read

Sura Ya Mia: Al-A’diyat

Imeshuka Makka na imesemekana ni Madina Ina Aya 11.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

وَالْعَادِيَاتِ ضَبْحًا {1}

Naapa kwa wanokwenda mbio wakihema.

فَالْمُورِيَاتِ قَدْحًا {2}

Wakitoa moto kwa kupiga kwato.

فَالْمُغِيرَاتِ صُبْحًا {3}

Wakishambulia wakati wa asubuhi.

فَأَثَرْنَ بِهِ نَقْعًا {4}

Wakatifua vumbi wakati huo.

فَوَسَطْنَ بِهِ جَمْعًا {5}

Wakaliingilia kati wakati huo kundi.

إِنَّ الْإِنْسَانَ لِرَبِّهِ لَكَنُودٌ {6}

Hakika mtu ni mtovu wa shukrani kwa Mola wake!

وَإِنَّهُ عَلَىٰ ذَٰلِكَ لَشَهِيدٌ {7}

Na hakika yeye bila ya shaka ni shahidi wa hayo!

وَإِنَّهُ لِحُبِّ الْخَيْرِ لَشَدِيدٌ {8}

Naye hakika ana mapenzi sana na mali!

أَفَلَا يَعْلَمُ إِذَا بُعْثِرَ مَا فِي الْقُبُورِ {9}

Kwani hajui watakapofufuliwa waliomo makaburini?

وَحُصِّلَ مَا فِي الصُّدُورِ {10}

Na yakadhihiirishwa yaliomo vifuani?

إِنَّ رَبَّهُمْ بِهِمْ يَوْمَئِذٍ لَخَبِيرٌ {11}

Hakika Mola wao siku hiyo bila ya shaka atakuwa na habari sana!

Maana

Katika Tafsir Majmau-lbayan na nyinginezo imeelezwa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alituma kikosi cha wapiganaji kwenye kitongo­ji kimoja cha Bani Kinana, kikachelewa. Basi wanafiki wakasema wameuliwa, ndio ikashuka Sura hii kumpa habari Nabii (s.a.w.) kuwa wako salama, na kuwakadhibisha wanaoneza uvumi.

Naapa kwa wanokwenda mbio wakihema.

Makusudio ya wanokwenda mbio hapa ni farasi. Imesemekana kuwa ni ngamia. Kuhema hapa ni kutuo pumzi mbele ya adui.

Wakitoa moto kwa kupiga kwato.

Yaani farasi wanatoa cheche za moto kwenye kwato zao zinapopiga mawe mbele ya adui.

Wakishambulia wakati wa asubuhi.

Farasi waliwashambulia maadui ghafla wakati wa asubuhi.

Wakatifua vumbi wakati huo, wakaliingilia kati wakati huo kundi.

Makusudio ya kundi hapa ni kundi la maadui. Maana ni kuwa farasi wali­washambulia maadui wakati wa asubuhi.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameapa kwa farasi wa vita. Kwa ufasha zaidi ni kuwa ameapa kwa nguvu na kuandaa maadui, ili awahimize waumini kufanya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuwa na silaha ya kumkemea adui wa Mwenyezi Mungu na wa ubinadamu.

Mwenye kufu­atilia Aya za Qur’an yenye hikima atakuta kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewahimiza waumini kwenye Aya kadhaa na kwa mifumo mbal­imbali, wawe na silaha za kuwaogofya wapituka mipka ambao hawafahamu lugha isipokuwa nguvu; miongoni mwa Aya hizo ni hizi zifuatazo:

وَأَعِدُّوا لَهُمْ مَا اسْتَطَعْتُمْ مِنْ قُوَّةٍ وَمِنْ رِبَاطِ الْخَيْلِ تُرْهِبُونَ بِهِ عَدُوَّ اللَّهِ وَعَدُوَّكُمْ {60}

“Na waandalieni nguvu kama vile muwezavyo na kwa farasi waliofungwa ili mumtishe adui wa Mwenyezi Mungu na adui yenu.” Juz. 10 (8:60).

 وَدَّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْ تَغْفُلُونَ عَنْ أَسْلِحَتِكُمْ {102}

“Wanataka wale waliokufuru lau kama nyinyi mwasahau silaha zenu.” Juz. 5 (4:102).

وَلَا تَكُونُوا كَالَّتِي نَقَضَتْ غَزْلَهَا مِنْ بَعْدِ قُوَّةٍ أَنْكَاثًا {92}

“Wala msiwe kama mwanamke ambaye ameufumua uzi wake baada ya kuusokota na
kuwa mgumu.” Juz. 14 (16:92).

Na Aya nyinginezo zisizokuwa hizo zinazoamuru kila jambo la kufanya tamko la haki liwe juu na la batili liwe chini. Hapa inatubainikia kwamba kutajwa farasi na kuhema kwake, kupiga kwato na kushambulia ni kinaya cha kuandaa nguvu za kuihifadhi haki na watu wake. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametumia farasi kuelezea nguvu, kwa vile ndio waliokuwa wakitu­mika zaidi wakati huo.

Sheikh Muhamad Abduh akiwa anafasiri Aya hizi anasema: “Si ni jambo la kushangaza kwamba watu, wanadai kuwa Qur’an ni Kitabu chao na wao ndio walioko mbali zaidi na ukakamavu na sifa zake.

Nimezungumza na Mwalimu katika wao kuhusu kunufaika na baadhi ya ilimu ili zifundishwe kwenye chuo cha Al-azhar, akasema: ‘kwa hiyo ni lazima tuwafundishe wanafunzi kupanda farasi?’ Alisema hivi ili aninyamazishe. Je, kauli yake hii inaafikiana na kuamini Kitabu cha Mwenyezi Mungu? Pima na uamue.”

Hakika mtu ni mtovu wa shukrani kwa Mola wake!

Hukumu ya Aya ni kuzingatia aghalabu ya watu sio watu wote. Maana ni kuwa watu wengi wanamsahau Mwenyezi Mungu kwenye neema wala hawamshukuru kwa kujitolea kwenye njia yake. Amesema Mtume (s.a.w.): “Mtovu wa shukrani ni yule anayekula peke yake, anampiga mtumishi wake na anazuia msaada wake.”

Na hakika yeye bila ya shaka ni shahidi wa hayo!

Yaani vitendo vya mtovu wa shukrani vinashuhudia kwa lugha ya mazin­gira kwamba yeye anazikufuru neema za Mwenyezi Mungu. Aina kubwa kabisa ya kumkufuru Mwenyezi Mungu na neema yake ni kuwakandamiza waja wa Mwenyezi Mungu kwa neema hiyo.

Naye hakika ana mapenzi sana na mali.

Neno mali hapa tumelifasiri kutokana na neno khair, kama walivyosema wafasiri. Hakuna mwenye shaka kwamba ambaye penzi lake kwa mali limezidi sana basi atakuwa amejivua na utu na kupinga misimamo yote isipokuwa kama ni nyenzo ya kukusanya mali. Na kama tutatafuta sababu zinazoleta maafa ya ubinadamu tutaona kuwa yanatokana na kushindania mali na kuikusanya. Harbert Marcuse ambaye alikuwa ni mwalimu katika vyuo vikuu vya Columbia, Harvad na Brandeis huko Amerika anasema katika kitabu chake ne dimensional man: “Itatoka wapi heri kwenye zama ambazo hakuna ila shari; ambapo mambo ya kimaada yamemtawala mtu kwa namna ambayo imemfaya mtu kuwa ni mtumwa na hiyo ndiyo bwana mkubwa mwenye nguvu na kutawala.”

Kwani hajui watakapofufuliwa waliomo makaburini? Na yakadhi­hirishwa yaliyomo vifuani? Kuwa hakika Mola wao siku hiyo bila ya shaka atakuwa na habari sana!

Anaelezewa mtu au mtovu wa shukrani, kuwa hajui mwisho wake? kudhi­hirishwa waliomo makaburini ni kufufuliwa. Kuwa na habari ni ishara yakuwa anayajua makusudio na matendo yao na atawalipa wanavyostahi­ki.

Aya hizi zinamhadharisha na kumpa kiaga kila mwenye kuzikufuru neema za Mwenyezi Mungu na kuzitumia kuwakandamizia waja wake mfano wa Aya hizi uko kwenye Aya kahaa zilizopita; ikiwemo ile ya Juz. 2 (2:235).