read

Aya 84-85:Tumeamini Mitume Yote

Maana

Aya hii ya 85 imekwishapita pamoja na tafsiri yake katika Sura ya Baqara Aya 136. Kwa ufupi ni kwamba mayahudi na manaswara wanaamini baadhi ya manabii na wanawakanusha baadhi yao. Ama waislam, wao wanaamini wote.

Kwa sababu, mwito wa manabii ni mmoja na lengo lao pia ni moja. Kwa hiyo, kujaribu kuwatofautisha ni sawa na kusema ndiyo na hapana kwa jambo moja tofuati ya kuamini unabii wao ni sawa na kitu kimoja, kwamba sawa ni hapana kwa pamoja.

Na mwenye kutaka dini isiyokuwa Uislamu haitakubaliwa kwake.

Makusudio ya Aya hii yatajulikana kwa kurudia tafsiri ya Aya ya 19 ya Sura hii. Nimewaona baadhi ya watu wakitoa dalili kuwa hakuna tofauti baina ya mwislam, myahudi na mkristo maadam wote wanamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, kwa Aya isemayo: "Hakika wale ambao wameamini na mayahudi na manaswara na wasabai, yeyote atayemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na akatenda mema, basi watapata malipo yao kwa Mola wao, wala haitakuwa hofu juu yao, wala hawatahuzunika." (2:62)

Hilo ni kosa kwa njia mbili: Kwanza kwamba makusudio ya waliotajwa katika Aya ni kila aliyekufa akiwa na imani na amali njema katika watu wa dini zilizomtangulia Muhammad (s.a.w.w.). Tumeyafafanua hayo wakati wa kufasiri Aya hiyo.

Pili: Hata kama dhahiri ya tamko la Aya inaonyesha kuwa inaenea wakati wote, lakini kauli yake Mwenyezi Mungu: Na mwenye kutaka dini isiyokuwa uislam hatakubaliwa," inaihusisha Aya hiyo na wale waliokuwa kabla ya wakati wa Muhammad tu.

Ama mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na asimwamini Muhammad baada ya kupewa kwake utume na ukawa mwito wake umemfikia, basi imani yake si chochote na yeye huko akhera atakuwa katika wenye kupata hasara.

كَيْفَ يَهْدِي اللَّهُ قَوْمًا كَفَرُوا بَعْدَ إِيمَانِهِمْ وَشَهِدُوا أَنَّ الرَّسُولَ حَقٌّ وَجَاءَهُمُ الْبَيِّنَاتُ ۚ وَاللَّهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ {86}

Atawaongozaje Mwenyezi Mungu watu waliokufuru baada kuamini kwao, na wakashuhudia kwamba mtume ni wa haki na zikawafikia hoja zilizo wazi. Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.

أُولَٰئِكَ جَزَاؤُهُمْ أَنَّ عَلَيْهِمْ لَعْنَةَ اللَّهِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ {87}

Hao malipo yao ni kushukiwa na laana ya Mwenyezi Mungu na ya Malaika, na ya watu wote.

خَالِدِينَ فِيهَا لَا يُخَفَّفُ عَنْهُمُ الْعَذَابُ وَلَا هُمْ يُنْظَرُونَ {88}

Ni wenye kudumu humo. Hawatapunguziwa adhabu wala hawatapewa nafasi.

إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا مِنْ بَعْدِ ذَٰلِكَ وَأَصْلَحُوا فَإِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَحِيمٌ {89}

Isipokuwa wale ambao wametubia baada ya hayo, na wakasahihisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe mwenye kurehemu.