read

Sura Ya Mia Na Tisa: Al-Kafirun

Imeshuka Makka Ina Aya 6.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu

قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ {1}

Sema: Enyi makafiri!

لَا أَعْبُدُ مَا تَعْبُدُونَ {2}

Siabudu mnachokiabudu.

وَلَا أَنْتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ {3}

Wala nyinyi si wenye kuabaudu ninayemwabudu.

وَلَا أَنَا عَابِدٌ مَا عَبَدْتُمْ {4}

Wala mimi si mwenye kuabudu mlichokiabudu.

وَلَا أَنْتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ {5}

Wala nyinyi si wenye kuabudu ninayemwabudu.

لَكُمْ دِينُكُمْ وَلِيَ دِينِ {6}

Mna dini yenu nami nina dini yangu.

Maana

Sema: Enyi makafiri! Siabudu mnachokiabudu, wala nyinyi si wenye kuabaudu ninayemwabudu.

Inasemekana kuwa watu katika makafiri wa Kikuraishi walimwendea Nabii (s.a.w.) na kumwambia: wewe ni bwana wa Bani Hashim na mwana wa mabwana wakubwa wao, haitakikani wewe kuzisafihi fikra za watu wako, lakini tutaabudu sisi Mungu wako kwa muda wa mwaka na wewe uabudu mungu wetu mwaka mmoja; ndio ikashuka Aya hii.

Unaweza kuuliza nini makusudio ya kukaririka huku? Kwani kauli yake wala siabudu mnachokiabudu si ni sawa na kauli yake: wala mimi si mwenye kuabudu mlichokiabudu?

Hakuna tofauti isipokuwa ile ni jumla ya isimu na hii ni jumla ya kitendo. Tena kuna jumla nyingine imerudiwa kwa herufi zake.

Wala nyinyi si wenye kuabudu ninayemwabudu.

Sasa itakuwaje?

Wamelijibu hilo kwa jawabu mbali mbali; ikiwemo ile ya mwenye ajmaul bayan kwamba ya kwanza ni ya muda wa sasa na ya pili ni ya muda ujao. Lakini ieleweke kuwa zote mbili zinakubaliana na hali ya sasa na ya baadae, kwa hiyo inahitajia dalili.

Jibu jingine ni lile alilolisema Abu Muslim na akalichagua Sheikh Muhammad Abduh, kwamba ya kwanza ni anayeabudiwa na ya pili ni ibada yenyewe; yaani muabudiwa wangu sio muabudiwa wenu na ya pili iwe ibada yangu sio ibada yenu. Pia hapa ieleweke kuwa hakuna ibada bila ya muabudiwa na kwamba kuta­ja moja kunatosheleza kutaja nyingine.

Jibu jingine ni kuwa kukaririka huku kunafahamisha msisitizo, na kila inapohitajika kusisitiza basi kukaririka ni vizuri zaidi. Sisi tuko pamoja na rai hii.

Mna dini yenu nami nina dini yangu.

Yaani nyinyi mna kufuru na shirki na mimi nina ikhlasi na tawhid, wala sina mfungamano wowote na kile mnachokiabudu, na nyinyi ni hivyo hivyo kwangu. Hili ni kemeo na hadhari; mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukukufu:

 أَنْتُمْ بَرِيئُونَ مِمَّا أَعْمَلُ وَأَنَا بَرِيءٌ مِمَّا تَعْمَلُونَ {41}

“Nyinyi hamna jukumu kwa ninayoyatenda, na mimi sina jukumu kwa mnayoyatenda.”
Juz. 11 (10:41).