mungu bila ya kutofautiana mwema na muovu, isipokuwa kwamba mwema humwamini Mwenyezi Mungu kwa hiyari katika maisha haya. Na muovu atamwamini kwa nguvu siku ya kiyama itakapoondoka pazia, na kila mkanushaji ataona adhabu kinaga ubaga. Mwenyezi Mungu anasema: "Walipoiona adhabu yetu wakasema: Tunamwamini Mwenyezi Mungu pekee na tunawakataa tuliokuwa tukiwashirikisha naye." (40:84).

Haya ndiyo maana ya 'wapende wasipende' tulivyofasiri ambayo si mazito kufahamiwa na yeyote vyovyote alivyo. Lakini Razi amefasiri kwa tafsiri ya kifalsafa. Aliyoyasema yako karibu, lakini ni kwa watu maalum watakaoelewa sio wote. Na hapa tunayanakili kwa ajili yao sio kwa ajili ya hawa:

"Kila kisichokuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kinawezekana kwa dhati yake; na kila chenye kuwezekana kwa dhati yake hakipatikani ila kwa kukipatisha yeye na hakikosekani ila kwa kukikosesha yeye. Kwa hiyo, kila kisichokuwa Mwenyezi Mungu ni chenye kumnyeyekea Mwenyezi Mungu Mtukufu katika njia zote mbili za kupatikana kwake na kukosekana kwake, Na, huo ndio ukomo wa kunyenyekea."

قُلْ آمَنَّا بِاللَّهِ وَمَا أُنْزِلَ عَلَيْنَا وَمَا أُنْزِلَ عَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالْأَسْبَاطِ وَمَا أُوتِيَ مُوسَىٰ وَعِيسَىٰ وَالنَّبِيُّونَ مِنْ رَبِّهِمْ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِنْهُمْ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ {84}

Sema tumemwamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyoteremshiwa na yale aliyoteremshiwa Ibrahim na Ismail na Is-haq na Yaqub na wajukuu zao na alichopewa Musa na Isa na manabii kutoka kwa Mola wao; hatutofautishi baina yao hata mmoja na sisi ni wenye kusilimu kwake.

وَمَنْ يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَنْ يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ {85}

Na mwenye kutaka dini isiyokuwa uislam haitakubaliwa kwake, naye katika akhera ni miongoni mwa wenye kupata hasara.