read

Sura Ya Sabini Na Tisa: An-Naziaa’t

Imeshuka Makka Ina Aya 46.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

وَالنَّازِعَاتِ غَرْقًا {1}

Naapa kwa zinazotoa kwa nguvu.

وَالنَّاشِطَاتِ نَشْطًا {2}

Na kwa zinazotoa kwa upole.

وَالسَّابِحَاتِ سَبْحًا {3}

Na zinazoogelea sana.

فَالسَّابِقَاتِ سَبْقًا {4}

Na zinazoshindana mbio.

فَالْمُدَبِّرَاتِ أَمْرًا {5}

Zikapangilia mambo.

يَوْمَ تَرْجُفُ الرَّاجِفَةُ {6}

Siku itakapotetemeka mtete­meko.

تَتْبَعُهَا الرَّادِفَةُ {7}

Ifuate ya kufuatia.

قُلُوبٌ يَوْمَئِذٍ وَاجِفَةٌ {8}

Nyoyo siku hiyo zitadundadun­da.

أَبْصَارُهَا خَاشِعَةٌ {9}

Macho yake yatanyenyekea.

يَقُولُونَ أَإِنَّا لَمَرْدُودُونَ فِي الْحَافِرَةِ {10}

Wanasema: Hivi kweli tutarudishwa hali ya kwanza?

أَإِذَا كُنَّا عِظَامًا نَخِرَةً {11}

Pindi tutakapokuwa mifupa iliyooza?

قَالُوا تِلْكَ إِذًا كَرَّةٌ خَاسِرَةٌ {12}

Wanasema: Hayo ni marejeo yenye hasara!

فَإِنَّمَا هِيَ زَجْرَةٌ وَاحِدَةٌ {13}

Kwa hakika hayo ni ukelele mmoja tu.

فَإِذَا هُمْ بِالسَّاهِرَةِ {14}

Mara watakuwa juu ya ardhi.

Aya 1- 14: Zinatoa Kwa Nguvu

Maana

Naapa kwa zinazotoa kwa nguvu.

Kauli za wafasiri zimekua nyingi kuhusu maneno haya; annazia’t ghar­qa na yanayoyafuatia. Tutaelezea kwa muhtasari kauli ya Sheikh Muhammad Abduh kwa jinsi ya alivyokusudia yeye.

Mwenye kufuatilia Aya za Qur’an yenye hikima, atakuta kuwa Mwenyezi Mungu ameapa kwa nyakati, mahali na vitu vinginevyo. Mwenye kutaa­mali yote yale aliyoyaapia Mwenyezi Mungu atakuta ama ni jambo amba­lo watu wamelikana, au kulidharau au hawakujua dalili zilizomo ndani yake za uweza wake Mwenyezi Mungu na ukuu wake.

Kwa hiyo Mwenyezi Mungu Mtukufu akaapa kwa lile wanalolikana ili kuthibitisha kuweko kwake; akaapa kwa lile wanalolidharau ili kulitukuza au akaapa kwa kutanabahisha lile lenye dalili ya uwezo wake ambaye umetukuka ukuu wake. Hapa ameapa kwa baadhi ya viumbe vyake kudhihirisha ufundi wake wa kuvifanya na faida zake, ili wajue wakadhibishaji kuwa mwenye uwezo wa kuyafanya hayo, basi ana uwezo zaidi wa kufufua wafu.

Makusudio ya zinazotoa, hapa ni nyota zinazotupa kama unavyotupa mshale, kwa vile nyota zinatupa vimondo. Waarabu wanalitumia neno hili nazi” kwa maana ya kutupa kwa mshale na pia gharq kwa maana ya mkazo wa kutupa mshale.

Na kwa zinazotoa kwa upole.

Waarabu wanatumia neno nasht, tulililofasiri kwa maana ya kutoa kwa maana ya upole, kwa mtu anayetoka sehemu moja hadi nyingine. Kwa hiyo maana ni kuwa nyota zinatoka kwenye buruji moja hadi nyingine.

Na zinazoogelea sana; yaani nyota zinaogoelea angani

Na zinazoshindana mbio; yaani zinazokamilisha mzunguko wake kwa haraka kwenye kile zinachokizunguka. Na inaeleweka kuwa kasi ya kila kitu ni kulingana na ukubwa wake.

Zikapangilia mambo; yaani nyota zinadhihirisha athari yake kwa yale wanayonufaika nayo watu; kama vile kujua nyakati, mielekeo, kutofau­tiana majira ya mwaka na mambo mengineyo ya maisha.

Huu ndio muhtasari wa kurasa tatu, kutoka Juzuu Amma ya Sheikh Muhammad Abduh, kuhusiana na maneno haya.

Sisi hatukubaliani naye moja kwa moja wala pia hatukubaliani moja kwa moja na waliosema kuwa makusudio ni malaika; au mengineyo yaliyosemwa; kwa vile hayana mategemezi yoyote. Na waliozama katika ilimu wanakiri kutojua na kushindwa maarifa ya ghaibu, wala hawasemi wasiyoyajua.

Siku itakapotetemeka mtetemeko.

Itakayotetemeka hapa ni ardhi kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

يَوْمَ تَرْجُفُ الْأَرْضُ وَالْجِبَالُ وَكَانَتِ الْجِبَالُ {14}

“Siku ambayo ardhi itatikisika na milima.” Juz. 29 (73:14).

Maana ni kuwa ardhi Siku ya Kiyama itavigonganisha viliomo ndani yake na kuharibika.
Ifuate ya kufuatia.

Hiyo ni mbingu ambayo itafuatia kuharibika na kubomoka. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

إِذَا السَّمَاءُ انْفَطَرَتْ {1}

وَإِذَا الْكَوَاكِبُ انْتَثَرَتْ {2}

“Mbingu itakapopasuka Na nyota zitakapopukutika.” (82:1-2).

Nyoyo siku hiyo zitadundadunda, macho yake yatanyenyekea.

Makusudio ya nyoyo hapa ni nyoyo za wakosefu, pale zitakapotambua adhabu itakazozipata, zitapigapiga kwa hofu na athari yake itajitokeza machoni; ambapo hapo nyuma zilikuwa kama nyoyo za wanyama na kama jiwe kwa kususuwaa kwake.

Wanasema: Hivi kweli tutarudishwa hali ya kwanza?

Maneno ‘hali ya kwanza tumeyafasiri’ kutokana na neno la kiarabu Hafira lenye maana ya kurudia kwenye hali iliyokuwako baada ya kuitoka. Maana ni, vipi tunaweza kuwa hai baada ya kuutoka uhai na kuwa wafu? Ni maa­jabu!

Pindi tutakapokuwa mifupa iliyooza kweli tutapata umbo jipya?

Wanasema: Hayo ni marejeo yenye hasara.

Walipinga ufufuo, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawahadharisha na adhabu ya moto; kisha wakasema kwa madharau: basi kama ni hivyo sisi tutakua wenye hasara Siku ya Kiyama. Ndio hivyo hasa, si ajabu hilo, wao watakuwa wenye hasara:

وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ يَوْمَئِذٍ يَخْسَرُ الْمُبْطِلُونَ {27}

“Na siku itakaposimama saa, Siku hiyo watahasirika wenye batili.” Juz. 25 (45:27).

Kwa hakika hayo ni ukelele mmoja tu.

Haya ni maneno ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akiwarudi wakadhabishaji wanaofanya madharau. Maana yake ni kuwa ni jambo jepesi sana kwa Mwenyezi Mungu kuwafufua:

إِنْ كَانَتْ إِلَّا صَيْحَةً وَاحِدَةً  {53}

“Haitakuwa ila ukelele mmoja tu.” Juz. 23 (36:53).

Mara watakuwa juu ya ardhi.

Yaani ukiisha ukelele tu, wao watakusanywa kwenye uwanja.

هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ مُوسَىٰ {15}

Je, imekujia hadithi ya Musa?

إِذْ نَادَاهُ رَبُّهُ بِالْوَادِ الْمُقَدَّسِ طُوًى {16}

Alipomwita Mola wake katika bonde takatifu la Tuwaa:

اذْهَبْ إِلَىٰ فِرْعَوْنَ إِنَّهُ طَغَىٰ {17}

Nenda kwa Firauni. Kwani hakika yeye amepituka mpaka.

فَقُلْ هَلْ لَكَ إِلَىٰ أَنْ تَزَكَّىٰ {18}

Mwambie je, unataka kuji­takasa?

وَأَهْدِيَكَ إِلَىٰ رَبِّكَ فَتَخْشَىٰ {19}

Na nikuongoze kwa Mola wako upate kumcha?

فَأَرَاهُ الْآيَةَ الْكُبْرَىٰ {20}

Basi akamwonyesha Ishara kubwa.

فَكَذَّبَ وَعَصَىٰ {21}

Lakini akakadhibisha na akaasi.

ثُمَّ أَدْبَرَ يَسْعَىٰ {22}

kisha akarudi nyuma na akafanya juhudi.

فَحَشَرَ فَنَادَىٰ {23}

Akakusanya akanadi.

فَقَالَ أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ {24}

Akasema: Mimi ndiye mola wenu mkuu.

فَأَخَذَهُ اللَّهُ نَكَالَ الْآخِرَةِ وَالْأُولَىٰ {25}

Basi Mwenyezi Mungu akamshika kumwadhibu kwa la mwisho na la kwanza.

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَعِبْرَةً لِمَنْ يَخْشَىٰ {26}

Hakika katika hayo kuna mazingatio kwa wenye kuo­gopa.

أَأَنْتُمْ أَشَدُّ خَلْقًا أَمِ السَّمَاءُ ۚ بَنَاهَا {27}

Je, ni vigumu zaidi kuwaumba nyinyi au mbingu aliyoijenga?

رَفَعَ سَمْكَهَا فَسَوَّاهَا {28}

Akainua kimo chake na akaifanya sawa.

وَأَغْطَشَ لَيْلَهَا وَأَخْرَجَ ضُحَاهَا {29}

Akautia giza usiku wake na akautokeza mwanga wake.

وَالْأَرْضَ بَعْدَ ذَٰلِكَ دَحَاهَا {30}

Na baada ya hapo akaitandika ardhi.

أَخْرَجَ مِنْهَا مَاءَهَا وَمَرْعَاهَا {31}

Akatoa humo maji yake na malisho yake.

وَالْجِبَالَ أَرْسَاهَا {32}

Na milima akaiimarisha.

مَتَاعًا لَكُمْ وَلِأَنْعَامِكُمْ {33}

Kwa manufaa yenu na mifugo yenu.

Aya 15 – 33: Hadith Ya Musa

Maana

Je, imekujia hadithi ya Musa?

Hii ni hali ya kumfariji Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Mtume wake mtukufu, Muhammad (s.a.w.); kwamba atamnusuru na maadui zake, kama alivy­omnusuru Musa aliyezungumza na Mwenyezi Mungu. Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 16 (20:9).

Alipomwita Mola wake katika bonde takatifu la Tuwaa.

Bonde hilo liko chini ya Mlima Sinai, jina lake ni Tuwaa. Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:12).

Nenda kwa Firauni. Kwani hakika yeye amepituka mpaka na kuzidi uasi mpaka akadai uungu. Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 16 (20:25).

Mwambie je, unataka kujitakasa?

Je, unapendelea kujitwaharisha na shirki na uchafu?

Na nikuongoze kwa Mola wako upate kumcha?

Mwenye kumcha Mwenyezi Mungu hawezi kupituka mipaka na kufanya ufisadi katika ardhi.

Firauni alimdharau Musa na kusema: Hivi huyu mpuzi anaweza kuongoza! Basi Musa akamwonyesha Ishara kubwa ya fimbo kugeuka nyoka, laki­ni akakadhibisha na akaasi.

Aliupinga muujiza na kusema kuwa ni uchawi; kisha akarudi nyuma na akafanya juhudi ya kumpangia njama Musa; akakusanya akanadi. Alikusanya wachawi na wasaidizi wake akasema:

Mimi ndiye mola wenu mkuu;’’ wala simjui mungu mwingine kwenu asiyekuwa mimi.
Huu ni ubainifu na tafsiri ya kunadi kwake kwa wachawi wake na wasaidizi wake. Watu wengi leo, kabla yake na baada yake wanadai uungu lau wanapata atakayewasadiki.

Basi Mwenyezi Mungu akamshika kumwadhibu kwa la mwisho na la kwanza.

Alimwadhibu kwa kumgharikisha duniani na kumwunguza Akhera.

Hakika katika hayo kuna mazingatio kwa wenye kuogopa mwisho, hivyo wanajitoa shakani na kujiokoa. Lakini mwenye kupuuza atamwad­hibu kwa kujiamini kwake.

Je, ni vigumu zaidi kuwaumba nyinyi au mbingu aliyoijenga?

Maneno yanaelekezwa kwa wale waliokadhibisha ufufuo. Maana ni lipi lenye ugumu zaidi kati ya kurudishwa mtu kama alivyokuwa mara ya kwanza na kuaanzisha kujenga hii mbingu kwa mpangilio wake na nid­hamu yake?

Mfano wake ni kauli yake:

 أَهُمْ أَشَدُّ خَلْقًا أَمْ مَنْ خَلَقْنَا ۚ {11}

“Je, hao ni wenye umbo gumu zaidi au hao wengine tuliowaumba?” Juz. 23 (37:11).

Sheikh Muhammad Abduh anasema: Kujenga ni kukusanya sehemu tofau­

ti na kuzichanganya pamoja mpaka ziwe jengo moja. Hivi ndivyo alivy­ofanya Mwenyezi Mungu kwa nyota; aliiweka kila nyota mahali pake panapolingana; kila moja ikiwa na kani ya mvutano kwa nyingine. Mkusanyiko huu ndio ukawa jengo moja linaloitwa mbingu.

Na hii ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu: akainua kimo chake na akaifanya sawa; yaani aliinua gimba lake juu ya vichwa vyetu akaliweka sawa kila gimba mahali pake.

Akautia giza usiku wake na akautokeza mwanga wake.

Dhamiri ya wake ni ya mbingu, kwa sababu inakuwa na giza kwa kutua jua na inakuwa na mwanga kwa kutokeza jua.

Na baada ya hapo akaitandika ardhi; yaani aliitandaza kwa namna ya kufaa kukaliwa na kutembea juu yake.

Katika kitabu uhawalatu lifahmi asriy liqur’an, imeandikwa hivi, ninanukuu: “Dahaaha, maana yake ni kuwa ameifanya kama yai, jambo ambalo linaungwa mkono na fikra za sasa za kifalaki kuhusu umbo la ardhi… Na neno hilo pia lina maana ya kutandaza.Hili ni neno la kiarabu pekee lenye maana ya kutandaza na kukunja kwa wakati mmoja. Kwa hiyo linakuwa neno bora kwa ardhi iliyokunjuliwa kwa dhahiri na kukunjwa (kuwa mviringo) kiuhakika... Na huu ni ufundi na uficho wa hali ya juu wa kuchagua tamko la undani lililo wazi.

Akatoa humo maji yake na malisho yake.

Maji yote yaliyoko ardhini yanatoka mbinguni; Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “ Juz.18 (23:18). Kisha Mwenyezi Mungu anayabu­ubujiza maji haya kuwa chemichemi na mito; inatoka mimea itakayoliwa na watu na wanayama. Na milima akaiimarisha, ili isiyumbe ardhini wakangona waliomo:

وَأَلْقَىٰ فِي الْأَرْضِ رَوَاسِيَ أَنْ تَمِيدَ بِكُمْ  {15}

“Na akaweka katika ardhi milima ili isiyumbe nanyi.” Juz. 14 (16:15).

Kwa manufaa yenu na mifugo yenu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameiumba ardhi akaitandika na kuiimarisha, kisha akachimbua maji na kutoa mimea; yote hayo ni kwa ajili ya kheri ya mtu na mifugo anayonufaika nayo huyo mtu.

Je, yote haya yamekuja kwa sadfa na bila ya mpango? Au yule aliyeanzisha yote hayo mara ya kwanza atashindwa kuyarudisha mara ya pili?

وَهُوَ الَّذِي يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَهُوَ أَهْوَنُ عَلَيْهِ ۚ {27}

“Naye ndiye ambaye anaanzisha uumbaji kisha ataurudisha.” Juz. 21 (30:27).

فَإِذَا جَاءَتِ الطَّامَّةُ الْكُبْرَىٰ {34}

Basi itakapofika hiyo balaa kubwa.

يَوْمَ يَتَذَكَّرُ الْإِنْسَانُ مَا سَعَىٰ {35}

Siku atakayokumbuka mtu aliyoyahangaikia.

وَبُرِّزَتِ الْجَحِيمُ لِمَنْ يَرَىٰ {36}

Na Moto ukadhihirishwa kwa mwenye kuona.

فَأَمَّا مَنْ طَغَىٰ {37}

Basi ama yule mwenye kupituka mipaka.

وَآثَرَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا {38}

Na akaathirika na maisha ya dunia.

فَإِنَّ الْجَحِيمَ هِيَ الْمَأْوَىٰ {39}

Kwa hakika Moto ndio makazi!

وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ وَنَهَى النَّفْسَ عَنِ الْهَوَىٰ {40}

Na ama mwenye kuogopa kusimama mbele ya Mola wake na akaizuilia nafsi na matamanio.

فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِيَ الْمَأْوَىٰ {41}

Basi hakika Pepo ndio makazi!

يَسْأَلُونَكَ عَنِ السَّاعَةِ أَيَّانَ مُرْسَاهَا {42}

Wanakuuliza saa itakuwa lini?

فِيمَ أَنْتَ مِنْ ذِكْرَاهَا {43}

Una nini na kuitaja?

إِلَىٰ رَبِّكَ مُنْتَهَاهَا {44}

Ni kwa Mola wako ukomo wake.

إِنَّمَا أَنْتَ مُنْذِرُ مَنْ يَخْشَاهَا {45}

Hakika wewe ni muonyaji tu wa anayeiogopa.

كَأَنَّهُمْ يَوْمَ يَرَوْنَهَا لَمْ يَلْبَثُوا إِلَّا عَشِيَّةً أَوْ ضُحَاهَا {46}

Kama kwamba wao siku watakapoiona hawakukaa ila jioni moja au asubuhi yake.

Aya 34 – 46: Balaa Kubwa

Maana

Basi itakapofika hiyo balaa kubwa.

Kitakaposimama Kiyama ulimwengu, ikiwemo ardhi na mbingu yake, utaharibika na hakuna kitakachobaki isipokuwa Muumba wa kila kitu. Hiyo ndio balaa kubwa. Kuna jambo gani kubwa kuliko hilo? Ndio kuanzia hapa ikasemwa: Hakuna balaa isipokuwa juu yake kuna balaa na Kiyama kiko juu ya balaa zote.

Siku atakayokumbuka mtu aliyoyahangaikia.

Akishagura kutoka kwenye kuisha kwenda kwenye kubakia ataona daftari la matendo yake; yakiwa ni kheri basi ni kheri na yakiwa ni shari basi ni shari. Hapo ndio atakumbuka aliyoyahangaikia katika maisha ya dunia na yaliyochumwa na mikono yake.

Na Moto ukadhihirishwa kwa mwenye kuona.

Hakuna kizuizi cha kuuona wala mlinzi wa kumzuia nao; fauka ya hayo:

وَإِنْ مِنْكُمْ إِلَّا وَارِدُهَا ۚ كَانَ عَلَىٰ رَبِّكَ حَتْمًا مَقْضِيًّا {71}

“Hakuna miongoni mwenu ila ni mwenye kuifikia. Ni hukumu ya Mola wako, ni lazima itimizwe.” Juz. 16 (19:71).

Basi ama yule mwenye kupituka mipaka, na akaathirika na maisha ya dunia, kwa hakika Moto ndio makazi yake. Na ama mwenye kuogopa kusimama mbele ya Mola wake na akaizuilia nafsi na matamanio, basi hakika Pepo ndio makazi yake.

Mwenye kufuata matamanio yake yatamwingiza kwenye maangamizi, na mwenye kuyashinda anakuwa ameona njia na kufikia ukomo wa heri.

Matamnio ni ila ya ila zote; amesema kweli aliyesema; “Mwenye kuyatii matamanio yake amempa adui matakwa yake.”

Mwengine naye akasema: “Hakika ya mtu ni nafsi yake; matamanio yake yakishinda nafsi yake basi atakuwa kiumbe mwingine asiyefanana na mtu katika moyo wake wala akili yake.”

Miongoni mwa aliyoyasema Imam Ali katika wasifu wa anayeipima haki kwa matamanio yake ni: “Hajui mlango wa uongofu akaufuata, wala mlan­go wa upofu akajitanibu nao; huyo basi ni maiti hai.”

Hakika ilivyo, ni kuwa Makusudio ya matamanio ni yale yanayohalifu haki na uadilifu; vinginevyo nikuwa nafsi huwa inatamani mambo ya halali, kama inavyotamani haramu.

Wanakuuliza saa ya Kiyama itakuwa lini? Yaani Kiyama kitakuwa lini? Una nini na kuitaja? Ni kwa Mola wako tu ukomo wake. Hakika wewe ni muonyaji tu wa anayeiogopa.

Wanakutaka wewe Muhammad uwaelezee siku ambayo Kiyama kita­tokea; wala hili halihusiani nawe wala na wadhifa wako.

Linalotakikana kwako ni kuwahadharisha watu na hicho Kiyama na vituko vyake; ama kitakuwa lini, ilimu yake iko kwa Mwenyezi Mungu, na hiki­ma yake imetaka kukificha kwa waja wake; hata manabii na wenye kuku­rubishwa. Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7:187).

Kama kwamba wao siku watakapoiona hawakukaa ila jioni moja au asubuhi yake.

Walikikana Kiyama mpaka watakapokiona ndio watakuwa na yakini kuwa ni haki isiyokuwa na shaka na kwamba ndio nyumba ya kubakia na dunia ni mapitio ya kukiendea, kikiwakunja watu kwa mauti wataona kuwa umri wao ulikuwa ni sawa na wakati mdogo au saa moja tu ya mchana.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 11 (10:45).