read

Sura Ya Themanini: Abasa

Imeshuka Makka Ina Aya 42.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

عَبَسَ وَتَوَلَّىٰ {1}

Alikunja uso na akageuka.

أَنْ جَاءَهُ الْأَعْمَىٰ {2}

Kwa sababu alimjia kipofu!

وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّهُ يَزَّكَّىٰ {3}

Na nini kitakujulisha huenda akatakasika?

أَوْ يَذَّكَّرُ فَتَنْفَعَهُ الذِّكْرَىٰ {4}

Au akakumbuka ukamfaa ukumbusho?

أَمَّا مَنِ اسْتَغْنَىٰ {5}

Ama anayejiona amejitosha.

فَأَنْتَ لَهُ تَصَدَّىٰ {6}

Ndio wewe unamshughulikia?

وَمَا عَلَيْكَ أَلَّا يَزَّكَّىٰ {7}

Na si juu yako asipojitakasa.

وَأَمَّا مَنْ جَاءَكَ يَسْعَىٰ {8}

Ama mwenye kukujia mbio mbio.

وَهُوَ يَخْشَىٰ {9}

Naye anaogopa.

فَأَنْتَ عَنْهُ تَلَهَّىٰ {10}

Ndio wewe unajipurukusha naye?

كَلَّا إِنَّهَا تَذْكِرَةٌ {11}

Si hivyo! Hakika hizo ni ukumbusho.

فَمَنْ شَاءَ ذَكَرَهُ {12}

Anayetaka amkumbuke.

فِي صُحُفٍ مُكَرَّمَةٍ {13}

Zimo katika kurasa zilizo­hishimiwa.

مَرْفُوعَةٍ مُطَهَّرَةٍ {14}

Zenye kuinuliwa zilizo­takaswa.

بِأَيْدِي سَفَرَةٍ {15}

Zimo mikononi mwa wajumbe.

كِرَامٍ بَرَرَةٍ {16}

Watukufu, wema.

Aya 1 – 16: Alikunja Uso Na Akageuka

Ni Nani Aliyekunja Uso?

Wameafikiana wafasiri kuwa kipofu ni Ibn Ummi Maktum, swahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) mtoto wa mjomba wa Khadija, mke wa Mtume. Na wamehitalifiana kuhusu aliyekunja uso. Ikasemekana kuwa hajulikani. Kauli hii ina mwelekeo kutokana na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuleta dhamir ya ghaibu (ya asiyekuweko). Mfano huu katika Qur’an ni mwingi; kama vile kauli yake Mwenyezi Mungu : “Kisha akenda kwa watu wake kwa matao.” Juz. 29 (75:33).

Pia imesemekana ni mtu mmoja katika Bani Umayya alikuwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), basi alipomwona kipofu akaona kinyaa na kugeuka.

Kauli iliyo mashuhuri kwa wafasiri na wengineo ni kuwa aliyekunja uso na kugeuka ni Mtume (s.a.w.); na sababu ni kuwa Ibn Ummi Maktum alimjia Mtume alipokuwa na vigogo wa kikuraishi, wenye jaha na mali, wakiwe­mo Utba na Shaiba-watoto wa Rabiaa, Abu Jahl, Walid bin Al-Mughira na wengineo.

Mtume alikuwa amewaacha wengine akiwakabili hawa akiwapa mawaid­ha ya Mwenyezi Mungu na kuwahadharisha na mwisho mbaya wa shirki na dhulma na kuwaahidi heri ya dunia na Akhera, kama wakisilimu. Alifanya hivyo akitaraji kuongoka kwao na kuwa na nguvu ya uislamu au angalau wazuie shari yao. Wakati huo Uislamu ulikuwa bado haujapata nguvu

Basi kipofu fukara akamkatiza Mtume mazungumzo yake, na kusema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, nifundishe nitakayonufaika nayo kati­ka yale aliyokufundisha Mwenyezi Mungu. Mtume akaendelea na maneno yake pamoja na wale jamaa.

Aliporudia kipofu, Mtume alikirihika na likadhihirika hilo kwenye uso wake; ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Nabii wake mtukufu kwa dhamiri ya asiyekuweko ghaibu: Alikunja uso na akageuka; kisha kwa dhamiri ya moja kwa moja mukhatab: Ama anayejiona amejitosheleza wewe unamshughulikia?

Haya ndiyo waliyokwenda nayo wafasiri wengi; na yana mwelekeo wenye nguvu zaidi kuliko ule wa kwanza kutokana na dhamiri ya kuelekeza moja kwa moja ukhatab-wewe, ambayo, kwa dhahiri, makusudio ni Mtume, na inakuwa ni ubainifu na tafsiri ya dhamiri ya ghaibu, kwa kugeukia kwenye mukhatab.

Lakini kauli ya wafasiri kuwa Mwenyezi Mungu alimkaripia Mtume, kwa hilo, haina mwelekeo kabisa, kwani hakuna lililowajibisha karipio wala lawama katika tendo la Mtume (s.a.w.); kwa vile yeye alikuwa akipatiliza fursa pamoja na wale vigogo kwa masilahi ya Uislamu na waislamu, sio kwa masilahi yake wala ya familia yake. Kumfundisha Mwislamu hukumu na matawi kuna wakati mrefu usiokuwa na mpaka, bali kunawezekana wakati wowote.

Kwa ibara ya wanafikhi ni: Kusilimu kafiri wakati wake ni finyu sana (inapopatikana fursa ndio wakati wake huo, hakuna mwingine) lakini kum­fundisha Mwislamu hukumu za dini kuna wasaa mkubwa, inawezekana kutekeleza wakati wowote. Kwa hiyo ulio finyu ni muhimu zaidi na wenye wasaa ni muhimu (ahammu na muhimmu), na la muhimu zaidi ndilo linalotangulizwa, kwa hukumu ya akili. Kwa hiyo basi alivyofanya Mtume ni kheri na hikima.

Unaweza kuuliza: Ikiwa ni hivyo basi wakulaumiwa na kukaripiwa ni kipofu, naye Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemsifu na kumtetea, sasa itakuwaje?

Jibu: Hapana lawama wala karipio katika Aya hizi, si kwa Nabii wala kipo­fu; isipokuwa hali halisi ni kuwadharau na kuwatahayariza washirikina waliokabiliwa na Mtume kwa lengo la kuwavutia kwenye Uislamu; kwa Mwenyezi Mungu kumwambia Mtume wake: Una haraka gani ya nusra ya dini ya Mwenyezi Mungu mpaka ukafikia kuwa na tamaa ya kuongoka viumbe hawa waovu zaidi na walio mafisadi na wapotevu? Achana nao! Hawa ni watu duni zaidi wa kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu na hawana nguvu yoyote ya kuuendeleza Uislamu; kwani Mwenyezi Mungu atawadhalilisha maadui zake, hata wakiwa na nguvu kiasi gani, na ataidhi­hirisha dini yake kuwa juu ya dini zote wajapochukia washirikina.

Aya hizi ziko karibu katika maana yake na Aya isemayo:

فَلَا تَذْهَبْ نَفْسُكَ عَلَيْهِمْ حَسَرَاتٍ ۚ  {8}

“Basi roho yako isitoke kwa kuwasikitikia.” Juz. 22 (35:8).

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akagura kwenda kwenye ripoti ya kiu­jumla na uhakika ambayo ni ‘Mtukufu wenu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule mwenye takua zaidi katika nyinyi.’ Ameiripoti kwa mfumo mwingine ambao ni yule mwenye kucha akawa anajitakasa na kunufaika na mawaidha ndiye anayestahiki takrima na taadhima, lakini yule anayeikataa haki wala asinufaike na mawaidha, inapasa kumtupilia mbali na kumdharau, hata kama ni tajiri wa matajiri na bwana wa wenye jaha.

Maana

Alikunja uso na akageuka, kwa sababu alimjia kipofu ambaye ni Ibn Ummi Maktum aliyemkusudia Mtume (s.a.w.) ili amuulize maswali ya hukumu ya dini yake, lakini akamuacha kwa kushughulika kwake na jambo muhimu, kama tulivyotaja.

Kipofu huyu ni miongoni mwa wahajiri wa mwanzo mwanzo na ni mwad­hini wa pili wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Mara kwa mara alikuwa akimwakilisha Mtume (s.a.w.) kuswalisha watu Madina.

Inasemekana kuwa alizaliwa kipofu na jina lake ni Abdallah. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimpa wasifu wa kipofu kwa kuashiria udhuru wake wa kuwa na hamu ya kujua masuala.

Na nini kitakujulisha huenda akatakasika au akakumbuka ukamfaa ukumbusho?

Yaani ni jambo gani linalokufanya ujue hakika ya kipofu huyu? Lau ungelijibu matakwa yake na ukamweleza baadhi ya hukumu za dini angelinufaika na kuyatumia yale utakayomfunza.

Ama anayejiona amejitosha, ndio wewe unamshughulikia?

Umemuacha yule aliye na haja na kumkabili yule anayejiona kuwa hana haja na Mwenyezi Mungu na wewe kutokana na mali anayomiliki na jaha; ukitarajia kuongoka kwake na kurejea kutoka kwenye upotevu. Je, unatara­jia uongofu kwa yule aliyepofushwa na matamanio na ujinga?

 أَفَأَنْتَ تَهْدِي الْعُمْيَ وَلَوْ كَانُوا لَا يُبْصِرُونَ {43}

“Je, wewe unaweza kuwaongoza vipofu ingawa hawaoni?” Juz. 11 (10:43).

Na si juu yako asipojitakasa.

Si juu yako wala juu ya Uislamu ukafiri wa kafiri na upotevu wake. Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَإِنْ تُعْرِضْ عَنْهُمْ فَلَنْ يَضُرُّوكَ شَيْئًا ۖ {42}

“Na ukiachana nao, hawatakudhuru chochote.” Juz. 6 (5:42).

Ama mwenye kukujia mbio mbio naye anaogopa ndio wewe unajipu­rukusha naye?

Umejishughulisha na washirikina na ukaghafilika na mumin aliyekukusu­dia wewe kufaidika na ilimu yako akitegemea imani yake na kwamba wakati wa mafunzo ni mpana; kwa hiyo achana na mataghuti na umkabili yule aliyeufungua moyo wake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu peke yake.

Si hivyo! Mwenyezi Mungu hawezi kuinusuru dini yake kwa yule anayejiona amejitosheleza, akiwa hana haja na Mwenyezi Mungu wala wewe; kwa vile ana mali na cheo; isipokuwa nusra ya haki itakuja na watu wema, mfano wa kipofu huyu, hata kama ni fukara na masikini.

Hakika hizo ni ukumbusho, anayetaka amkumbuke.

Hizo ni hizo Aya za Qur’an au inawezekana kuwa ni huo uongofu.

Anayekumbukwa ni Mwenyezi Mungu au inawezekana kuwa ni, na aikumbuke hiyo Qur’an. Maana ni kuwa hakika hii Qur’an inatosheleza kuwa ni mwongozo kwa anayeutaka, na si juu yako ewe Muhammad isipokuwa kufikisha tu na kukumbusha; anayetaka naamini na anayetaka na akufuru; kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akaisifu hii Qur’an na mafun­zo yake na hukumu zake kwa kusema:

Zimo katika kurasa zilizohishimi­wa. Ni shani yake iliyoje na utukufu wake mbele ya Mwenyezi Mungu? Zenye kuinuliwa kwa kutukuzwa kutokana na mafunzo yake yenye kun­ufaisha na hikima yake ya hali ya juu zilizotakaswa zisichezewe na upote­vu.

Zimo mikononi mwa wajumbe, watukufu, wema.

Kurasa hizo za Mwenyezi Mungu ziko katika hifadhi isiyofikiwa wakizinukuu malaika kutoka kwa mtukufu aliye juu hadi kwa manabii wake walio maasumu, kwa umakini na uaminifu.

قُتِلَ الْإِنْسَانُ مَا أَكْفَرَهُ {17}

Ameangamia mtu, si ukafiri wake huo!

مِنْ أَيِّ شَيْءٍ خَلَقَهُ {18}

Kwa kitu gani amemuumba?

مِنْ نُطْفَةٍ خَلَقَهُ فَقَدَّرَهُ {19}

Kwa tone la manii amemuum­ba akamkadiria.

ثُمَّ السَّبِيلَ يَسَّرَهُ {20}

Kisha akamfanyia nyepesi njia.

ثُمَّ أَمَاتَهُ فَأَقْبَرَهُ {21}

Kisha akamfisha akamtia kaburini.

ثُمَّ إِذَا شَاءَ أَنْشَرَهُ {22}

Kisha anapotaka atamfufua.

كَلَّا لَمَّا يَقْضِ مَا أَمَرَهُ {23}

Si hivyo! Bado hajatekeleza aliloamrishwa.

فَلْيَنْظُرِ الْإِنْسَانُ إِلَىٰ طَعَامِهِ {24}

Hebu na atazame mtu chakula chake.

أَنَّا صَبَبْنَا الْمَاءَ صَبًّا {25}

Hakika tumeyamimina maji mminiko

ثُمَّ شَقَقْنَا الْأَرْضَ شَقًّا {26}

Kisha tukaipasua ardhi mpa­suko.

فَأَنْبَتْنَا فِيهَا حَبًّا {27}

Tukaotesha humo nafaka.

وَعِنَبًا وَقَضْبًا {28}

Na zabibu na mboga.

وَزَيْتُونًا وَنَخْلًا {29}

Na mizaituni na mitende.

وَحَدَائِقَ غُلْبًا {30}

Na mabustani yenye miti mingi.

وَفَاكِهَةً وَأَبًّا {31}

Na matunda na ndishwa.

مَتَاعًا لَكُمْ وَلِأَنْعَامِكُمْ {32}

Kwa ajili ya manufaa yenu na ya wanyama wenu.

فَإِذَا جَاءَتِ الصَّاخَّةُ {33}

Utakapokuja ukelele mkubwa.

يَوْمَ يَفِرُّ الْمَرْءُ مِنْ أَخِيهِ {34}

Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye.

وَأُمِّهِ وَأَبِيهِ {35}

Na mama yake na baba yake.

وَصَاحِبَتِهِ وَبَنِيهِ {36}

Na mkewe na wanawe.

لِكُلِّ امْرِئٍ مِنْهُمْ يَوْمَئِذٍ شَأْنٌ يُغْنِيهِ {37}

Kila mtu katika wao siku hiyo atakuwa na jambo la kum­tosha.

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ مُسْفِرَةٌ {38}

Siku hiyo kuna nyuso zitaka­zonawirika.

ضَاحِكَةٌ مُسْتَبْشِرَةٌ {39}

Zitacheka, zitafurahika.

وَوُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ عَلَيْهَا غَبَرَةٌ {40}

Na nyuso nyingine siku hiyo zitakuwa na mavumbi.

تَرْهَقُهَا قَتَرَةٌ {41}

Zimefunikwa na giza.

أُولَٰئِكَ هُمُ الْكَفَرَةُ الْفَجَرَةُ {42}

Hao ndio makafiri waovu.

Aya 17 – 42: Ameangamia Mtu Si Ukafiri Wake Huo!

Maana

Ameangamia mtu, si ukafiri wake huo!

Makusudio ya ameangamia hapa ni kuduiwa mtu kwa kuombewa adhabu na maangamizi.

Amesema katika afsir Ar-Razi akinukuu kundi la wafasiri: “Makusudio ya mtu hapa ni kila tajiri aliyejiinua kwa mafukara kwa sababu ya utajiri na ufukara.” Sisi tuko pamoja na kauli hii, kwa sababu hali halisi inashuhudia hilo na kulipa nguvu. Lau si tamaa na ulafi wa kurundika mali angeliishi kila mtu katika raha na amani.

Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Hakika kuduiwa huku kwa mtu kwa maduizo mabaya kabisa ni kinaya cha kuwa mtu amefikia ubaya ambao hastahili kuishi. Chimbuko la kinaya hiki ni ni kusahau kwake neema alizo nazo na kughafilika kwake mpaka akikumbushwa haki anakataa.”

Hakuna shaka kuwa kupatikana, kuwa na utambuzi, kusikia na kuona ni neema; bali ni katika neema kubwa, lakini neema hii haimpelekei mtu kujikuza na kupituka mipaka. Linalomtoa mtu mkosefu kwenye mipaka yake na kumpelekea kufanya dhulma na uadui ni kule kuhisi kwake kuwa ni tajiri na kutofautiana kwake na wengine.

Kwa kitu gani amemuumba? Kwa tone la manii amemuumba akamkadiria.

Makusudio ya kumkadiria ni kumtoa kwenye umbo moja hadi jingine na makuzi baada ya makuzi mengine. Maana ni una nini wewe mtu dhaifu mpaka ukawa unajizuia kumtii Mwenyezi Mungu na kujikuza kwa waja wake? Fikiria asili yako jinsi ulivyogura kutoka umbo moja hadi nyingine na mwenendo wako na mwishilio wako. Ni nani aliyekufanya uweko baada ya kutokuweko, na akakuanzisha kwenye tumbo la mama yako kuto­ka hali moja hadi nyingine. Kisha akakutoa katika umbo zuri? Je, sadfa ndio iliyoyafanya yote haya?

Kisha akamfanyia nyepesi njia.

Mtu ameandaliwa njia ya heri kwa mambo mawili: la kwanza ni kumuon­goza kwenye hiyo heri na kumhimiza. La pili, ni akili na uwezo wa kufanya. Vile vile ameandaliwa njia ya maisha kwa mambo mawili: Kwanza, ni maumbile ya heri zinazotosheleza mahitaji yake. Pili, ni nguvu na maandalizi ya kuweza kuzitumia heri hizo vile atakavyo.
Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa ikiwemo ile iliyoko Juz. 29 (76:1-3).

Kisha akamfisha, baada ya kwisha muda wake, akamtia kaburini.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameamrisha kuzikwa mtu baada ya kufa kwake na akakataza kutupiwa wanyama na ndege, kwa kuashiria heshima ya mtu mbele ya Mwenyezi Mungu hata akiwa amekufa; sikwambii tena akiwa hai.

Kisha anapotaka atamfufua.

Amemuumba, akamfisha, akamtia kaburini kisha atamfufua, kama alivyokuwa mwanzo, kwa ajili ya hisabu na malipo. Lau si ufufuo huu ingelikuwa kuwako mtu ni mchezo ndani ya mchezo. Tazama Juz. 11 (10:4) kifungu ‘Hisabu na malipo ni lazima,’ Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Kisha anapotaka,’ inafahamisha kuwa Yeye pekee ndiye anayejua lini utakua ufufuo na mkusanyiko.

Si hivyo! Bado hajatekeleza aliloamrishwa.

Ambaye hajatekeleza hapa ni mtu mwenye makosa anayepuuza. Maana ni kuwa tumempa mtu nishati zote za kufanya heri na mambo mema, wala hatukumwachia visababu vya kutoa, lakini pamoja na hayo watu wengi wamepuuza na kufanya uzembe; bali wengi katika wao wamepituka mipa­ka na kufanya dhulma, wakazifanya neema za Mwenyezi Mungu ni nyen­zo za ufisadi na kuwafanyia uadui waja. Hebu na atazame mtu chakula chake kilicho mbele yake ambacho ni mhimili wa uhai wake na kuweko kwake.

Aangalie na aiulize akili yake ni nani aliyemsahilishia chakula hiki? Je, ni maumbile? Basi ni nani aliyeyaleta hayo maumbile? Je, ni sadfa? Je, sadfa ina akili ya kukadiria na kupangilia kuweza kuleta maumbile yenye sababu za chakula na kinywaji na mengineyo ya ufundi wa hali ya juu?

Hapana! Hakika tumeyamimina maji mmiminiko. Ni Mwenyezi Mungu tu pekee ndiye aliyeyaleta maji na akayateremsha kutoka mbinguni.

Tumewahi kuelezea mara nyingi kwamba dhahiri ya maumbile inatege­mezwa kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa sababu Yeye ndiye chim­buko la kuweko yote na ndiye msababishi wa sababu.

Kisha tukaipasua ardhi mpasuko, tukaotesha humo nafaka na zabibu na mboga; yaani mimea inapasua ardhi ili itoke; kama kifaranga kinavy­opasua ganda la yai na kutoka mahali alipokuwako.

Na mizaituni na mitende, na mabustani yenye miti mingi; yaani bustani zenye miti na matunda mengi na pia vivuli vyake na uzuri wake.

Na matunda na ndishwa, kwa ajili ya manufaa yenu na ya wanyama wenu.

Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Imepokewa kwamba Abu Bakr ali­ulizwa kuhusu neno Abb (tulilolifasiri kwa maana ya ndishwa), akasema: “Ni mbingu gani itakayonifunika na ni ardhi gani itakayonimeza, nikisema katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu sijui?”

Anaendelea kusema Sheikh Muhammad Abduh: “Imepokewa kutoka kwa Umar Bin Al-khattwab, kwamba yeye alisoma Aya hii akasema: “Yote haya tumeyajua, lakini ni nini abb?” Akavunja fimbo iliyokuwa mkononi mwake, akasema: “Naapa kwa Umri wangu! Hii ndio taklifa, huna neno ewe mwana wa mamie Umar kutojua nini abb…’’ Usidhanie kuwa Sayyidna Umar anakataza kufuatilia maana ya Qur’an; isipokuwa anataka kukufahamisha kuwa lililo wajibu kwako, kama mumin ni kufahamu maana kiujumla.”

Utakapokuja ukelele mkubwa unaziba masikio kukaribia kufanya kizi­wi.

Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye, na na mama yake na baba yake, na mkewe na wanawe. Kila mtu katika wao siku hiyo atakuwa na jambo la kumtosha.
Siku ya Kiyama hakuna mapenzi wala nasabu, kwa sababu kila mtu atakuwa anajishughulikia mwenyewe bila ya kumwangalia mwingine. Hii ni kuashiria kwamba wale anaowapupia mtu duniani na kumuasi Mwenyezi Mungu kwa ajili yao, hawatamfaa kitu akhera wala yeye hatawafaa na chochote.

Katika baadhi ya tafsir imeelezwa kuwa, kutajwa ndugu katika Aya kumekuja kwa mpangilio wa kimaumbile yalivyo; kwa kutangulizwa ndugu kisha wazazi na mwisho mke na watoto.

Kwani mapenzi ya mtu kwa wazazi wake yana nguvu zaidi kuliko ya nduguye, na mapenzi kwa mkewe na wanawe yana nguvu zaidi kuliko ya wazazi wake; ni kama kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Mtu atamkimbia nduguye, hata mama yake na baba yake pia, bali hata mkewe na wanawe.

Siku hiyo kuna nyuso zitakazonawirika, zitacheka, zitafurahika kwa kufurahia malipo makubwa na ya heshima aliyoziandalia Mwenyezi Mungu.

Na nyuso nyingine siku hiyo zitakuwa na mavumbi, zikiwa zimesawiji­ka kwa huzuni. Zimefunikwa na giza la udhalili na uduni. Hao ndio makafiri waovu.

Ukafiri kuupa sifa ya uovu kunaashiria kwamba muovu mwenye kuangamiza yuko sawasawa na kafiri mbele ya Mwenyezi Mungu, hata kama atadumisha swala tano kwa nyakati zake.

Sheikh Muhammad Abduh ana maneno marefu kuhusiana na Aya hii tutayafupiliza kwa namna ifuatayo: Mwenye kuitafuta haki kwa njia ya haki na akaitumia, au akafikiwa na mauti akiwa bado anaitafuta, huyo ndiye atakayecheka na kufurahi Siku ya Kiyama, kwa fadhilia ya Mwenyezi Mungu.

Na mwenye kuidharau akili yake, akajishughulisha na visababu vya kufuata matamanio na akashikamana na ubatilifu, kama walivyokuwa wakifanya maadui wa manabii, basi huyo ndiye ambaye uso wake utafunikwa na giza la huzuni na vumbi la udhalili Siku ya Kiyama.

Hayo ni kutokana na kuwa dini inakataza maovu na yeye anayafanya, dini inaamuru kuchunga masilahi ya umma na yeye anayavunja, dini inawata­ka watu kujitolea mali katika njia ya heri, yeye anaipora ili aitumie katika njia ya shari, dini inaamuru uadilifu na yeye ndiye dhalimu wa madhalimu, dini inaamuru kusema ukweli, yeye anasema uwongo na kuwapenda waon­go… Mwenye kuwa katika hali hii atakuwaje siku atayojitokeza Aliye jabari na kuondoka sitara!