read

Sura Ya Mia Na Sita: Quraysh

Imeshuka Makka Ina Aya 4.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu

لِإِيلَافِ قُرَيْشٍ {1}

Kwa ajili ya kuzowea maku­raishi.

إِيلَافِهِمْ رِحْلَةَ الشِّتَاءِ وَالصَّيْفِ {2}

Kuzowea kwao safari ya kusi na kaskazi.

فَلْيَعْبُدُوا رَبَّ هَٰذَا الْبَيْتِ {3}

Basi wamwabudu Mola wa nyumba hii.

الَّذِي أَطْعَمَهُمْ مِنْ جُوعٍ وَآمَنَهُمْ مِنْ خَوْفٍ {4}

Ambaye amewalisha wasipate njaa na akawasalimisha na hofu.

Maana

Wametofautiana kuhusu Sura hii kuwa je, inajitegemea kama Sura moja peke yake, au inaungana na Sura Fiyl na kuwa sura moja?

Anasema Al-hafidh Al-Kalabiy katika afsir Attashil: “Kauli ya kuwa hizo ni Sura moja inatiliwa nguvu kwamba, kwenye msahafu wa Ubayya bin Kaa’b, hazikutengenishwa. Vile vile Umar alizisoma pamoja katika rakaa moja kwenye Swala ya maghrib.

Hii inaafikiana na kauli ya Shia Imamiya. Na amesema mwenye Dhilal: “Sura hii inaonyesha kuwa ni mwendelezo wa sura iliyo kabla yake, kwa maudhui yake na mazingira yake.

Mwenye kuifanya Sura hii kuwa inaungana na ya kabla yake anasema maneno ‘Kwa ajili ya kuzowea Makuraishi yanaungana na akawafanya kama majani yaliyoliwa, kwa ajili ya kuzowea Makuraishi.
Na mwenye kusema kuwa ni sura inayojitegemea, anasema: Kwa ajili ya kuzowea Makuraishi, basi wamwabudu Mola….
Kwa ajili ya kuzowea makuraishi.

Kuraishi ni jina la kabila la waraabu wa kizazi cha Nadhr bin Kinana. Katika baadhi ya tafsiri imesemwa kuwa neno Kuraishi limetokana na neno qarash lenye maana ya biashara. Waliitwa hivyo kwa vile walikuwa wafanyibiashara; hilo likiashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukukufu:

Kuzowea kwao safari ya kusi na kaskazi.

Katika karne ya sita (A.D.) wakazi wa Makka walikuwa makundi matatu: La kwanza likuwa ni Makuraishi waliokuwa na haki zote. La pili ni marafi­ki wa Makuraishi, lililokuwa la waarabu wengineo. Na la tatu lilkuwa la watumwa waliokowa hawamiliki chochote hata nafsi zao pia.

Makuraishi walikuwa na misafara miwili ya kibiashara kila mwaka: msa­fara wa kwenda Yemen katika majira ya baridi na msafara wa kwenda Sham katika majira ya joto.

Walikuwa wakienda na kurudi kwa amani kwenye misafara yao, bila ya kuguswa na yeyote kwa uovu, kwa vile walikuwa ni wakazi wa Makka walio jirani na nyumba ya Mwenyezi Mungu, tukufu; kama walivyosema wafasiri au kama tunavyodhania sisi, kwamba waarabu ni lazima waje wahiji Makka; wakiogopa kama watauchokoza msafara wa makuraishi basi watakuja walipizia kisasi watakapokuja kwenye mji wao.

Wapokezi wanasema kuwa ni katika misafara hii ndio Muhammad (s.a.w.) aliwahi kusafiri na ami yake Abu Twalib kwenda Sham. Wakati huo umri wake mtukufu ulikuwa ni miaka 12, lakini hakuwahi kufika naye Sham, bali walirudi haraka Makka kutokana na ushauri wa mtawa wa kinaswara (mkiristo) aliyemuusia kumlinda na njama za Mayahudi na wanaswara.

Vile vile wanasema wapokezi kuwa Muhammad (s.a.w.) alitoka na ami yake Zubeir kwenda Yemen katika msafara wa kusi, wakati akiwa na umri wa miaka ishirini na kidogo; na msafara huo ulikuwa kabla ya kwenda Sham na mali ya Khadija.

Basi wamwabudu Mola wa nyumba hii.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawaamuru waache kuaabudu masanamu na wamwabudu mmoja aliye pekee, ambaye amewalisha wasipate njaa na akawasalimisha na hofu.

Katika Aya hii Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawakumbusha waasi wa kiku­raishi, wanaoabudu masanamu, badala ya Mwenyezi Mungu, na kumkad­hibisha Nabii wake mtukufu Muhammad (s.a.w.), tukio la ndovu jinsi alivyowaokoa Mwenyezi Mungu na Abrah na jeshi lake. Lau si fadhila zake Mwenyezi Mungu wangelikuwa wao ndio kama majani yaliyoliwa badala ya watu wa ndovu.

Vile vile anawakumbusha jinsi alivyowaneemesha Mwenyezi Mungu kwa riziki kwa sababu ya misafara miwili, ambayo kama si hiyo wangelikufa na njaa; kwa sababu wao wako katika bonde lisilokuwa na mimea. Fauka ya hayo amewafanya wawe na amani na utulivu kwa mali yao na roho zao katika misafara yao.

Lau si fadhila yake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Watu wangeliwapora kila mahali. Hivi baada ya yote haya wanaweza kuabudu masanamu, kuzikufuru neema za Mwenyezi Mungu na kumkadhibisha Mtume wake mtukufu? Kweli mtu ni dhalimu mkubwa wa nafsi yake na mjinga sana.