read

Sura Ya Mia Na Kumi Na Tatu: Al-Falaq

Imeshuka Makka Ina Aya 5.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ {1}

Sema: Najikinga kwa Mola wa asubuhi.

مِنْ شَرِّ مَا خَلَقَ {2}

Na shari ya alivyoviumba.

وَمِنْ شَرِّ غَاسِقٍ إِذَا وَقَبَ {3}

Na shari ya giza la usiku liin­giapo.

وَمِنْ شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ {4}

Na shari ya wanaopulizia mafundoni.

وَمِنْ شَرِّ حَاسِدٍ إِذَا حَسَدَ {5}

Na shari ya hasidi anapo­husudu.

Maana

Sema: Najikinga kwa Mola wa asubuhi.

Neno asubuhi tumelifasiri kutoka na neno falaq lenye maana ya kupasua. Neno hili hutumika kwa maana ya viumbe wote, kwa sababu Mwenyezi Mungu amevitoa kutoka kutokuwepo; kama kwamba vilikuwa vimefichi­ka akavifunua.

Pia hutumika, neno hili, kwa maana ya asubuhi, kwa sababu asubuhi inaondoa giza. Hayo ndiyo makusudio yake hapa kama walivyose­ma wafasiri wengi. Kauli hii inatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu pale aliposema kwa kulitumia neno hili falaq:

فَالِقُ الْإِصْبَاحِ {96}

“Ndiye mpambazuaji wa asubuhi.” Juz. 7 (6:96).

Vyovyote iwavyo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni Mola wa asubuhi na Mola wa viumbe wote, na amemwarisha Mtume wake kumtaka hifad­hi.

Na shari ya alivyoviumba; yaani na shari ya kila chenye shari; awe mtu au asiyekuwa mtu. Hakuna kiumbe chochte ila kina maandalizi kamili ya kufanya heri au shari - nguvu chanya na hasi.

Wala hakuna katika vilivy­opo kilicho na heri tupu, isipokuwa muumba wa vilivyoko. Tazama Juz. 5 (4:78-79) kifungu cha ‘Haiwezekani kuongeza zaidi ya ilivyo.’

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kumwamuru Mtume wake mtukufu kujihifadhi na shari ya kila mwenye shari, hapa amehusisha kuyataja aliy­oyaashiria, kama ifuatavyo:

Na shari ya giza la usiku liingiapo.

Makusudio ya shari ya usiku hapa ni mambo ya kuchukiza yanatokea usiku; kama kupanga njama, kuiba, kuua, ufasiki na mengineyo.

Na shari ya wanaopulizia mafundoni.

Makusudio ya kupuliza hapa sio uchawi au wachawi wanaume wala wanawake; kama walivyosema wafasiri wengi. Isipokuwa makusudio ni kila mwenye kuifanyia mazingaombwe misingi na misimamo, ni sawa awe atafanya kiini macho kwa kudai kuwa anawatumia majini, kwa uwongo na unafiki au asifanye hivyo. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amehusisha kutaja hivyo hapa, kwa sababu mazingaombe na mauzauza ni anuani ya unafiki.

Wapokezi wamepokea kutoka kwa Aisha kwamba myahudi aliyeitwa Labid bin Al-asam alimroga Mtume (s.a.w.) na akaathirika mpaka akawa anaona anafanya kitu kumbe hafanyi, na kwamba Sura hii ilishuka kwa sababu hiyo.

Riwaya hii ni wajibu kuitupilia mbali kisharia na kiakili. Kiakili ni kuwa Nabii ni maasumu, hatamki isipokuwa wahyi, kwa hiyo itakuwa muhali kwake kufikiria kuwa anapewa wahyi kumbe hapewi wahyi. Ama kisharia ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameukadhibisha uchawi na watu wake, pale aliposema:

 فَإِذَا حِبَالُهُمْ وَعِصِيُّهُمْ يُخَيَّلُ إِلَيْهِ مِنْ سِحْرِهِمْ أَنَّهَا تَسْعَىٰ {66}

 وَلَا يُفْلِحُ السَّاحِرُ حَيْثُ أَتَىٰ {69}

“Mara kamba zao na fimbo zao zikaonekana, kwa uchawi, kuwa zinak­wenda mbio... na mchawi hafanikiwi popote aendapo.” Juz. 16 (20:66,69).

Vile vile amewakadhibisha washirikina waliompa Mtume sifa ya uchawi:

 إِذْ يَقُولُ الظَّالِمُونَ إِنْ تَتَّبِعُونَ إِلَّا رَجُلًا مَسْحُورًا {47}

“Wanaposema hao madhalimu: Nyinyi hamfuati isipokuwa mtu aliyerog­wa.” Juz. 15 (17:47).

Tazama tuliyoyaandika kuhusu uchawi na hukumu yake katika Juz. 1 (2:102) na Juz. 9 (7:113) kwa anuani ya ‘Uchawi.’

Ya kushangaza ni yale aliyoyanukuu Sheikh Muhammad Abduh kutoka kwa waigaji wengi, kama alivyowaita mwenyewe, pale waliposema: “Imekua sahihi habari ya kuwa uchawi uliathiri nafsi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) na mwenye kukana hivyo atakuwa ameleta bid’a katika dini, kwa sababu Qur’an imeelezea usahihi wa uchawi.”

Sheikh Muhammad Abduh aliongezea kwenye kauli hiyo kwa kusema: “Angalia jinsi waigaji wanavyoibadilisha dini sahihi kwenye bid’a, waki­toa hoja kwa Qur’an, iliyoukana uchawi, kwa kuthibitisha uchawi uliomwathiri Mtume wa Mwenyezi Mungu, sawa na walivyosema washirikina: Huyo ni mtu aliyerogwa.

Na shari ya hasidi anapohusudu.

Hasidi ni yule anayetamani neema aliyo nayo mwingine imwondokee na awe nayo yeye. Hadith inasema: “Hasidi anahusudu na mumin anakuwa na ari.” Yaani anatamani awe na neema kama aliyo nayo mwenzake, lakini hatamani imwondokee huyo mwenzake.

Husuda ni mama wa maovu mengi; kama chuki, lawama, uwongo, kusen­genya, fitina, vitimbi na hadaa, kwa kujaribu kila njia ili mwingine aon­dokewe na neema aliyo nayo. Ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akamwamuru Mtume wake mtukufu ajilinde na shari ya hasidi.

Hapa inatubainikia kuwa makusudio ya shari ya hasidi na makusudio yake mabaya pamoja na kauli na vitendo vyake, sio jicho; kama walivyosema wafasiri wengi. Ya kushangaza ni yale waliyoyaandika baadhi yao katika tafsiri kuwa kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mashuhuri kwa kuwadhu­ru watu kwa jicho lake mpaka ikawa watu wanamkodisha kwa lengo hilo.
Siku moja alikodishwa na mwanamke ili amhusudu hasimu wake na amuue kwa jicho lake. Akaenda naye hadi kwa huyo mtu na kumwambia ndiye huyu basi mhusudi. Hasidi akamwambia: “Macho yako ni mazuri sana!” Basi alipomaliza tu maneno yake yule mwanamke akapofuka.