read

Sura Ya Mia Na Mbili: At-Takathur

Imeshuka Makka, na imesemekana ni Madina Ina Aya 8.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

أَلْهَاكُمُ التَّكَاثُرُ {1}

Kumewashughulisha kujifa­harisha kwa wingi!

حَتَّىٰ زُرْتُمُ الْمَقَابِرَ {2}

Mpaka mkayazuru makaburi!

كَلَّا سَوْفَ تَعْلَمُونَ {3}

Si hivyo! Mtakuja jua!

ثُمَّ كَلَّا سَوْفَ تَعْلَمُونَ {4}

Tena si hivyo! Mtakuja jua!

كَلَّا لَوْ تَعْلَمُونَ عِلْمَ الْيَقِينِ {5}

Si hivyo! Lau mngelijua kwa ujuzi wa yakini.

لَتَرَوُنَّ الْجَحِيمَ {6}

Hakika mtauona Moto!

ثُمَّ لَتَرَوُنَّهَا عَيْنَ الْيَقِينِ {7}

Kisha, hakika, mtauona kwa jicho la yakini.

ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ {8}

Kisha hakika mtaulizwa siku hiyo juu ya neema.

Maana

Kumewashughulisha kujifaharisha kwa wingi, mkaacha haki na maten­do mema na kujifaharisha kwa wingi wa mali na mengineyo mfano wake; kama kusema: Mimi nina mali nyingi au nina cheo kikubwa kuliko wewe.

Mpaka mkayazuru makaburi.

Mmepita kwenye mghafala mpaka yakawafikia mauti. Imam Ali (a.s.) ana maneno marefu aliyoyasema baada ya kusoma Aya hii; miongoni mwayo ni: “Hivi wanajifaharisha kwa wazazi wao walio wafu, au wanajifaharisha kwa wingi wa idadi ya walioangamia? …. Ilitakikana hayo yawe mazinga­tio badala ya kujifaharisha.”

Si hivyo!

Acheni kujifaharisha kwa wingi, kwani hakuwafai chochote.

Mtakuja jua!

Adhabu itakayowapata.

Tena si hivyo! Mtakuja jua!

Huu ni msisitizo wa kutoa hadhari.

Si hivyo! Lau mngelijua kwa ujuzi wa yakini.

Yaani lau mngelikuwa mnajua kwa ujuzi wa uhakika matokeo ya kujifa­harisha kwa wingi, basi mngelikoma kufanya hivyo. hapo kuna ishara kwamba ilimu bila ya matendo ni sawa na ujinga. Katika hilo Imam Ali (a.s.) anasema: “Ilimu inatoa mwito wa kufanya, asipouitikia inamwondo­ka.

Hakika mtauona Moto!

Hii ni kumhadharisha mwenye kuukadhibisha huo Moto, au akauamini lakini asifanye kwa mujibu wa imani yake. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameleta kinaya cha kuona kwa maana ya kuuingia.

Kisha, hakika, mtauona kwa jicho la yakini.

Hii ni kusisitiza kuwa wataujua na kwamba wataujua kwa macho.

Inaonyesha kuwa nadharia yoyote isiyotegemea kuonekana na kushuhudi­wa na macho moja kwa moja au kwa kupitia kitu kingine, basi hiyo sio ilimu. Kwa hiyo ilimu ya kweli ni kuliona jambo lenyewe au kuona athari yake inayolifahamisha. Ya kwanza inaitwa ilimu ya uoni na ya pili ni ilimu ya dalili.

Kisha hakika mtaulizwa siku hiyo juu ya neema.

Makusudio ya neema hapa ni mali wanayojifaharisha nayo, kwa lugha ya kusema au ya hali. Wataulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu: wameipata wapi? Wameitumia vipi? Je, waliipata kwa jasho lao au kwa kupora? Je, wameitumia katika njia ya halali au haramu?

Ama mahitaji ya kawaida, kama chakula, mavazi na makazi, sio neema inayokusudiwa hapa.