read

Sura Ya Sabini Na Nane: An-Nabai

Imeshuka Makka Ina Aya 40.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

عَمَّ يَتَسَاءَلُونَ {1}

Ni lipi waulizanalo.

عَنِ النَّبَإِ الْعَظِيمِ {2}

Ni ile habari kubwa,

الَّذِي هُمْ فِيهِ مُخْتَلِفُونَ {3}

Ambayo kwayo wanahitalifi­ana.

كَلَّا سَيَعْلَمُونَ {4}

Si hivyo! Punde tu watajua.

ثُمَّ كَلَّا سَيَعْلَمُونَ {5}

Tena si hivyo! Punde tu wata­jua.

أَلَمْ نَجْعَلِ الْأَرْضَ مِهَادًا {6}

Kwani hatukuifanya ardhi kuwa ni tandiko?

وَالْجِبَالَ أَوْتَادًا {7}

Na milima kuwa ni vigingi?

وَخَلَقْنَاكُمْ أَزْوَاجًا {8}

Na tukawaumba kwa jozi.

وَجَعَلْنَا نَوْمَكُمْ سُبَاتًا {9}

Na tukaufanya usingizi wenu ni kufa?

وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ لِبَاسًا {10}

Na tukaufanya usiku ni vazi?

وَجَعَلْنَا النَّهَارَ مَعَاشًا {11}

Na tukaufanya mchana ni maisha?

وَبَنَيْنَا فَوْقَكُمْ سَبْعًا شِدَادًا {12}

Na tukajenga juu yenu saba zenye nguvu?

وَجَعَلْنَا سِرَاجًا وَهَّاجًا {13}

Na tukafanya taa yenye mwangaza na joto kali?

وَأَنْزَلْنَا مِنَ الْمُعْصِرَاتِ مَاءً ثَجَّاجًا {14}

Na tukateremsha maji yenye kububujika kutoka kwenye yanayokamuliwa.

لِنُخْرِجَ بِهِ حَبًّا وَنَبَاتًا {15}

Ili tutoe kwayo nafaka na mimea.

وَجَنَّاتٍ أَلْفَافًا {16}

Na mabustani yenye miti iliy­ofungamana?

Aya 1- 16

Maana

Ni lipi waulizanalo. Ni ile habari kubwa, ambayo kwayo wanahitalifi­ana.

Misingi ya kuamini Uislamu ni mitatu: Kuamini umoja wa Mwenyezi, utume wa Muhammad na Siku ya Mwisho. Kaumu ya Mtume (s.a.w.) ilikuwa mbali kabisa na misingi hii mitatu; kwa hiyo waliulizana kwa mshangao wakisema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ {5}

“Amewafanya miungu wote kuwa ni Mungu Mmoja tu? Hakika hili kweli ni jambo la ajabu.”
Juz. 23 (38:5).

Vile vile walizidisha mshangao kwa Muhammad kuwa Mtume, si kwa lolote ila kwa kuwa ni fukara wa mali, wakasema miongoni mwa waliyose­ma:

 لَوْلَا أُنْزِلَ عَلَيْهِ كَنْزٌ  {12}

“Mbona hakuteremshiwa hazina?” Juz. 12 (11:12).

Kuhusu ufufuo wakasema:

أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَدِينُونَ {53}

“Ati tukishakufa tukawa udongo na mifupa, ndio tutahisabiwa?” Juz. 23 (37:53).

Misingi hii mitatu ndiyo iliyokuwa habari kubwa ambayo washirikina walikuwa wakiulizana. Kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.): ‘ambayo kwayo wanahitlaifiana,’ inaashiria kuwa miongoni mwao kuna waliosadi­ki kwa ndani bila ya kujionyesha na waliokadhibisha kwa ndani na nje au kutaradadi.

Si hivyo! Punde tu watajua. Tena si hivyo! Punde tu watajua.

Hii ni kuurudi ukanusho wao na kuwahadharisha na inadi yao. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameisisitiza hadhari hii kwa kuikariri, kisha akabainisha dalili za uweza wake na ishara za hikima yake, asaa wapinzani warejee kwenye uongofu na wahofie siku ya hisabu na malipo, ambayo amewa­hadharisha nayo Mtume; ndipo akasema mtukufu wa wasemaji:

Kwani hatukuifanya ardhi kuwa ni tandiko?

Yaani hamuoni jinsi Mwenyezi Mungu alivyoitiisha ardhi mnufaike nayo na kuitandika kama mnavyotandika kitanda cha mtoto.

Na milima kuwa ni vigingi?

Milima kwa ardhi ni kama vigingi kwenye hema; lau si hivyo basi ardhi ingelitingishika na kuwagonganisha wakazi wake.

Na tukawaumba kwa jozi, mwanamume na mwanamke, ili kuhifadhi kizazi na kujenga jamii.

Na tukaufanya usingizi wenu ni kufa? Kwa sababu usingizi ni aina ya mauti. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

وَهُوَ الَّذِي يَتَوَفَّاكُمْ بِاللَّيْلِ {60}

“Naye ndiye anayewafisha usiku.” Juz. 7 (6:60).

Usingizi ni lazima kwa ajili ya roho na mwili; wala uhai hauwezi kuwa bila ya huo; hata hivyo haipendekezwi kuuzidisha. Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Jihadharini na kulala sana, kwani mwenye kufanya hivyo ni fukara siku ya Kiyama.” Imam As-sadiq (a.s.) anasema: “Usingizi unaondoa dini na dunia.”

Na tukaufanya usiku ni vazi?

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameufananisha usiku na vazi kwa vile unamsi­tiri mtu na yale asiyotaka yaonekane.

Na tukaufanya mchana ni maisha?

Yaani wakati wa harakati na kufanya kazi kwa ajili ua uhai. Kwenye Aya nyingine, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema:

 وَجَعَلَ النَّهَارَ نُشُورًا {47}

“Na akaufanya mchana ni wa mtawanyiko.” Juz. 19 (25:47).

Kwa hiyo usingizi ni kama mauti na mchana ni kama kufufuka kuwa hai.

Na tukajenga juu yenu saba zenye nguvu? Makusudio ya saba hapa ni sayari saba zilizo maarufu kwa watu; vinginevyo ni kuwa mbali ya hizi ziko nyingine zisizo na idadi.

Mwenyezi Mungu amezipa sifa za kuwa na nguvu kwa vile zimepangiliwa vizuri. Tumeyazungumzia kwa ufafanuzi haya katika Juz. 28 (65:12).

Na tukafanya taa yenye mwangaza na joto kali. Makusudio ya taa hapa ni Jua ambalo mwangaza wake unatumika kwa viumbe kwa ajili ya maisha yao.

Na tukateremsha maji yenye kububujika kutoka kwenye yanayoka­muliwa.

Yanayokamuliwa hapa ni mawingu. Yameitwa hivyo kwa sababu upepo unayakamua mpaka yanatoa maji hayo yanayobubujika. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu ameteremsha mvua kutoka mawinguni.

Ili tutoe kwayo nafaka na mimea.

Ardhi inapata uhai kwa maji baada ya kufa kwake na inatoa chakula cha binadamu, wanyama na wengineo. Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

كُلُوا وَارْعَوْا أَنْعَامَكُمْ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِأُولِي النُّهَىٰ {54}

“Kuleni na mchunge wanyama wenu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa wenye akili.”
Juz. 16 (20:54)
.

Na mabustani yenye miti iliyofungamana.

Yaani matawi yake yameingiliana kwa sababu ya kukurubiana miti. Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kuyaweza maajabu haya basi anawa uwezo zaidi wa kuwafufua wafu.

Maana haya yamekaririka mara nyingi; ikiwemo ile isemayo:

حَتَّىٰ إِذَا أَقَلَّتْ سَحَابًا ثِقَالًا سُقْنَاهُ لِبَلَدٍ مَيِّتٍ فَأَنْزَلْنَا بِهِ الْمَاءَ فَأَخْرَجْنَا بِهِ مِنْ كُلِّ الثَّمَرَاتِ ۚ كَذَٰلِكَ نُخْرِجُ الْمَوْتَىٰ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ {57}

“Hata zinapobeba mawingu mazito tunayasukuma kwa ajili ya mji ulioku­fa. Kisha tunateremsha hapo maji. Kwa hayo tukaotesha kila matunda. Kama hivi tutawafufua wafu ili mpate kukumbuka.” Juz. 8 (7:57)

إِنَّ يَوْمَ الْفَصْلِ كَانَ مِيقَاتًا {17}

Hakika Siku ya upambanuzi imewekewa wakati.

يَوْمَ يُنْفَخُ فِي الصُّورِ فَتَأْتُونَ أَفْوَاجًا {18}

Siku itakapopulizwa para-panda nanyi mtakuja makun­di makundi.

وَفُتِحَتِ السَّمَاءُ فَكَانَتْ أَبْوَابًا {19}

Na mbingu zitafunguliwa ziwe milango.

وَسُيِّرَتِ الْجِبَالُ فَكَانَتْ سَرَابًا {20}

Na milima itaondolewa iwe sarabi.

إِنَّ جَهَنَّمَ كَانَتْ مِرْصَادًا {21}

Hakika Jahannam inangoja!

لِلطَّاغِينَ مَآبًا {22}

Kwa walioasi ndio marejeo.

لَابِثِينَ فِيهَا أَحْقَابًا {23}

Wakae humo siku nyingi.

لَا يَذُوقُونَ فِيهَا بَرْدًا وَلَا شَرَابًا {24}

Hawataonja humo baridi wala kinywaji.

إِلَّا حَمِيمًا وَغَسَّاقًا {25}

Isipokuwa maji ya moto na usaha.

جَزَاءً وِفَاقًا {26}

Ni malipo muwafaka.

إِنَّهُمْ كَانُوا لَا يَرْجُونَ حِسَابًا {27}

Hakika wao walikuwa hawatarajii kuhisabiwa.

وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا كِذَّابًا {28}

Na wakazikadhibisha Ishara zetu kuzikadhibisha.

وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ كِتَابًا {29}

Na kila kitu tumekidhibiti kwa kukiandika

فَذُوقُوا فَلَنْ نَزِيدَكُمْ إِلَّا عَذَابًا {30}

Basi onjeni! Hatutawazidishia ila adhabu!

Aya 17 – 30: Siku Ya Upambanuzi

Maana

Hakika Siku ya upambanuzi imewekewa wakati.

Siku ya upambanuzi ni Siku ya Kiyama; ndani yake itapambanuliwa haki na batili na ina wakati maalum, lakini haujui isipokuwa Mwenyezi Mungu. Wakati huo ndipo ulimwengu utaisha na viumbe hai na waliokufa watagur­ishwa kupelekwa kwenye ulimwengu mwingine usiofanana na dunia yetu na chochote. Ulimwengu usiokuwa na batili wala kwisha, wala kuwa na kazi au maombi.

Hakuna chochote isipokuwa neema kwa mwenye kufanya wema na moto kwa mwenye kufanya uovu. Miongoni mwa dalili zake ni aliyoaashiria Mwenyezi Mungu kama ifuatavyo:-

Siku itakapopulizwa parapanda nanyi mtakuja makundi makundi.

Parapanda ni baragumu lenye sauti kubwa. Hatujui kuwa Mwenyezi Mungu amekusudia maana yake halisi au ni kinaya tu cha kufufuliwa waliomo makaburini? Vyovyote iwavyo, sisi hatukukalifishwa kuitafuta ilimu hii, wala haina uhusiano na maisha yetu kwa mbali wala karibu.

Na mbingu zitafunguliwa ziwe milango.

Hiki ni kinaya cha kuparaganyika ulimwengu wa juu, zikiwemo nidhamu za sayari na kuondoka mshikamano wake. Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Inawezekana kuwa mbingu ziwe ni milango kwetu, tuuingie ule tunaoutaka kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.”

Na milima itaondolewa iwe sarabi; yaani iwe kama hakuna kitu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَبُسَّتِ الْجِبَالُ بَسًّا {5}

فَكَانَتْ هَبَاءً مُنْبَثًّا {6}

“Na milima itaposagwasagwa, iwe mavumbi yanayopeperushwa.” Juz. 27 (56:5-6).

Yaani itavurugika iwe kama uji, au kama vumbi linalokwenda na upepo.

Hakika Jahannam inangoja, kwa walioasi ndio marejeo.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja dalili za uweza wake, sasa anawahadharisha wale wanopinga utume wa Muhammad (s.a.w.) kuwa Jahannam inawangojea nayo ndio makazi yao pekee na marejeo yao.

Wakae humo siku nyingi.

Neno siku nyingi tumelifasiri kutokana na neno la Kiarabu Ahqab lenye maana ya muda usiojulikana mwisho wake. Imesemekana kuwa maana ya neno hilo ni miaka thamanini. Maana ni kuwa watakaa muda usiokuwa na kikomo wala mwisho.

Hawataonja humo baridi wala kinywaji.

Kwani maji yanaweza kuwa pamoja na Moto?

Isipokuwa maji ya moto na usaha.

Huku ni kuvua kunakoambatana na kinachovuliwa, kwa sababu mwili ndio maji yanayotokota motoni na usaha unaomiminika kutoka kwenye mwili unaounguzwa na Moto.

Ni malipo muwafaka.

Adhabu inaafikiana na matendo yao na maovu yao katika maisha ya dunia:

وَجَزَاءُ سَيِّئَةٍ سَيِّئَةٌ مِثْلُهَا ۖ {40}

“Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo.” Juz. 25 (42:40).

Hakika wao walikuwa hawatarajii kuhisabiwa, na wakazikadhibisha Ishara zetu kuzikadhibisha.

Starehe za dunia zilipofua macho na akili zao, vipi watatarajia kukutana na Mwenyezu Mungu na hali wanaona ishara na ubainifu wake kisha wanaukadhibisha?

Na kila kitu tumekidhibiti kwa kukiandika.

Hakifichiki kwa Mwenyezi Mungu chochote kilicho kwa waja wake, wali­chokifanya usiku au mchana; hata kile wanachokiwazia katika nafsi zao na kinachowapitia katika dhamiri zao.

Basi onjeni! Hatutawazidishia ila adhabu!

Hamna chochote isipokuwa adhabu, wala msiwe na matumaini isipokuwa kuongezewa.

إِنَّ لِلْمُتَّقِينَ مَفَازًا {31}

Hakika wenye takua wana pa kufuzu.

حَدَائِقَ وَأَعْنَابًا {32}

Mabustani na mizabibu.

وَكَوَاعِبَ أَتْرَابًا {33}

Na wasichana walio marika mamoja.

وَكَأْسًا دِهَاقًا {34}

Na bilauri zilizojaa.

لَا يَسْمَعُونَ فِيهَا لَغْوًا وَلَا كِذَّابًا {35}

Hawatasikia humo upuuzi wala uwongo.

جَزَاءً مِنْ رَبِّكَ عَطَاءً حِسَابًا {36}

Malipo kutoka kwa Mola wako, kipawa chenye kuhis­abiwa

رَبِّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا الرَّحْمَٰنِ ۖ لَا يَمْلِكُونَ مِنْهُ خِطَابًا {37}

Mola wa mbingu na ardhi na viliomo kati yake, Mwingi wa rehema; hawamiliki usemi mbele yake.

يَوْمَ يَقُومُ الرُّوحُ وَالْمَلَائِكَةُ صَفًّا ۖ لَا يَتَكَلَّمُونَ إِلَّا مَنْ أَذِنَ لَهُ الرَّحْمَٰنُ وَقَالَ صَوَابًا{38}

Siku atakaposimama Roho na malaika kwa safu. Hawatasema ila atayepewa idhini na Mwingi wa rehema na atasema yaliyo sawa.

ذَٰلِكَ الْيَوْمُ الْحَقُّ ۖ فَمَنْ شَاءَ اتَّخَذَ إِلَىٰ رَبِّهِ مَآبًا {39}

Hiyo ndiyo siku ya haki. Basi anayetaka na ashike njia kurejea kwa Mola wake.

إِنَّا أَنْذَرْنَاكُمْ عَذَابًا قَرِيبًا يَوْمَ يَنْظُرُ الْمَرْءُ مَا قَدَّمَتْ يَدَاهُ وَيَقُولُ الْكَافِرُ يَا لَيْتَنِي كُنْتُ تُرَابًا {40}

Hakika tunawaonya na adhabu iliyo karibu; siku mtu atakapoona yaliyotangulizwa na mikono yake; na kafiri aseme: Laiti ningelikuwa mchanga.

Aya 31 – 40: Wenye Takua Watafuzu

Maana

Hakika wenye takua wana pa kufuzu, kwa kupata thawabu za Mwenyezi Mungu na radhi zake na pia kuokoka na dhabu yake na ghadhabu yake. Pakufuzu, ni Peponi.

Mabustani na mizabibu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amehusisha kutaja mizabibu kutokana na umuhimu wake kwa waliokuwa wakiambiwa.

Na wasichana walio marika mamoja. Hurilaini walio na umri mmoja na ambao matiti yao yamesimama. Na bilauri zilizojaa kinywaji kinachoshuka kooni kwa ladha na uzuri wake.

Hawatasikia humo upuuzi wala uwongo.

Hatasema wala kusikia maneno yasiyokuwa na msingi wala kutokuwa ya kawaida. Hapa kuna ishara kwamba watu wa Peponi ingawaje hawana kazi yoyote, lakini hawatakuwa na upuuzi wa watu wavivu wa duniani.

Malipo kutoka kwa Mola wako, kipawa chenye kuhisabiwa.

Neno malipo linaasharia kuwa thawabu kwa matendo mema ni haki isiyokuwa na shaka, na neno kipawa linaonyesha kuwa Mwenyezi Mungu atawazidishia kwa fadhila yake ziada ya kutosheleza katika yale wanayoy­apendelea na kuyatamani. Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa, ikiwemo ile ya Juz.16 (19:60-63).
Mola wa mbingu na ardhi na viliomo kati yake, Mwingi wa rehema; hawamiliki usemi mbele yake. Ambao watamiliki ni viumbe ambao wameashiriwa kwa kutajwa mbingu na ardhi; kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye Mola wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake.

Maana ni kuwa hizo bustani na neema nyiniginezo za Mwenyezi Mungu alizowapa wenye takua zinatokana na Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu na ni Mmiliki, ambaye hakuna yeyote atakayemhoji kuhusiana na thawabu na adhabu Siku ya Kiyama. Yeye peke yake ndiye atakayefanya vile atakavyo.

Siku atakaposimama Roho na malaika kwa safu. Hawatasema ila atayepewa idhini na Mwingi wa rehema na atasema yaliyo sawa.

Imesemekana kuwa Makusudio ya Roho hapa ni Jibril, kwa vile Mwenyezi Mungu alimwita Roho mwaminifu katika Juz. 19 (26:194). Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Roho ni katika maumbile ya Mwenyezi Mungu yaliyoghaibu kwetu, ambayo hatukukalifishwa kutafuta uhakika wake.”

Maana ni kuwa Malaika watajipanga safu siku ya Kiyama na wataijaza mandhari kwa kuhofisha na kupendeza, wakiwa kwenye utiifu wao na kujikurubisha kwao kwa Mwenyezi Mungu; hawatakua na harakati yoyote wala kusema lolote wao au mwenginewe isipokuwa kwa ruhusa yake Mwenyezi Mungu Mtukufu; wala Mwenyezi Mungu hatamruhusu isipokuwa ambaye maisha yake yote ni usawa, ukweli, uadilifu na haki. Vile vile atakayeruhusiwa hatasema isipokuwa anayoyapenda na kuyataka Mwenyezi Mungu.

Hiyo ndiyo siku ya haki. Basi anayetaka naashike njia kurejea kwa Mola wake.

Siku ya Kiyama ni haki isiyokuwa na shaka, na watu siku hiyo watakuwa makundi mawili: Kundi la motoni litakalokuwa mbali na Mwenyezi Mungu na rehema yake, na kundi jingine litakuwa karibu na Mwenyezi Mungu na rehema yake. Njia ya kuelekea huko iko wazi na imeandaliwa; nayo ni ukweli wa nia. Kwa hiyo basi, ni juu yake mtu kufanya, kwa ikhlasi, kwa mujibu wa utashi wake na raghaba yake ya kuingia Peponi.

Hakika tunawaonya na adhabu iliyo karibu ambayo ni adhabu ya Siku ya Kiyama, kwa sababu kila lijalo liko karibu. Je, kuna jambo lililo karibu zaidi na mtu kuliko mauti?

Siku mtu atakapoona yaliyotangulizwa na mikono yake katika maisha ya duniani yawe ya kheri au ya shari. Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Juz. 3 (3:30).

Na kafiri aseme: Laiti ningelikuwa mchanga. Siku ya haki atatamani mkosefu kuwa mchanga unaokanyagwa na nyayo, kutokana na shida atakayokuwa nayo na kukata tamaa na kuokoka. Hivi ndivyo yalivyo majuto!