read

Sura Ya Mia Na Mmoja: Al-Qari’aa

Imeshuka Makka Ina Aya 11.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

الْقَارِعَةُ {1}

Inayogonga!

مَا الْقَارِعَةُ {2}

Nini inayogonga?

وَمَا أَدْرَاكَ مَا الْقَارِعَةُ {3}

Na nini cha kukujuilisha nini inayogonga?

يَوْمَ يَكُونُ النَّاسُ كَالْفَرَاشِ الْمَبْثُوثِ {4}

Siku ambayo watu watakuwa kama panzi waliotawanyika.

وَتَكُونُ الْجِبَالُ كَالْعِهْنِ الْمَنْفُوشِ {5}

Na milima itakuwa kama sufi zilizochambuliwa!

فَأَمَّا مَنْ ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ {6}

Basi yule ambaye mizani yake itakuwa nzito.

فَهُوَ فِي عِيشَةٍ رَاضِيَةٍ {7}

Huyo atakuwa katika maisha ya kuridhiwa.

وَأَمَّا مَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ {8}

Na yule ambaye mizani yake itakuwa hafifu.

فَأُمُّهُ هَاوِيَةٌ {9}

Basi mama yake atakuwa Hawiya!

وَمَا أَدْرَاكَ مَا هِيَهْ {10}

Na nini kitachokujuilisha nini hiyo?

نَارٌ حَامِيَةٌ {11}

Ni Moto mkali!

Maana

Inayogonga!

Hilo ni mojawapo ya majina ya siku ya Kiyama. Kwa sababu kinagonga nyoyo; mfano wake ni Tukio la haki, Ukelele, Balaa kubwa n.k.

Nini inayogonga?

Ni swali lenye lengo la kulikuza jambo.

Na nini cha kukujuilisha nini inayogonga?

Ni jambo gani la kukujulisha kuwa siku hiyo iko zaidi ya inavyofikiriwa.

Siku ambayo watu watakuwa kama panzi waliotawanyika.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amefananisha hali ya viumbe Siku ya Kiyama na hali ya panzi katika kutojua wafanye nini na wengi wao kuanguka motoni.

Na milima itakuwa kama sufi zilizochambuliwa kwa kutawanyika. Basi yule ambaye mizani yake itakuwa nzito.

Yaani yule ambaye matendo yake yatakuwa mema, Huyo atakuwa katika maisha ya kuridhiwa; yaani atayaridhia na kuyafurahia.

Na yule ambaye mizani yake itakuwa hafifu; yaani matendo yake yaki­wa mabaya.

Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi katika Juz. 17 (21:45-50).

Basi mama yake atakuwa Hawiya!

Makusudio ya mama hapa ni mahali atakapofikia na patakapomkumbatia. Hawiya ni Jahannam. Neno hili lina maana ya kuangukia. Imeitwa hivyo kwa sababu mwenye hatia ataaangukia hapo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amelibainisha hilo kwa kusema:

Na nini kitachokujuilisha nini hiyo Hawiya? Ni Moto mkali!

Haya ndiyo unayoweza kuyafahamu kuhusiana na Jahannam. Ama kuijua hakika yake, utashindwa kufahamu, kwa sababu shimo lake liko ndani sana na adhabu yake ni kali.