read

Sura Ya Mia Na Nane: Al-Kawthar

Imeshuka Makka Ina Aya 3.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ {1}

Hakika tumekupa wingi sana.

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ {2}

Basi swali kwa ajili ya Mola wako na uchinje.

إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ الْأَبْتَرُ {3}

Hakika mwenye kukubughud­hi, yeye ndiye mwenye kuishi­wa.

Maana

Hakika tumekupa wingi sana.

Neno wingi sana tumelitoa kwenye neno kawthar lenye maana ya uzaidi wa wingi. Wametofautiana kuhusu wingi huu wa zaidi. Lililo karibu zaidi na ufahamu ni lililonukuliwa na wafasiri, kutoka kwa Ibn Abbas na Said bin Jubayr, kwamba makusudio ya wingi sana ni yote yale aliyomneeme­sha Mwenyezi Mungu Mtume wake mtukufu. Kwa sababu neno kawthar linatumika kwa wingi wa wingi usiokuwa na ukomo wala udhibiti.

Saidi aliambiwa kwamba watu wanasema kuwa kawthar ni mto katika Pepo.
Akasema: “Hakika mto huu ni katika heri nyingi alizompa Mwenyezi Mungu Muhammad (s.a.w.), lakini waasi wapenda anasa wanadharau heri hizi nyingi na hawezioni ni chochote; huku wakasema kuhusiana na Mtume mtukufu:

 لَوْلَا أُنْزِلَ عَلَيْهِ كَنْزٌ {12}

“Mbona hakutermshiwa hazina?” Juz. 11 (11:12).

Basi swali kwa ajili ya Mola wako na uchinje.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kumkumbusha Nabii wake mtukufu, neema alizompa, sasa anamwamrisha kushukuru na kwamba swala yake na dhabihu zake ziwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu peke yake.

Kuna riwaya nyingine inayosema kuwa makusudio ya neno wanhar tulilo­lifasiri kwa maana ya uchinje, hapa lina maana kuinua mikono hadi kufika mkabala wa shingo wakati wa kuelekea Qibla kwenye Swala.

Hakika mwenye kukubughudhi, yeye ndiye mwenye kuishiwa.

Hii ni jumla nyingine inayoanza upya. Wametofautiana kuhusu aliyeishi­wa. Kauli iliyo karibu zaidi ni kuwa adui wa Muhammad (s.a.w.) ni bure tu asiyekuwa na athari yoyote wala utajo wowote. Lakini utajo wake Mtume una athari na utabakia kwa kubakia Mwenyezi Mungu.

Wafasiri wengi wamesema kuwa mmoja wa washirikina alisema: “Muhammad ameishiwa hana mtoto,” ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akampa habari Mtume wake kuwa mwenye kusema hivi ndiye aliyeishiwa hata kama ana watoto. Hakuna kizuizi cha kuchanganya maana zote mbili.

Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Mwenye kumbughudhi Muhaammad hakuubughudhi utu wa Mtume (s.a.w.) kwa sababu alikuwa ni kipenzi cha nyoyo; isipokuwa waliobughudhi walichukia uongofu aliokuja nao…Na walioishiwa wanaingia wale walioacha Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kushikamana na dhana na kauli za wasiokuwa maa­sumu… wakijiambatanisha na bid’a katika dini.

Wanapotajiwa Qur’an wanapeta vichwa vyao…si ajabu kuwa ghadhabu ya Mwenyezi Mungu inawafuata kila mahali na wanapatwa na udhalili baada ya udhalili wakiwa hawatambui; bali wanacheka.”