read

Sura Ya Mia Na Tano: Al-Fil

Imeshuka Makka. Ina Aya 5.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيلِ {1}

Je, hukujua namna gani alivy­owafanya Mola wako wenye ndovu?

أَلَمْ يَجْعَلْ كَيْدَهُمْ فِي تَضْلِيلٍ {2}

Je, hakuvifanya vitimbi vyao ni vyenye kupotea?

وَأَرْسَلَ عَلَيْهِمْ طَيْرًا أَبَابِيلَ {3}

Na akawapelekea ndege makundi makundi.

تَرْمِيهِمْ بِحِجَارَةٍ مِنْ سِجِّيلٍ {4}

Wakawatupia mawe ya udon­go mkavu.

فَجَعَلَهُمْ كَعَصْفٍ مَأْكُولٍ {5}

Akawafanya kama majani yaliyoliwa!

Kisa Kwa Ufupi

Kisa cha ndovu kilitokea mwaka aliozaliwa Mtume mtukufu (s.a.w.). Kwa ufupi ni: Baada ya wahabeshi kuishinda Yemen waliikusudia Makka kwa nia ya kuivunja Al-Ka’aba. Basi wakaenda huku wakimtanguliza au kuwatanguliza ndovu.

Walipofika karibu na Makka mahali panapoitwa Al-Mughammas, walishuka na wakampeleka raisi wao, Abraha, kama wanavyomwita wapokezi, kwa makuraishi awape habari kuwa wao hawakuja kupigana nao isipokuwa wamekuja kuivunja Al-Ka’aba, na kama hawatawasumbua na vita basi nao hawana haja na damu yao.

Kabla ya Abrah kutekeleza lengo lake, Mwenyezi Mungu alimtumia jeshi la ndege wakiwatupia vijiwe vidogo, kila kinayempata basi anashikwa na maradhi ya ndui na nyama humpukutika na kuanguka chini, jeshi likaogo­fywa na likakimbia. Abraha naye pia alipatwa na ugonjwa huo, akafia Sanaa.

Dkt Twaha Hussein, katika Kitabu ir-atul-slam, anasema: “Katika tukio hili Abdul Muttwalib, alionyesha subira, ushujaa na uimara kwa namna ambayo hajawahi kuionyesha yeyote katika watukufu wa kikuraishi. Hilo ni kwa kuwa aliwashauri makuraishi waikimbie Makka na watu wake wakamsikiza, lakini yeye alibakia Makka bila ya kuondoka na akasimama mbele ya Al-Ka’aba, akimuomba Mwenyezi Mungu na kumtaka nusra.

Wapokezi wanasema kuwa jeshi liliteka ngamia wa makuraishi, akaja Abdul-Muttwalib kwa Abrah. Alipofika hakumwambia lolote zaidi ya madai ya ngamia wake. Abrah akamdharau na kumwambia: “Mimi nad­hani umekuja kuzungumza nami kuhusu Makka na hii nyumba ambayo mnaitukuza?” Abdul-Muttwalib akamwambia: “Mimi ninakuzungumzia mali yangu ninayoimiliki, lakini hiyo nyumba ina Mlezi wake, ataihami akitaka.”

Basi Mwenyezi Mungu akampelekea, Abraha na jeshi lake, ndege hao waliowatupia mawe ya udongo mkavu ukawafanya kama majani yaliyoli­wa. Makuraishi wakarudi Makka na wakazidi kumtukuza Abdul­Muttwalib, kwa ushujaa, uthabiti na uimara wake.

Maana

Je, hukujua namna gani alivyowafanya Mola wako wenye ndovu?

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), na swali ni kuelezea hali halisi ilivyo; yaani unajua ewe Muhammad vile Mwenyezi Mungu alivyowafanya wenye ndovu. Hii ni kumtuliza Mtume kwamba aliyewaangamiza watu wa ndovu ana uwezo pia wa kuangamiza wakadhibishaji.

Je, hakuvifanya vitimbi vyao ni vyenye kupotea?

Makusudio ya vitimbi ni kupanga njama. Maana ni kuwa Wahabeshi wali­panga njama mbaya dhidi ya nyumba ya Mwenyezi Mungu tukufu, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alivipoteza vitimbi vyao na juhudi yao ikaenda bure.

Na akawapelekea ndege makundi makundi.

Wafasiri na wapokezi wanasema yalikuja makundi kwa makundi ya ndege wadogo kutoka baharini, wakawatupia mawe ya udongo mkavu, uliokuwa jiwe.

Akawafanya kama majani yaliyoliwa.

Neno majani tumelitoa kwenye neno Asf ambalo maana yake ni kupeperu­ka. Yameitwa hivyo kwa vile yanapeperushwa. Makusudio ya kuliwa hapa ni kama kuliwa na wadudu.

Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Inawezekana uamini kuwa ndege hawa walikuwa ni mbu au nzi waliochukua viini vya magonjwa na kwam­ba mawe haya yalikuwa ni udongo ulio na sumu inayopeperushwa na upepo na kushika kwenye miguu ya wanyama hawa, ikifika kwenye mwili wa mtu mtu kumwambukiza sumu hiyo na kuathiri mwili na kuanguka nyama zake.”

Ilivyo ni kuwa kauli yake, inawezekana uamini kuwa ndege hawa walikuwa ni mbu au nzi... na kwamba mawe haya yalikuwa ni udongo ulio na sumu, kauli hii haiwezi kuwa ni sawa ila ikitegemea kwenye dalili mkataa au ushahidi wa kuonekana, kulingana na maneno yake huyo huyo Sheikh Muhammad Abduh.

Lau angelisema: Inawezekana uone kuwa kuna uwezekano, angalau inge­likuwa iko karibu na usawa.

Ama sisi tunachukua dhahiri ya matamko, kama walivyofanya waislamu wa mwanzo, maadamu akili hailikatai hilo.