read

Sura Ya Mia Na Nne: Al-Humaza

Imeshuka Makka Ina Aya 9.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

وَيْلٌ لِكُلِّ هُمَزَةٍ لُمَزَةٍ {1}

Ole wake kila msingiziaji, msengenyaji!

الَّذِي جَمَعَ مَالًا وَعَدَّدَهُ {2}

Aliyekusanya mali na kuyahis­abu.

يَحْسَبُ أَنَّ مَالَهُ أَخْلَدَهُ {3}

Anadhani ya kuwa mali yake yatambakisha milele!

كَلَّا ۖ لَيُنْبَذَنَّ فِي الْحُطَمَةِ {4}

Si hivyo! Bila shaka Atavurumishwa katika Hutwama.

وَمَا أَدْرَاكَ مَا الْحُطَمَةُ {5}

Ni nini cha kukujulisha ni nini Hutwama.

نَارُ اللَّهِ الْمُوقَدَةُ {6}

Ni Moto wa Mwenyezi Mungu uliowashwa?

الَّتِي تَطَّلِعُ عَلَى الْأَفْئِدَةِ {7}

Ambao unapanda nyoyoni.

إِنَّهَا عَلَيْهِمْ مُؤْصَدَةٌ {8}

Hakika huo utafungiwa juu yao.

فِي عَمَدٍ مُمَدَّدَةٍ {9}

Kwenye maguzo marefu.

Maana

Ole wake kila msingiziaji, msengenyaji!

Msingiziaji na msengenyaji tumeyafasiri kutokana na maneno humaza na lumaza. Imesemekana pia maana ya lumaza ni kutumia jicho, kubinua mdomo na mkono, na lumaza ni kutumia ulimi.

Ni sawa sifa mbili ziwe na maana moja au mbalimbali, lakini yote yanashirikiana katika kuudhi watu na kuwavunjia heshima kwa kauli au kwa vitendo. Mazoewa haya mabaya huwa yanatokana na kujihisi mtu kuwa na upungufu, ndio anajaribu kuu­funika upungufu wake kwa kuwatia ila wenzake.

Imam Ali (a.s.) anasema: “Muovu zaidi wa watu ni yule asiyewamwamini yeyote kwa dhana yake mbaya na asiyeaminiwa na yeyote kwa vitendo vyake vibaya.”

Aliyekusanya mali na kuyahisabu.

Ameyakusanya mali kutokana na halali na haramu na kuyahisabu kila mara kwa kuipenda sana. Hii ndiyo iliyomfanya kuwasingizia na kuwasengenya wengine; akiwa amesahau kwamba haya yote atayaacha muda mchache ujao na atabakiwa na hisabu yake itakyomfuatia.

Anadhani ya kuwa mali yake yatambakisha milele!

Hivi anadhani kwamba mali hii aliyoikusanya na kuihisabu itamkinga na mauti au kumwokoa na hisabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake?

Si hivyo! Bila shaka Atavurumishwa katika Hutwama ambayo ni Jahannam itakayowapondaponda wakosefu, (kama linavyofahamisha neno hutwama). Kuvurumishwa ni neno linalotambulisha udhalili.

Ni nini cha kukujulisha ni nini Hutwama, iko zaidi ya unavyofikiria. Ni Moto wa Mwenyezi Mungu uliowashwa. Ni moto wa Mwenyezi Mungu sio moto wa watu na ni moto wa ghadhabu sio moto wa kuni.

Ambao unapanda nyoyoni.

kupanda tumelifasiri kutokana na neno tatwaliu. Imesemekana makusudio ni kujua na maarifa. Lakini kauli hii iko mbali na ufahamu wa kiujumla. Nyoyo ni kinaya cha kuwa Moto utakaopanda na kuunguza kila kiungo katika viungo vya wakosefu. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amehusisha kutaja nyoyo kwa sababu ndio tumbo la ukafiri na lawama.

Hakika huo utafungiwa juu yao, hakuna kukimbia.

Kwenye maguzo marefu. Hiki ni kinaya cha umadhubuti wa kufunikwa.

Umetangulia mfano wake katika Juzu hi tuliyo nayo (90:20).