read

Sura Ya Mia Na Kumi Na Nne: An-Nas

Imeshuka Madina Ina Aya 6.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ {1}

Sema: Najikinga kwa Mola wa watu.

مَلِكِ النَّاسِ {2}

Mfalme wa watu.

إِلَٰهِ النَّاسِ {3}

Mungu wa watu.

مِنْ شَرِّ الْوَسْوَاسِ الْخَنَّاسِ {4}

Na shari ya mwenye kutia wasiwasi mwenye kurejea nyuma.

الَّذِي يُوَسْوِسُ فِي صُدُورِ النَّاسِ {5}

Anayetia wasiwasi katika vifua vya watu.

مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ {6}

kutokana na majini na watu.

Maana

Sema: Ninajikinga kwa Mola wa watu, Mfalme wa watu Mungu wa watu

Maneno yanaelekezwa kwa Nabii (s.a.w.), lakini wanakusudiwa watu, kwa sababu Nabii hakimbilii wala hatakimbilia isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu peke yake.

Neno Mola linatumika kwa mfalme, bwana mwenye kuneemesha, neno mfalme linatumika kwa maana ya mtawala na mwenye uweza, na neno Mungu linatumika kwa Muumbaji, mwanzilishi mwenye kudhibiti na mwenye kutoa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni Muumba wa watu, Mwenye kuneemesha Mwenye kuangilia mambo yao. Kwa hiyo ndiye mwenye kus­tahiki kuabudiwa na kumtaka hifadhi Yeye peke yake.

Unaweza kuuliza: Si Mwenyezi Mungu ni Muumba na Mfalme wa kila kitu, kwa nini amehusisha kutaja kuwa ni wa watu?

Jibu: kwa sababu watu ndio waliomtilia shaka Muumba wao, wakazikufu­ru neema zake na wakamtaka msaada mwinginewe, au wamekuwa ni wenye kupituka mipaka zaidi kuliko viumbe wengine kwa ujumla; ndio akawahusu wao kuwataja, ili waongoke.

Na shari ya mwenye kutia wasiwasi.

Wasiwasi ni sauti ya ndani inayojificha. Makusudio yake hapa ni wahaka wa moyo kutokana na fikra mbovu zinazopinga haki na njia yake. Hakuna yeyote asiyekuwa na mazungumzo ya nafsi na wasiwasi, isipokuwa aliye­hifadhiwa na Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hamchukulii mja kwa wasiwasi ila kama utaji­tokeza kwenye kauli au kitendo. Mtume (s.a.w.) amesema: “Kila moyo una wasiwasi, ukipasua hijabu ya moyo na kutamkwa na ulimi, basi mja atachukuliwa hatua, na kama hautapasua hijabu ya moyo wala usitamkwe na ulimi, basi hakuna ubaya.”

Mwenye kurejea nyuma.

Makusudio ya wasifa huu ni kwamba mtu akitanabahi wasiwasi wa kishetani na kumtaka hifadhi Mwenyezi Mungu kwa ikhlasi, basi hum­wondokea na kujificha.

Anayetia wasiwasi katika vifua vya watu, kutokana na majini na watu.

Dhahiri ya Aya inafahamisha kwa uwazi kuwa wenye kutiwa wasiwasi ni aina moja nao ni watu tu, lakini wanaotia wasiwasi ni aina mbili: majini na watu. Wasiwasi unaotoka kwa mtu ni kama kumpambia kosa na kumhadaa. Hili liko wazi na linakuwa mara nyingi.

Ama vipi jinni anavy­omtia wasiwasi mtu, Mwenyezi Mungu ndiye anayejua zaidi. Inawezekana kuwa makusudio ya wasiwasi wa jini kwa mtu ni mazungumzo ya ndani ya nafsi yake mwenyewe ambayo hayakutokana na wengine.

Vyovyote litakavyokuwa chimbuko la wasiwasi, lakini muhimu ni mja kumkimbilia Mola wake na kumtaka hifadhi na kila shari ya wasiwasi; iwe imetokana na yeye mwenyewe au na mwinginewe.

Imemalizika tafsiri hii jioni ya mwezi 15 Jamadil-Akhar 1390 (A.H.) sawa na 18 April 1970 (A.D.) Kazi hii imenichukua miaka mine mfululizo wa usiku na mchana.

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliyenisaidia kuifasiri Qur’an yake, na kunifanyia wepesi ufafanuzi na ubainifu wake. Ni Yeye pekee mwenye kuombwa kunifanya niwe katika wenye kushikamana na kamba yake na kuifanya ni akiba siku ya kufanyiwa akiba na kufunuliwa siri, na anizidishie fadhila zake na hisani yake… Hakika yeye ni Manani aliye mkarimu.

Na rehema na amani zimshukie Muhammad na kizazi chake kitakatifu. Nami namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kukamilisha tarjuma hii kutoka kwenye lugha ya Kiarabu, leo Mwezi 20 Dhulhijja 1430 AH (8-12-2009) -Mtarjumu