read

Sura Ya Mia Na Kumi Na Tatu: Al-Ikhlas

Imeshuka Makka Ina Aya 4.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ {1}

Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni mmoja.

اللَّهُ الصَّمَدُ {2}

Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kukusudiwa kwa haja.

لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ {3}

Hakuzaa wala hakuzaliwa.

وَلَمْ يَكُنْ لَهُ كُفُوًا أَحَدٌ {4}

Wala hana anayefanana naye hata mmoja.

Maana

Misingi ya Uislamu ni mitatu: Tawhid, Utume na Ufufuo. Ya kwanza inazalisha sifa zake Mwenyezi Mungu Mtukufu, ya pili inazaa Qur’an na sharia na ya tatu inazaa malipo na hisabu. Sura hii tukufu inaeleza hii ya kwanza.

Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni mmoja katika dhati yake, sifa zake na vitendo vyake.

Hana mshirika katika chochote, wala hafanyi kitu kwa kujiletea manufaa au kujikinga na madhara. Tumezungumzia kwa ufafanuzi zaidi kuhusu Tawhid katika Juz. 5 (4:48-50), kwa anuani ya ‘dalili ya umoja na utatu.’

Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kukusudiwa kwa haja.

Makusudio yake hapa ni kujitosheleza na kila kitu, si mhitaji bali kila kitu kinamhitajia Yeye, kwa sababu yeye ndiye muumba wa kila kitu na ndiye chimbuko.

Hakuzaa.

Hii ni kuwarudi wale wanaodai kuwa Mwenyezi Mungu ana watoto wa kiume au mabinti Maulamaa wa theolojia wanasema: “Lau Mwenyezi Mungu angelikuwa na mtoto, basi angelikuwa na mafungu na kila mwenye mafungu anakuwa na mwisho kwa kuisha mafungu yake. Usawa zaidi ni kusema: Lau Mwenyezi Mungu angelikuwa na mtoto angelikuwa na wa kufanana naye na wa kumrithi.

Kwa sababu mtoto anashabihiana na mzazi wake na anam­rithi: Imam Ali (a.s.) anasema: “Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuzaliwa akawa na mshirika katika utukufu, wala hakuzaa akawa na mrithi na kufa.”

Wala hakuzaliwa.

Hii ni kumrudi mwenye kudai kwamba kuna miungu waliozaliwa. Lau angelikuwa Mungu amezaliwa angelikuwa na tarehe ya kupatikana kwake. Imam Ali (a.s.) anasema: “Hakuzaa akawa naye ni mwenye kuzaliwa, wala hakuzaliwa akawa na kiwango cha wakati.” Yaani kuweko kwake kuanzia tangu alipozaliwa.”

Wala hana anayefanana naye hata mmoja, si katika kuweko kwake wala dhati yake au sifa zake wala vitendo vyake.

Nilipokuwa nikifasiri Sura hii nilisoma rejea nyingi kuanzia Asfar cha Mulla Sadra hadi tafsiri za kawaida, kama Al-baydhawi.

Nikachunguza sana humo ili nichague kauli zilizo bora zaidi; sikupata kauli ya ufupi zaidi na yenye kuweka wazi kuliko kauli ya Imam Husein (a.s.) alipoulizwa na watu wa Basra kuhusu maana ya neno Swamad, (mwenye kukusudiwa kwa haja) akasema: Mwenyezi Mungu amelifasiri neno hilo kwa kusema: hakuzaa wala hakuzaliwa wala hana anayefanana naye hata mmoja.”

Kutokana na tafsiri hii fupi iliyokusanya maana, inafaa tuseme kuwa maana ya Mwenyezi Mungu ni mmoja ni Mwenye kukusudiwa kwa haja, na maana ya Mwenye kukusudiwa kwa haja ni hakuzaa wala hakuzaliwa, na maana ya hakuzaa wala hakuzaliwa ni hana anayefanana naye hata mmoja.