read

Sura Ya Mia Na Kumi Na Moja: An-Nasr

Imeshuka Madina. Ina Aya 3.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

إِذَا جَاءَ نَصْرُ اللَّهِ وَالْفَتْحُ {1}

Itakapokuja nusra ya Mwenyezi Mungu na ushindi.

وَرَأَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِي دِينِ اللَّهِ أَفْوَاجًا {2}

Na ukawaona watu wanaiingia katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi makundi.

فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَاسْتَغْفِرْهُ ۚ إِنَّهُ كَانَ تَوَّابًا {3}

Basi zisabihi sifa za Mola wako na umtake maghufira; hakika yeye ni Mwingi wa kukubali toba.

Maana

Itakapokuja nusra ya Mwenyezi Mungu na ushindi.

Jamhuri ya wafasiri imesema kuwa hii ni bishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa Nabii wake mtukufu ya ushindi wa kuiteka Makka na kuwashinda maadui wa Mwenyezi Mungu na wake.

Na ukawaona watu wanaiingia katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi makundi.

Dini ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Makabila mengi ya waarabu yalikuwa yakingojea kutekwa Makka ndio yaingie kwenye Uislamu. Basi Mwenyezi Mungu alipompa ushindi huo Mtume wake, Uislamu ulienea Bara arabu yote kwa muda mchache, na Uislamu ukaleta maadili mapya kwa waarabu, ukawaunganisha baada ya kuwa wametengana na ukawapa nguvu baada ya kuwa na udhalili. Ukawafanya wawe ni umma unaooneka na ukiwa na mwelekeo wa heri na utengeneo.

Basi zisabihi sifa za Mola wako na umtake maghufira.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimwamrisha Mtume wake amsabihi na kumsi­fu baada ya kuona ushindi, kuwa ni shukrani kwa neema za Mwenyezi Mungu Mtukukufu na kuitakasa nafsi isilewe na ushindi na furaha. Hakuna mwenye shaka kwamba lengo la hilo ni kujipamba kwa maadili ya Qur’an na kupata mawaidha yake. Imam Ali (a.s.) anasema: “Ukimmudu adui yako, kufanye kumsamehe ni shukrani ya huko kummudu.”

Hakika yeye ni Mwingi wa kukubali toba.

Kumkubalia toba Mwenyezi Mungu maasumu maana yake ni rehema kwake na radhi, na kumkubalia toba mwenginewe ni kumsamehe. Yametangulia maelezo kuhusiana na hilo katika Juz. 11 (9:117).

Kuna mapokezi yanayosema kuwa Mtume (s.a.w.) alisema iliposhuka Sura hii: “Ni tanzia yangu mimi mwenyewe.” Binti yake Fatima, aliposikia hivyo akalia. Akamwambia: usilie, kwani wewe ni wa kwanza kuungana nami. Basi akacheka. Kama kwamba Mtume (s.a.w.) alijua kutokana na Sura hii kuwa muda wake wa kuishi umeisha na kazi yake imekwisha baada ya kupatikana ushindi na kuingia watu katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi kwa makundi.