read

Sura Ya Mia Na Kumi Na Mbili: Al-Lahab

Imeshuka Makka Ina Aya 5.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ {1}

Imeangamia mikono ya Abu Lahab na yeye ameangamia.

مَا أَغْنَىٰ عَنْهُ مَالُهُ وَمَا كَسَبَ {2}

Haitamfaa mali yake na ali­chokichuma.

سَيَصْلَىٰ نَارًا ذَاتَ لَهَبٍ {3}

Atauingia moto wenye miali.

وَامْرَأَتُهُ حَمَّالَةَ الْحَطَبِ {4}

Na mkewe mchukuzi wa kuni.

فِي جِيدِهَا حَبْلٌ مِنْ مَسَدٍ {5}

Shingoni mwake mna kamba iliyosokotwa.

Maana

Imeangamia mikono ya Abu Lahab na yeye ameangamia.

Mikono ya Abu Lahab ni kinaya cha mwenyewe hasa; kama inavyosemwa: Mikono ina majukumu ya ilichokichukua mpaka itekeleze. Kwa sababu mikono ni udhihirisho wa nguvu na ni chombo cha kazi.

Jina kamili la Abu Lahab ni Abdul Uzza bin Abdul-Muttwalib bin Hashim. Ni ami yake Mtume (s.a.w.), lakini alikuwa ndiye adui yake mkubwa zaidi.

Wafasiri na wapokezi wamesema kuwa Mtume (s.a.w.) siku moja alipanda kilima cha swafaa akawaita watoto wa kuraishi, wakakusanyika akiwemo Abu Lahab. Akasema: Hivi nikiwaambia kuwa jeshi la wapanda farasi liko hapo bondeni linataka kuwashambulia mtanisadiki? Wakasema: ndio huja­jaribu kutuambia uwongo.

Akasema: Basi mimi ninawaonya na yule ambaye ana adhabu kali. Abu Lahab akasema: Hivi umekutukusanya kwa hili? Uangamie wewe. Ndipo ikashuka Sura hii.

Haitamfaa mali yake na alichokichuma.

Kesho kwenye hisabu na malipo haitafaa mali wala cheo au watoto. Yote hayo yatakuwa ni hoja juu yake na maangamizi.

Atauingia moto wenye miali.

Haya ndiyo malipo yake na makazi yake ni Jahannam, mwishilio mbaya.
Na mkewe mchukuzi wa kuni.

Mke wa Abu Lahab ni Ummu Jamil bint Harb, dada yake Abu Sufyani na shangazi yake Mua’wiya. Kuni ni kinaya cha shari na dhambi zitakazom­peleka motoni. Alikuwa na uadui na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kwa hali ya juu sana; akitembea kumfitini na watu ili kuzima mwito wake.

Uhusiano wa moto na kuni unajulikana. Zaidi ya hayo waarabu walikuwa wakimpa jina la mbeba kuni mtu aliyekuwa mfitini, kwa sababu anawasha moto wa fitina. Na imesemekana alikuwa akikusanya miba na kuitawanya kwenye njia anayopita Mtume.

Shingoni mwake mna kamba iliyosokotwa.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kumpa sifa ya mbeba kuni, sasa anam­pa picha hii ya ajabu. Anafunga kuni kichwani mwake kwa ncha moja ya kamba na ncha nyingine iko shingoni mwake. Kama kwamba kuni ndio taji na kamba ni mkufu.

Unaweza kuuliza: waliompiga vita na kumuudhi ni wengi katika mataghuti wa kikuraishi; kama Uqba bin Abi Mui’t, Abu Jahl, Walid Bin Almughira, A’si bin Wail na wengineo, lakini Qur’an haikuyataja majina yao; kwanini basi hapa ikamuhusu kumtaja Abu Lahab na kumteremshia sura nzima kinyume na wengine?

Sheikh Muhammad Abduh amejibu kuwa Abu Lahab alikuwa ni mpinzani mashuhuri zaidi wa Mtume (s.a.w.) na alikuwa ndiye mwakilishi wa madui. Nabii aliathirika na harakati zake; ndio maana Mwenyezi Mungu akamuhusu kumtaja kinyume na wengine.

Sheikh Muhammad Abduh alimalizia kuifasiri sura hii kwa kusema: Mwenye kukuambia kuwa haifai kuitegemeza hukumu yoyote kwenye kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna ya Nabii wake kwa kiwango cho­chote cha ilimu uliyofikia, bali unatakikana umrudie fulani kwenye kauli yake, basi huyo ni Abu Lahab. Na kila mwanamke anayeenda kuwafitini watu na kufanya ufisadi baina ya watu basi huyo ni mchukuzi wa kuni, shingoni mwake mkiwa na kamba ya kusokotwa.