read

Aya 90-91: Kisha Wakazidi Kukufuru

Hakika wale ambao wamekufuru baada ya kuamini kwao, kisha wakazidi kukufuru, haitatakabliwa toba yao.

Maana ya kukufuru baada ya kuamini yako wazi. Ama kuzidisha kukufuru, kunakuwa kwa dhambi anazozifanya mwenye dhambi hasa kueneza ukafiri na kuwapiga vita waumini kwa kuwa tu ni waumini.

Unaweza kuuliza; Hakika Mwenyezi Mungu amehukumu - katika Aya iliyotangulia - kumtakabalia toba mwenye kukufuru baada ya imani; na katika Aya hii amehukumu kutomtakabalia. Kuna wajihi gani wa kuungana haya?

Wafasiri wamejibu kwa majibu mengi. Yenye nguvu zaidi ni kwamba kukufuru baada ya kuamini kuko mafungu matatu.

1. Kutubia toba ya kweli ambayo Mwenyezi Mungu ameitaja kwa kusema: Isipokuwa wale waliotubia.

2. Toba isiyo ya kweli ambayo Mwenyezi Mungu ametaja kwa kusema: Haitotakabaliwa toba yao."

3. Ni kufa juu ya ukafiri kulikotajwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Hakika wale ambao wamekufuru na wakafa hali ya kuwa wao ni makafiri.

Jibu tunaloliona sisi, ni kwamba mtu anaweza akahisi usahihi wa jambo au kutokuwa sahihi. Kisha akachangayikiwa na kuwaza kuwa hisia zake zimebadilika na kuwa si sahihi au kuwa ni sahihi baada ya kutokuwa sahihi; ingawaje hisia zake hasa hazijabadilika; ambapo kuitakidi kwake kuwa zimebadilika ni kwa mawazo tu.

Vilevile mapenzi na chuki, mfano, mtoto wako anaweza kukufanyia ubaya na ukachukulia kuwa yeye ni mtu anayemchukia zaidi kuliko watu wote, na kwamba unataka aangamie, lakini huruma za ubaba bado ziko kwenye nafsi yako bila ya kutambua, mara ngapi tunashuhudia mtu akifanya jambo au kuliacha kwa kufuata desturi, kuiga au kwa kwa kuhurumia huku mwenyewe kiitakidi kuwa ni kwa njia ya dini.

Pia inaonyesha watubiaji wengi wa dhambi zao kuwa ni wa kweli, lakini kwa ndani bado wamebakia nayo waliyokuwa nayo. Watubiaji hawa ndio walielezwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu: Hawatatakabaliwa toba yao. Ama wale walioelezwa na Aya iliyotangulia (Isipokuwa wale waliotubia), ni wale watubiaji wa kweli na wa haki.

Hakika wale ambao wamekufuru na wakafa hali ya kuwa wao ni makafiri, basi haitakubaliwa kwa yeyote katika wao hata fidiya ya dhahabu kwa kujaza ardhi yote.

Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kuishiliza maisha yake kwa ukafiri atahisabiwa hisabu ya makafiri.

Unaweza kuuliza; kuwa hakuna dhahabu siku ya kiyama wala hakuna njia yoyote ya kuweza kuimiliki wala kuitoa. Sasa kuna faida gani ya kuitaja.

Jibu: Makusudio ni kwamba hakuna njia ya kujikomboa kwa namna yoyote ile. Kimsingi ni kuwa kukadiri muhali si muhali. Katika aliyoyasoma Imam Ali, kuisifu Jahannam ni: "Haondoki mkazi wake wala hakombolewi mateka wake."