read

Sura Ya Mia Na Tatu: Al-A’sr

Imeshuka Makka Ina Aya 3.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

وَالْعَصْرِ {1}

Naapa kwa Zama!

إِنَّ الْإِنْسَانَ لَفِي خُسْرٍ {2}

Hakika mtu bila ya shaka yumo katika hasara.

إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ {3}

Ila wale walioamini, na waka­tenda mema, Na wakausiana haki, na wakausiana kusubiri.

Maana

Naapa kwa Zama!

Neno zama tumelifasiri kutokana na neno A’sr, ambalo wafasiri wameto­fautiana katika makusudio yake kwa kauli mbali mbali:

Ya kwanza, ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameapa kwa Swala ya alasiri, kwa lengo la kutanabahisha ubora wake kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ {238}

“Angalieni sana Swala na ile Swala ya katikati.” Juz. 2 (2:238).

Kauli hii iko mbali na ufahamu wa kiujumla.

Kauli ya pili, ni kwamba makusudio ni zama za Mtume (s.a.w.). Kauli hii iko mbali zaidi kuliko ile ya kwanza.

Kauli ya tatu, ni wakati wa alasiri, mwisho wa mchana. Kwamba Mwenyezi Mungu hapa ameapa na mwisho wa mchana, kama alivyoapa na mwanzo wa mchana kwenye Juzuu hii tuliyo nayo (91:1). Kauli hii haiko mbali sana na ufahamisho wa tamko.

Kauli ya nne, kwamba makusudio ya Al-a’sr ni wakati wowote ambao unatukia matukio na matendo. Mfumo wa maneno unaashiria kwenye kauli hii; kwani kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Hakika mtu bila ya shaka yumo katika hasara,’ iliyokuja moja kwa moja bila ya kuweko kati maneno mengine, inatambulisha kuwa mtu ndiye aliye katika hasara na wala sio zama.

Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Ni desturi ya waarabu kukusanyika wakati wa alasiri na kuzungumza mambo yao. mara nyingine mazungum­zo yao yanapelekea yale yanayowachukiza, watu wakaushutumu wakati huo. Ndio Mwenyezi Mungu akaapia nao ili kuwabainishia kuwa wakati haushutumiwi; isipokuwa vinavyoshutumiwa ni vitendo vya kuchukiza na wakati ni wa mambo mema na maovu na utukufu na udhalili.

Hakika mtu bila ya shaka yumo katika hasara; ila wale walioamini, na wakatenda mema.

Hili ndilo jawabu la kiapo. Makusudio ya mtu ni yule mwenye majukumu ya kauli yake na vitendo.

Mtu huyu, kwa hukumu ya Qur’an, ni mwenye hasara, hata kama ni tajiri aliye na mamilioni, au mtaalmu anayejua siri za maumbile na kuzitumia kwa masilahi yake, au mwenye nguvu za kuwatawala watu, au mwenye ufasaha anayeweza kutengeneza maneno na mawaidha.

Huyu atakuwa hana kitu na ni mwenye hasara tu, isipokuwa akimwamini Mwenyezi Mungu, halali yake na haramu yake, Moto wake na Pepo yake; na imani yake hii iakisi kwenye kauli yake na vitendo vyake; vinginevyo imani bila ya matendo ni kiasi cha fikra tu na nadharia.

Miongoni mwa niliyoyasoma, ni kuwa wanaanga watatu wa kimarekani waliorusha bomu la nyuklia kule Hiroshima Japan, kila mmoja wao alikuwa na nakala ya ‘Biblia takatifu’ pembeni mwa kombora la maangamizi!!

Unaweza kuuliza: kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Hakika mtu bila shaka yuko katika hasara,’ si inafahamisha kwa dhahiri yake, kuwa mtu ni mwenye hasara kwa maumbile yake; na kwamba watu wako sawa kwenye hasara? Ikiwa ni hivyo basi haifai kuwagawanya watu kwenye wema na uovu, hasara na faida. Kwa sababu dhati haiwezi kubadilika; hati­mae kuna haja gani ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Ila wale walioamini na wakatenda mema?

Jibu: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuhukumu maumbile ya mtu kwenye hasara, kama mtu; isipokuwa ni kwa uaghlabu. Mfano huu kwenye Qur’an ni mwingi; kama vile kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 إِنَّ الْإِنْسَانَ لَظَلُومٌ كَفَّارٌ {34}

“Hakika mtu ni dhalimu mkubwa mwingi wa kukufuru.” Juz. 13 (14:34)

Pia kauli yake:

 وَكَانَ الْإِنْسَانُ قَتُورًا {100}

“Mtu ni mchoyo sana.” Juz. 15 (17:100).

Kwa hiyo basi mtu kwa maumbile yake hahisabiwi kuwa ni mwenye hasara wala mwenye faida, kwa sababu yeye ana uwezo na maandalizi ya yote mawili. Hivyo kumchukila kwenye moja wapo itakuwa ni kutia nguvu bila ya nguvu. Atachukuliwa, kwa moja wapo ya sifa mbili, kwa kuangalia itikadi yake na matendo yake; sio kuangalia dhati yake na maumbile yake.

Mara nyingi tumeeleza kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amempa mtu akili na uwezo wa kufanya shari na heri, akamwamrisha hili, wa akamkataza lile na akamwachia hiyari bila ya kumlazimisha dini na matendo kwa kuyaum­ba kama anavyoumba viumbe. Kama angelifanya hivi angeliuondoa utu wa mtu; kwa kuwa hakuna utu bila ya uhuru na utashi.

Kwa hiyo mtu hawi na hasara ila kwa itikadi yake na matendo yake. Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Hakika mtu bila ya shaka yumo katika hasara ila wale walioamini, na wakatenda mema,’ inamaanisha kuwa wale ambao hawakuamini au wameamini lakini wasitende, basi hao ndio walio na hasara, lakini walioamini na wakatenda hao ndio wenye faida na wenye kufuzu.

Na wakausiana haki, na wakausiana kusubiri.

Maneno haya yanaungana na walioamini na wakatenda. Maana ni kuwa wenye kufuzu kesho ni wale waliomwamini Mwenyezi Mungu na sharia yake, wakatenda kwa mujibu wa imani yao hiyo na wakausiana kushika­mana na haki na subira.

Sheikh Muhammad Abduh ameielezea haki kuwa: “Ni ile inayoongoza kwenye dalili mkataa au kuonekana na kushuhudiwa.”

Hii ni taarifa ya hakika sio ya haki. Tofauti iliyoko ni kwamba hakika ni mtoto wa dalili, ama haki inajisimamia hiyo yenyewe; ni sawa iwe imefa­hamishwa na dalili au haikufahamishwa. Watu wengi huwa wanashindwa kuithibitisha haki yao kwa dalili mkataa na ushahidi.

Vyovyote iwavyo ni kuwa kila tendo lililo na radhi ya Mwenyezi Mungu na masilahi kwa watu basi hiyo ni haki, heri na uadilifu. Ama subira ni kuthibiti kwenye haki na kumwambia anayeivunja: La! Kwa namna yoy­ote yatakavyokuwa matokeo.

Kwa ufupi ni kuwa kubwa lilio kwa mtu na neema muhimu aliy­oneemeshwa na Mwenyezi Mungu mtu, ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu amempa mtu uwezo wa kutosha kuwa malaika au shetani, mwenye faida au hasara; na kwamba hikima yake Mtukufu, imempa uhuru mtu peke yake kujichagulia mwenyewe analolitaka; uovu na hasara au faida na wema, na kwamba Mwenyezi Mungu atamchukulia kwa lile alilo­jichagulia mwenyewe - faida au hasara, baada ya kumpa mwongozo wa njia mbili. Kuna fadhila gani kuu kuliko hii na uadilifu gani mkubwa kuliko huu.