read

Aya 86-90: Atawaongozaje Makafiri

Maana

Atawaongozaje Mwenyezi Mungu watu waliokufuru baada ya kuamini kwao, na wakashuhudia kwamba mtume ni wa haki na zikawafikia hoja zilizo wazi wazi.

Makusudio ya Mtume ni Muhammad (s.a.w.); na watu, ni wanavyuoni wa kiyahudi na wa kinaswara kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewataja kuwa ni watu walioamini na wakashuhudia utume wake, lakini baada ya kuletwa na kuwajia wao ubainifu na dalili wazi juu ya utume wake, walimkanusha na wakakataa kumfuata.

Sifa hizi zinalingana kabisa na wanavyuoni wa kiyahudi na wa kinaswara, kwa sababu, wao walikuta jina la Muhammad limeandikwa katika Tawrat na Injil, kwa hivyo wakawa wamemwamini kabla ya kuja kwake isipokuwa tu alipoletwa na kuwajia wao dalili walikufuru kwa chuki na hasadi na wakaifuta kila Aya inayofahamisha kwa uwazi au kwa umbali.

Unaweza kuuliza kuwa dhahiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu; Atawaongozaje Mwenyezi Mungu watu waliokufuru baada ya kuamin kwao, inaonyesha kuwa Mwenyezi Mungu hataki warudie tena kwenye uislamu hata kama watajaribu kutubia; jambo ambalo litawafanya wasistahili adhabu wala kuwa na lawama yoyote.

Jibu: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anamsimamishia mja dalili za haki, akiamini, basi atakuwa katika wenye kuongoka; na uongofu wake utatokana na Mwenyezi Mungu. Kwa sababu, Mwenyezi Mungu ndiye aliyemsimamishia dalili za haki. Vile vile uongofu utakuwa umetokana na mja mwenyewe. Kwa sababu yeye ameongoka kwa hiyari yake. Akirtadi baada ya uongofu kwa kiburi na inadi, basi Mwenyezi Mungu atamwachilia mbali katika maisha haya, na wala hatamwekea dalili mpya.

Vilevile hawezi kumlazimishia uongofu kwa sababu hakuna taklifu ikiwa kuna kulazimisha.

Hao malipo yao ni kushukiwa na laana ya Mwenyezi Mungu na ya Malaika, na ya watu wote.

Yaani wanastahili hilo. Laana ya Mwenyezi Mungu ni kuelezea ghadhabu yake na machukivu yake. Na laana ya watu wote na Malaika ni dua yao ya kumtaka Mwenyezi Mungu awaadhibu na kuwaweka mbali na rehema yake.

Katika Nahjul-balagha imeelezwa kwamba Ali (a.s.) alikuwa akihutubu katika mimbari Kufa. Ash'ath akamkatiza na kumwambia "Laana ikushukie." Amirul-Muminini akasema: "Wajuaje laana itanipata au la, Mungu akulaani wewe na wakulani wanaolaani." Sheikh Muhammad Abduh katika kulifafanua hilo anasema: "Ash'ath katika masahaba wa Ali alikuwa kama Abdullah bin Ubayy katika masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) wote walikua viongozi wa wanafiki.

Ni wenye kudumu humo, hawatapunguziwa adhabu wala hawatapewa nafasi.

Dhamiri ya humo ni ndani ya Jahannam. Hawatapewa nafasi, yaani hawatapewa muda, bali wataadhibiwa haraka sana.

Isipokuwa wale ambao wametubia baada ya hayo, na wakasahihisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe, mwenye kurehemu. Imekuja Hadith isemayo:

"Mwenye kutubia ni kama asiyekuwa na dhambi." Imam Ali anasema: Mungu hamfungulii mja mlango wa toba, akamfungia wa msamaha."

Unaweza kuuliza: Mtu akisilimu, kisha akartadi, kisha akarudi kwenye Uislamu lakini akapuuza hukumu sio misingi; kama vile kuacha Swala na Saumu kwa uvivu na kupuuza. Je, toba yake itakubaliwa?

Jibu: Ndio, atakubaliwa. Kwa sababu, toba ilikuwa ya kukufuru, sio ya Swala au Saumu. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na wakasahihisha, ni kuzitengeneza dhamiri zao na kuthibiti kwenye uislam na kutortadi mara ya pili.

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بَعْدَ إِيمَانِهِمْ ثُمَّ ازْدَادُوا كُفْرًا لَنْ تُقْبَلَ تَوْبَتُهُمْ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الضَّالُّونَ {90}

Hakika wale ambao wamekufuru baada ya kuamini kwao, kisha wakazidi kukufuru, haitatakabliwa toba yao; na hao ndio waliopotea.

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَمَاتُوا وَهُمْ كُفَّارٌ فَلَنْ يُقْبَلَ مِنْ أَحَدِهِمْ مِلْءُ الْأَرْضِ ذَهَبًا وَلَوِ افْتَدَىٰ بِهِ ۗ أُولَٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ وَمَا لَهُمْ مِنْ نَاصِرِينَ {91}

Hakika wale ambao wamekufuru na wakafa hali ya kuwa wao ni makafiri, basi haitakubaliwa kwa yeyote katika wao hata fidia ya dhahabu kwa kujaza ardhi yote lau angeliitoa. Hao watapata adhabu iumizayo wala hawatakuwa na msaidizi.