read

Sura Ya Mia Na Saba: Al-Maa’un

Imeshuka Makka. Imesekana si hivyo. Ina Aya 7.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu

أَرَأَيْتَ الَّذِي يُكَذِّبُ بِالدِّينِ {1}

Je, umemwona ambaye anakadhibisha dini?

فَذَٰلِكَ الَّذِي يَدُعُّ الْيَتِيمَ {2}

Huyo ni ambaye humsukuma yatima.

وَلَا يَحُضُّ عَلَىٰ طَعَامِ الْمِسْكِينِ {3}

Wala hahimizi kumlisha mask­ini.

فَوَيْلٌ لِلْمُصَلِّينَ {4}

Basi ole wao wanaoswali.

الَّذِينَ هُمْ عَنْ صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ {5}

Ambao wanasahau Swala zao.

الَّذِينَ هُمْ يُرَاءُونَ {6}

Ambao wanafanya ria.

وَيَمْنَعُونَ الْمَاعُونَ {7}

Na wanazuia msaada.

Maana

Je, umemwona ambaye anakadhibisha dini?

Maana ya kumuona ni kumjua. Tamko ni la swali na maana yake ni kukanusha yaliyotokea. Maneno yanaelekezwa kwa wote; kwa sababu Sura hii kwa ujumla wake inajulisha udugu baiana ya dini na matendo na kuzingatia kuwa ni sehemu yake isiyoachana. Kisha dini inawakana wale wanaosifika na uovu ufuatao:

Huyo ni ambaye humsukuma yatima.

Makusudio ya kumsukuma hapa ni kumzuilia haki yake iwe ni kwa nguvu au bila ya nguvu, kumdharau au kumuudhi au kwa kumkalia kwa namna yoyote ya dhulma. Makusudio ya yatima hapa ni kila mdhaifu asiyejiweza; awe mdogo au mkubwa. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amehusisha kumtaja yatima kwa vile ni mdhaifu zaidi ya wadhaifu.

Maana ni kuwa kila dhalimu ni kafiri mwenye kukadhibisha dini ya Mwenyezi Mungu; hata kama ataswali na kufunga. Kwa sababu dini ya Mwenyezi Mungu haitosheki na mambo ya dhahiri na nembo; isipokuwa pamoja na takua na kujizuia na yaliyo haramu.

Ni kweli kuwa kila mwenye kusema: ailaha illa llah uhammadur-rasulullah, anachukuliwa kuwa ni mwislamu duniani, lakini hukumu yake Akhera ni ya kafiri. Tazama Juz. 19 (25:55).

Wala hahimizi kumlisha maskini.

Makusudio ya kuhimiza hapa ni kusaidiana na wengine kuwashughulikia wasiojiweza. Makusudio ya masikini ni kila asiyemiliki sababu za riziki na kutekeleza mahitaji. Umetangulia mfano wake katika Juz. 29 (69:34) na Juzuu hii tuliyo nayo (89:18).

Basi ole wao wanaoswali, ambao wanasahau Swala zao.

Kusahau hapa sio makusudio, kwa sababu mwenye kusahau hana majuku­mu kiakili na kisharia. Mtume mtukufu (s.a.w.) anasema: “Umma wangu umeondolewa kukosea na kusahau.” Kwa hiyo basi hapana budi kuchuku­lia kusahau kwa maana nyingine. Maana yenyewe Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anayabainisha kwa kusema:

Ambao wanafanya ria na wanazuia msaada.

Yaani hawasaidii kwa kujikurukubisha kwa Mwenyezi Mungu bali wanafanya kwa kujionyesha kwa watu. Ujumla wa maana ni kuwa wenye kusahau Swala zao wanaswali, lakini kwa ria na unafiki na kuwahofia watu sio kumhofia Mwenyezi Mungu. Wao wanadhihirisha uzuri na kuficha ubaya.

Hivi ndivyo walivyo katika matendo yao yote; wanajikurubisha kwayo kwa waja wa Mwenyezi Mungu na kujiweka mbali kwayo na Mwenyezi Mungu Mtukukufu na radhi zake; hata msaada pia hawautoi ila kwa ria na unafiki.

Hii inatufichulia kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja msaada kufanan­isha ria yao katika kila kitu, sio katika swala tu, bali hata kwenye mambo madogo kama kuazima.